Makamu wa Rais ataka wanaodhalilisha watoto waadhibiwe

Kurzweil

JF-Expert Member
May 25, 2011
6,622
8,399
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kuwafichua watu wanaonyanyasa na kudhalilisha watoto kijinsia ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Mama Samia ameyasema hayo leo wakati akihitimisha kampeni ya kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kinyerezi, Dar es Salaam.

Vile vile amesema, wanaofanya vitendo vya udhalilishaji wa watoto wapo miongoni mwa jamii hivyo ni jukumu la Serikali, walezi na wazazi kuwafichua watenda maovu hao ili kukomesha vitendo hivyo na kuwafanya watoto waishi kwa amani nchini.

“Katika kukabiliana na hali hiyo, nimeviagiza vyombo vya dola kutofumbia macho vitendo hivyo pindi wanapopata taarifa za matukio ya udhalilishaji wa watoto na badala yake wachukue hatua za haraka za kuwakamata na kuwachukulia hatua stahiki watu wanaofanya vitendo hivyo vibaya,” amesema Samia.

Mama Samia ameongeza kuwa kufanya hivyo kutawasaidia watoto kuwa salama katika mazingira ya nyumbani hata wakiwa mashuleni kwani watu wabaya wanaofanya vitendo hivyo watawajibishwa kulingana na matendo maovu wanayofanya watoto.

Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kote nchini kuwapa taarifa walimu wao na polisi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu na umuhimu wa mtoto duniani. Maadhimisho haya hufanyika Juni 16 kila mwaka tangu ilipotangazwa rasmi na Jumuiya ya Umoja wa Afrika mnamo mwaka 1991.
 
Back
Top Bottom