Malumbano Ya Ccm Na Kafu Hayatufikishi Popote:::

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
48,851
18,948
Malumbano haya ya CCM na CUF hayatufikishi kokote
Mhariri
Daily News; Thursday,May 15, 2008 @00:01

Katika kipindi cha siku nne zilizopita tumeshuhudia malumbano, lawama na makombora ya maneno ambayo viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) wamekuwa wakirushiana kuhusiana na kukwama kwa mazungumzo ya namna ya kumaliza mpasuko wa kisiasa huko Visiwani.

Wakati CCM wiki iliyopita ilielekeza lawama kwa CUF kwa madai ya kupotosha na kutoboa siri za mazungumzo hayo kinyume cha makubaliano, wenzao CUF juzi waliibuka na kabrasha zima la dondoo za vikao hivyo na kudai kwamba CCM haisemi ukweli kwamba makubaliano yalikwishafikiwa kuhusu suala la kuundwa kwa Serikali shirikishi.

Kwa kufuatilia namna vyama hivyo vinavyoshambuliana kwa kauli na shutuma nzito, kuna hatari kwamba kwa siku kadhaa Watanzania watakuwa mashuhuda wa matukio ya siasa yanayoweza kulinganishwa na mchezo wa kuigiza, huku wakikatishwa tamaa kuhusu uwezekano wa kupatikana haraka kwa suluhu ya vuta nikuvute ya kisiasa huko Zanzibar.

Kwa maoni yetu, kiu ya Watanzania ni kumalizika mara moja kwa malumbano haya, ambayo kwa hakika hayastahili kuwapo na si malumbano. Katika kipindi hiki ambacho umebaki muda mfupi kabla ya kufanyika tena kwa uchaguzi mkuu mwaka 2010, licha ya kushughulikia masuala ya utulivu wa siasa, nguvu zaidi na ya pamoja inapaswa ielekezwe katika shughuli za ujenzi wa nchi na kujitoa katika dimbwi la umasikini.

Ingawa tunatambua kwamba jitihada hizo za ujenzi wa taifa haziwezi kuwa na tija kama nchi haina mshikamano wala utulivu wa siasa, tunawakumbusha viongozi wa CCM na CUF kwamba dhamana, umuhimu na heshima ambayo vyama vyao vinapewa katika kushughulikia mpasuko wa Zanzibar visitumike kama kigezo na kisingizio cha kuifanya nchi itumie nguvu na raslimali zake nyingi katika kushughulikia suala hilo tu.

Wakati umefika wa umma kuwaambia inatosha. Acheni malumbano na kwa maslahi ya taifa rejeeni katika meza ya mazungumzo na kusawazisha pale ambako mliteleza. Vinginevyo, na kwa kauli na matendo yenu, mtazidi kuchochea moto wa mgawanyiko wa siasa na jamii Visiwani
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom