Makamu wa Rais awataka Watendaji wa Mahakama kujipima mafanikio yao kwa kutenda haki kwa makundi yote

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,499
9,279
Viongozi na Watendaji wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) na watendaji wa Mahakama nchini wametakiwa kupima mafanikio ya utendaji wao kwa kutumia nafasi walizonazo kuhakikisha uamuzi wanaotoa unatafsiri haki sawa kwa makundi yote kwenye jamii.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alitoa angalizo hilo jana jijini Mwanza kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Mwigulu Nchemba, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Majaji wanawake Tanzania ( TAWJA).

“Mafanikio yenu yasipimwe kwenye hukumu na maamuzi mangapi yaliyoandikwa na kutolewa, idadi ya vikao vya kesi ulivyohudhuria au idadi ya mizozo iliyomalizika, bali ni kwa jinsi gani nafasi yako katika Mahakama na maamuzi yametafasiriwa katika kuiwezesha jamii kupata haki sawa,” alisema Samia.

Aliwashauri wanachama wa TAWJA kutimiza majukumu yao bila kujali vikwazo wanavyokutana navyo ili kumfanya mwanamke aonekane shupavu, mpambanaji anayekataa kuonekana muathirika wa vitendo vya ukatili.

Aliwataka wanachama na vongozi hao kutumia muda na nafasi walizonazo kushughulikia vitendo vya ukatili vinavyowakumba wanawake akisisitiza kuwa kwa mujibu wa historia mwanamke ana mchango mkubwa katika jamii kuhakikisha kuna utulivu na amani.

Akitoa mfano, alisema kwa mujibu wa tafiti kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2015-16 asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa miaka 12 hadi 15 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia na bado kuna mitazamo hasi katika jamii kuwa wanawake ni viumbe dhaifu.

Alisema amefurahishwa na kutiwa moyo kwa kazi zinazofanywa na TAWJA katika kupigania haki sawa kwa wote na kwa wakati pamoja na kusimamia utawala wa sheria, kwa kufanya kazi bila kuchoka kwa kipindi cha miaka 20 mfululizo tangu kuanzishwa kwa chama hicho.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma aliwataka wanachama wa TAWJA kutunza takwimu sahihi za utendaji kazi wao hasa wanaposhughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake.

Aliwapongeza kwa kujitolea kuandika kitabu kinachoeleza mashauri na namna ya kukabiliana na masuala ya ukatili wa kijinsia kwenye jamii.

Mwakilishi wa Wanawake kutoka Umoja wa Mataifa, Julia Broussard aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi na jinsi ambavyo imekuwa ikishughulikia changamoto za kijinsia zinazowakabili nchini.
 
Back
Top Bottom