Mali za walioiba bilioni 124/- za Ushirika kutaifishwa

elivina shambuni

JF-Expert Member
Joined
May 31, 2018
Messages
462
Points
500

elivina shambuni

JF-Expert Member
Joined May 31, 2018
462 500
Vyama vya ushirika vimekumbwa na kashfa nzito ya ubadhirifu na wizi wa zaidi ya Sh bilioni 124.05, ambazo ni fedha za wanachama kutokana na ukaguzi wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika (Coasco) katika mwaka 2018/19.

Orodha ya vyama vilinavyotuhumiwa kuhusika na ubadhirifu wa Sh 124,053,250,874.00, amekabidhiwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Brigedia Jenerali John Mbungo kwa ajili ya kuchunguza na kuwafikisha mahakamani wahusika wa ubadhirifu wa fedha hizo.

Akizungumza na wanahabari jijini hapa jana, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema ripoti ya Coasco inaonesha kuna dosari katika vyama hivyo, ndio maana vingi kati yake vimepata hati zenye mashaka, isiyoridhisha na hati mbaya baada ya kufanyiwa ukaguzi maalumu unaonesha kuna ubadhirifu na viashirika vya wizi.

Amesema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 113.4 hazionekani zilipo zimeyeyuka na hazionekani zimekwenda wapi, Sh 87,694,976,970 zimepotea kwa nia ovu, lakini Sh bilioni 22.9 ni hasara kutokana na kutendwa kwa uzembe huku Sh bilioni 2.8 zimeibwa.

Alisema ukaguzi maalumu uliofanyika kati ya mwaka 2018/19, ulibaini kwamba Sh bilioni 10.66 zilikuwa zimepotea, ambapo kati yake Sh bilioni 6.3 zimepotea kwa nia ovu, wakati Sh bilioni 2.6 ni hasara na Sh bilioni 1.7 zimepotea kwa wizi na ubadhirifu na hivyo kufanya Sh bilioni 124.05 kupotea.

Hasunga alisema hadi 30 Juni 2019, vyama vya ushirika vilivyosajiliwa vilikuwa 11,410 ambavyo kati ya vyama hivyo, vyama hai ni 6,463, vyama sinzia ni 2,844 na vyama ambavyo havipatikani 2,103.

Alisema hadi 30 Juni 2019, Coasco ilikagua vyama vya ushirika vipatavyo 4,413 sawa na asilimia 102.63 ya lengo la serikali la kukagua vyama 4,300.

Alisema katika vyama hivyo 4,413 vilivyokaguliwa, vyama 303 sawa na asilimia 6.87 vilipata hati inayoridhisha, vyama 2,378 sawa na asilimia 53.89 vilipata hati yenye shaka, vyama 879 sawa na asilimia 19.92 vilipata hati isiyoridhisha na vyama 853 alisema 19.32 vilipata hati mbaya.

Katika orodha ya vyama 4,413, vilikuwapo vyama vikuu 38, vyama vya mazao (Amcos) 2,710, vyama vya akiba na mikopo (Saccos) na vyama vingine 217.

Katika orodha ya vyama vikuu 38, vyama vinne vilipata hati safi, vyama 22 vilipata hati yenye shaka, tisa vilipata hati isiyoridhisha na vitatu hati mbaya.

Vyama vikuu vitatu vilipata hati mbaya kuhusu hoja zenye viashiria vya ubadhirifu, navyo ni Runali Sh milioni 856.35, SCCULT Sh milioni 4.9 na KYECU ambayo kulikosekana hati za kuhesabu mali za kudumu mwisho wa mwaka.

Alisema Chama Kilele ambalo ni Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC), kimepata hati isiyoridhisha, ambayo inajumuisha fedha benki zisizofanyiwa malinganisho na pia kutooneshwa katika taarifa za fedha kiasi cha Sh bilioni 1.5.

“Katika orodha hiyo ya vyama vya Ushirika wa Mazao (AMCOS) 2,710 vilivyokaguliwa, vyama 15 vilipata Hati Safi, 1347 Hati yenye Shaka, 599 Hati Isiyoridhisha na vyama 749 vilipata Hati Mbaya,” alisema waziri.

Alisema matatizo makuu katika Amcos ni kushindwa kuandika vitabu vya hesabu, malipo mengi kutokuwa na vielelezo vya malipo, mifumo dhaifu ya udhibiti wa makusanyo na mauzo ya mazao, kukosekana kwa daftari la mali za vyama na watendaji wa vyama kutokuwa na weledi wa kuandika vitabu na taarifa za fedha za vyama.

Aliwataka waajiri ambao wanakata fedha za wanachama na kutozifikisha kwenye vyama vya akiba na mikopo wafanye hivyo mara moja.

Kutokana na uchunguzi huo, kati ya Saccos 1,448, 261 zilipata hati safi, 887 yenye shaka, 218 isiyoridhisha na 82 hati mbaya.

Alisema matatizo makuu ya Saccos ni kushindwa kuandika vitabu ipasavyo, marejesho ya mikopo ya wanachama kutofanyika kwa wakati, baadhi ya waajiri kuchelewesha kuwasilisha makato ya wanachama, madeni makubwa yanayothiri utendaji, miamala ya benki kutofanyiwa malinganisho na baadhi ya miamala kuwa na ubadhirifu.

Alisema Wizara ya Kilimo inakabidhi Takukuru taarifa ya Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika ya Mwaka 2019 ili itumie sheria na madaraka kufanya uchunguzi na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali Mbungo alisema wanatoa nafasi kwa waliohusika na ubadhirifu wa mamilioni ya fedha kuzirudisha, na kama watashindwa kufanya hivyo, Takukuru itachukua hatua za kutaifisha mali zao, mifugo, nyumba na rasilimali zao wanazomiliki hadi sasa. Alisema hakuna jiwe litakalosalia juu ya lingine.

Alisema wale watakaobainika kuhusika na ubadhirifu wa mali na rasilimali na fedha za wana ushirika na vyama vya ushirika, watataifishwa mali zao zote ili kufidia.

Alisema watakaoshindwa kurudisha, basi uchunguzi ukikamilika, watawafikishwa mahakamani na lengo ni kuhakikisha fedha hizo wanazirudisha.

Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini, Dk Titus Kamani alisema watatoa ushirikiano kwa Takukuru, kuhakikisha wale wote waliojichukulia mali za vyama vya ushirika na waliodai mali za ushirika hazina mwenyewe na kuzitumia kwa maslahi yao, wanarudisha mali hizo
 

Forum statistics

Threads 1,381,744
Members 526,189
Posts 33,810,776
Top