Malezi - TAFITI: Watoto wanaoangalia sana TV wanaweza 'Kuharibu Miundo ya Ubongo'

Sema Tanzania

JF-Expert Member
May 18, 2016
251
465
Kuangalia sana Televisheni kunaweza kubadilisha muundo wa ubongo wa mtoto na hivyo kumletea madhara, kulingana na utafiti mpya uliofanywa na wataamu toka Chuo Kikuu cha Tohoku kilichopo katika jiji la Sendai nchini Japan. Watafiti hawa waligundua kuwa kadiri mtoto anavyotumia muda mwingi zaidi kuangalia Televisheni ndivyo madhara ya mabadiliko kwenye ubongo wake yanavyozidi kuwa makubwa

Watafiti hawa toka Japan walifuatilia maisha ya watoto 276 wenye umri kati ya miaka mitano na 18, ambao huangalia Televisheni takribani masaa manne kwa siku, huku wastani wa jumla ya muda wanaotumia kwenye Televisheni kwa pamoja ukifikia hadi masaa mawili kila mmoja wao

Watafiti hao wanasema ukweli ni kwamba kuangalia Televisheni ni tofauti na kujifunza vyombo vya muziki, kusoma vitabu, n.k. kwani 'uzoefu' katika kuangalia Televisheni hakuongezi ujuzi kama ilivyo kwa vitabu n.k. bali hufinyanga miundo ya ubongo inayohusika na ufahamu. Kwa kutumia muda mwingi kwenye Televisheni sehemu ya ubongo inayohusika na uelewa haikui bali husinyaa kwa kukosa changamoto mpya kwani Televisheni hubakia kuwa ni jambo hilohilo na kuunyima ubongo kukua

Kwa kumalizia, watafiti hawa wasema kuangalia Televisheni huhusisha moja kwa moja na ukuaji na maendeleo ya sehemu ya ubongo wa mtoto inayohusika na ufahamu. Hivyo wanashauri kwamba wazazi wanapaswa kuwa waangalifu na kuzingatia athari hizi katika muda wanaotenga kwa ajili ya watoto wao kuangalia Televisheni.

Ingawa tafiti kama hizi haziwezi Kutoa majibu ya moja kwa moja juu ya madhara na athari ya Televisheni hapa kwetu hasa za kijamii, athari za kielimu na hata kidini, bado zina nafasi kutupa picha ya nini kinaendelea katika bongo za watoto wetu kwa kukaa kwenye Televisheni muda mrefu. Kikubwa tunachoona hapa ni kupangilia muda mtoto anaokaa kuangalia Televisheni kwa siku. Muda kati ya saa moja hadi saa moja na nusu kwa siku unatosha kabisa kumpa mtoto ‘elimu’ toka katika vipindi vya Televisheni kwa siku.

Mifano ipo ya watoto kushinda kutwa kwenye Televisheni hasa wakati wa likizo ama wakiwa wametoka shule kila siku! Hii ni hatari kwani watoto kama binadamu wengine wanahitaji kujifunza kuhusiana na binadamu wenzao kupitia michezo, kuwatembelea marafiki na ndugu na kujuliana hali. Vinginevyo tunaandaa taifa la watu wasioujua ‘utu’ wala kuuthamini kwani hawakuzwi kuishi na watu.

Upande mwingine wa muhimu ni swali kuwa huwa watoto wanaangalia nini katika Televisheni? Watoto katika umri mdogo sana wanaanza kuangalia mambo yasiyoendana na umri wao na yasiyo-maadili. Je unajua kwamba unaweza kudhibiti na kupangilia mtoto wako anachoangalia kila siku kwenye Televisheni? Ving'amuzi vingi sasa vinakuja na mifumo ya kukusaidia mzazi kupanga nini mwanao aangalie hata kama haupo nyumbani. Hivyo unawajibika kutenga muda kupangilia jambo hili kwani unaweza ukawa unampoteza mwanao bila wewe mwenyewe kujua kupitia vipindi potofu vinavyoonyeshwa kutwa katika televisheni wakati ukiwa kazini ama mihangaikoni.

Usiiache Televisheni ukufundishie mwanao maadili kwani tafiti zinaonyesha kwamba Televisheni ni mojawapo ya vitu vinavyochangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili katika jamii zetu za leo.

Makala haya yameandaliwa na vijana wataalamu wa makuzi toka asasi ya C-Sema inayotafiti na kujifunza namna bora za kukuza watoto Tanzania kupitia mifano na tabia bora za malezi toka kote Afrika na Duniani kwa ujumla. C-Sema inataka kuona Tanzania ambayo jamii nzima iko makini katika makuzi, malezi na maendeleo ya watoto wake. Inawezekana!

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
 
Mkuu unafeli sana vipindi vya tv vingi vinasema umri sahihi wa muangaliaji kabla hakijaanza kipindi pia kama wewe ni mzazi na tv anaangalia mwanao kwenye setting kuna sehemu ya parental guidness (PG) unaweza kufungia channel zenye maydhui mabaya kwa mwanao
 
Back
Top Bottom