Malezi: Nani anawajibika na jukumu la kujenga maadili ya watoto wetu?

Sema Tanzania

JF-Expert Member
May 18, 2016
251
465
Sisi wananchi tumekaa kimya tukiangalia watoto wetu wakifanyiwa vitendo vya kidhalimu na unyanyasaji mitaani na vijiji katika mamlaka zote za serikali za mitaa. Tumekaa tu na kukubali aina hizi za matukio kama vile ni mambo ya kawaida, wakati kwa kweli ni msiba wa kitaifa wa maadili.

Wapo wanaume na wanawake wachache walojitoa kukemea vitendo vya kidhalimu na unyanyasaji dhidi ya watoto. Ungana nasi kuwapa heko kwa jitihada zao watu hawa wema. Bila ujasiri wa watu kama wao, kweli nchi yetu ingekuwa katika hali mbaya zaidi. Katika makala haya tunataka kuibua mjadala juu ya nani anayepaswa kulaumiwa, kwa kuwa tuna ushahidi unaoonesha kwamba unyanyasaji wa watoto hutokea katika nyumba zetu, mahali pa ibada na katika shule zetu. Pia tunajua kwamba wahusika wakuu wa vitendo vya kidhalimu dhidi ya watoto ni wazazi, walimu, viongozi wa dini na watoto wanaowanyanyasa watoto wenzao.

Tumezoea kupokea barua toka kwa shule wanazosoma watoto wetu hasa wakati wanaporudi nyumbani kwa ajili ya mapumziko / likizo. Hapa chini tunakuwekea barua inayoonekana kuandikwa na uongozi wa shule kwenda kwa wazazi / walezi, tumeipata kupitia ukurasa wa Twitter wa ndugu Mmassy Jr. (II), ambapo inasema ifuatavyo.

‘Ndugu Mzazi,

Tungependa kuwakumbusha kuwa maneno yalojaa maadili kama salaam, tafadhali, samahani, pole na asante - yote watoto wanaanza kujifunzia nyumbani.

Pia ni nyumbani ambapo watoto hujifunza kuwa waaminifu, kutunza muda, kuwa na bidii, kuwa wenye kuwajali wenzao, na kuonyesha nidhamu na heshima kwa watu wazima pamoja na walimu.

Nyumbani pia ndipo wanajifunza kuwa wasafi, ndipo wanajifunza kutozungumza huku kinywa kikiwa kimejaa chakula, na ndipo wanapojifunza namna bora ya kutupa takataka.

Nyumbani ndipo wanapojifunza namna ya kupangilia mambo yao, kutunza mali zao vizuri, na nymbani ndipo wanapojifunza kwamba si sawa kugusa watoto wengine bila idhini yao.

Hapa shuleni, kwa upande mwingine, tunafundisha lugha, hisabati, historia, jiografia, fizikia, sayansi, na elimu namna hiyo. Sisi kazi yetu nyingine ni kuimarisha elimu ya maadili ambayo watoto hupata nyumbani kutoka kwa wazazi / walezi wao.’


Naam, tumeamua kukubaliana na barua ya mwalimu hapo juu, kwa sababu ameweka majukumu ya kufunda maadili kwa mtu sahihi, mzazi. Wewe mzazi ndiye kilelezo cha mwenendo wa maadili katika maisha ya watoto wako. Toka wakati wa kuzaliwa - watoto watahitaji mafunzo yako, watakapo pevuka watauhitaji muda wako katika mazungumzo juu ya mada ngumu kama vile elimu ya ngono na wakati wao nao wanaanza kuwa wazazi, watahitaji maelekezo yako juu ya kulea watoto wachanga. Yote haya ni mambo ambayo yanakuhusu takuhita mzazi / mlezi - si jamii, si walimu.

Tunapendekeza kuwa malezi ni kazi nzito inayokuja na majukumu ya kudumu kwa miaka iliyobaki ya maisha yako yote. Kwamba shughuli hii adhimu huanza mara tu unapoitwa mzazi. Hivyo hata kabla hujaanza kupanga kuwa na mtoto, fikiri kwa kina iwapo uko tayari kuitwa mama, kitwa baba. Kwamba je uko tayari kutegemewa? Je ukiitwa na majukumu ya malezi – utaitika?

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
 
Back
Top Bottom