Mama anauawa kisha unashuhudia njia ya maisha yako inapofungwa ghafla.............! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mama anauawa kisha unashuhudia njia ya maisha yako inapofungwa ghafla.............!

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by Mtambuzi, May 22, 2012.

 1. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #1
  May 22, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  1955484629_695e7507bd.jpg
  Picha hii haihusiani na habari hii.............
  Ni kidonda kikubwa cha hisia, lakini nimemudu kukiponyesha na sasa limebaki kovu tu ambalo halina mauamivu kwangu. Kidonda hiki cha kihisia kilitokana na mkwaruzo ulioanzia kwenya familia yetu, yaani kwa wazazi wangu. Ndoa ya wazazi wangu haikuwa ndoa imara na wala mtu asingepaswa kuiita ndoa.

  Nilizaliwa mwaka 1965 katika kijiji cha Segera, mkoani Tanga, kabla ya wazazi wetu hawajahamia Sindeni wilayani Handeni wakati huo, ambako ndiko nyumbani kwa baba yetu. Mama yetu alikuwa anatokea maeneo ya Mombo mkoani Tanga. Tulizaliwa wawili tu kwa baba na mama, mimi na mdogo wangu wa kike.

  Nakumbuka Tangu nikiwa mdogo sana, nilishuhudia mama yangu akiwa anadhalilishwa. Alikuwa anapigwa sana, wakati mwingine alikuwa anavuliwa nguo mbele yetu au hata kutoka nje akikimbia uchi. Nakumbuka hata nilipokuwa naanza darasa la kwanza kuna siku nilichelewa darasani na mwalimu aliyekuwepo aliniuliza kama nilikuwa naamua ugomvi wa baba nyumbani ndio maan nikachelewa. Darasa zuima lilicheka na jambo hili sikulisahau kirahaisi. Ni ajabu kwamba hata zamani kulikuwa na waalimu wahuni.

  Tukiwa wawili, mimi na mdogo wangu nyumbani, tulikuwa kama wakiwa kabisa. Mama yetu kwa kweli alikuwa mama ambaye ni adimu kumpata kwa ukarimu na uadilifu wake. Sisemi hivyo kwa sababu ni mama yangu, hapana. Hata jirani na waliomfahamu walijua jambo hilo na kulisema. Nakumbuka kila wakati alipenda sana kutupa moyo kwamba, maisha ni juhudi, uvumilivu na hekima.

  Nikiwa darasa la nne mwaka 1975 na mdogo wangu akiwa anaanza la kwanza ndipo jambo baya kabisa lililotugusa na pengine kunifanya hivi nilivyo leo lilipotokea. Ilikuwa ni jumamosi nakumbuka nikiwa nimetokea shambani kuhamia ndege wasiharibu mpunga.

  Niliporudi nyumbani hapakuwa na dalili ya kuwepo mtu. Giza lilikuwa limeingia, lakini nyumbani kulikuwa hakujawashwa taa. Niliingia ndani na kumwita mdogo wangu aliyekuwa akiitwa Selina. Lakini hakukuwa na jibu, wakati nikitaka kutoka nje nilisikia kama sauti ya mtu huko chumbani kwa wazazi wangu.

  Niliita 'mama' na nilihisi kama nimeitikiwa. Nilibisha hodi na kuingia chumbani kwa wazazi wangu. Kwa sababu kulikuwa na giza sikuweza kuona vyema madhari ya chumba. Nilitoka na kwenda nje kwenye kibanda kilichokuwa kinatumika kama jiko. Nilichukuwa kiberiti na kurudi chumbani. Niliwasha taa.

  Mama yangu alikuwa amelala kitandani akiwa ametapakaa damu usoni. Hakuwa na uwezo wa kuongea kwa sauti ingawa alikuwa akiongea . Nilimsogelea huku nikiwa nimeogopa sana. Alinyoosha mkono kama vile kuomba nimshike. Nilimshika mkono na alizungumza kwa shida sana. ‘Ni …ba…baba yako, laki….lakini msamehe tu. Mungu…..' Halafu alinyamaza.

  Wakati huo huo watu wawili waliingia ndani. Walikuwa ni wanawake rafiki zake mama. Pamoja nao alikuwepo Selina, ambaye kumbe alitumwa na mama kwenda kuwaita. Wanawake wale walikwenda moja kwa moja pale kitandani na kumkagua mama hukuwakimsemesha. Lakini bila shaka waligundua kwamba mambo sio shwari. Mmoja alitoka haraka.

  Nilitoka na kusimama sebuleni, wakati huo huo tulimwona baba akiwa na katibu kata pamoja na viongozi wengine wa kijiji, wakiingia. Naye baba alikuwa na jeraha usoni lillokuwa likitoka damu bado.
  ‘Basi , wakamshambulia hapa, mimi kufika, ndio nikapigwa panga la uso nikadondoka….' Alisema baba akiashiria kwamba, mama alikuwa ameshambuliwa na watu fulani. Viongozi wale waliingia chumbani kwa wazazi wetu moja kwa moja na huko tulimsikia yule mama aliyebaki mle chumbani akilia.

  Ndivyo mama yetu alivyokufa na bila shaka ni mimi na mama na pia mungu ndio tuliojua kwamba, aliyemuuwa alikuwa ni baba na sio hao watu ambao baba aliwasingizia.
  Tulianza sasa kuishi maisha magumu sana ambayo siyo rahisi mtu kuamini unaposimuliwa. Tulikuwa tunakula kwa kubahatisha, shule tulisimama kwa sababu baba alikuwa kama vile anataka kuona tunakufa kama mama yetu……………

  Nakumbuka kuna siku alinipiga sana kwa sababu tulichukua unga na kukoroga uji na kutumia sukari yake kidogo iliyokuwa mle nyumbani.
  Alinipiga hadi nikapoteza fahamu. Wakati ananipiga alikuwa akiniambia kuwa ataniuwa kama mama. Ukweli ni kwamba ilifika mahali ambapo niliona ni vyema kufanya jambo moja tu, ama kufa au kutoroka. Lakini nilipofikiria kufa, wazo la mdogo wangu lilinifanya kurudi nyuma. Niliamua kwamba, ingekuwa ni vizuri kwetu kutoroka. Mdogo wangu alikuwa mwerevu na mwenye upendo mkubwa na alinikumbusha mama yetu kila wakati.

  Kama baba angekuwa anawaruhusu jirani au wale rafiki mama kutusaidia, huenda tungeishi kwa shida, lakini tungesoma. Lakini baba alikuwa mbogo kwa mtu yeyote ambaye alikuwa anajaribu kutupa msaada. Tulipanga na mdogo wangu tuondoke pale nyumbani na kwenda kwa dada yetu, mtoto wa mama yetu mkubwa aliyekuwa akiishi Mtibwa ambapo nauli yake ilikuwa ni kama shilingi tano.

  Lakini usiku wa kuamkia siku ambayo ilikuwa tuondoke, Selina alianza kujisikia vibaya.
  Usiku alikuwa amepandwa sana na joto na alikuwa anatetemeka. Alikuwa na malaria bila shaka. Hali hii ilimuanza kama wiki wiki mbili nyuma, lakini ilikuwa ikiisha baada ya kunywa vidonge vya aspro. Ilikuwa kama saa sita usiku na baba alikuwa hajarudi. Niliamua kwenda kuwajulisha majirani ili waje watupe msaada. Wakati natoka nilikutana na baba mlangoni. Aliniuliza nilipokuwa naenda na nilimweleza.

  'Kwani umeambiwa mimi sijui kulea, yaani mwanangu akasaidiwe kama manamba, rudi ndani.'
  Aliniambia na kunipiga kibao. Nilirudi ndani nikiwa ninalia kwa uchungu na mambo mengi. Baba aliupiga mlango komeo na kuutia kufuli kwa ndani. 'Toka nione, unajifanya kidume sana.'
  Hakuja kumwangalia Selina na mimi nilikaa kwenye kitanda cha mdogo wangu hadi asubuhi. Kulipokucha na baba alipoondoka nilikimbia kwa majirani kuwambia kwamba, mdogo wangu alikuwa amezidiwa. Ukweli ni kwamba wakati huo mdogo wangu alikuwa amezidiwa kupita kiasi.

  Jirani walifika kwa woga na kuamua kwenda kwanza kwa katibu kata kutoa taarifa ili baba asiwafanyie vurugu. Waliporudi tulimchukuwa mdogo wangu hadi kituo cha afya, Alifanyiwa vipimo na kuonekana ana malaria na tatizo la tumbo. Aliandikiwa dawa. Inasikitisha sana kusema kwamba Selina alifariki usiku wa siku ile. Najua hivyo ndivyo ilivyo, kwamba sitakuja kulia kama nilivyolia siku ile. Maishani mwangu naamini sitakuja kum-miss mtu kama nilivyom-miss mdogo wangu mpendwa. Hata mke wangu siku hizi huwa ninamwambia na anakubali kwamba hata angekuwa yeye ingekuwa hivyo hivyo.

  Kifo cha mdogo wangu kimenisumbua kwa miaka mingi hadi mwaka 2001nilipoanza kusoma gazeti la Jitambue, ndipo nilipojifunza kusahau na kujua kwamba kila jambo linakuja kwa sababu maalum na kwa kawaida ni vizuri tu, kama tutapenda iwe hivyo. Tulimzika mdogo wangu na hakukuwa na matanga. Hakuna jirani ambaye alikuwa tayari kufanya matanga ya kifo cha aina ile. Usiku wa siku ile ndipo nilipoondoka pale kijijini na nasikitika kusema kwamba, sikurudi tena kijijini hapo hadi nilipokuwa mtu mzima, ambapo nilikwenda kutengeneza kaburi la mama na la mdogo wangu Selina.

  Nilifika Mtibwa na kuulizia kiwandani ambapo nilielekezwa. Niliulizia hadi nikafika kwa dada yangu. Huwezi kuamini kwamba, swali la kwanza aliloniuliza huyo dada yangu ni kama nilikuwa nimekwenda pale kuishi au kusalimu tu. Nilipomsimulia kisa chote, Alinimbai kuwa pale kwake siyo nyumba ya kutunza watoto yatima. Alimsimulia mume wake kwamba mama yangu alikuwa mtu mbaya sana. Alieleza kwamba, mimi na marehemu mdogo wangu tulikuwa tumelelewa kwa kudekezwa na hatukuwa watoto wanaoweza kishi na mtu. Inashangaza kwa sababu, huyu dada yangu mwenyewe nilikuwa najuana naye siku ile, nilikuwa simjui bali kumsikia tu kutoka kwa marehemu mama.

  Mumewe alisikiliza maneno yake bila kusema neno. Baadae, huyo shemeji yangu aliniambia tunyooshe miguuili nikakijue kiwanda cha sukari. Tukiwa njiani alinimbia kwamba haamini kuwa dada yangu , yaani mkewe anasema kweli.
  Aliniambia kwamba, anachojua ni kwamba atanisaidia hadi nisome na kumaliza masomo yangu.
  Mwaka 1976 nilianza masomo ya darasa la nne kwenye shule ya msingi Turiani. Kutoka shuleni hadi tulipokuwa tunaishi kwenye kambi za watumishi wa kiwanda cha sukari ni mbali sana, kiasi cha kilomita nane. Nilikuwa natoka asubuhi sana nyumbani nikiwa sijanywa chai na kurejea jioni.

  Mwezi wa kwanza tangu kuanza masomo hali ilikuwa mbaya ingawa siyo sana. Kuna wakati nilikuwa ninalala na njaa, hasa zile siku ambazo shemeji yangu alikuwa akiingia usiku. Shemeji yangu alikuwa ni dereva wa magari ya kusomba miwa kutoka mashambani kwenda kiwandani. Kulikuwa na shifti mbili za kazi, usiku na mchana.

  Shemeji yangu alikuwa ndiye mlinzi wangu kutoka katika shutuma, kashfa na mateso kutoka kwa dada yangu, ambaye marehemu mama alikuwa akimsema kwa uzuri siku zote. Kwa maana hiyo ni kwamba, nilikuwa nimeweza kwenda shule kwa sababu, shemeji yangu alikuwa upande wangu, niliweza kula na kulala kwa sababu ya shemeji yangu.

  Huyu dada alikuwa na watoto wanne, mmoja wa kiume na watatu wa kike. Watoto watatu walikuwa walikuwa wannichukia na kunitendea kama kwamba nilikuwa nimeokotwa na kuletwa pale nyumbani kwao. Mmoja wa kike ambaye alikuwa darasa la pili, ndiye aliyekuwa ananijali na kunihurumia. Kama kweli watoto huchukuwa roho za wazazi wao kama watu wanavyosema, huyu alichukua roho ya baba yake.

  Mwezi wa pili tangu kuanza shule, shemeji yangu alipatwa na malaria na kulazwa kwenye hospitali ya misheni inayoitwa Bwagala. Kwa wiki moja aliyolazwa, nilijua hasa maana ya roho mbaya. Ile siku alipolazwa sikula chakula na asubuhi yake nilikuta nguo zangu za shule zimeloweshwa na kutupwa nje. Dada yangu alinipiga sana, akidai kwamba mimi ni mchawi na ninaharibu bure pesa za mume wake, kwani sikuwa na uwezo wa kusoma.

  Kama sio jirani mmoja ambaye namkumbuka kwa jina hadi sasa, Richard, kuingilia kipigo kile, naamini ningevunjwa mbavu au eneo fulani la mwili lingedhurika. Watoto wa dada mabo ni wapwa zangu walikuwa wakishangilia wakati napigwa na shule hawakwenda siku hiyo. Niliondoka hapo nyumbani baada ya kipigo hicho hadi hospitalini Bwagala. Nilikuwa mtu wa kwanza kuingia wodi ya wagonjwa siku ile.

  Shemeji yangu aliponiona alijua kuna jambo. Sikutaka kumsimulia, lakini aliniomba nimwambie kumetokea kitu gani. Nilimsimulia. Alinitazama kwa muda mrefu sana kabla hajaniuliza, ‘lakini masomo unayaonaje?' nilimwambia, ninaamini akiendelea kuwepo nitafaulu darasa la saba na kusoma zaidi. Alitabasamu na kuniambia ‘nitakuwepo na utafika mbali, mungu hawezi kukunyang'anya kila kitu.'

  Nilimwona akigeukia upande wa pili wa kitanda chake na nina uhakika alilia.
  Aligeuka tena kunitazama kama baada ya dakika kumi. Aliingiza mkono wake mfukoni kwenye lile pajama la hospitalini alilokuwa amevaa na kutoa kitu. Alinyoosha mkono na kunipa. Zilikuwa ni hela. Sikumbuki zilikuwa ni kiasi gani, ingawa kwa kiwango cha sasa ninaweza kusema zilikuwa ni shilingi 2,000.

  Nilisita kuzipokea, lakini macho yake yalinilazimisha kuzipokea. ‘Kafue hizo nguo zako, kesho uende shule. Kumbuka ukitoka shuleni pita pale midizini ule kabisa mghahawani, kabla hujaenda nyumbani.
  Usimwambie una hela au umekula.' Aliniambia. Nilimtazama yule mtu pale kitandani na kuanza kulia. Nilishindawa hata kumwambia ‘asante,' Nilikutana na dada yangu mlangoni wakati naondoka pale wodini. ‘Nyooo, mwanaharamu …..' Nilimsikia akisema.

  Kwa shida shida hivyohivyo nilimaliza darasa la nne na kuingia darasa la tano. Muhula wa kwanza na wa pili wa darasa la nne nilikuwa mtu wa kwanza darasani. Hii ilisaidia na kuniumiza pia. Nilianza kupata marafiki wa nje na nyumbani ambao walikuwa wakinisaidia nilipokuwa na shida kwa sababu walikuwa wakihitaji msaada wangu kimasomo. Lakini kwa nyumbani hali hiyo iliongeza chuki kutoka kwa dada na wapwa zangu. Ni kale kadogo tu, kalikokuwa kanaitwa Msekwa ndiko kalikokuwa kanafurahiya mafanikio yangu.

  Shemeji aliamua kuwa na utaratibu wa kunipa senti kumi kila siku kwa ajili ya kula shuleni na ikawa ni siri yangu. Kuna wakati alikuwa akifika shuleni kuulizia maendeleo yangu, nadhani kwa makusudi ili waalimu wajue kwamba alikuwa na mtoto mwenye akili sana. Hii ilitokana na ukweli kwamba, hakuwa anaulizia matokeo ya watoto wake, ambao walikuwa wakishika namba za mwisho mwisho. Lakini bila shaka alikuw akitaka kunipa moyo, kunionesha kwamba kuna mtu anayenijali. Hii ilinipa nguvu sana na nilimchukulia kama baba yangu kabisa. Nilianza kuona uzito wa kumwita shemeji.

  Lakini upande wa ndoa yake kulikuwa na tatizo. Kila siku kulikuwa na zogo kati ya shemeji na mkewe , yaani dada yangu. Jambo ambalo nilijifunza kwa shemeji ni subira na uvumilivu. Hakuwa akipenda sana kelele na kila zogo lilipoanza alikuwa akijibu kidogo na akiona dada haelewi alikuwa akijiondokea zake kunyoosha miguu kama alivyokuwa akiita mwenyewe. Kwa mara ya kwanza nilianza kuonja upendo wa mzazi wa kiume na kuonjeshwa roho mabaya inavyokuwa kwa mwanamke. Nilimshukuru mungu.

  Lakini hali hiyo haikudumu. Nikiwa darasa la sita, jambo ambalo halikutegemewa na mtu lilitokea. Shemeji yangu alipata ajali ya gari wakati akitoka kusomba miwa. Gari lake lilimgonga mwendesha baiskeli na kumjeruhi sana. Kutokana na kosa hilo, alisimamishwa kazi, na baadae alifukuzwa. Kwa hiyo alitakiwa kuhama kwenye nyumba ile ya kampuni. Ilikuwa bahati kwamba wakati akiwa kazini alikuwa amejenga nyumba ya vyumba viwili iliyoezekwa kwa makuti kijijini Manyinga, umbali wa kilomita mbili kutoka kiwandani.

  Ilibidi tuhamie hapo Manyinga. Alijitahidi kutafuta kazi kila mahali, lakini ilishindikana. Dada yangu alimwongezea machungu kwa kumsimanga. Nakumbuka siku moja walikuw2a wakigombana huko chumbani kwao usiku. Nilimsikia dada akimwambia shemeji kwamba, asipoangalia ataolewa. Alimwambia maneno hayo kwa kizigua. Baada ya kauli hiyo sikusikia tena sauti ya shemeji na mimi binafsi niliumia kuliko hata yeye bila shaka. Asubuhi kabla sijaenda shuleni, shemeji aliniita na kuzungumza nami. ‘Nasafiri leo, usimwambie mtu. Nataka kwenda Moshio kwa kaka yangu, nikajaribu kama nitafanikiwa kupata kazi. Nina kaka yangu yuko kule TPC, nadhani atanisaidia.' Halafu aliendelea. ‘Jitahidi, nikiwa kule nitajitahidi kuhakikisha kwamba unasoma hadi ufike Makerere.'
  Alisema na kutabasamu. ‘Una akili sana na mungu amekupangia jambo kubwa maishani. Vumilia shida, kwa sababu zitakufundisha kuishi na kukabiliana na lolote baya maishani.' Halafu akatoa shilingi 120 kutoka mfukoni na kunipa.

  Niliondoka kwenda shule na inasikitisha kusema kwamba huo ulikuwa mwisho wa kuonana na shemji yangu nikiwa mtoto. Alipoondoka yale mateso yalianza na bila shaka yalikuwa makubwa kuliko mtu anavyoweza kufikiria. Ni mengi kiasi kwamba siwezi kuyaeleza yote. Lakini nayakumbuka yale makubwa ambayo pia ni mengi sana kiasi kwamba nikianza kuyasimulia nitakuchosha wewe msomaji. Lakini kubwa kuliko yote lilikuwa ni lile la kuunguzwa na kwa mafuta ya kula shavuni. Nasema kuwa hili ndilo kubwa zaidi kwa sababu ndilo lililobadili kabisa maisha yangu.

  Hili lilitokea wakati niliwa darasa la saba, ikiwa ni miezi minne tu kabla ya kufanya mtihani wa mwisho.Nilikuwa na uhakika kwamba ningeweza kufaulu iwe au isiwe. Sikuw nauwezo wa kubahatisha kwa kweli. Nilikuwa ninayaelewa maisha. Nakumbuka baada ya shemeji kutoroka, dada yangu hakuwa na njia isipokuwa kuanza biashara ya maandazi na vitumbua. Mimi ndiye niliyekuwa naandaaa unga wa vitumbua na kukanda ule wa maandazi na pia kuchoma vitumbua na maandazi. Pamoja na kufanya kazi hizo kila siku sikuwa ninaruhusiwa kuonja hata kipande cha andazi wala kitumbua. Nilikuwa ninaondoka nyumbani asubuhi bila kunywa chai.

  Siku ya tukio nilikuwa ndio namalizia kuchoma maandazi kwenye saa 12.30asubuhiili nijiandae kwenda shule.
  Mama alikuja na kukagua kazi. Aliona andazi moja likiwa limeungua. Alilichukuwa na kuniuliza, ‘Hivi mama yako ndiye ananunua unga huu unaouchezea?' Nilitaka kujiteta lakini kabla sijafanya hivyo , nilihisi kitu fulani kikiparuza katika shavu langu. Ni mafuta ya moto! Dada alikuwa amechukuwa kijiko mcha mboga kilichokuwa hapo karibu na kuchota mafuta ya moto na kunimwagia. Halafu nilihisi maumivu ambayo ni vigumu kuyaelezea. Nilikurupuka kutoka pale na kutoka nje nikipiga kelele. Huko nje nilishika shavu langu na kutoka na ngozi. Nilikuwa nimeungua sana.

  Kama vile kujihami dada yangu alitoka nje na kupiga kelele kwamba nimemwibia fedha zake zote za biashara. Majirani walikuja kuona kulikoni. Namkumbuka Mzee mmoja wa kichaga au kipare ambaye alikuwa na duka hapo kijijini, aliponiona alisema, ‘tumpeleke hospitalini, ameungua sana' Wazo lake lilikubaliwa haraka na majirani wengine nilikimbizwa Bwagala Hospitalini.

  Je wewe unaamini katika ndoto au maono? Mimi naamini kwa sababu nilishuhudia. Endela kufuatilia mkasa huu wenye kusikitisha lakini pia unafundisha…………...

  Mwendelezo.......Bofya hapa chini:

  https://www.jamiiforums.com/mahusiano-mapenzi-urafiki/267869-mama-anauawa-kisha-unashuhudia-njia-ya-maisha-yako-inapofungwa-ghafla-sehemu-ya-mwisho.html
   
 2. fazaa

  fazaa JF-Expert Member

  #2
  May 22, 2012
  Joined: May 20, 2009
  Messages: 2,986
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Tunaendela na tutaendela kufatilia thread hi na miksaa yake....sababu uwezo wakufatilia tunao, na sababu tunaza na macho ya kusomea thread hii tunayo :biggrin:

  Aisay hio ya kuziwiwa kuonja mandazi na vitumbua ni noma sana.

  Afu unamchoma kwa mafuta ya moto sababu kaunguza andazi...kuna watu wana roho aisay.
   
 3. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #3
  May 22, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Sema tu ukweli, hukusoma between line......LOL
  Yaani una speed ya kusoma kushinda hata ROCKET...............!
   
 4. fazaa

  fazaa JF-Expert Member

  #4
  May 22, 2012
  Joined: May 20, 2009
  Messages: 2,986
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Utani pembeni kama umejua vile, ni kweli sikusoma yote :poa
   
 5. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #5
  May 22, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  fazaa Hata hivyo wewe ni kichwa.....ume-comment as if umesoma yote...............LOL
  Haya nimeshaweka sehemu ya mwisho ya mkasa huu........Unaweza kutii kiu yako.........LOL
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 6. HorsePower

  HorsePower JF-Expert Member

  #6
  May 22, 2012
  Joined: Aug 22, 2008
  Messages: 3,617
  Likes Received: 38
  Trophy Points: 145
  Kaaaaa, ni ukatili ulioje na roho mbaya ya kiwango gani hiki!
   
 7. Riwa

  Riwa JF-Expert Member

  #7
  May 22, 2012
  Joined: Oct 11, 2007
  Messages: 2,601
  Likes Received: 234
  Trophy Points: 160
  Wooow....Mtambuzi tell me hii stori ni ya kutunga..ni ya kutunga haiwezi kuwa kweli!?
   
 8. Mr Rocky

  Mr Rocky JF-Expert Member

  #8
  May 22, 2012
  Joined: Oct 10, 2007
  Messages: 15,186
  Likes Received: 570
  Trophy Points: 280
  Mkuu kisa cha kusikitisha sana
  Ila malizia bana umekikatisha aise
   
 9. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #9
  May 22, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Riwa ni stori ya kweli kabisa na mhusika yupo na anaendelea kulitumikia Taifa........Soma sehemu ya mwisho ya mkasa huu ambayo nimeshaiweka humu MMU utajua ukweli halisi wa kile kilichotokea................
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 10. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #10
  May 22, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Mr Rocky nimeshaweka sehemu ya mwisho ya mkasa huu hapa hapa MMU
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 11. Ruttashobolwa

  Ruttashobolwa JF-Expert Member

  #11
  May 22, 2012
  Joined: Feb 22, 2012
  Messages: 43,748
  Likes Received: 12,842
  Trophy Points: 280
  so sad
   
 12. Mr Rocky

  Mr Rocky JF-Expert Member

  #12
  May 22, 2012
  Joined: Oct 10, 2007
  Messages: 15,186
  Likes Received: 570
  Trophy Points: 280
  Mkuu Mtambuzi nimeisoma
  Dunia hii mtendee mwenzako jema as hujui kesho na kesho kutwa atakuwa nani na atakuwa wapi
  Wengi wengi tunawafanyia visa na mikasa watu bila kujua wala kuwaza kuwa kuna jambo alilowapangia Mungu maishani mwao
  hatuna utu wala hatujali na haswa inapotokea tunaowafanyia sio watoto wetu ila watu tulioaminiwa kukaa nao majumbani mwetu
  Siku ya siku utakapokutana na the same person ambaye ulimnyanyasa na kumtukana na kumtesa yuko kwenye position ambayo unaona hata aibu kumfuata unaishia sasa kuanza kuomba sahamani na kujiona mjinga
   
 13. chuki

  chuki JF-Expert Member

  #13
  May 22, 2012
  Joined: Mar 10, 2011
  Messages: 2,691
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Sasa utaendelea lini? Utai-ttitle namna gani ili tujue ni mwendelezo wa story yenyewe.
  Lakini uwe makini shigong'o asiione.
   
 14. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #14
  May 22, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 15. Ndahani

  Ndahani JF-Expert Member

  #15
  May 22, 2012
  Joined: Jun 3, 2008
  Messages: 14,343
  Likes Received: 1,810
  Trophy Points: 280
  Mhhh! Mpaka naogopa
   
 16. mkomatembo

  mkomatembo JF-Expert Member

  #16
  May 22, 2012
  Joined: Dec 17, 2011
  Messages: 1,466
  Likes Received: 503
  Trophy Points: 280
  Aisee huyu dada ni katili kweli kweli, ngoja nisome sehemu ya mwisho ! sasa mie sijaelewa Mtambuzi, huyu dada ni mtoto wa yule baba alouwa au vipi? na je huyu baba alikamatwa? ngoja nisome the second part ! lakini bwana leo SIO IJUMAA mbona umechakachuwa ?
   
 17. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #17
  May 22, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  mkomatembo .....Hii sio kesi kama zile za Ijumaa ....Hii ni simulizi tu ya kisa cha kweli ambacho kiliwahi kuandikwa katika gazeti la JITAMBUE mwaka 2007... Nimeona nikirejee kisa hiki hapa JF kwa sababu naamini wengi hawakupata bahati ya kukisoma wakati ule.............

  Huyo dada alikuwa ni mtoto wa mama yake mkubwa (RIP) na Joseph na baba yake hakukamatwa kwa sababu alidanganya kwamba walivamiwa na majambazi na miaka ile ya 70s, huko vijijini sheria haikuwa na mkono mrefu kama ilivyo sasa.
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 18. Lushinde

  Lushinde Member

  #18
  May 22, 2012
  Joined: Apr 25, 2012
  Messages: 11
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Watu wana roho mbaya kudadadeki. Yaani unaua mke na watoto hivi hivi. Lakini dogo ana roho nzuri sana
   
 19. queenkami

  queenkami JF-Expert Member

  #19
  May 22, 2012
  Joined: Feb 8, 2010
  Messages: 1,340
  Likes Received: 25
  Trophy Points: 135
  Najuta kuisoma mbele za watu.
  Nimepambana na machozi lkn yamenishinda,yanatiririka kama mvua. Mtambuzi please naomba uniambie kama hii ni hadithi ya kutunga au kisa cha kweli.
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 20. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #20
  May 22, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Hii sio hadithi queenkami , ni ushuhuda wa kweli kabisa kama nilivyoeleza na mhusika yupo anaendelea kulitumikia Taifa
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
Loading...