- Ashangazwa na kauli yake dhidi ya CCM
- Si maneno aliyoyatazamia yatoke kwake
Na Mwandishi Wetu
Septemba 15, 2006
KATIBU Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, amesema kadri anavyomfahamu Paul Sozigwa haiwezekani maneno yaliyoandikwa katika gazeti la Rai wiki hii awe aliyasema na inawezekana alinukuliwa vibaya.
Sozigwa alinukuliwa na gazeti hilo la kila wiki lililotoka juzi akisema CCM imepoteza uwezo wake wa kutoa maamuzi kutokana na idadi kubwa ya wala rushwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi.
Makamba alisema Sozigwa ni kada wa CCM ambaye amekuwa kiongozi kwa muda mrefu na anaijua CCM kuwa ni imara kiitikadi, kimaadili na kioganaizesheni, na kwamba kutokana na hazina kubwa ya viongozi wake wenye hekima na busara, haijashindwa kufanyia uamuzi jambo lolote.
Alisema ana hakika Sozigwa, kupitia uzoefu wake alipokuwa mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, anayajua maamuzi mazito yaliyokwishashughulikiwa na CCM juu ya mstakabali wa nchi.
"Yeye mwenyewe amekuwa kiongozi kwa muda mrefu na anajua uwezo wa CCM katika kushughulikia mambo mbali mbali. Siamini kuwa maneno hayo kweli aliyasema Mzee Sozigwa. Bila shaka amenukuliwa vibaya," alisema Makamba.
Alisema Sozigwa kabla ya kustaafu utumishi katika CCM hivi karibuni ndiye alikuwa mkuu wa Kitengo cha Usalama na Maadili katika Chama na anafahamu vikao vya Chama vinavyosimamia masuala ya kimadili bila kuyumba.
Alisema Sozigwa anawajua kwa majina baadhi ya viongozi waliochukuliwa hatua kwa kukiuka maadili ya Chama, akieleza kuwa wapo waliopewa onyo, karipio na wengine kuachishwa uanachama.
Makamba alisema CCM katika kuthibitisha kuwa inachukia rushwa wapo wanachama ambao haikuwateua kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM licha ya kushinda kura za maoni, ilipofahamika kuwa ushindi wao uligubikwa na wingu la rushwa.
"Mzee Sozigwa akiwa mkuu wa Kitengo cha Usalama na Maadili hakuna hata siku moja alipeleka hoja juu ya wana-CCM fulani kukiuka maadili ya chama kisha vikao vya Chama vikaipuuza," alisema Makamba.
Katibu Mkuu wa CCM alisema kuwepo watu wachache wanaokiuka maadili ya Chama si kigezo cha kujenga hoja kuwa CCM imepoteza uwezo wa kufanya maamuzi kwani ushahidi unaonyesha kuwa watu wa namna hiyo wamekuwa wakidhibitiwa na vikao vya Chama kila wanapobainika.
Makamba ameonya wana-CCM kujiepusha na kauli juu ya mambo ambayo hawajayafanyia utafiti wa kutosha ili kutowakwaza wanachama wenzao na Watanzania kwa ujumla, ambao kimsingi wanaamini CCM ndiyo kimbilio la wanyonge.