Hizi imani nyingine zitatufikisha pabaya!
Na Suleiman Abeid, Shinyanga
- Adai ni kutimiza matakwa ya mizimu ya kwao
JESHI la Polisi mkoani hapa linamshikilia mwanamke mkazi wa kitongoji cha Ndembezi mjini hapa akituhumiwa kumuua kwa kumkanyagakanyaga ndani ya beseni la maji mwanawe mwenye umri wa miezi mitano kwa alichodai ni kutumwa na mizimu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Shaibu Ibrahimu, alimtaja mwanamke huyo kuwa ni Bibi Regina Kashindye (38) na kwamba alifanya hivyo Juni mosi mwaka huu saa tisa usiku.
Kamanda Ibrahimu alisema mwanamke huyo awali aliondoka nyumbani kwa mumewe, baada ya ugomvi kati yao na kusababisha kutokuelewana na hivyo kurejea nyumbani kwa wazazi wake.
Hata hivyo, Kamanda alisema, siku ya tukio mwanamke huyo alirejea kwa mumewe akiwa na mwanawe huyo Joseph Deus, lakini saa nne usiku aliondoka tena nyumbani hapo bila kumuaga mumewe na kwenda kusikojulikana.
Ilipotimu saa tisa usiku, alirejea nyumbani kwa mumewe akiwa uchi huku kichwani amebeba beseni lenye nguo.
Alisema mumewe alishangazwa na hali aliyomwona nayo mkewe na kumuuliza alikomwacha mtoto akamwonesha beseni alimokuwa mtoto.
�...alipofunua nguo akamkuta mtoto akiwa ameshafariki dunia, alishangaa na hivyo kupiga mayowe kuomba msaada wa majirani na walipofika walimvika nguo kwanza, wakamchukua na kumpeleka katika kituo cha Polisi,� alieleza Kamanda Ibrahimu.
Kamanda alisema, katika mahojiano ya awali mwanamke huyo alisema aliamua kumuua mwanawe huyo ili kutekeleza maagizo aliyopewa na mizimu ya kwao.
�Kwa kweli ni kitendo cha kusikitisha, hivi sasa tunafanya taratibu za kumpeleka hospitali ili apimwe akili, tunahisi kuwa huenda alichanganyikiwa kabla ya kufikia uamuzi huo wa kumuua mwanawe huyo mchanga,� alieleza Kamanda Ibrahimu.
SOURCE: Majira