Malecela naye aitega Serikali Bungeni

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,820
287,889
Malecela naye aitega bungeni

Mwandishi Wetu Julai 16, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

Kutaibua ya Meremeta, Kiwira, Bulyanhulu, Buzwagi

WAZIRI Mkuu mstaafu, Mbunge wa Mtera (CCM), John Malecela, ameipa mtihani mkubwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kwa kufanikisha kujadiliwa bungeni kwa Taarifa iliyoibua utata mwingi, ya Kamati ya Rais ya kuishauri Serikali juu ya usimamizi wa sekta ya madini.

Wabunge mbalimbali waliozungumza na Raia Mwema, mjini Dodoma wiki hii, wamesema kwamba ingawa Serikali iliridhia mapendekezo yote ya taarifa ya kamati hiyo, iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Jaji Mark Bomani, bado ilikuwa haijajiandaa kukabiliana hadharani na changamoto nyingi zilizomo ndani ya taarifa hiyo.

Sababu wanazotoa wabunge hao ni kwamba kuna mambo mengi yenye utata ambayo Serikali haitapenda kuyajadili hadharani kwa sasa na mengine inajaribu kuyaficha ambayo yamo ndani ye taarifa hiyo iliyowasilishwa bungeni rasmi wiki iliyopita.

Malecela, wiki iliyopita, aliwasilisha hoja ya kutaka taarifa hiyo ijadiliwe bungeni kutokana na kukosekana muda wa kutosha kuijadili wakati wa kujadili bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, iliyowasilishwa na Waziri wake, William Ngeleja, sambamba na taarifa ya Kamati ya Madini.

"Ningeomba kuomba mwongozo wako chini ya ibara namba 68(7) (ya Kanuni za Bunge). Jana tuligawiwa Ripoti ya Bomani, mtu ambaye alijulishwa hapa kwamba ni mtu mashuhuri, na wote waliokuwa katika tume ile ni watu mashuhuri, na ripoti hii ina mambo mengi sana ya muhimu na mimi ninafikiri labda ndiyo pengine wakati muafaka wa nchi yetu kupata sera mpya ya madini.

"Kwa hiyo kutokana na kuomba huo Mwongozo, ningekwenda kwenye ibara namba 37(6), kuomba kwamba ripoti hiyo ili tuifanyie haki ipewe muda wake iwe debated, ili tuweze kutoa maoni yetu na kutoa mapendekezo yetu. Kwa hiyo naomba kutoa hoja chini ya kifungu 37(6) baada ya kupata muongozo wako," alisema Malecela akishangiliwa na wabunge; wa CCM na wa Upinzani.

Akijibu hoja ya Malecela, Naibu Spika, Anne Makinda, alisema suala la madini lina mvuto katika jamii na lina maslahi ya kitaifa, lakini lilishindwa kujadiliwa kutokana na kuwasilishwa bila kuwa katika orodha ya siku ilipowasilishwa na kukubaliana na maelezo ya kupatiwa muda wa kujadiliwa.

"Kwa sababu imeungwa mkono na watu wengi sana humu ndani, kwa hiyo tunafikiri tutapata muda wakati mzuri wa kuweza kuijadili. Kwa sababu kama hivi sasa tuna mambo mengi katika Wizara hii, kwa hiyo tunaweza kuzamia kwenye hii, haiwezekani kwa mujibu wa utaratibu wetu. Kwa hiyo tutaangalia muda muafaka wa kuweza kujadili hoja hiyo," alisema Anne Makinda.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Bomani, anaunga mkono hoja ya Malecela akisema kwamba hatua hiyo ya Mzee Malecela inaashiria mapinduzi makubwa katika demokrasia ndani ya Bunge, kwa kuwa ni historia kwa ripoti hiyo kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni kwa uwazi.

Kamati hiyo ya Jaji Bomani imegusa waziwazi mambo kadhaa yaliyoibua utata nchini kama miradi ya Meremeta, Kiwira na utata mkubwa katika kuuzwa kwa wawekezaji kwa migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi pamoja na mgodi wa almasi wa Mwadui.

Kamati hiyo pia ilitoa mapendekezo kadhaa kuhusiana na udhaifu mkubwa ndani ya Serikali katika kukusanya kodi kutoka katika makampuni makubwa ya madini yaliyowekeza nchini, huku wananchi katika maeneo yenye migodi hiyo wakiwa hawanufaiki kwa kiwango kinachostahili.

Katika maelezo na mapendekezo yake, kamati ya Bomani imezungumzia pia mradi wa dhahabu unaoihusisha kampuni tata ya Meremeta Limited, kampuni ambayo Serikali imekuwa ikiweweseka katika kuizungumzia. Mwishoni mwa mwezi uliopita Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliliambia Bunge kwamba suala la Meremeta linagusa siri za ulinzi na usalama.

Ndani ya taarifa hiyo inayorejewa sasa kama 'Ripoti ya Bomani' kuna mapendekezo kadhaa yanayotaja Meremeta yakitaka kampuni hiyo ifanyiwe uchunguzi wa kina.

Katika mapendekezo ya kamati hiyo Serikali imeshauriwa kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na kampuni ya Meremeta na Tangold ambazo zimetumika kuchota zaidi ya Sh bilioni 158 kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), pesa ambazo ni nyingi zaidi kuliko zilizochotwa EPA.

Kampuni hizo zimekuwa zikiendeshwa na watendaji wa zamani wa Serikali baadhi yao wakiwa bado wako madarakani na wengine kustaafu, kufukuzwa ama kujizulu akiwamo Andrew Chenge na aliyekua Gavana wa BoT, Dk. Daudi Ballali.

"Serikali ifanye uchunguzi wa kina juu ya uanzishwaji wa kampuni za Meremeta na Tangold, umiliki wa Serikali katika kampuni hizo na uhalali wa malipo ya dola za Marekani milioni 132 yaliyofanywa na BoT kwa benki ya Nedbank ya Afrika Kusini," inaeleza sehemu ya ripoti hiyo ambayo Raia Mwema imefanikiwa kuiona.

Mbali ya Chenge na Ballali ambao wakati Meremeta ikianzishwa walikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Gavana wa BoT, wamo pia Katibu Mkuu Hazina, Gray Mgonja, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Patrick Rutabanzibwa (sasa Wazara ya Maji) na Vincent Mrisho ambaye alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na JKT (sasa Ofisi ya Waziri Mkuu.)

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, taarifa za kampuni hizo zilizokuwa zikiendesha mgodi wa dhahabu wa Buhemba mkoani Mara hazikuwa za kuridhisha na hivyo kuifanya kamati itoe mapendekezo ya kutaka uchunguzi wa kina kufanyika.

Ndani ya ripoti hiyo, inaelezwa pia kwamba Mgodi wa Buhemba ulielezwa na Serikali kwamba ulikuwa ukimilikiwa na kampuni ya Meremeta ambayo inatajwa kuwa ya ubia kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya TRIENNEX Proprietary (Pty) Limited ya Afrika Kusini, inayodaiwa kuwa na hisa za asilimia hamsini.

Hata hivyo, sasa inafahamika kwamba mgodi wa Buhemba umesitisha shughuli zake kwa sababu zinazotatanisha ikiwamo kuwa na deni kubwa la kiasi cha dola za Marekani milioni 10 ilizokopa kutoka benki ya Nedbank kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli zake.

"Kwa taarifa ya Gavana, BoT iliilipa Nedbank jumla ya dola za Marekani milioni 132 sawa na shilingi bilioni 158 kuhusiana na kampuni ya Meremeta. Aidha kuna taarifa nyingine kuwa deni hilo lilikuwa la Dola za Marekani milioni 104.

"Kamati haikupata maelezo ya kina na ya kuridhisha kuhusiana na uanzishwaji, umiliki na ufilisi wa kampuni ya Meremeta na hatimaye uanzishwaji wa kampuni ya Tangold zilizosajiliwa nje ya nchi," inaeleza sehemu ya mapendekezo hayo ya Kamati.

Kampuni ya Meremeta ilianzishwa na kuchukua mikopo kutoka taasisi za fedha za kimataifa kwa baraka za serikali ya awamu ya tatu na kuna maoni kwamba mjadala utakaokuja unaweza kugusa ushiriki wa uongozi wa awamu hiyo katika mradi wa Meremeta.

Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), Ludovick Utouh, imetamka bayana kwamba haijawahi kukagua hesabu za Meremeta Gold, na kampuni hiyo tata inaelekea haimo katika orodha ya makampuni yanayomilikiwa na Serikali ama kwamba Serikali ina hisa katika kampuni hiyo.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, CAG, Utouh, alisema wazi kwamba Meremeta haimo katika orodha ya makampuni na mashirika ya umma ambayo yamewahi kukaguliwa na ofisi yake, na hivyo kuibua utata mwingine hasa baada ya kuwahi kutolewa kauli kwamba ni mali ya umma.

Hata hivyo, kuna taarifa kwamba Serikali kupitia Msajili wa Hazina ilitoa cheti ya kuithibitisha Meremeta kuwa kampuni ya umma tokea Oktoba Mosi, 1997, baada ya kudaiwa kwamba Serikali ilikuwa na hisa katika kampuni hiyo zilizokuwa zikishikiliwa na watendaji serikalini.

Kamati ya Bomani pia imebaini utata na udhaifu katika uhamishwaji wa asilimia 10 ya hisa za Serikali katika mgodi mkubwa wa dhahabu wa Bulyanhulu mwaka 1999, na kisha kuiacha kampuni ya Sutton Resources ikiuza hisa zake katika mgodi huo kwa dola za Marekani milioni 348 kwa kampuni ya Barrick Gold.

Mjadala mwingine unatarajiwa kuibuka kuhusiana na mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, ambao umekuwa ukihusishwa na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.

Kamati imependekeza Serikali ichukue hatua za haraka kuchunguza uhalali wa taratibu zilizotumika za kuubinafsisha mgodi huo uliomilikishwa kampuni ya Tanpower Resources Limited. Ndani ya kampuni hiyo yumo pia aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona.

Kamati ya Bomani imebaini pia kuwa kumekuwa na udhaifu katika udhibiti wa Serikali katika mgodi wa almasi wa Mwadui (WDL), udhaifu unaotokana na uhamishwaji wa asilimia 25 ya hisa za Serikali katika mgodi huo mwaka 1994 baada ya Serikali kuwa na umiliki wa nusu ya hisa katika kampuni hiyo tokea mwaka 1958. Hisa hizo zilihamishiwa kwa kampuni ya Wilcroft, ambayo ni kampuni tanzu ya kampuni kubwa duniani ya De Beers.

Kamati katika taarifa yake, inaeleza kushitushwa na mpango wa Serikali wa kutaka kuachia asilimia 25 ya hisa zilizosalia katika WDL kutokana na thamani ya mgodi huo kuendelea kupanda, tofauti na taarifa za Wilcroft. Taarifa ya kamati ilibaini kwamba Serikali ilitaka kubaki na asilimia tano tu ya hisa katika mgodi huo mkongwe nchini.

Katika eneo la kodi, kamati ya Bomani iliibua mapungufu mengi katika mfumo wa kodi, ikieleza kwamba kampuni nyingi za madini zimekuwa hazilipi kodi stahili chini ya sheria mbalimbali kutokana na kuwapo kwa vivutio vingi kupita kiasi na mapungufu kadhaa katika sheria za kodi katika eneo linalohusu sekta ya madini.

Akizungumzia kwa undani mjadala wa Ripoti ya Bomani, Zitto anasema: "Kwa kweli ni hatua muhimu sana katika mjadala mzima wa ulinzi wa rasilimali za nchi. Uundwaji wa Kamati hii Novemba 2007 ulileta maneno mengi sana na hata baadhi ya wananchi kuamini kuwa Kamati hii imeundwa ili kuzima joto la wanananchi kuhoji kuhusu usimamizi wa rasilimali za Tanzania, lakini sasa ukweli unabainika."

Zitto ambaye hakuwapo bungeni wakati wa kuwasilishwa kwa ripoti hiyo, alisema zimekuwapo kamati nyingi ambazo ziliundwa kushughulikia suala la madini lakini zilikuwa siri kubwa ya Serikali na matokeo yake pamekuwa hakuna ufuatiliaji wa karibu wa mapendekezo yanayotolewa na kamati hizo.

Amezitaja kamati hizo kuwa ni pamoja na Kamati ya kushughulikia matatizo ya uchimbaji Tanzanite Mererani iliyoongozwa na Jenerali (mstaafu) Robert Mboma, Kamati ya Kudurusu Sera ya Madini iliyoongozwa na Dk. Jonas Kipokola na Kamati ya Kupitia Mikataba ya Madini iliyoongozwa na Mbunge wa Nyamagana (CCM) Lawrance Masha, ambaye sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani.

Hata hivyo, Zitto ameliambia Raia Mwema kwamba, changamoto kubwa itakuwa ni utekelezaji na ufuatiliaji wa mapendekezo hayo, jambo ambalo alisisitiza kwamba ni jukumu la Watanzania wote kuisaidia Serikali na wadau wengine wa sekta ya madini.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo walikuwa ni pamoja na wabunge Dk. Harison Mwakyembe (Kyela-CCM), Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige (Msalala – CCM) na John Cheyo (Bariadi Mashariki-UDP).

Wajumbe wengine ni, Peter Machunde wa Soko la Hisa la Dar na David Tarimo mshauri wa mambo ya Kodi katika kampuni ya PricewaterhouseCooper na Maria Kejo ambaye ni Mkurugenzi wa Kitendo cha Madai na Sheria za Kimataifa wa Wizara ya Katiba na Sheria.

Wengine ni Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Makazi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Edward Kihundwa, Kamishina wa Sera katika Wizara ya Fedha, Mugisha Kamugisha na Salome Makange Mwanasheria katika Wizara ya Nishati na Madini.
 
Pinda alisema meremeta inahusu usalama wa nchi. Hivi bunge linaweza kumuadhibu ikithibitika kuwa alischosema ni uongo ?
 
Uongo? Ni muongo ndio hata kama bunge halikusema mimi mchukia fisadi nasema ni MUONGO. Kama si muogo mbona hiyo Meremeta yake iko katika ripoti ile? mbona waliruhusu tume iichunguze? ni muongo yule na mshirika wa mafisadi.
 
Duuu?? yaani hadi serikali ya zecomedy naionea huruma sasa, lakini waliyataka wenyewe kujipendekeza kuyatetea mafisadi, laiti wangejua wamwache kila mtu aubebe msalaba wake mwenyewe!

Hakika mwaka huu hapatoshi DOM
 
nimeipenda statement ya hapo juu... serikali ya kizecomedy.... ukitaka kuhakikisha angalia watiifu wabunge wanapomtwanga pinda maswali direct na namna anavyoyajibu.... yaani wanajiburudisha na majibu yake kwani hakuna masuala ya kimsingi zaidi ya burdani pale..... hii ni comment inayojirudiarudia bungeni kila baada ya kujibu maswali ya alhamisi...

serikali ya kizecomedy walah
 
Kumbukeni vita na De Beers sio ndogo.
Na hivyo Mzee Malecella anastahili five.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom