View attachment 3601438
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Dk Emmanuel Nchimbi anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Siku ya Mazingira Duniani (WED) 2026 akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassani, ambapo kitaifa yanafanyika leo Juni 5, 2026 jijini Dodoma katika Viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre (JKCC) jijini Dodoma.
Akizungumza Juni 4, 2026 baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku hiyo, jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, alitoa wito kwa sekta zote nchini kuimarisha juhudi za utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 yanafikiwa kwa ufanisi.
Alisema kuwa utunzaji wa mazingira ni ajenda ya kitaifa inayohitaji ushiriki wa kila sekta ya uchumi na si jukumu la taasisi au wizara moja pekee, akisisitiza kuwa maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira salama na yanayohifadhiwa ipasavyo.
Kwa mujibu wa Waziri Masauni, sekta mbalimbali ikiwemo mawasiliano, usafiri, kilimo, mifugo na uvuvi zinapaswa kuzingatia kanuni na miongozo ya uhifadhi wa mazingira katika utekelezaji wa shughuli zake za kila siku ili kupunguza athari zinazoweza kuhatarisha ustawi wa mazingira.
Alieleza kuwa Dira ya Taifa ya mwaka 2050 imeweka msisitizo mkubwa katika usimamizi wa mazingira na kuongeza uwezo wa taifa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo ushiriki wa sekta zote ni jambo lisiloepukika.
View attachment 3601440
“Mazingira ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2050, lazima kila sekta ihakikishe inachangia katika uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira,” alisema Masauni.
Aidha, Waziri Masauni alitoa wito kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kitakachofanyika kesho Juni 5, 2026, katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Alisema maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kuelimishana kuhusu changamoto za mazingira pamoja na kujadili mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumzia namna ya kukabiliana na changamoto za mazingira nchini, Waziri huyo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi mbalimbali na wadau wa maendeleo ili kupata suluhisho la kudumu la changamoto zinazolikabili taifa katika sekta ya mazingira.
Alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea ubunifu, uwekezaji na utekelezaji wa miradi inayolenga kulinda mazingira na kuongeza uwezo wa jamii kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa maonesho hayo wameeleza kuwa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yamekuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha jamii kuhusu wajibu wao katika kulinda mazingira, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza agenda ya maendeleo endelevu nchini.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu yamekusanya taasisi za umma na binafsi, wadau wa mazingira pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, yakilenga kuhimiza matumizi endelevu ya rasilimali na kuimarisha mapambano dhidi ya changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.