Makasisi, wanasiasa na ufundi wa kubishana kimaadili: Msiwapotoshe wengine mwaka 2022 na kuendelea

Mama Amon

JF-Expert Member
Mar 30, 2018
2,021
2,477
1640738108522.png


Mtandao wa intanet ni wa hivi punde na katika mambo mengi ni njia ya mawasiliano yenye nguvu zaidi kuliko watangulizi wake, yaani, telegrafu, simu, redio na televisheni.

Kwa watu wengi vyombo hivi vya habari vimeondoa hatua kwa hatua urefu wa muda na umbali wa kijiografia kama vizuizi vya mawasiliano vilivyokuwepo kwenye karne moja na nusu iliyopita.

Kwa hivyo, mtandao wa inatenti una mchango makubwa kwa watu binafsi, mataifa na ulimwengu.

Ni chombo chenye nguvu cha elimu na uboreshaji wa kitamaduni, kwa shughuli za kibiashara, ushiriki wa kisiasa, kwa mazungumzo ya kitamaduni na maelewano.

Kwa hivyo, intaneti imegeuza maandishi tuli kuwa majadiliano hai. Miaka arobaini iliyopita, waandishi waliandika kwa wasomaji na wasomaji kusoma baadaye. Leo, mtandao unawaruhusu wasomaji kujibu kwa haraka na maoni yao kurushwa kupitia majukwa, facebook, twitter, whatsapp na blogu.

Lakini bado intaneti ni kama sarafu yenye upande mwingine. Kama vile inavyoweza kutumiwa kwa manufaa ya watu na jamii, inaweza pia kutumiwa kunyonya, kukandamiza, kutawala, na kupotosha umma kupitia mazoea mapotovu ya kutunga hoja zenye sura ya udanganyifu.

Kwa hakika, wengi wanaoitikia jambo fulani mtandaoni huenda wakakubaliana nalo au wasikubaliane nalo. Kutokuelewana huwa kunawapa watu motisha zaidi kuliko kukubaliana, kwani mnapokubaliana kunakuwa na machache ya kusema.

Kutokubaliani pengine kunamaanisha kwamba unaingia katika eneo ambalo mwandishi wa kwanza huenda hakuwahi kuligusa hapo awali.

Matokeo yake, kuna mengi zaidi ya kutokubaliana yanayoendelea kwenye mtandao.

Lakini, ikiwa tutakataa hoja ya mtu baki, tunapaswa kuwa waangalifu kufanya mabishano kimaadili.

Inamaanisha nini kubishana kimaadili? Hapa, mtu anakuwa anakubaliana na ushauri wa Mtakatifu Paulo kwamba: "Huwezi kufanya mabaya kama njia ya kuleta matokeo mema" (Warumi 3:8)

Katika muktadha wa sasa, Mt, Paul anaonekana kusema: "Usijenge hoja potofu kama njia ya kushawishi upande mwingine kukubaliana nawe kuhusu lengo lako hilo kwa sababu hiyo?"

Kwa maana ikiwa utafanya hivi, utakuwa umejisajili kwenye mafundisho mabaya ya Machiavelism, yasemayoi kwamba, "malengo mema yanaweza kuhalalisha mbinu yoyote, nzuri au mbaya."

Njia nzuri tu na malengo mazuri pekee ndio huleta tabia njema ya kibinadamu. Mchanganyiko wa malengo mazuri na njia mbaya, au kinyume chake, huzaa maovu ya kibinadamu. Hii ndiyo sababu fundisho la Niccollo Machiavelli si sahihi.

Kwa maoni haya, katika mjadala wowote, wasomaji wengi wanyoofu wanaweza kutofautisha kati ya utukutu wa kuitana majina, kwa upande mmoja, na kukanusha hoja unyofu wa kimaadili.

Lakini, ngazi ya hatua ya utukutu wa kuitana majina na ngazi ya kukanusha hoja unyofu wa kimaadili, kuna hatua kadhaa katikati zijazohitaji kutajwa kwa majina halisi ili kuonyesha wazi namna ya kutambua hoja mbaya na kupuuza nia ovu za baadhi ya waandishi.

Kwa maana fulani, kuna piramidi ya mabishano iliyo na Hierarkia ya Ukosoaji yenye ngazi kadhaa, kila ngazi ya juu ikiwa bora kuliko ngazi iliyo chini yake:

Mabishano Ngazi ya 1 (MN1): Kubatiza majina mabaya.

Hii ndiyo aina ya chini kabisa ya mabishano, na pengine inayojulikana zaidi, yaani kushambulia mtoa hoja kwa kumbatiza jina baya.

Badala ya kujibu hoja, mtoa hoja anapewa jina ambalo halina uhusiano na swali lililopo mezani.

Ni sawa na maoni kama haya: "Wewe ni mgonjwa," "Wewe ni mwizi," "Wewe ni maskini," nk.

Ikiwa kuna kitu kibaya na hoja ya mzungumzaji, unapaswa kusema ni nini; na kama hakuna, haileti tofauti kwamba yeye ni mgonjwa, mwizi, au maskini.

Mabishano Ngazi ya 2 (MN2): Kushambulia Haiba ya Mleta Hoja.

Shambulio la kibinafsi sio dhaifu kama kumbatiza majina mabaya mtu. Linaweza kubeba uzito fulani, kwani huwa linahusiana na kesi iliyopo mezani.

Kwa mfano, ikiwa mbunge alisema kwamba "mishahara ya wabunge inapaswa kuongezwa," mtu anaweza kujibu hivi kwa kushambulia: "Bila shaka angesema hivyo, kwa kuwa yeye ni mbunge."

Hii haiwezi kupinga hoja ya mwandishi, lakini bado ni aina dhaifu sana ya kutokubaliana. Iwapo kuna kasoro kwenye hoja ya mbunge, unatakiwa useme ni nini; na kama hakuna, haileti tofauti kuwa yeye ni mbunge.

Mfano mwingine, ni kusema kwamba wazungumzaji hawana mamlaka wala weledi wa kuzungumza kuhusu mada. Hii ni kanusho isiyo na maana, kwa sababu mawazo mazuri mara nyingi hutoka kwa watu wa nje ya eneo la ubobezi.

Swali hapa ni kama waandishi wako sahihi au la. Ikiwa ukosefu wao wa mamlaka ulisababisha wafanye makosa, onyesha hivyo. Na ikiwa haikutokea, sio shida.

Mabishano Ngazi ya 3 (MN3): Kujibu toni au staili.

Ngazi ya mabishano inayofuata tunaanza kuona majibu ya kukosoa uandishi, badala ya kumshambulia mwandishi. Njia ya chini kabisa hapa ni kutokubaliana na toni au staili ya mwandishi. Kwa mfano:

Mwandishi anatupilia mbali hoja kwa njia inayomwonyesha kuwa mgonjwa kiakili."

Ingawa ni bora kuliko kushambulia mwandishi, hii bado ni aina dhaifu ya kubishana. Ni muhimu zaidi kama mwandishi si sahihi au sahihi kuliko toni na staili yake. Hasa toni na staili ni vigumu sana kuvihukumu.

Kwa hivyo ikiwa jambo baya zaidi unaweza kusema kuhusu kitu ni kukosoa toni au staili yake, hausemi mengi. Je, mwandishi amekurupuka, lakini ni sawa? Ni bora hivyo kuliko kufanya makosa makubwa ya kimaudhui. Na ikiwa mwandishi sio sahihi mahali fulani, unapaswa kusema wapi.

Mabishano Ngazi ya 4 (MN4): Kufanya ukinzani bila ushahidi.

Katika hatua hii hatimaye tunapata majibu ya kile kilichosemwa, badala ya kujadili toni, staili au wasifu wa mleta hoja.

Njia ya chini kabisa ya kujibu hoja ni kueleza tu kesi pinzani, bila ushahidi wowote wa kuunga mkono. Hii mara nyingi hujumuishwa na mbinu ya MN2, kama katika:

"Mwandishi anatupilia mbali hoja kwa njia inayomwonyesha kuwa mgonjwa kiakili. Lakini hoja hii inahusu nadharia halali ya kisayansi."

Ukinzani wakati mwingine unaweza kuwa na uzito fulani. Wakati mwingine kuona tu kesi pinzani ikitajwa wazi inatosha kuona kuwa ni sawa. Lakini kawaida ushahidi utasaidia.

Mabishano Ngazi ya 5 (MN5): Kuleta hoja mpya na kuchakachua hoja iliyoletwa

Tabia ya Kuleta hoja mpya "huvuruga" hadhira kutoka kwa suala halisi ili kuzingatia kitu kingine ambapo mjibu hoja anahisi vizuri na kujiamini. Hubadilisha mada ili kuwavuruga hadhira.

Kwa upande mwingine, kuchakachua hoja iliyoletwa hufanyika kwa kuirekebisha hoja ili kusudia msimamo wa mpinzani. mchakachuaji huweka lengo rahisi na la uwongo kwa ajili ya kuangusha hija iliyoletwa.

Kwa hivyo, tabia ya Kuleta hoja mpya ni kwa ajili ya "kuvuruga", wakati tabia ya kuchakachua hoja iliyoletwa ni kwa ajili ya "kupotosha".

Kwa hivyo, kwa mfano, ikiwa uko kwenye mjadala na unasema kwamba "Ninaamini mwanamke hupata hukumu nyepesi kuliko wanaume kwa uhalifu sawa kwa sababu majaji wengi ni wanaume".

Jibu linalotokana na tabia ya Kuleta hoja mpya lingekuwa: "Machafuko ndiyo njia ya kwenda, hakuna sheria, na tunajitawala, hatuhitaji polisi, sheria, au majaji!"

Ingawa jibu hili liko karibu na mada, haliangazii sababu ya wanawake kupata hukumu nyepesi au kukubaliana/kupinga madai kwamba wanawake wanapata hukumu nyepesi. Ni kauli isiyo na uhusiano wowote na mjadala.

Na jibu linalotokana na tabia ya kuchakachua hoja iliyoletwa litakuwa: "Hiyo ni kwa sababu unadhani kuwa wanawake wote ni vyombo vya anasa."

Ingawa mada inarejelea sababu moja inayowezekana ya hukumu nyepesi ambayo inaweza kutumika kwa majaji kuwaona wanawake kama vyombo vya anasa, bado inawakilisha dai hilo vibaya.

Kwa mfano, dai la asili lingeeleza ikiwa majaji wanaume wanaona wanawake kuwa dhaifu, au wasio na nia ya uhalifu, au sababu nyingine yoyote yenye kueleza kwa nini hakimu wa kiume anaweza kumhukumu mshtakiwa wa kike kwa kiwango cha chini kwa uhalifu sawa na ambazo sio lazima zimmfanye hakimu kumwangalia wanawake kama vyombo vya anasa.

Mabishano Ngazi ya 6 (MN6):Kusanifu hoja kinzani

Katika ngazi ya 6 tunafikia aina ya kwanza ya mabishano yanayoshawishi inayoitwa counter argument. Ngazi za awali zinaweza kupuuzwa kuwa hazithibitishi chochote.

Kusanifu hoja kinzani kunaweza kuthibitisha kitu. Shida ni kwamba, ni ngumu kusema ni nini haswa. Kusanifu hoja kinzani ni kufanya ukinzani pamoja na ushahidi wake.

Kama Kusanifu hoja kinzani kunapolenga hoja ya asili, kunaweza kusadikisha. Lakini kwa bahati mbaya, ni kawaida kwa hoja kinzani kulenga kitu tofauti kidogo.

Mara nyingi zaidi, watu wawili wanaobishana kwa shauku juu ya jambo fulani kwa kweli wanabishana juu ya vitu viwili tofauti.

Kunaweza kuwepo na sababu halali ya kubishana juu ya kitu tofauti kidogo na kile ambacho mwandishi asilia alisema. Lakini, hilo linakuwa halali pale unapoonyesha kuwa mwandishi asilia alikosa kubainisha kiini cha jambo hilo. Hata hivyo, unapofanya hivyo, unapaswa kusema wazi kuwa unafanya hivyo.

Mabishano Ngazi ya 7 (MN7): Kubomoa hoja.

Njia ya kushawishi zaidi ya kutokubaliana ni kubomoa hoja. Pia ni nadra zaidi, kwa sababu hii ni kazi ngumu. Hakika, mtiririko wa mabishano huunda muundo wa piramidi, lenye mabishano adilifu zaidi juu na mabidhano ya kihuni chini, kama picha hapo juu inavyoonyesha.

Ili kubomoa hoja ya mtu unapaswa kumnukuu. Lazima utafute kifungu chochote ambacho hukubaliani nacho na ambacho unahisi kimekosewa, na kisha ueleze kwa nini kimekosewa. Ikiwa huwezi kupata nukuu halisi ya kutokubaliana nayo, unaweza kuwa unajadili hoja hewa.

Ingawa kukanusha kwa ujumla kunahusisha kunukuu, kunukuu haimaanishi kukanusha.

Mabishano Ngazi ya 8 (MN8):Kukanusha Hoja ya Msingi

Nguvu ya kukanusha inategemea kile unachokanusha. Njia yenye nguvu zaidi ya kubishana ni kukanusha hoja kuu ya mtu.

Hata hadi ngazi ya MN6 bado wakati mwingine tunaona ukosefu wa uadilifu wa kimakusudi, kama vile mtu anapochagua pointi ndogo.

Kwa mfano, kusahihisha sarufi ya mtu, au kunukuu makosa madogo katika majina au nambari. Isipokuwa kwa hakika kama hoja inayobishaniwa inategemea mambo hayo, lengo pekee la kuyarekebisha mambo haya ni kumvunjia heshima mpinzani.

Kwa ujumla, kubomoa hoja ya mtu kunahitaji kukanusha mawazo yake makuu, au angalau wazo mojawapo. Na hiyo inamaanisha kuwa mtu lazima ajitoe kwa uwazi kwa ajili ya kuonyesha jambo kuu ni lipi. Kwa hivyo kukanusha kwa ufanisi kunaweza kuonekana kama:

  • Hoja kuu ya mwandishi inaonekana kuwa x. Kama anavyosema: <quotation>.
  • Lakini hoja hii si sahihi kwa sababu zifuatazo: <facts>

Nukuu unayosema kuwa imekosewa sio lazima kuwa taarifa halisi ya wazo kuu la mwandishi. Inatosha kukanusha kitu ambacho inategemea.

Hitimisho

Ili kuwa mdadisi mzuri lazima mtu aepuke makosa ya kimantiki. Kukumbatia makosa ya kimantiki kimakusudi ni kukosa maadili.

Kwa mfano, kutumia lugha ya kuudhi, matusi na kejeli (lugha ya affinabus) ni kukosa uadilifu. Ni sawa na kumwabudu Mungu wa Niccollo Machiavelli na kumsaliti Mungu wa Kweli wa Isaka, Yakobo, Musa na Yesu Kristo.

Ni kujisajili kwenye kambi ya shetani, na hivyo kupoteza uhalali wa kushika mamlaka ya kisiasa kama sio kupiteza uhalali wa kushika mamlaka ya kidini.
 
Back
Top Bottom