Katibu mkuu wa CCM bwana Yusuph Makamba amedai Mjadala wa EPA ufungwe kwa kuwa watuhumiwa wote wameshafikishwa mahakamani. Je ni kweli watuhumiwa wa EPA wote wameisha fikishwa mahakamani?
Adai suala hilo sasa limekwisha
Na Mussa Juma, Karatu
WAKATI Serikali ikisema inaendelea na mchakato wa kuwashughulikia watuhumiwa waliosalia wa ufisadi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ili waweze kufikishwa mahakamani, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba, ameomba mjadala wa tuhuma za ufisadi ufungwe kwa madai tayari watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani.
Kauli ya Makamba kwamba watuhumiwa wote wa EPA wameishashitakiwa, hivi karibuni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliwaambia wahariri wa vyombo vya habarinchini kuwa bado serikali inashughulikia tuhuma hizo na kwamba mengi zaidi juu ya watuhumiwa wa EPA na Richmond yatakuwa hadharani hivi karibuni.
Pia Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea, aliahidi kuwa majina zaidi ya 'sangara' wa ufisadi yatafahamika kabla ya mwisho wa mwaka huu ikimaanisha kuwa mjadala wa EPA kuendelea.
"Tunamwogopa nani sisi? Hakuna tunayemwogopa, maji yanachemka. Nakuthibitishia kama Mkurugenzi wa Takukuru kuwa tuna uchungu na mali ya nchi hii. Kuanzia mwezi huu (Novemba) angalieni, mtaona matendo kwa mafisadi," alinukuliwa Hosea.
Hata hivyo watuhumiwa waliofikishwa mahakami ni miongoni mwa walihohusika na ufisadi wa Sh Sh90.3 bilioni za EPA zilizohakikiwa, bila kuwahisisha waliorudisha fedha hizo ambao Mwendeshs Mashitaka wa Serikali, Eliezeri Feleshi alisema wanaweza pia kufikishwa mahakamani.
Mamoja na hayo bado kuna watuhumiwa wa Sh42.6 bilioni za EPA ambazo zinaendelea kuhakikiwa ambaowatajulikana pia wanatakiwa kuchukuliwahatua za kisheria.
Akizungumza na wananchi wilaya ya Karatu na Ngorongoro juzi, Makamba alisema anashangaa kuona bado kuna viongozi wa upinzani wanashabikia ajenda hizo za EPA na ufisadi wakati wakijua suala hilo limekwisha.
Makamba ambaye yupo katika ziara ya kuiimarisha CCM mkoani Arusha, alisema kuna viongozi wa upinzani wamekuwa wakipita mikoani na kuendelea kulizungumza suala la EPA na ufisadi, hoja ambayo sasa imeisha.
Ndugu zangu mjadala wa EPA na ufisadi umekwisha, Rais Kikwete tayari amechukua hatua watuhumiwa wapo mahakamani, sasa hili jambo kila siku kuendelea kulizungumza ni ajabu sana, alisema Makamba.
Alisema viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika operesheni Sangara yao na kila kukicha wamekuwa wakizungumzia EPA na ufisadi ambao umeshashughulikiwa. Umefika muda watafute hoja nyingine.
Mimi najua operation hiyo ni nguvu ya soda na itakuwa operesheni dagaa siku si nyingi kila siku EPA si imekwisha hiyo hoja, alisema Makamba.
Hata hivyo, alieleza kuwa CCM inajipanga kuyatwaa majimbo ya Karatu na Tarime katika uchaguzi mkuu ujao ili kuonyesha kuwa CCM bado ni chama imara.
Leo nimefurahi sana kwa mapokezi yenu hapa Karatu na nina imani mmeanza kuonesha kuwa lazima tulichukuwe ili jimbo, alisema Makamba.
Hata hivyo, alihimiza umoja na mshikamano ndani ya viongozi wa CCM nchini ili kuhakikisha wanashinda uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na hatimaye Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Leo Makamba anatarajia kuendelea na mikutano ya hadhara wilayani Ngorongoro kabla ya kuondoka kesho kutwa kwenda mkoani Kilimanjaro.
Hivi sasa watuhumiwa wote wa mabilioni ya fedha EPA walioshtakiwa wameshaachiwa huru kwa dhamana.
Ufisadi ambao umebainika katika hesabu za BoT za mwaka 2005/06, unahusu Sh90.3 bilioni ambazo ziliibwa na makampuni 13 kwa kutumia nyaraka za kughushi.
Pia unahusu Sh42.6 bilioni zilizolipwa kwa makampuni tisa, katika mazingira yenye utata huku taarifa nyingine za wizi huo zikiwa nje ya nchi, hali iliyomfanya Rais kuongeza muda wa uchunguzi kutoka Agosti hadi leo Oktoba 31.
Source: Mwananchi