Makala: Tumeshindwa....Tuibomoe, Tuijenge Upya Tanzania -Part I Supplement

IsangulaKG

JF-Expert Member
Oct 14, 2010
706
385
Jana Tuliona jinsi Mkulukulu alivyosikitishwa na watu wazima Kujisaidia Vichakani, baada ya kulinganisha hali ile na maisha ya nyumbani kwake, akamuagiza mkuu wa bajeti kutenga fungu la kujenga vyoo vya kisasa kijijini. Matofali yakanunuliwa na kusubiri hadi wakati wa Kampeni. Siku ya kampeni akaamuru ujenzi uanze mara moja....leo naendelea......


Hata chama vya Fulani kilipokuja pale kijijini na kutoa ‘data' za kiwango halisi cha fedha iliyokuwa imetengwa ambacho kimeliwa juu kwa juu na wakubwa hakuna aliyesikiliza. Hata walipoeleza gharama halisi zilizotumika kuchapa vitenge, kofia na t sheti za ''Chagua mkulukulu'' ambazo zingetumika kujenga shule, waliambulia miluzi na kuzomewa na wazameaji waliokuwa wamendaliwa na watu walioapa kuwa wao na mkulukulu kufa kuzikana. Wakati wa uchaguzi, kijiji hiki kiliongoza kwa kumpigia kura mkulukulu, mbunge, madiwani, wenyeviti wa mtaa na hata wajumbe wa nyumba kumi wote walitoka katika chama cha mkulukulu.
Matofali ya bloku, simenti, mchanga vilijazwa pale kijijini, huku baadhi ya wanakiji wakijitwalia matofali kadhaa na kupeleka majumbani mwao na kuyapanga vizuri kama ‘makochi' ya kukalia ,wengine wakiweka kama milingoti ambayo baadaye waliweka miti na jamvi juu yake ikawa kama magodolo maarufu ya banco, wakapumzisha mbavu zao baada ya mihangaiko ya kila siku mashambani. Japo wananchi, mwenyekiti wa kijiji, mafundi, mweka hazina na mkuu wa bajeti walijipatia karibu robo tatu ya fedha zilizotengwa kwa mradi huu mwisho wa siku ulikamilika huku ufa mkubwa kati ya maliwato ya tano na sito uliotokana na kuchakachuliwa kwa vifaa.
Muda wa uzinduzi ukafika, hapo mkuu wa bajeti ,mweka hazina wakatuma fungu kwa mkuu wa wilaya ili kuhakikisha ufa kama upo unaficha kwa hali na mali, maliwato ipakwe rangi, mazingira karibu na maliwato yasafishwe, watume magari ya maji yaweke maji pale, maua yapandwe, risala iandaliwe na atafutwe mwanakijiji wa kuisoma, t sheti na vitenge vya ‘asante mkulukulu' viandaliwe. Vikundi vya sanaa vitafutwe kwa kuwa mwezi unaofuata mkulukulu alikuwa anaenda kuzindua maliwazo za kisasa.Uzinduzi ukapambwa na msululu wa magari, meusi kwa meupe, na wanajeshi na FFU utadhani walikuwa wakienda kumwondoa nduli aliyevamia kijiji. Helkopta ikazunguka hewani kulinda usalama hapa kijijini ambapo hata Osama asingefikiria kufika hata siku moja. Nyimbo zikaimbwa zikaimbika, vigelegele vikapigwa vkapigika, miluzi ikapigwa ika sikika, ngojera na mashairi mpaka tenzi na bendi maarufu aliyokuja nayo mkulukulu toka mjini. Vyombo vya habari vikapambw na habari za mkulukulu alivyo na roho safi na moyo wa upendo kwa wananchi hasa wa vijijini. Hadi vyombo vya kimataifa CNN, BBC, Reuters vikamtangaza mkulukulu kama shujaa wa kuwaokoa wananchi wa vijijini dhidi ya adha ya kuchomwa mida na kupata monyoo kwa kujisaidia maporini wakisahau kuwa kijiji hiki ni kimoja tu kati ya vijiji maelfu nchini na angalau hiki kiko barabarani.Risala ikasomwa:'sisi wana kijiji tunakushukulu saana mkulukulu kwa upendo ulionao kwetu, sasa umetukomboa dhidi ya adha ya kuchomwa na miba, kuumwa na majoka, kuliwa na simba na kupata minyoo kutokana na kujisaidia vichakani. Tunakuahidi tutavitunza vyoo hizi ili vidumu"

Baada ya Risala wazee wakamvisha mkulukulu vazi la kimila na kumtambua kama mmoja wapo wa wazee wa kijiji japo mkulukulu alikuwambali sana kufikia umri wa kuitwa mzee. Akapewa zawadi kuanzia kuku, mbuzi hadi ng'ombe.


Katika hotuba yake mkulukulu akasema, 'serikali yangu imedhamiria kupambana na umasikini wa wananchi, tumeweka mipango thabiti na mikakati ili kuondoa umasikini wa wananchi., Mwaka jana awamu ya kwanza ya mpango wa kuendelea kilimo ulioandaliwa na wataalamu wa wizara ya kilimo pale wizarani ulimalizika na kuonesha mafanikio katika maeneo kadhaa. Ninaomba mtuunge mkono pale tutakapoanza kutekeleza awamu ya pili yampango huu uliofadhiliwa na banki ya dunia'

Ukweli ni kwamba kuna baadhi ya wananchi ambao hawakujua hata kinachoongelewa. Mzee Mwamba, ambaye ni mkulima maarufu wa mpunga, aliwahi kwenda kwa mkuu wa wilaya aliposikia kuna karatasi za pembejeo za kilimo lakini akaambiwa zimeisha, akakumbuka kuwa aliwahi kusikia katika redio yake ya mbao aina ya 'Panasonic' kuwa hizo karatasi zitagawiwa kwa wanakijiji wote katika ofisi ya mkuu wa wilaya kwa tarehe alizoenda lakini hzikuwepo. Akanyannyua mkono ili kumuuliza mkulukulu swali, lakini mkuu wa wilaya alipomwona akamtambua akamkonyeza msaidizi wake akamvute Yule mzee pembeni. Hatamkulukulu aliposem nimeona mkono hapo, mkuu wa wilaya akamwambi ‘ni mzee mwamba alitaka kukupa zawadi ya mazao yake' na tumemwomba , kw kuwa ratiba yako ni finyu aiwakilishe kwetu na mimi binasfi nitaileta katika hekalu lako'

Baada ya uzinduzi wa mbwembwe huku utepe ukikatwa katika maliwato hizi za kisasa kabisa kuwahi kujengwa kijijini katika nchi zinazoendelea, na mkulukulu akatoa mfano kwa kuwa mtu wa kwanza kunawa mikono katika mojawapo ya mabomba yaliyopo hapo maliwatoni akiashiria kuruhusu matumizi maramoja. Kisha akaondoka kwa mbwembwe kama alivyokuja huku gari moja likiwa limejaa viazi, Magimbi, Mbuzi, Kuku, Mayai, Karanga , Mihogo na vikolokolo kibao toka kwa wanakijiji toka kwa wanakijiji. kwa ujumla vitu vyote vilipatikana kutokana na umahiri wa uongozi wa kijiji kukusanya Michango kwa wanakijiji huku wasiochanga wakitishiwa 'kukiona' baada ya mkulukulu kuondoka.....

Itaendelea wiki ijayo
 
Back
Top Bottom