Malezi: Umuhimu na mambo ya kuyafanya unapoandaa ratiba ya kila siku ya mtoto wako

OLS

JF-Expert Member
Oct 12, 2019
419
670
Na Justine P. Kakoko.

Ratiba ni dira inayotoa muongozo kwa mtu yeyote yule katika kuelekea ukamilishaji wa majukumu yake mbalimbali kwa ufanisi. Ili mtu aweze kukamilisha jambo lolote lile ni lazima awe na ratiba, yaani ajue wakati gani nitafanya nini na ni kwa muda gani.

Wazazi/walezi wengi mara nyingi sana huwa wanatamani kuona watoto wao wanakamilisha majukumu yao mbalimbali kwa wakati na ufanisi, lakini wasichojua ni kwamba, ili watoto wao waweze kukamilisha mambo hayo kwa namna wanavyotaka basi ni lazima watoto wao wawe na ratiba, lakini, mtoto hana uwezo wa kuandaa ratiba peke yake bila usaidizi wa mzazi/mlezi wake hivyo mzazi/mlezi ni lazima ashirikiane na mtoto wake katika kuandaa ratiba hiyo.

Nimekuwa nikiulizwa na wazazi/walezi wengi sana juu ya jinsi gani wawasaidie watoto wao kuandaa ratiba zao za kila siku na pia umuhimu wake ni upi haswa? Katika makala hii nitawaonyesha wazazi/walezi umuhimu na mambo ya kuyazingatia pindi waandaapo ratiba za kila siku za watoto wao.

Yafuatayo ni mambo ya muhimu ya kuyazingatia pindi unapomsaidia mtoto wako katika kuandaa ratiba yake ya kila siku.

i. Mtoto ashirikishwe mwanzo hadi mwisho wa kuandaa ratiba yake. Mtoto asipangiwe ratiba bali ushirikiane naye katika kuandaa ratiba hiyo husika. Hii itasaidia mtoto kujihisia anawajibu na pia mzazi/mlezi utapata kujua namna ambavyo muda wake upo na jinsi ya kuupangilia kuendana na vipaumbele vyake.

ii. Ratiba iwekwe wazi au kubandikwa sehemu ambayo kila mmoja ndani ya nyumba anaweza kuiona.
Hii itasaidia kumkumbusha mtoto juu ya ratiba yake kila mara anapoiona na pia, itawaepusha watu ndani ya familia kuingilia ratiba ya mtoto wako

iii. Ratiba iheshimiwe na kila mtu ndani ya familia. Kupanga ratiba bila kuheshimiwa ni kazi bure, ratiba iliyopangwa kwa ajili ya mtoto lazima iheshimiwe na wote, upande wa mtoto na upande wa wazazi/walezi. Muda wa kujisomea mtoto asitumwe dukani, muda wa mapumziko mtoto asiruhusiwe kwenda kucheza n.k ili ratiba iheshimiwe ni lazima mzazi/mlezi wa mtoto uwe msimamizi katika kulihakikisha jambo hilo.

iv. Mtoto asipoifuata ratiba aliyoshirikishwa kuiandaa zitafutwe njia za kumuwajibisha.
Mtoto asipotekeleza na kuifuata ratiba yake ni lazima awajibishwe ili kuifuata maana mafanikio yake yote hutegemea sana kwenye kupanga na kuheshimu ratiba yake.

v. Ratiba ni lazima izingatie magawanyo wa vipaumbele vyote vya mtoto
, yaani masomo (50%), majukumu ya nyumbani (20%), michezo (10%) na mapumziko (20%). Hii itaondosha ile hali ya ratiba ya mtoto kuegemea katika jambo moja au mawili tu. Mtafutie mtoto marafiki watakaoshirikiana katika kutekeleza majukumu yake yaliyoko kwenye ratiba hususani majukumu ya kielimu. Hii itampa mtoto wako hamasa ya kuzingatia zaidi ratiba yake kwani watoto hupenda na kufurahia zaidi kufanya majukumu yao wakiwa na wenzao.

vi. Mtoto afundishwe kuifuata ratiba kwa mapenzi yake mwenyewe bila kusukumwa.
Hili ni jambo muhimu sana. Mtoto asisukumwe kila muda katika kuifuata ratiba yake. Mzazi/mlezi ni lazima utumie mbinu mbalimbali katika kumfanya mtoto wako anafuata ratiba yake kwa mapenzi yake yeye mwenyewe.

vii. Ratiba isimzidie au kumuelemea mtoto. Ratiba ipangwe kuendana na umri na uwezo wa mtoto. Majukumu yasiwekwe mengi sana katika ratiba kiasi kwamba akashindwa kuyatekeleza kwa wakati na ufanisi.

viii. Ratiba iweke wazi inalenga kutimiza lengo gani kwa mtoto
. Ratiba isiyo na lengo mahususi ni ngumu sana kufuatwa hata kama kuna usimamizi mzuri kiasi gani. Mzazi/mlezi ni lazima uhakikishe ya kuwa kama lengo la kupanga ratiba na mtoto wako ni kuongeza ufaulu katika masomo yake basi hakikisha lengo hilo linakuwa wazi na kueleweka kwa mtoto wako.

Tumeangalia mambo ya kuyazingatia unapopanga ratiba ya kila siku na mtoto wako sasa tuangalie umuhimu wa kupanga ratiba:-

i. Ratiba huleta matumizi sahihi na mazuri ya muda kwa mtoto. Mtoto mwenye ratiba muda wake utatumiwa vizuri na kwa usahihi ukilinganisha na mtoto asiye na ratiba.

ii. Ratiba humjulisha mtoto nini anachotakiwa kufanya kwa kila wakati husika. Ratiba humpa dira mtoto wako ya afanye nini na kwa wakati gani hivyo ni ngumu sana majukumu yake kuingiliana. Muda wa kusoma mtoto atasoma tu, muda wa kucheza mtoto atacheza tu na muda wa shughuli za nyumbani mtoto atafanya shughuli za nyumbani tu.

iii. Ratiba huweza kupunguza uvivu wa mtoto katika kufanya majukumu yake. Mara nyingi uvivu hutokana na mtu kutojua anatakiwa kufanya nini kwa wakati gani hivyo kwa kupanga ratiba mtoto mzazi/mlezi utaondosha tabia hii ya uvivu kwa mtoto wako na kuongeza uzalishaji katika ufanyaji wa mambo yake.

iv. Ratiba huweza kupunguza migogoro isiyo ya lazima kati ya mzazi/mlezi na mtoto wake. Migogoro kati ya wazazi na watoto mara nyingi hutokana na mzazi/mlezi na mtoto wake kutojua mtoto anajukumu gani, katika wakati gani. Unakuta mtoto yupo kucheza mzazi/mlezi anataka awe ndani anasoma au mtoto anasoma mzazi/mlezi anataka awe jikoni kupika. Hivyo kwa kuwa na ratiba kutaondosha migongano isiyo ya lazima ya muda na majukumu kati ya mzazi/mlezi na mtoto.

v. Ratiba huweza kuongeza ufanisi/ufaulu katika elimu ya mtoto wako. Mtoto mwenye ratiba anayoizingatia na kuiheshimu daima maendeleo yake huwa ni mazuri katika kila anachokifanya kwa sababu ratiba umfanya siku isipite bila ya yeye kufanya kitu chochote kile hata kama ni kidogo, hali inayompelekea kila siku kupiga hatua kwenda mbele.

vi. Ratiba hutengeneza uwajibikaji na kujituma kwa mtoto katika kufanya majukumu yake. Mtoto mwenye ratiba kila siku hujituma ili kuhakikisha anakamilisha kufikia majukumu yaliyopo kwenye ratiba yake. Kujituma humfanya mtoto kuwa muwajibikaji.

Mzazi/mlezi jitahidi sana kumsaidia mtoto wako kuandaa ratiba ya kila siku ili kumuhakikishia mafanikio katika kila atakachokifanya.

1576733520518.png
 
1. Mzazi umtafutie mtoto marafiki katika kutimiza majukumu (ratiba) yake? Marafiki kutoka wapi?
2. Ratiba kwa context ya kibongo ni suala gumu ( itabaki nadharia) kama wewe ulivyosoma kitabuni. Eg. Mzazi anadamka mapema kwenda kazini na kurudi usiku nan atekeleze hayo? house maid?
 
Ukiwa serious unaweza tu, sijaona kitu kigumu! Hapo sio lazima umtafutie marafiki but ujue anacheza na akina nani nadhani ndio muhimu.
1. Mzazi umtafutie mtoto marafiki katika kutimiza majukumu (ratiba) yake? Marafiki kutoka wapi?
2. Ratiba kwa context ya kibongo ni suala gumu ( itabaki nadharia) kama wewe ulivyosoma kitabuni. Eg. Mzazi anadamka mapema kwenda kazini na kurudi usiku nan atekeleze hayo? house maid?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Hebu tusaidie utakavyoweza nasi tujifunze kwa kuandaa ratiba ya (m)wanao kila siku
Sidhani kama ni kuandaa ratiba kila siku, unless I got it wrong. Mimi kwangu wanaamka asubuhi, wako wawili, mmoja yuko form three sasa boarding kwa hio tuzungumzie mfano wa huyu ambaye bado Niko nae. Anaamka asubuhi maandalizi ya shule yanajulikana akirudi SAA tisa jioni anakula, anaoga, analala kidogo (sometimes kwa lazima), anaamka anafanya homework, akimaliza anaangalia katuni, anatakiwa kuandaa vyomba vya chakula mezani, kula then kuondoa vyombo. Kusali na kwenda kulala SAA tatu.

Weekend, jumamosi ni jumuiya, tukirudi anafagia uwanja, nimemtengea eneo LA kufagia at least ajizoeshe, anaoga, anakunywa chai anaendelea na utawala binafsi but kama kuna kazi nyingine atafanya pia. Jioni ataandaa nguo kwa akili ya ibada, Mama yake atazipiga pasi na sometimes kumchagulia nguo sahihi, tutakula na ratiba itajirudia kama kawaida, kesho ibadani tukirudi ratiba kama ya Jana!

At least tunaweza kufanya hicho kidogo kwa kiwango hicho! Mkubwa akiwa likizo kama SAA hizi ni kazi tu hakuna kwenda tuition! Anatakiwa afanye na hizi kazi nyingine
 
Back
Top Bottom