Makalla; achana na siasa za kina Kingunge

Asha Abdala

JF-Expert Member
Mar 21, 2007
1,130
44
Na Irene Mark

KAZI ya mbwa wa polisi, ni kukamata mhalifu pindi anapotakiwa kufanya hivyo na anayemuongoza.

Ni wazi kuwa, mbwa wa polisi hutunzwa kwa ajili ya kazi maalum ambayo ni kusaidia polisi wakati wa upekuzi na kukamata mhalifu.

Katika makala hii, nimetumia mfano wa mbwa wa polisi ili kuwasilisha ujumbe wangu, kwa njia rahisi zaidi kwa yeyote atakayeisoma.

Hapa nitazungumzia kauli za ajabu zilizotolewa hivi karibuni na Amos Makalla, ambaye ni mtunza fedha wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), wakati wa mahojiano yake katika luninga ya taifa (TvT).

Mahojiano hayo, yenye lengo la kufahamu mustakabali wa vijana katika siasa na uzalendo wao, yalimhusisha pia Mkurugenzi wa Vijana Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika.

Kila mmoja kwa wakati wake alizungumza alivyofahamu kuhusu uzalendo wa vijana na mustakabali wa siasa za nchi kwa watu wa rika lao.

Nimeanza kwa mfano wa mbwa wa polisi nikasema tena kauli zilizonistaajabisha kutoka kwa Makalla. Sipendi kunukuliwa vibaya, hivyo naweka msisitizo hapa kwamba nimetumia mfano huo, kurahisisha uelewa kwa msomaji wa makala hii.

Makalla, alitumia vibaya nukuu za Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere. Alifika mbali zaidi kwa kuingiza suala la ukabila ambalo laiti muda ungekuwapo, akaendelea kulijadili, basi angeamsha hisia za ubaguzi.

Kwanza, alinukuu kauli ya Mwalimu kuwa bila CCM madhubuti, nchi itayumba. Ni kweli, tena ilimpasa Baba wa Taifa kusema hivyo kwa sababu wakati huo chama alichokiongoza kilikuwa madarakani.

Napenda kuamini kuwa kauli hiyo ingeenda kwa chama chochote cha siasa kilichoshika dola au hata jeshi, kwamba bila jeshi madhubuti nchi itayumba. Mwalimu, aliwataka viongozi walioshika nchi kupitia CCM kuwa makini na kiutendaji ndani na nje ya chama chao.

Hapo, watafiti wa mambo wanamshangaa Makalla kwa kushindwa kusoma alama za nyakati na kujikuta akiushangaza umma.

Pili, msomi huyo na mshika mikoba ya fedha za chama tawala, alizidi kunishangaza alipozungumzia ukabila ndani ya Chadema.

Bila soni, alidiriki kusema asilimia kubwa ya viongozi wa chama hicho ni wenyeji kutoka mkoa mmoja. Namnukuu: "Hawa wenzetu wa upande wa pili, kwa mfano ukiangalia Chadema, viongozi wake karibu wote wametoka mkoa mmoja."
Napenda kumkumbusha msomi huyo ambaye pia ni mtaalam wa propaganda ndani ya UVCCM, kauli ya Mwalimu Nyerere kuwa, dhambi ya ubaguzi ni kama kula nyama ya mtu, ukianza huwezi kuacha.

Binafsi si msemaji wala mfuasi wa chama chochote cha siasa nchini, isipokuwa uzalendo unanisukuma kutumia kalamu yangu kuitahadharisha jamii kuhusu propaganda hizi ambazo mwisho wake ni chuki ya ukabila.

Kwa ninavyofahamu, ndani ya Chadema, Mwenyekiti wake wa taifa Freeman Mbowe ni Mchaga, Katibu Mkuu wake, Dk. Wilibrod Slaa (Mmbulu), Naibu Katibu Mkuu Bara, Kabwe Zitto (Muha) na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Bara, Dk. Amani Walid Kabourou (Mmanyema). Hata hivyo, Kabourou kwa sasa yuko CCM na nafasi hiyo bado iko wazi.

Mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei ni Mchaga na Mwenyekiti aliyechukua nafasi ya Mtei baada ya kustaafu, Bob Makani ni Msukuma. Orodha ya viongozi na makabila yao ni ndefu kiasi cha kuhitaji ukurasa mzima kuorodhesha.

Narejea kwenye hoja yangu, swali la kujiuliza, kwani Wachaga hawana haki kuwa sehemu ya viongozi katika taifa au chama? Makalla, usipokuwa makini utaligawa taifa hili kwa ukabila.

Hata katika CCM na serikali yake, nashangazwa na kauli za Makalla, kwa kushindwa kufikiria idadi kubwa ya mawaziri, manaibu na wabunge wa kuteuliwa kuwa wengi ni Wachaga au wenye asili ya Mkoa wa Kilimanjaro kuliko wengine. Si hapo tu nenda Hazina ambako kulishawahi kuwa na malalamiko ya kuwapo wafanyakazi wengi kutoka Mkoa wa Kilimanjaro, nenda TRA na sehemu nyingine.

Mimi si Mchaga, lakini lazima tuwe wakweli kwamba kinachowafanya Wachaga kuwapo sehemu nyingi serikalini na katika sekta zingine nyeti ni elimu, na Makala anapaswa kutambua kuwa yapo makabila yaliyoelimika zaidi kuliko mengine na yanashika sehemu nyeti serikalini na hata katika sekta binafsi.

Kama vile haitoshi, mwanaCCM huyo mwadilifu anadiriki kusema amani iliyopo inatokana na uongozi mzuri wa chama chake.

Si kweli, katika hili napingana na Makalla kwa sababu msingi wa amani na utulivu uliimarishwa na Baba wa Taifa, majeshi yetu ya ulinzi na usalama. Lakini pia nguvu za viongozi wa dini lazima zitambuliwe katika hili, lakini kubwa zaidi ni uvumilivu tuliofunzwa tangu mwanzo.

Mwanapropaganda huyo anaficha ukweli kwamba ndani ya CCM hakuna amani. Ndiyo, nasema hakuna amani hata kidogo, kwa sababu dira ya chama imebadilishwa kutoka kwa wakulima na wafanyakazi, kwenda kwa wafanyabiashara.

Amani itatoka wapi wakati mwenye pesa hamjui mwenye njaa? Pengo la maskini na matajiri limeongezeka sana ndani ya CCM hadi kwenye serikali, ukweli ambao Makalla hakubaliani nao hata kidogo.

Imefika mahala ili uwe kiongozi ndani ya chama hicho kikongwe cha siasa, lazima uwe na fedha za kutosha kwa ajili ya kununua nafasi uitakayo, tofauti na malengo ya waasisi wa CCM kuwa busara, umakini, uadilifu na usafi wa matendo ya mwanachama ndiyo tiketi ya kuongoza wengine.

Kwa kauli za Makalla, ni wazi kuwa amefundwa kukataa hata ukweli. Amebaki na mawazo mgando ya kudumisha fikra za mwenyekiti bila kujali uzalendo.

Napenda kumshauri kijana huyo mwenye nafasi kubwa na nyeti ndani ya CCM, kuwa makini na kauli zake kwa sababu siasa ya zama hizi zinakwenda kwa sayansi na teknolojia. Hizi ni zama za 'dot com', achana na siasa za akina Kingunge Ngomabale Mwiru, zimepitwa na wakati.

Kijana unatakiwa kusoma alama za nyakati, unapojibu hoja ni budi kuwa na vielelezo ili kuonyesha usomi wako, si kukataa hoja kwa kuanzisha hoja bila mantiki.

Nakuuma sikio mwanakwetu, iliangushwa Roma sembuse CCM ambayo sasa imeanza kumwaya mwaya! Tazama vema 'mjomba' rudi kundini, waeleze viongozi wako kwamba, kasi ya wapinzani wenu ipo juu. Msipokuwa makini nchi itatawaliwa na chama chochote chenye kujali maslahi ya taifa.

Mwandishi wa Makala hii anapatikana kwa barua Pepe imarkmeero@yahoo.com
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/12/5/makala2.php
 
Kwa kauli za Makalla, ni wazi kuwa amefundwa kukataa hata ukweli. Amebaki na mawazo mgando ya kudumisha fikra za mwenyekiti bila kujali uzalendo. Napenda kumshauri kijana huyo mwenye nafasi kubwa na nyeti ndani ya CCM, kuwa makini na kauli zake kwa sababu siasa ya zama hizi zinakwenda kwa sayansi na teknolojia. Hizi ni zama za 'dot com', achana na siasa za akina Kingunge Ngomabale Mwiru, zimepitwa na wakati. Kijana unatakiwa kusoma alama za nyakati, unapojibu hoja ni budi kuwa na vielelezo ili kuonyesha usomi wako, si kukataa hoja kwa kuanzisha hoja bila mantiki.

Maneno mazito sana, kijana huyu ndiye chaguo la Nchimbi, kumrithi uenyekiti wa UVCCM, yeye ndiye Mtandao haswaa na partly ndiye sababu ya vita vikubwa alivyokuwa akipigwa ac, sasa na yeye anataka madaraka zaidi whatever it takes, maana wakati wa uchaguzi wa 2005 huyu ndiye hasa aliyetumika sana kwenye kuwatukana kina Salim, ameonja kidole sasa anataka mkono mzima,

Mungu atunusuru na bongo yetu na heshima kwa mwandishi wa hii article kwa kujaribu kumkumbusha commonsense!
 
Huyu naona hata haya kumuita msomi maanake itakua ni TUSI kubwa kwa maprofesa na madokta wote.

Duh,hizi akili nyingine kiama
 
Mungu wangu!

Siku moja nilimuona Makalla alipokuwa akihopojiwa kwenye TV!

Kuhusu chama cha mapinduzi nk! Na pia alipoulizwa nini mtizamo wake kuhusu barua ya Butiku kwa mkapa!

HUYU BWANA ANAVYOJIBU MASWALI NI MNAFIKI UTADHANI NI MZEE WA MIAKA 62!

ANAONEKANA KWANZA NI MUONGO, PILI HANA AIBU ANAPOSEMA UONGO WAKE!, TATU ANAJIAMINI NA HUO UONGO WAKE! NNE ANAONEKANA NI KATI YA WALE WANAOSEMA KUJIPENDEKEZA HAKUNA GHARAMA, TANO INAONEKA ANA NDOTO ZA ALINACHA ZA YEYE KUJA KUWA KIONGOZI NA HAPO TUTAKUWA TUMEKWISHA.

LAKINI NIONAVYO MIMI ASIPOFUATA USHAURI WA BURE ALIOPEWA BASI ATAISHIA KUONDOLEWA HATA KWENYE HIYO NAFASI YA UTUNZA HAZINA MAPEMA!

AKIHOJIWA ANAJIGEUZA GEUZA KWENYE KITI KAMA KINA MOYO VILE!

ETI OOHH MAISHA MAZURI KWA KILA MTANZANIA YAPO ILA TU WATANZANIA WAJITUME NA KWAMBA ccm HAIKUSEMA KUWA ITWALETEA MAISHA MAZURI BALI ILISEMA WANACHI WAJITUME NK.

KWA KIFUPI SIKU HIYO NILICHUKUIA KUMBE WENGI WALISHA MUONA.

MAKALLA HATUFAUI HATUFAI HATA KIDODO, AMEZUNGUKA HUYO HAYA BUTIMA KWENYE KABURI LA MWALIMU KESHA FIKA!

KUMBE INAWEZEKANA HATA HUKO UVccm AMEWAUMIZA SANA WENZAKE!
 
Duh, Mkira, naona huyu jamaa atakuwa ali-bore sana siku nile, ninavyosoma maelezo yako ni kama vile nakuona jinsi ulivyokasirika usoni!
 
Mungu wangu!


HUYU BWANA ANAVYOJIBU MASWALI NI MNAFIKI UTADHANI NI MZEE WA MIAKA 62!

ANAONEKANA KWANZA NI MUONGO, PILI HANA AIBU ANAPOSEMA UONGO WAKE!, TATU ANAJIAMINI NA HUO UONGO WAKE! NNE ANAONEKANA NI KATI YA WALE WANAOSEMA KUJIPENDEKEZA HAKUNA GHARAMA, TANO INAONEKA ANA NDOTO ZA ALINACHA ZA YEYE KUJA KUWA KIONGOZI NA HAPO TUTAKUWA TUMEKWISHA.

LAKINI NIONAVYO MIMI ASIPOFUATA USHAURI WA BURE ALIOPEWA BASI ATAISHIA KUONDOLEWA HATA KWENYE HIYO NAFASI YA UTUNZA HAZINA MAPEMA!

AKIHOJIWA ANAJIGEUZA GEUZA KWENYE KITI KAMA KINA MOYO VILE!

...nimecheka hapa sina mbavu
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom