BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,009
Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk Makongoro Mahanga.
Na Na Leon Bahati
NAIBU Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk Makongoro Mahanga amesema makada wa CCM wanaodai kupambana na ufisadi wanapaswa kudhibitiwa ili wasikivuruge chama kwa kuwa mafisadi ndani ya chama hicho hawazidi wanne.
Akizungumza na gazeti hili jana Mahanga ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, alisema makada hao wasipodhibitiwa watakivuruga chama na kukifanya kipoteze viti vingi vya ubunge kwa wapinzani katika uchaguzi mkuu mwakani, kwa kudhaniwa kimejaa mafisadi.
"Hawa wanaoitwa mafisadi wako wangapi? Mbona hawatajwi?" alihoji Dk Mahanga akibainisha kuwa tathmini yake inaonyesha kuwa kelele zote za ufisadi zinawalenga watu ambao hawazidi wanne ndani ya chama hicho, na kwamba miongoni mwao, tayari wameanza kushughulikiwa.
Alipotakiwa kuwataja hao mafisadi wanne, Mahanga alisema hiyo ni tathmini yake na hakuna haja ya kutaja majina yao kwa vile wanafahamika.
Kwa kauli hiyo, Dk Mahanga anakuwa mtu wa pili ndani ya CCM kupingana na Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, John Malecela ambaye Ijumaa iliyopita alitoa kauli kutaka mafisadi wadhibitiwe kwa nguvu zote, ili wasikiweke chama katika wakati mgumu kwenye uchaguzi huo. Tayari kauli hiyo imepingwa na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.
Lakini jana Dk Mahanga alisema ajenda ya ufisadi imekuwa ikitumiwa vibaya na watu ambao wanafikiri wanajijengea mazingira mazuri kisiasa ili washinde ubunge mwakani, lakini hawafikirii kwamba njia wanayoitumia inalenga kuiharibia CCM.
"Kuna watu ndani ya chama wamedhamiria kuiangusha CCM huku wakijifanya wanapambana na mafisadi ndani ya chama," alisema Dk Mahanga jana katika mahojiano na Mwananchi Jumapili na kuongeza:
"Kama wapinzani wangesimama majukwaani wakisema ndani ya CCM kuna mafisadi, hakuna mtu ambaye angeshangaa kwa sababu malengo yao ya kisiasa ni kukichafua chama tawala ili kianguke na wao wachukue nafasi hiyo," alisema Dk Mahanga ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga.
"Suala hilo linapozungumzwa hadharani na wanachama wa CCM ni hatari. Hapa wanakichafua chama na ndio wanaosaidia vyama (vya siasa) vya upinzani," alisema.
Naibu waziri alishauri: "Kama kuna tatizo, lipelekwe kwenye vikao na siyo kwenda kupiga kelele kwenye majukwaa na kukichafua chama machoni pa wananchi."
Alipoulizwa kama haoni kulizungumzia suala hilo hadharani kutasaidia kuzuia ufisadi nchini, alisema: "Namna suala hilo linavyozungumzwa sasa, inaonyesha kana kwamba kuna kundi kubwa la wanaCCM wanaojihusisha na ufisadi, lakini ukweli ni kwamba watuhumiwa wa ufisadi, hawazidi wanne."
Kuhusu kuwepo kwa mtandao wa watu ndani ya CCM waliopanga mbinu za makusudi za kuwaangusha wabunge waliopo mstari wa mbele kwenye mapambano dhidi ya ufisadi, Mahanga alisema:
"Huo ni woga tu. Hakuna kitu kama hicho. Naunga mkono maelezo yaliyotolewa na Katibu wangu Mkuu (Yusuf Makamba) kupitia gezeti lenu (Mwananchi) toleo la leo jana akisema hayo ni mambo ya kufikirika," alisema Dk Mahanga.
Alisema kuwa woga huo unatokana na baadhi ya wabunge kuwa na wasiwasi kwamba, wanachama wengine ndani ya CCM wanaweza kuchukua nafasi zao, hivyo kutumia suala la ufisadi kama njia ya kupambana nao.
Alitoa mfano kuwa katika jimbo lake tayari wamejitokeza wana-CCM saba wanaotaka kumrithi, lakini hapigi kelele kwa sababu anajua ni haki yao ya kikatiba na hana wasiwasi na yupo tayari kupambana nao kupitia michakato ya uteuzi ndani ya CCM.
"Hili liko wazi. Hata wengi wao mwaka 2005 kwenye majimbo yao walikuwepo wabunge ambao waliwaondoa na kuchukua nafasi zao," alisema Dk Mahanga.
Alisema hata kama watu wachache wanaodaiwa kuwa ni mafisadi wakifukuzwa ndani ya CCM bado suala la wabunge kupata upinzani ndani ya chama litakuwa pale pale.
Aliwataka wana-CCM wenye nyadhifa mbalimbali kufahamu kuwa wapo wanachama wengi waliokuwa wanazitamani na hata sasa wanazitaka nafasi wanazozishikilia na wakati huo huo wapo wapya wanaojitokeza kuziwania.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Zamani, Cleopa Msuya amesema kwamba msimamo wa serikali kuhusu mafisadi unajulikana na tayari vyombo vyake husika vimeanza kuwashughulikia, hivyo akataka visiingiliwe,viachwe vifanye kazi yake.
"Mimi sina cha kusema juu ya hilo tatizo, tunaandika sana, hebu tuviachie vyombo vya utekelezaji vifanye kazi yake," alisema Msuya ambaye alikuwa waziri mkuu katika utawala wa serikali ya awamu ya kwanza na ya pili.
Fisadi Mkapa, Papa fisadi RA, fisadi Mramba, Fisadi Chenge, Fisadi Karamagi, Fisadi Makamba, Fisadi Lowassa, Fisadi Msabaha and the list goes on. Aaache usanii huyu wa kuturushia Watanzania changa la macho.