Makaratasi ya Uchochezi dhidi ya Serikali - Sehemu ya pili na ya mwisho

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,912
30,253
MAKARATASI YA "UCHOCHEZI" DHIDI YA SERIKALI SEHEMU YA PILI NA YA MWISHO

Wakati Ally Sykes yuko ndani nyumbani kwake Mtaa wa Kipata anachapa mikaratasi yake ya "kuchochea," wananchi kujiunga na TAA mtego ulikuwa ushategwa unangojewa kufyatuka.

Inawezekana kuwa kulikuwa na makachero nje ya nyumba yake pale Mtaa wa Kipata wakiiangalia nyumba na labda walipoona mlango wa mbele unafungwa pamoja na madirisha kwao ikawa ni ishara kuwa mtambo ushawashwa ndani unachapa mikaratasi ya uchochezi.

Bila shaka walisubiri kwa muda kidogo ndipo wakagonga mlango.

Bi. Zainab ananihadithia anasema, "Baba yako akaniambia nichungulie mlangoni kuangalia nani anagonga.

Nikarudi ndani mbio kumweleza kuwa kuna askari mlangoni."

Ally Sykes pale pale kwa haraka alikusanya makaratasi yote akaenda kuyatia chooni baada ya kuyachana.

Siku zile vyoo vilikuwa vya shimo.

Haraka akachukua ili mashine ya kuchapia ikarushwa ua wa pili wa nyumba inayopakana na nyumba yao.

Nyumba ya pili ikaiokota mashine ikatupwa ua wa nyumba inayofuatia mkono kwa mkono mashine ikawa inayoyoma.

Muda mfupi mashine imepotezwa sehemu ya tukio.

Huku askari kwa vishindo wanapiga kelele, "Fungua mlango au tutavunja."

Bi. Zainab kwa ndani anapiga kelele, "Subirini tunafungua."

Mlango ulipofunguliwa askari wamejitoma ndani kwa fujo mbele katangulia Amiri Kweyamba.

Amri Kweyamba akawa uso kwa uso na Ally Sykes.

Amri Kweyamba katoa "search warranty," askari wanapekua nyumba nzima, vyumba vyote hadi chini ya kitanda kila kitu kinapinduliwa.

Hawakukuta kitu lakini ni wazi taarifa zao hazikuwa za kubahatisha hata kidogo zilikuwa na ithibati tosha.

Ndani ya TAA muajiriwa wao mmoja kama Katibu, Alexander Thobias alikuwa mtu wao akiwapa taarifa zote na pia alikuwapo mtu wao mwingine, Ali Mwinyi Tambwe, Katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika akiripoti moja kwa moja kwa Gavana Twining.

Sijaweza hadi leo kuhakikisha bila shaka yoyote ni nani alipekeka taarifa za Ally Sykes kwa Waingereza kwani ni wazi makachero walikuwa wengi mbali na Alexander Thobias na Ali Mwinyi Tambe wakiwachimba viongozi wa TAA.

Alexander Thobias aligundulikana kwa sababu alichukua mafaili ya TAA akawapa Special Branch kwa kitita kikubwa cha fedha.

Huyu Alexander Thobias aliajiriwa na TAA mwaka wa 1950 pale New Street wakati TAA ilipokuwa sasa inaanza kuelekeza nguvu zake UNO ikawa ofisi inahitaji mtu wa kuwa ofisini muda wote kushughulika na kazi za kila siku.

Katika mkutano wa kuasisi chama cha TANU mwaka wa1954 agenda ya kwanza ilikuwa kufukuzwa kazi Alexander Thobias.

Alexander Thobias ndiye aliyekuwa akiandika barua kwa Chief Secretary kuwaombea ruhusa ya kusafiri wakati Ally Sykes na Denis Phombeah walipoalikwa na Kenneth Kaunda Katibu wa African National Congress (ANC)Northern Rhodesia, kuhudhuria mkutano wa vyama vya siasa vinavyopigania uhuru wa nchi zao Kusini ya Jangwa la Sahara.

Ally Sykes na Denis Phombeah wakakamatwa Salsbury uwanja wa ndege wakiwa "transit," kuelekea Lusaka.

Huu ni mkasa mwengine tutautafutia siku yake kuueleza In Shaa Allah.

Yawezekana taarifa zote hizi za safari ya wazalendo hawa na mawasiliano yao na Kaunda yalifika Special Branch kutokea kwa Alexander Thobias.

Turejee kwa Ally Sykes na Amri Kweyamba.

Amri Kweyamba hakujua kuwa Ally Sykes alikuwa mwanajeshi na kapigana Burma kwa hiyo anajua mbinu za vita kuwa unaposhambulia adui unaacha nyuma yako njia ya kutorokea kujinusuru na adui pale adui atakapokuzidi nguvu.

Amri Kweyamba alitoka nyumbani kwa Ally Sykes mikono mitupu na kichwa ameinamisha.

Dar es Salaam nzima ikavuma mambo yaliyotokea siku ile kwa Ally Sykes kuvamiwa nyumbani kwake.

Siku zote Ally Sykes akimlaumu Nyerere kwa kumuacha Amri Kweyamba na makachero wenzake kazini kuitumikia Tanganyika huru katika nafasi zao zile zile.

1642303743630.png

Ally Sykes na mkewe Bi. Zainab wakati wa ujana wao.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom