Makamba kuendelea kuula CCM

jamadari

JF-Expert Member
Feb 13, 2010
295
92
makamba%202.jpg


CCM imesema haina mpango wa kufanya mabadiliko yoyote ya uongozi hadi wakati wa uchaguzi mkuu wa chama hicho uliopangwa kufanyika mwaka kesho, uamuzi ambao unamfanya katibu mkuu wa sasa, Yusuf Makamba utakapofika kuwa na uhakika wa kumalizia kipindi chake. Baada ya tofauti kubwa zilizojitokeza kwenye kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, kupoteza viti vingi vya ubunge na ushindi wa mgombea urais wa chama hicho kupungua kwa takriban asilimia 20, ilibashiriwa kuwa CCM ingefanya mabadiliko makubwa, ikiwa ni pamoja na kumuondoa Makamba ambaye amekuwa akilaumiwa kwa kushindwa kumudu nafasi yake hasa wakati wa migogoro.

CCM pia ilikuwa imeitisha kikao chake cha kamati kuu Desemba mosi jijini Dar es salaam ambacho kilibashiriwa na wengi kuwa kingefanya mabadiliko hayo, lakini ikasemekana kuwa pande mbili zilianza kupingana kuhusu uamuzi wa kumng'oa Makamba. Kikao hicho sasa kimeahirishwa. “Kwa katiba ya chama chetu, viongozi wanaongoza kwa kipindi cha miaka mitano... kwa sasa hakuna mpango wowote wa kumbadilisha katibu mkuu; narudia tena hakuna mpango wowote wa kumbadilisha katibu mkuu,” alisema makamu mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa. “Kwa viongozi wote wa CCM uchaguzi wetu utafanyika mwaka 2012, wakati huo viongozi wote tuliochaguliwa mwaka 2007 muda wetu utakuwa umekwisha.

Kuna magazeti, lakini siyo Mwananchi; weka kwenye mabano hiyo, kazi yake ni kuandika habari za uongo, uzushi na uzandiki. "Andika maneno hayo kama nilivyo yataja halafu ishia hapohapo tena uiweke hiyo headline.” Habari ambazo Mwananchi ilizipata zinasema kuwa kikao hicho cha kamati kuu kiliahirishwa kutokana na pande mbili kutofautiana katika suala hilo la kumuondoa Makamba ili kuimarisha chama.

Habari hizo zilisema kuwa CCM ilikuwa inakusudia kufanya mabadiliko makubwa katika safu zake za uongozi baada ya kufanya vibaya kwenye uchaguzi mkuu ambao ulianza kwa wanachama kutofautiana kwenye kura za maoni na baadaye halmashauri kuu kupitisha majina ya watu ambao walishindwa na kuendelea kwa makundi yaliyoibuka wakati wa kura za maoni ambayo pia yalichangia kuanguka kwa CCM kwenye ubunge, hasa Tanzania Bara.
Vyombo vya habari viliripoti mapema wiki hii kuwa waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Makazi, John Chiligati hakurejeshwa kwenye uwaziri ikiwa ni mkakati wa kumuandaa kumbadili Makamba katika nafasi ya ukatibu mkuu. Chiligati amekuwa ni katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, kazi ambayo wachambuzi wanadai aliifanya vizuri.

Habari zaidi zinadai kwamba kundi ambalo lisingependa Makamba ang’oke ndilo lililosababisha kuahirishwa kwa kikao hicho cha kamati kuu ya CCM, uamuzi uliotafsiriwa kuwa ni ushindi kwa kundi hilo katika harakati zake za maandalizi kwa ajili ya kumuwezesha mtu wao kuingia Ikulu mwaka 2015. Hata hivyo, habari zaidi zinasema kuwa pamoja na kuahirishwa kwa kikao hicho, suala la Makamba litaibuka wakati CCM itakapokutana kujadili majina ya wagombea umeya wa maeneo mbalimbali kutokana na upande mmoja kutoridhishwa na uamuzi wa kutomuondoa kada huyo.

Lakini Msekwa aliiambia Mwananchi kuwa kuahirishwa kwa kikao cha kamati kuu kunatokana na kutokamilika kwa ajenda ya uteuzi wa mameya ambayo alisema ilikuwa ajenda kuu. Kwa mujibu wa Msekwa, mkutano huo ulikuwa na ajenda moja tu ya watu wanaogombea nafasi za umeya kupitia chama hicho. Spika huyo wa zamani wa Bunge alifafanua kuwa kwa sababu majina hayo yalikuwa hayajawa tayari, mkutano huo uliahirishwa mpaka utakapoitishwa tena. “Siwezi kukwambia ni lini tutafanya tena huo mkutano; tarehe tunaijua wenyewe, lakini hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kuuahirisha,” alisema Msekwa.

Kikwete alikabidhiwa uenyekiti wa CCM Juni 25, 2006, ikiwa ni miezi michache baada ya kuchaguliwa kuiongoza nchi na baadaye alipendekeza sekretarieti yake, akimteua Makamba kuwa katibu mkuu kushika nafasi ya Phillip Mangula. Katika sekretarieti hiyo, nafasi ya naibu katibu mkuu wa Bara ilikwenda kwa Jaka Mwambi wakati ya Zanzibar ilichukuliwa na Salehe Ramadhan Ferouz. Nafasi ya katibu wa uchumi na fedha ilikwenda kwa Amos Makala ambaye alichukua nafasi ya Rostam Aziz na nafasi ya katibu wa organaizesheni ilichukuliwa na Kidawa Hamid.
Wengine waliochakuliwa katika mkutano huo walikuwa ni Aggrey Mwanri aliyeteuliwa kuwa katibu wa itikadi na uenezi, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na John Chiligati. Nafasi ya katibu wa siasa na uhusiano wa kimataifa ilichukuliwa na Dk Asha Rose Migiro ambaye kwa sasa ni naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN). Naye Msekwa ambaye atamaliza muda wake kipindi hicho alishika nafasi ya umakamu mwenyekiti wa chama hicho akirithi mikoba ya John Malecela

Chanzo: Gazeti la Mwananchi
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom