MAKALA YA UCHUNGUZI-Waumini Wilayani Ngara wanaodai kuagizwa na Mungu kuishi Porini

Mathias Byabato

JF-Expert Member
Nov 24, 2010
1,020
691
Makala hii ina mambo mengi ya kujifunza hebu ipitie na utoe comment zako.-

Na Theonestina Juma,Kagera
NI zaidi ya miezi minne sasa tangu waumini wa kanisa la Pentekoste kukimbia nyumba zao na kupiga kambi kati kati ya pori la Nyakafandi ambalo liko umbali wa zaidi ya kilomita 60 kutoka Ngara mjini.

Pori hilo ambalo liko katika kijiji cha Mukubu Kata ya Muganza Tarafa ya Murugwanza waumini hao wameamua kuchukua hatua hiyo, kutokana na kukataa kutekeleza zoezi la serikali la wilayani humo kunyunyiziwa dawa ya ukoko ili kuua mazalia ya mbu waenezao malaria katika nyumba zao kwa madai kuwa inapingana na imani ya dini yao.

Tangu Julai 15 mwaka huu, wapige kambi katika eneo hilo, hadi sasa hakuna hatua yoyote madhubuti iliochukuliwa na uongozi wa wilaya hata mkoa, huku waumini hao wakiendelea kukaa katika pori hilo, ambalo wakihitaji huduma yoyoye ile mfano kama chumvi ya sh.150 sharti watembee umbali wakilomita 34 hadi Rulenge kwenda na kurudi kufuata bidhaa hiyo na pia wanaonekana kuwa kero kwa wananchi wa kijiji hicho.

Baadhi ya kero hizo ni pamoja na kuwaimbisha watoto nyimbo za kumtukuza Mungu muda mwingi bila kupumzika, kupinga suala nzima ya maendeleo, kukiuka haki za binadamu kwa kuwakataza watoto kupelekwa kliniki kwenda shule, kutotambua serikali aina yoyote ile na kuwazuia waumini wake kutumia dawa aina yoyote iwe ya hospitali au ya miti shamba kwa madai kuwa inapingana na imani yao.

Kama hilo halitoshi, waumini hao hawaruhusiwi kuoa wala kuolewa, hata kushiriki tendo la ndoa kwa wale walioko katika ndoa, zaidi ya kumtegemea Mungu na kumsubiri kuja kuwachukua muda wowote kulingana na maandiko ya Biblia wanayoiamini huku maisha wanayoishi ikiwa ni ya dhiki, ambapo hata nyumba wanamo lala hunyeshewa na mvua na hata chakula kwao kikiwa ni tabu kupata kwao ambapo watoto hulazimika kulishwa viporo huku watu wazima wakipata mlo mmoja kwa siku pekee.

Pia asilimia yao kuwa hawana mavazi ambapo kila mmoja anayo nguo mmoja mmoja kutokana na nyumba waliokuwa wamejenga hapo awali kuchomwa kwa moto na mmoja wanawanakijiji hicho, kwa madai kuwa serikali imeshindwa kuwaondoa watu hao katika eneo hilo.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Bulinda katika kijiji cha Mukubu, Bw. Thobias Nkenke anasema yeye kama kiongozi wa kitongoji hicho, amekuwa akikabiliwa na matatizo mengi kiuongozi katika kitongoji hicho ambacho asilimia kubwa ya waumini wake wanatoka katika kitongoji chake na baadhi yao hasa uongozi wa kanisa hilo kuwagomesha wananchi kutoshiriki katika suala lolote la kimaendeleo hasusan elimu kwa madai kuwa hayamfikishi mtu mbinguni na ni ya kishetani.

Anasema kutokana na waumini hao kukaa bila kufanya kazi, imekuwa ikiwafanya baadhi ya wananchi wengine, kushindwa kuendelea kuwa na moyo wa kujitolea kufanya kazi kutokana na madai kuwa waumini hao wamekuwa wakitumia rasilimali ya nchi, huku wakitegemea nguvu zao, ambapo hata ujenzi wa nyumba za walimu wa shule ya msingi Nyakafandi unaoendelea katika eneo hilo, huku katika pori hilo ndiko wananchi wanajikusanya kutafuta mawe kwa ajili ya ujenzi huo,hawashiriki kabisa.

Anasema kulingana na imani ya waumini hao, kila mtu wanayemwona akipita karibu na walikopinga kambi wanamkemea kuwa ni pepo, hata serikali wanaiita kuwa ni pepo, hivyo hata michango aina yoyote ile uongozi ukifika hapo kuwaomba hugoma kutoa.

Anasema waumini hao hatua walikofikia, kwa upande wa ngazi yao inawatia shaka, kwani imefikia hatua ya kuteketeza kila kitu hadi shahada za kupingia kura, radio zao, saa, vyandarua na vyeti vya kliniki za watoto wao kwa madai kuwa Mungu hataki waumini wake kuwa na vitu kama hivyo zaidi ya biblia pekee ndiyo nyaraka waliobaki nayo.Ambapo hata katika uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, mwaka huu hawakushiriki kwa wale waliokuwa na sifa.

Bw. Nkenke anasema mkewe Bi. Christina ambaye pia ni muumini wa dini hiyo, sasa ni miaka mitatu hajashiriki naye katika tendo la ndoa, ambapo akimwomba humkimea na kumweleza kuwa imani yao ya dini haikubali.

"Pale mke wangu ana mtoto wangu wa miaka miwili anaitwa Shimael Thobias, lakini siendi hata kuwatembelea, ni kama ndoa yangu hiyo imeshavunjika, na sidhani kama naweza kurudiana naye, hivi hiyo ni ndoa gani ya mwanamke kukukatalia kushiriki naye wakati ni haki yangu….imenilazimu kuoa mke mwingine"anasema.

Naye mkazi wa kitongoji cha Nyakafandi, Bw. Lucas Joseph (31) anasema anachokihurumiwa kwa waumini hao ni watoto sita kati ya umri wa miaka miwili hadi mitano ambao wamekuwa wakifanyishwa kazi ya kuimba muda wote huku kulala kwao ukiwa ni usiku wa manane.

Anasema watoto hao, mtoto anayepiga ngoma huku wenzake wakiimba ni wa umri wa miaka mitatu.Anataja jina la mtoto huyo kuwa ni Joshua Bonphace.Mtoto huyo anavishwa kamba ya ngoma shingoni na kisha ngoma yenyewe kuwekewa juu ya mapaja na kuanza kupiga huku wenzake wakiimba, wakiwa katika mtindo mbali mbali wa kuraka ruka, kusimama, kucheza cheza na pengine hukaa chini wakiwa wamechoka huku wakiendelea na zoezi hilo.

Halikadhalika waumini hao bila kujali rika hulazimika kulala chini kwenye majamvi ndani ya nyumba moja wanayoitumia kama kanisa huku wakiabiliwa na upungufu wa mashuka ya kujifunika usiku, nguo za kuvaa na chakula kutokana na kanisa lao waliokuwa wamejenga kuchomwa moto na mmoja wa wananchi wa eneo hilo kwa madi kuwa serikali imeshindwa kuwachukulia hatua waumini hao kwa kuwaondoa.
Kwa upande wa Mtendaji wa kijiji cha Mukubu, Bw.Nicodem Daniel anasema tukio la kanisa hilo limeweza kusababisha baadhi ya ndoa za watu kuvunjika licha ya kuwa hajapata taarifa hizo rasmi za wanandoa hao kumlalamikia Mchungaji wa kanisa hilo, kwa kuvunja ndoa zao.

"Taarifa za ndoa za baadhi ya watu kuvunjika, zipo lakini sijazipokea rasmi kutoka kwa walalamikaji, mmojawapo akiwemo mwenyekiti wa Kitongoji cha Bulinda"anasema

Anasema dini hiyo pamoja na waumini wake, kwa sasa yeye ameshindwa kuwafuatilia kwa undani zaidi kutokana na juhudi za serikali za kijiji kutoonekana zikiungwa mkono na serikali kuu ambayo ni ngazi ya wilaya na matokeo yake wao wa chini ndiyo wanaonekana ni wabaya.

"Katika hili, serikali ya kijiji imebaki kuangalia tu, kwani imefanya juhudi nyingi, lakini matokeo yake imekuwa hasi, wakati wakiendelea kukaa kwa waumini hao katika pori hilo, inaonesha kana kwamba serikali imeshindwa kutekeleza wajibu wake wakati ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu zikiendelea kukiuwa katika eneo lile"alisema.

Pia Mtendaji wa kata ya Muganza, Bw. Paul Paschal anasema kwa upande ngazi ya kata kanisa lile hawalitambui kwa vile halijasajiliwa.Kwani kama ni taarifa juu ya kanisa hilo na uongozi mzima tayari zimeshafika ngazi za juu, na hivyo, anabaki kushang'aa ni kwa nini ngazi za juu zimeshindwa kuchukua hatua.

Anasema uongozi wa kanisa hilo, kiujumla haushiriki kikamilifu katika suala nzima ya maendeleo hasa kilimo ambacho ndicho tegemeo kubwa la wakazi wa eneo hilo.
Anasema pamoja na kuwepo kwa waumini hao katika eneo hilo, Mchungaji huyo anawapotosha na kuwadang'anya wa vile yeye taarifa walizonazo ni kuwa mumewe alifariki na kumwachia mali kama ng'ombe ambao inasemekana kuwa wako Biharamulo kwa baadhi ya ndugu zake.

Anasema kwa mwaka 2009 waumini wa kanisa hilo, waligoma pia kunyunyiziwa dawa ya ukoko, ambapo serikali iliamuwa kuwaacha bila kuwafuatilia, jambo ambalo hata mwaka huu zoezi hilo lilipotakiwa kufanyika kwao tena walionesha kuendelea na msimamo wao.

Kuhusu elimu anasema kuna baadhi ya wananfunzi waliokuwa wakisali katika dini hiyo, ambapo serikali iliweza kuingilia kati na kurudi makwao, ambapo kwa sasa kuna utaratibu unaofanyika wa kuweza kumkamata mchungaji huyo ili aweze kufikishwa mahakamani kuhusiana na utoro wa mwanae ambaye hahudhurii shuleni kabisa.

Hata hivyo, kwa upande wa Kaimu Afisa Elimu wilaya ya Ngara, Bw.Oswald Rujuba anasema suala nzima ya waumini hao na elimu inajulikana, ambapo mikakati ya wilaya katika kutokomeza suala hilo zimeanza kuchukuliwa na kwamba hawezi kuzitaja kwa vile si msemaji wa Halmashauri hiyo.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa wilaya ya Ngara, Bw.Mathias Mwangwi anasema katika suala nzima inayohusiana na kamati ya ulinzi na usalama hahusiani hayo kwani ni kazi ya Mkuu wa wilaya, Kanali Salum Nyakoji.

Anasema suala la ukiukwaji wa haki za watoto zinazofanywa na waumini hao, hajawahi kufia katika eneo la tukio na hafuatilii masuala ya waumini hao zaidi ya Mkuu huyo wa wilaya.

Kwa upande wa Mganga Mkuu wa wilaya ya Ngara, Dkt.Godian Beanga anasema hawezi kuzungumzia suala lolote juu ya waumini hao hasa kwa upande wa watoto wadogo na matatizo yanayowakabili kiujumla bila kupata ridhaa kutoka kwa Mkuu wake wa kazi, ambaye ni Mkurugenzi.

"Labda umwombe Mkurugenzi, aniruhusu niweze kuzungumza nawe juu ya suala hilo, lakini bila ridhaa yake siwezi kusema lolote kwa vile mimi si msemaji wa Halmashauri"alisema Dkt. huyo.

Mchungaji anayendesha kanisa hilo, ambaye anajitambulisha kwa jina la Anna Mulengera huku watu wengine wakijitambulisha kwa jina la ‘Annamaria' anasema sababu kubwa iliowapelekea kuhamishia makazi yao katika pori hilo, ni sauti ya Mungu pekee, wanafanya kazi ya Mungu pekee na hata Mkuu wa wilaya alipozuru hapo hakuweza kuwafanya jambo lolote.

Anasema licha ya kuwa kuwepo kwao katika eneo hilo linaonekana kutowapendeza watu wengi, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa wanawaonea wivu yeye pamoja na waumini wa kanisa hilo, ambao hawakufukuzwa katika kitongoji walikokuwa wakiishi awali, zaidi ya kufuata sauti ya Mungu pekee, Licha ya kuwa kazi ya Mungu inaupinzani mkali na hali hiyo inajidhihirisha jinsi maisha yao yalivyo.

Bi.Mulengera anasema wivu huo unatokana kuwavutia watu wengi kufika eneo hilo walikopiga kambi, kama Mkuu wa wilaya ya Ngara,Kanali Mstaafu Salum Nyakoji pamoja na baadhi ya viongozi wenzake waliofika hapo kuwatembelea, jambo ambalo analielezea kuwa ni nadra kuona baadhi ya viongozi wakizuru katika pori hilo.

Anasema yeye aliyeamua kuokoka tangu mwaka 1998, ambapo wakati wakihamishia makazi yao katika pori hili,walikuwa waumini wapatao 42, huku asilimia kubwa wakiwa ni wanafunzi wa shule za msingi kuanzia shule ya awali hadi darasa la sita.

Anasema kutokana na kuwa na waumini hao, ilitokea kutoelewana na serikali, ambapo alipata misuko suko mingi kutoka serikalini na hivyo baadhi ya wanafunzi hao ambao ni waumini wake, kuanza kurejea taratibu makwao na hajui kama kweli wanaenda ama la.

"Pamoja na hayo, mimi niliweza kuwauliza wanafunzi hao wachague moja kurudi walikotoka ama kueneza neno la Mungu, lakini watoto hao wenyewe waliweza kunijibu kuwa miaka yote wamekaa shuleni lakini hawaelewi kitu chochote hivyo tunaona bora tukae hapa tuhubiri injili"anasema huku akicheka.

Anasema licha ya watoto hao awali kuridhia jambo hilo kwa pamoja ya kukaa eneo hilo pamoja na kutakiwa na serikali kurudi shuleni, watoto hao walianza tabia mbaya za udokozi na zingine jambo ambalo liliwafanya kuanza kuondoka mmoja baada ya mwingine.

Anasema pamoja na kuwa wameondokana, hajui kama wanaenda shule kweli ama la kutokana na uelewa wao ni mdogo kwani baadhi yao hawajui hata kusoma na kuandika.

"Unafikiri hata kama wamerudi shuleni ama kwa wazazi wao wanajua nini, hata ukiwaonesha hii ni herufi gani mtoto hajui kusoma, Ah…ahahaha…mimi naweza kusema kuwa kuondoka kwao ulitokana na wivu tu….lakini hawatajua chochote "anasema Mchungaji huyo kwa furaha tele.

Kuhusu idadi ya waumini anasema hadi kufikia Novemba 5, mwaka huu alikuwa wamebaki jumla ya waumini 18 kati yao watoto wakiwa ni saba na watu wazima 12.

Hata hivyo, anasema idadi ya waumini wake wamekuwa wakipungua kutokana na kile kinachoolezwa na baadhi ya waumini wake kuwa Mungu amechelewa kushuka huku wakiendelea kutaabika kwa maisha magumu, jambo ambalo analieleza kuwa inatokana na wale ambao hawana mioyo ya uvumilivu, kwani kwenda mbinguni kunahitahili ustahimilivu wa hali ya juu.

Kuhusu imani ya kanisa lake, hilo ambalo halina usajili, anasema waumini wake hawatakiwi kwenda hospitali, kusikiliza redio, kuvaa saa, hakuna kutumia dawa za kienyeji na watoto nao hawatakiwi upelekwa kliniki kwani yote hayo yanapingana na imani yao na Mungu hataki chang'anya.

Anasema hapo walipo ndipo wamefika na hajui watarejea lini kwenye nyumba zao, labda hadi wasikie sauti ya Mungu ikiwataka warejee ndipo wataondoka lakini kwa sasa wala hawana mpango kama huo.

Anasema sauti ya Mungu aliwaambia kuwa katika eneo hilo, kuna watu kutoka mataifa mbali mbali watakuja kuwatembelea na kusikia jinsi wanavyomtukuza na hivyo hawapaswi kuondoa katika eneo hilo na kwamba hatuahiyo ilitokana na baada ya mtoto mmoja aitwaye Obadia Emmanuel (4) alishikwa na ugonjwa wa ajabu na kushindwa kupumua kabisa kwa saa kadhaa, jambo ambalo walianza kumwombea hadi kupona bila kutumia dawa aina yoyote.

Ambapo hata hivyo, mama wa mtoto Obadia, anayemtaja kwa jina la Alphonsina Emmanuel aliondoka naye pamoja na watoto wake wengine wawili, baada ya kutembelewa na Mkuu wa wilaya aliyeweza kutoa maneno yao ya kuwasihi kurejea makwao ili kuendelea na shughuli zao za kila siku na kutokana na imani yake kuwa haba aliweza kutekeleza hayo ya Mkuu wa wilaya.

"Unajua si kwamba mkikaa watu 10 hadi 20 imani yenu inakuwa pamoja, hivyo mama yake Obadia aliamua kuondoka naye urudi nyumbani na siku nyingine akaja kana kwamba anakuja matembezi kumbe alikuja kuwaiba watoto wengine wawili waliobaki na baba yao na kumwacha mumewe, Bw. Emmanuel Revelian (27) hapa pekeyake akiendelea kueneza neno la Mungu.

Akizungumzia kupungua kwa waumini wake anasema hali hiyo inatokana na baadhi ya watu kumwona mzee wa miaka 70 kufikia hatua ya kuzeeka bila Yesu kurudi kumchukua na hivyo jambo kama hilo linawafanya baadhi ya watu wengine kuvunjika moyo, kutokana na Yesu kuchelewa kurudi kuwachukua huku wakiendelea kuteseka hapa duniani.

Anasema miaka yote tangu waamue kumpokea Yesu kama mwokozi wa maisha yao, wamekuwa wakimtegemea wa kila jambo, kwani vitu vingine vya kidunia kwao ni anasa ambayo Mungu hapendi.

Pia waumini wa kanisa hilo wanaishi kama kaka na dada na hivyo hakuna kuoa wala kuolewa na hakuna kufanya vitendo vya ngono kwa wale walioko kwenye ndoa.
Mkuu wa wilaya ya Ngara, Kanali Mstaafu Salum Nyakoji anasema pamoja na kuwa wanaumini hao wamekimbia nyumba zao, kwa kukataa serikali kutekeleza azma yake ya kuangamiza mbu waenezao malaria, chini ya Jeshi la polisi wilayani humo, waliweza kuwanyunyizia dawa hiyo kwa nguvu.

Anasema kitendo cha waumini hao kukataa nyumba zao kunyunyiziwa dawa kwa madai kuwa ni kinyume na imani yao, kwani wao wamekuwa wakimtegemea kwa kila jambo, aliliona halina msingi wowote na hauwezi kuzuia serikali kutekeleza azma yake hasa katika suala nzima ya maendeleo kwa wananchi wake ambao ni pamoja na wao.Hasa ikizingatiwa kuwa mbu ndicho chanzo malaria inayoongoza kuua watu hapa nchini hususan katika wilaya hiyo.

Anasema hatua hiyo aliweza kuichukua mara baada ya kupata taarifa ya waumini hao kukimbilia porini na kufunga nyumba zao, kwa kukataa kunyunyiziwa dawa ya ukoko.

Anasema alilazimika kwenda huko kambini akiongoza na kamati yake ya afya ya wilaya na kuongea na uongozi wa kanisa hilo, ambaye ni Mchungaji Annamaria Mulengera na kumwelezea umuhimu wa serikali kutekeleza azma yake ya kunyunyuzia dawa ya ukoko kwenye nyumba zao kama ilivyo kwa watu wengine.
Na hivyo siku iliofuata walienda kwa nguvu na kutekeleza zoezi hilo, ambapo sehemu wanapoishi, anasema kuwa ni sehemu ya mkusanyiko tu ambayo ni nyumba ya majani na ni kwa ajili ya ibada lakini wana nyumba zao wanakoishi.

Hata hivyo, katika uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini licha ya waumini hao kukimbilia porini uongozi wa wilaya unangalia jambo hilo kama ni la kawaida tu, ambapo suala hilo katika ngazi ya mkoa hakuna kiongozi yeyote wa ngazi hiyo anayejua suala hilo.

Akiongea sakata hilo Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa Kagera, Vitus Mlolere anasema kanisa la mchungaji huyo halitambuliwi na serikali kutoana na kusajiliwa na hivyo, amelazimika kuwaagiza kitengo cha upelelezi kuwamkamata chungaji huyo pamoja na waumini wake kwa ajili ya uchunguzi zaidi na pindi wanakapobainia kuendesha kanisa bila usajili wafikishwe mahakamani mara moja.
==============================================================
 
Anasema kwa mwaka 2009 waumini wa kanisa hilo, waligoma pia kunyunyiziwa dawa ya ukoko, ambapo serikali iliamuwa kuwaacha bila kuwafuatilia, jambo ambalo hata mwaka huu zoezi hilo lilipotakiwa kufanyika kwao tena walionesha kuendelea na msimamo wao.


Kuhusu elimu anasema kuna baadhi ya wananfunzi waliokuwa wakisali katika dini hiyo, ambapo serikali iliweza kuingilia kati na kurudi makwao, ambapo kwa sasa kuna utaratibu unaofanyika wa kuweza kumkamata mchungaji huyo ili aweze kufikishwa mahakamani kuhusiana na utoro wa mwanae ambaye hahudhurii shuleni kabisa.[/QUOTE]

Ni makala nzuri ambayo inaonesha wajibu wa waandishi wetu kutembelea maeneo ya vijijini kuibua masuala kama haya,kwani ninavyosikia ni kuwa Ngara ni mbali sana kutoka Makao makuu ya Mkoa huo.

Hata hivyo nadnani kuna haja ya Serikali ngazi ya mkoa na wilaya,kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya imani na siyo kukamata watu na kuwafikisha mahakani.

Uenda mchungaji huyo akaachiwa hutru kwani sidhani kama anaweza kupatikana na hatia kwa mazingira haya.
 
hii makala inanyongeza ya mtazamo na maoni binafsi ya mwandishi na hivyo kunguza uwezo wa msomaji kupata picha halisi!!
 
Back
Top Bottom