Malipo pensheni ya wazee yanavyompandisha Dk Shein

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameanza kutekeleza kwa haraka ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2015-2020 aliyoinadi wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka jana, hatua ambayo imewakuna viongozi wa chama hicho na wananchi kwa ujumla.

Miongoni mwa ahadi alizoanza kutekeleza katika kipindi kifupi ni pamoja na pensheni ya jamii kwa wazee wenye umri wa miaka 70 sambamba na kutangaza kima kipya cha chini cha mishahara ya watumishi serikalini. Akizungumza na gazeti hili, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Vuai Ali Vuai anasema chama hicho kimemepata faraja kubwa kutokana na kasi ya Rais Shein kuanza mara moja utekelezaji wa ilani pamoja na ahadi zake kwa wananchi wa Unguja na Pemba.

Anasema utekelezaji huo umepokelewa kwa furaha kubwa na CCM kwa sababu ndiyo mkataba wa kazi kati ya Rais aliyepeperusha bendera ya chama hicho pamoja na wananchi ambao wapiga kura. Anasema hatua ya Serikali ya Dk Shein kuanza mara moja kutekeleza suala la wazee kulipwa pensheni ili kupunguza ugumu wa maisha imepokelewa kwa furaha na wananchi wakiwemo ambao waliona kama ahadi hiyo ni porojo za kuombea kura.

Anasema uamuzi wa kulipwa pensheni wazee waliofikia umri wa miaka 70 ni kitendo cha kupigiwa mfano ambacho hakipo katika nchi nyingi za Bara la Afrika na baadhi ya nchi dunia. “Huu ni uamuzi wa kiungwana sana unaozingatia ubinadamu na thamani yake kwa ujumla kwa wazee ambao walitumia muda wao mwingi kwa ajili ya kulitumikia taifa kwa uaminifu mkubwa,” anasema.

Anaongeza: “Chama Cha Mapinduzi kinatoa pongezi za dhati kwa Rais Shein alivyoonesha uungwana wa kutekeleza ahadi zake ambazo alizitoa katika kipindi cha mikutano ya kampeni Unguja na Pemba.” Anasema wapo waliokejeli kauli zake katika kipindi cha mikutano ya hadhara eti kwa kusema atapata wapi fedha za kulipa wazee wengi waliostaafu kazi pamoja na kuongeza mshahara kima cha chini kuwa 300,000 kwa mwezi “lakini sasa wanabaki na aibu”.

Tayari jumla ya wazee 18,371 wameanza kulipwa pensheni ya jamii katika maeneo mbalimbali Unguja na Pemba. Akizungumza na waandishi wa habari, mratibu anayesimamia zoezi hilo, Salum Rashid anasema zoezi la ulipaji wa pensheni kwa wazee waliofikisha umri wa miaka 70 limepokelewa vizuri na jamii hiyo kujitokeza kwa wingi. Anasema zoezi hilo limetekelezwa kwa mafanikio ambapo asilimia 86 ya walengwa 18,371 walilipwa fedha hizo kati ya wastaafu waliokusudiwa 21,000 na kwamba idadi iliyobakia ni wale ambao hawakupata taarifa kikamilifu kuhusu tarehe kamili ya malipo na wengine ni wagonjwa.

“Zoezi la kulipa fedha za pensheni ya jamii kwa wananchi ikiwemo wazee waliostaafu limefanikiwa kwa asilimia 86 huku walengwa wakijitokeza kwa wingi sana,” anasema. Rashidi anasema utafiti na uchunguzi uliofanywa umebaini kwamba bado ipo idadi kubwa ya wazee wenye sifa za kulipwa fedha hizo ambao hawajasajiliwa.

Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji Ustawi wa Jamii, Wazee, Wanawake na Watoto, Fatma Gharib Bilali, anasema kazi kubwa inayofuata kwa sasa ni kufanya usajili kwa baadhi ya wazee ambao hawajaorodheshwa kupata fedha hizo. Anasema lengo la serikali ni kuhakikisha kwamba wazee wote wenye sifa za kulipwa fedha hizo wanasajiliwa na kutambuliwa rasmi kwa ajili ya malipo hayo.

“Tutahakikisha tunawasajili kwa ajili ya kuwatambua wazee wengine ambao hatukuwafikia katika zoezi la awali la utambulisho kwani lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha wote wenye sifa wapate stahili yao,” alisema. Mzee Ali Haji Ussi, mkazi wa Magomeni Unguja alikuwa miongoni mwa wazee waliofaidika na fedha za pensheni ya jamii ambapo anasema anaishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Shein kwa kuja na kitu ambacho faida yake ni kubwa na haitosahaulika milele na wananchi.

“Naishukuru kwa dhati kabisa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kubuni kitu kama hichi ambacho kimetunufaisha sote ikiwemo wazee ambao hatukubahatika kufanya kazi serikalini,” anasema. Pensheni ya jamii inatolewa kwa wazee wote waliofikia umri wa miaka 70 bila ya kujali kama aliwahi kufanya kazi serikalini au la.

Akizindua pensheni ya jamii kwa wastaafu, Kiembesamaki mjini Unguja, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Khalid Salum Mohamed alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya kuhakikisha wazee wanaenziwa na kupata huduma zote muhimu kwa kutambua mchango wao wakati wa utumishi wa umma. Aliwataka watendaji na wasimamizi wa kutoa fedha za pensheni kwa wastaafu kuwa watulivu na wastahamilivu kwa kutoa lugha nzuri wakati wanapowahudumia wazee.

“Utoaji wa fedha za pensheni ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya kuhakikisha wazee wanatunzwa na kuenziwa kwa kupata huduma zote ili kuwapunguzia mzigo wa ugumu wa maisha,” anasema. Katika bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2015-2016 katika utoaji wa fedha za pensheni kwa wazee wastaafu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga jumla ya Sh bilioni 3 kwa ajili hiyo.

Katika kuhakikisha Serikali inatekeleza dhana ya utoaji wa pensheni kwa wazee wastaafu, zipo baadhi ya taasisi zilizofanya kazi kubwa ya ushawishi ikiwemo Jumuiya ya Wazee na Wastaafu (Jumaza). Aboud Talib ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi Jumaza ambaye ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutekeleza na hatimaye kutimiza ndoto ya kutoa pensheni ya wastaafu waliotimiza umri wa miaka 70.

Anasema pensheni hiyo ni mkombozi kwa wazee katika juhudi za kupambana na hali ngumu ya maisha na kusema Zanzibar ni nchi ya kwanza katika Afrika ya Mashariki na Kati kutoa pensheni ya aina hiyo kwa watu wake. “Jumaza tunaipongeza kwa dhati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutekeleza ahadi zake za kutoa pensheni kwa wazee waliofikisha umri wa miaka 70 bila ya kujali aliyewahi kuwa mtumishi Serikali au ambaye hakufanya kazi ya ajira,” anasema.

habari leo
 
Hizo pesa zinatoka bara, znz haina uchumi wala majukumu
Wanalipa pensheni watueleze, muungano kwa ujumla wanachangia nini?
Hawana majukumu kwanini wasiwe na za pensheni za uzeeni?
 
Back
Top Bottom