Malezi ~ Changamoto wanazopitia akina mama waliotelekezwa

Sema Tanzania

Verified Member
May 18, 2016
247
500
Malezi ya mtoto huwa si kazi rahisi, ikiwa ni pamoja na kumuogesha, kumfulia, kumpa chakula na kuhakikisha afya nzuri na elimu bora ya mtoto. Hali hii ni ngumu zaidi kwa mzazi mmoja ambaye mzigo wa kifedha na malezi umo mikononi mwake.

Tamaduni zetu za kiafrika zinaasa malezi ya watoto kufanywa na wazazi wote wawili, mama na baba. Majira sasa yameanza kubadilika na leo si jambo la kushangaza kuona watoto wakilelewa na mzazi mmoja mara nyingi akina mama.

Katika makala haya tutaangazia baadhi ya changamoto za malezi wanazokutana nazo akina mama waliotelekezwa na wazazi wenzao na namna wanavyoweza kutumia vyombo vya serikali kutatua changamoto hizi. Takwimu toka kituo cha huduma ya simu kwa mtoto kupitia namba 116, (National Child Helpline) zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 25 ya kesi zote zinazoshughulikiwa – zinahusu utelekezaji wa jukumu la malezi ya watoto kwa akina mama na mara nyingi akina mama hawa ama bado ni mabinti wadogo au hawana kipato cha kuwawezesha kutimiza mahitaji ya malezi kwa watoto.

Changamoto hii hupelekea watoto wao kukosa baadhi ya huduma za msingi ikiwemo elimu bora, huduma bora za afya na hata lishe bora ya milo mitatu ilokamilika. Vyote hivi huathiri makuzi ya mtoto kimwili na kiakili. Vilevile mama naye kama binadamu huathirika na changamoto za kimazingira na msongo na ugumu wa maisha.

Hii huweza kupelekea hasira kali na kumkaripia hata kumchapa mwanae mara kwa mara. Hii pia huonyesha ni vipi mtoto anavyoweza kuathirika kwa kutokuwepo mzazi wa kiume. Inafika mahali mama hajui afanyeje wala kesho mtoto ale na avae nini

Huku jamii inayomzunguka ikimpa ‘jicho’ la kejeli kwa kulea/kuzaa mtoto nje ya ndoa. Mama anapozidiwa na msongo wa mawazo kutokana na hali kama hii anaweza kuwa mkali kupitiliza ama akawa hana ukaribu na mwanae. Changamoto nyingine ni watoto kukuzwa bila kujua wazazi na ndugu zao wa familia tandaa (upande wa baba mzazi) kutokana na wazazi wa kiume kutelekeza ujauzito, kutelekeza watoto na kukimbia majukumu yao ya kuwahudumia watoto au familia kwa ujumla kama wazazi.

Hali hii hupelekea akina mama waliotelekezwa kuwaficha watoto chimbuko lao bila kujua wanatenda kosa la jinai. Sheria ya Mtoto, 2009 inamtaka mlezi kumfahamisha mtoto wazazi wake wa kumzaa na ndugu zake wengine. Iwapo mzazi mwenza ametelekeza mtoto na kukataa kutoa huduma kwa mtoto ingawa uwezo anao.

Hii ni kosa la jinai na ukikumbana nalo nenda katika ofisi za ustawi wa jamii, dawati la jinsia na watoto kituo cha polisi, toa taarifa katika ofisi ya serikali za mitaa/kijiji ama tupigie simu namba 116 bila malipo maalumu kwa huduma za mtoto. Sheria ya mtoto inazipa mamlaka ya ‘ulezi’ wa watoto wote hamlashauri zote za wilaya, miji na majiji. Hii ina maana kwamba huduma za afya, elimu na ustawi wa watoto kwa ujumla wake ziko chini ya usimamizi wa halmashauri hizi.

Hii ni pamoja na kuwachukulia hatua stahiki wazazi wasiotaka kutimiza majukumu yao ya kutoa huduma za msingi kwa watoto ikiwemo chakula, malazi na mavazi. Wito wetu ni kwa wazazi wa kiume kote Tanzania, thamini mchango wa akina mama popote ulipo. Hasa pale ambapo unamuona mama akiwa katika hali ya uhitaji na wewe unao uwezo wa kumsaidia

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom