Malezi ~ Wazazi wana hadhi sawa katika malezi ya watoto

Sema Tanzania

JF-Expert Member
May 18, 2016
251
465
Yawezekana unazo sababu nzuri tu za kukufanya utake kudhoofisha mahusiano ya mwanao na mzazi mwenzio. Labda alimkataa mtoto (ujauzito), ama hatoi matunzo (pesa na mengineyo) kwa mtoto. Ingawa sababu hizi zina mashiko, makala yetu yanataka kuangazia athari anazopata mtoto mzazi ukiamua kumtenga na mzazi mwenzako.

Ifahamike kuwa ni jambo la kawaida kuona watoto wakipendelea mzazi mmojawapo kati ya baba au mama. Kisaikolojia mtoto wa kike humpenda baba zaidi na wa kiume humpenda mama zaidi kwa sababu ya mvuto wa kijinsia, ambapo baba huwa ni rafiki wa kwanza wa kiume kwa mtoto wa kike na vivyo hivyo mama kwa mtoto wa kiume

Ukiamua kumtumia mtoto ‘kulipiza visasi’ vya ungomnvi wa kimahusiano baina yenu wazazi, kwanza utalazimika ‘kumponda’ mwenzio na maneno yasiyofaa ukidhamiria kumfanya aonekana si lolote na kwamba ni mtu mbaya wa tabia na mambo mengine kama hayo. Kumbuka, huyu ni mzazi kwa mtoto hata kama humpendi bora ukae kimya kuliko kumwambia mtoto baba/mama yake ni mtu asiyefaa. Ukifanya hivi unamwepushia balaa la kukua na chuki katika umri mdogo. Ndio kwanza anaanza maisha, kwanini aanze na mizigo ya chuki unazombebesha maishani?

Wapo baadhi ya wazazi ambao kufanya hivi makusudi lakini tunaamini wapo ambao hufanya hivi bila kujua kama wanakosea na hivyo kupelekea kuharibu mahusioano kati ya mtoto na mzazi mmoja, hali hii inaweza kumfanya mtoto kujitenga na mzazi kiasi ambacho anaweza kuonyesha ubaya na chuki aliyonayo dhidi yake na kukataa kabisa kujihusisha naye.

Mzazi mwenye lengo la kumharibia mzazi mwenzie mahusiano na mtoto wake huweza kumnenea mabaya mzazi mwenzie, kumlaghai mtoto kwa maneno au zawadi, kumzuia mzazi mwenzie kupata muda wa kuwa na mtoto. Tabia za namna hii inasaidia kumfunza mtoto misamiati ya kibaguzi, na lugha nzito aina hiyo katika umri mdogo kitu ambacho hakihitaji toka kwako mzazi

Mtoto ataanza kumuona mzazi mmojawapo kama asiyefaa, mkorofi asiye na upendo. Utofauti wanao tengenezewa watoto dhidi ya wazazi wao hupelekea watoto kuchanganyikiwa, kukosa muelekeo na kushindwa kuwaelewa wazazi wao na hivyo kuwa na tabia ambazo sio nzuri kwa ukuaji wao. Tunajua kuwa watoto hujifunza kwa kuangalia maisha ya wazazi na jamii zao siku hata siku, hivyo upo uwezekano wa wao kuendeleza tabia hizo za kibaguzi katika familia zao na hivyo kujenga tabia za malezi hasi katika jamii. Vivyo hivyo uzoefu unaonyesha kuwa watoto wanapoanza kukua na kupata uwezo wa kupambanua mambo huwapuuza wazazi walokuwa wanaishi kwa ‘kuwaponda’ wazazi wenzao. Tena watoto watakuona ‘mnafiki na muongo’.

Ili kuondokana na tabia hizi kwenye malezi na familia kwa ujumla, wazazi hawana budi kuepuka malezi ya kibaguzi. Vyema kuthaminiana, kuheshimiana na kulea watoto kwa ushirikiano kama timu. Iwapo kuna migogoro baina ya wazazi ni vyema kutafuta njia zingine ‘kupambana’ na kulipana visasi na kamwe usijaribiwe kumtumia mtoto kulipiza visasi.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
 
Back
Top Bottom