Makala Raia Mwema: UKAWA tutarejesha heshima ya Tanzania kimataifa

Ben Saanane

JF-Expert Member
Jan 18, 2007
14,581
18,124

Na Ben Saanane


KUPITIA makala hii, naamini Watanzania watatumia fursa ya uchaguzi Oktoba 25, kuifufua Tanzania ya Mwalimu Nyerere kupitia sanduku la kura kwa kuichagua Serikali ya Ukawa.

Mwasisi wa taifa letu, Mwalimu Nyerere aliipenda Tanzania na Afrika, hakupenda ukandamizaji ndani na nje ya mipaka yetu.Tanzania ilijiweka katika ramani ya dunia kutokana na msimamo na uongozi shupavu wa Mwalimu Nyerere kiitikadi, kifalsafa na kimaono.

Aliposimama katika Jukwaa la Umoja wa Mataifa kule New York, Afrika na mataifa mengine yaliyopinga ukandamizaji yalikuwa nyuma yake. Aliposimama katika Jukwa la Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), kule Addis Ababa-Ethiopia, wanamajumui (Pan-Africanist) walisimama nyuma yake.

Hakika Afrika na dunia katika changamoto za leo itamkosa sana gwiji huyu mwana halisi wa Afrika. Kwa Tanzania siku ya leo ni msiba zaidi. Tutapata fursa ya kupunguza majonzi haya kwa kuifufua Tanzania ya Nyerere Oktoba 25, kwa kufanya mabadiliko kupitia sanduku la kura na kuichagua Serikali ya Ukawa.

Itakuwa hatari sana kumchagua Rais mwenye upeo mdogo kimataifa. Rais asiyejua hata Saddam Hussein alikuwa Rais wa nchi gani? Anasema hadharani kwa ujasiri kuwa alikuwa Rais wa Kuwait? Yaani kama hajui mtu maarufu wakati wa vita ya Marekani na Iraq, Saddam Hussein alikuwa Rais wa nchi gani ataelewa nini kuhusu sera ya Tanzania Mashariki ya Kati na Bara Asia? Kweli ataweza kuirejesha heshima ya Tanzania ya Mwalimu Nyerere katika ramani ya dunia? Ataelewa nini kuhusu diplomasia ya uchumi?

Katika dunia ya leo pale ambapo dunia yetu inafanywa kama kijiji, huku mataifa yakiungana na kuridhia uhusiano wao juu ya masuala mbalimbali na hasa ya kiuchumi, taifa kuwa na sera ya nje makini inayolinda maslahi yetu katika uhusiano wetu na mataifa mengine ni kitu muhimu sana. Ukitazama namna mataifa yenye viongozi makini yanavyoendesha siasa zake za nje, utakuta suala la maslahi ya kiuchumi limepewa kipaumbele sana. Diplomasia ya uchumi ndio kiongozi wa nchi miongoni mwa mataifa mengine.

Hivyo ni jambo lililo wazi kuwa hata wakija hapa, habari yao kubwa itakuwa ni diplomasia ya uchumi. Watanzania tutumie fursa hii kujiuliza je, Tanzania kama taifa huru limejiandaa vipi katika uhusiano huu ili kuhakikisha kuwa raia wake wanafaidika na uhusiano huo? Sera yetu ya nje inasemaje?

Wagombea urais na vyama vyao wanasemaje kuhusu nafasi ya Tanzania katika medani za kimataifa? Sera zao zinalinda vipi maslahi yetu wote?

Je, viongozi wetu wanaitekeleza hata sera ya serikali iliyotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM)? Haya tunayoyashuhudia hivi sasa ikiwemo safari nyingi za gharama kubwa za Rais wetu aliyefikisha idadi ya ziara zaidi ya 410 nje ya nchi (zaidi ya mwaka mmoja ) katika awamu zake mbili madarakani, ni utekelezaji wa sera yetu wenyewe? Je, utekelezaji wa sera yetu unaleta uwiano mzuri na sera za mataifa mengine na jumuiya za kimataifa?

Je, sera hiyo inaleta uwiano mzuri na sera zetu za ndani na hasa katika masuala ya uchumi? Je, tunaweza kusimama na kuizungumza sera hiyo kwa mwananchi wa kawaida na akatuelewa na kuona maslahi yake kama Mtanzania ndani yake? Je, inatekelezeka?

Maneno Diplomasia na Sera ya Mambo ya Nje yamekuwa yakitumika wakati mwingine kumaanisha kitu kimoja (Interchangeably), ingawa yana maana tofauti.

Kwa mfano diplomasia maana yake ni uhusiano wa kimataifa kati ya nchi na nchi na kati ya nchi na mashirika ya kimataifa (Mult-National Corporations). Uhusiano huu hutengenezewa mbinu na mikakati endelevu (sustainable strategies) ya utekelezaji wake kwa kila nchi kupitia sera zao za mambo ya nje.
Sera ya Mambo ya Nje (Foreign Policy) ni tamko la nchi lenye kutoa mwongozo na mwelekeo kuhusu madhumuni, malengo na misingi ya nchi katika kuhusiana na nchi, mashirika ya kimataifa na wadau wengine nje ya nchi. Tamko hili pia ni mwendelezo wa sera ya ndani ya nchi kama vile kwenye sera ya elimu, viwanda na biashara, nishati, ulinzi, afya, kilimo na vitu vingine kama dira ya maendeleo . Sera ya Mambo ya Nje ya nchi ni chombo kinachobeba dhana na mbinu za utekelezaji wa diplomasia.

Sera hutoa mwelekeo juu ya misimamo ambayo nchi inaipigania na ile isiyokubaliana nayo katika medani za kimataifa na itataka kutambuliwa msimamo wake wazi kupitia sera. Sera hii ndiyo kitambulisho cha taifa husika katika kulinda tunu (values) zake na kujipambanua miongoni mwa mataifa. Kwa hiyo ni jambo muhimu kwa kuwa ni utambulisho wa nchi kimataifa, na tamko hili huakisi sera na misingi ya ndani ya nchi husika.

Kwa kawaida mratibu mkuu (coordinator) wa utekelezaji wa sera hii ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, na sera hii hutekelezwa na serikali nzima na wadau wengine ndani ya nchi, ambao shughuli zao zinahusiana na masuala ya kimataifa.

Mkuu wa nchi ndiye mwanadiplomasia namba moja, na Waziri wa Mambo ya Nje ni mwanadiplomasia namba mbili katika nchi yoyote. Hawa ndio sura ya nchi mbele ya dunia na ndiyo maana inabidi kuwa makini sana katika uchaguzi hasa uchaguzi wetu mkuu kwani Uchaguzi Mkuu pamoja na kuwa unamchagua Rais wa Watanzania lakini pia unamchagua mtu atakayebeba haiba ya Watanzania nje ya nchi, misimamo yake ndiyo itakayowakilisha Watanzania nje ya nchi.

Ni lazima kuwa na Rais mwenye uzoefu wa kiuongozi, mwanadiplomasia kwa muonekano na kifikra. Tanzania ina sera ya mambo ya nje ya mwaka 2001 ambayo ilipaswa kutoa mwongozo katika kufikia malengo ya nchi nje.

Kama zilivyo nchi nyingine nyingi baada ya Uhuru tulikuwa na sera ya ukombozi ndiyo maana tulijikuta tumechagua maadui na marafiki wakati wa ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.

Diplomasia yetu sasa tofauti na awali, inatakiwa ilete manufaa ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kufungua masoko kwa biashara za Watanzania, bidhaa, kuvutia wawekezaji na kuongeza watalii. Mkakati huu wa kutekeleza sera, umepewa jina la Diplomasia ya Uchumi.

Diplomasia, kama ilivyo mikakati mingine inayo vigezo na vipimo vyake. Diplomasia hufanyiwa tathmini mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya kidunia.

Uimara wa diplomasia ya nchi ni ushawishi wake kimataifa. Ushawishi wa nchi, kihistoria umekuwa ukiambatana na nguvu ya kiuchumi au kijeshi (Diplomasia ya Nguvu). Nguvu hizi mbili ni matokeo ya sera za ndani ya nchi. Pamoja na kuwa, si lazima kuwa kila nchi yenye moja au vigezo hivyo viwili kufanikiwa katika diplomasia. Ziko nchi ambazo zimefanikiwa sana kuwa na ushawishi mkubwa, pamoja na kutokuwa na nguvu hizo duniani, kutokana na uimara wa sera yake ya mambo ya nje, na wanadiplomasia wake (Nguvu ya Diplomasia).Tanzania chini ya Mwalimu Julius Nyerere na Wanadiplomasia kama akina Salim Ahmed Salim ilikuwa miongoni mwa nchi hizo.

Tanzania imekuwa ikitoa misimamo mikali katika medani za kimataifa chini ya Mwalimu Nyerere kutokana na haiba na misimamo yake kifikra iliyobeba mantiki za kiushawishi kidiplomasia miongoni mwa mataifa makubwa.

Tanzania kama mwanachama wa jumuiya ya kimataifa ni lazima irejeshe heshima na utambulisho wake uliopotea baada ya utawala wa Mwalimu Julius Nyerere.

Serikali ijayo chini ya Ukawa imepanga kuanzisha harakati mpya za kuwezesha kuwepo mfumo wa uchumi na biashara duniani wa haki na usiokandamiza nchi changa na pia kuendelea na harakati za kujenga msingi wa nchi masikini kushirikiana zaidi ikiwemo kufanya biashara zaidi baina yetu. Ni harakati za kurekebisha taasisi za utawala wa siasa za kimataifa zizingatie matakwa na maslahi ya mataifa mengi zaidi

Lazima kuendelea kupambana na ukoloni-mamboleo (Neo-Colonialism) ambao kila kukicha unachukua sura mpya ikiwemo kuhusisha misaada kwa nchi yetu na maslahi ya kibiashara ya mashirika ya nchi zinatoa misaada hiyo, kupewa masharti ya kupata misaada isiyo na msingi, na mashinikizo ya kufuata sera na kuchukua misimamo isiyo na manufaa kwa nchi yetu.

Tanzania imeshindwa kutoa misimamo yake thabiti kwenye majukwaa ya kimatifa kukemea udhalilishji wa kushinikizwa kupewa misaada kwa masharti ambayo ni kufuru katika Imani ya dini zote hasa masharti ya ndoa za jinsia moja.

Yote haya ni kwa sababu sera yetu imepoteza mwelekeo na diplomasia yetu sio ya uchumi bali ni diplomasia ya kuomba na kushukuru kutoka kwa mataifa makubwa yenye kiu na ndoto za ubeberu.

Serikali mpya ya Ukawa inalenga kuhakikisha kuwa utambulisho na sifa ya Tanzania kimataifa inabebwa na Watanzania nje ya nchi badala ya sifa ya Rais kutunukiwa shahada lukuki zisizo na tija katika medani za kiuchumi.

Diplomasia yetu kimataifa ni lazima ilenge katika utamaduni, uchumi na biashara kuliko ilivyo sasa ambapo diplomasia yetu ni ya kisiasa zaidi na haimgusi Mtanzania wa kawaida. Rais wa nchi anapowekeza katika sifa na ufahari binafsi kwa kutunukiwa medali ambazo hazina manufaa kiuchumi kwa Watanzania sio diplomasia ya uchumi bali ni diplomasia inayotumikia na kutumikishwa kisiasa.

Majirani zetu Kenya kwa mfano, wanapotoka nje ya mipaka yao na kujitambulisha kuwa wao ni Wakenya moja kwa moja wanatambulika kutokana na umahiri wao katika mchezo wa riadha. Riadha ni mchezo lakini unakuza uchumi wa Wakenya na utambulisho wao kimataifa.

Nchi kama India na wananchi wake kwenye sura ya kimataifa wanatambulika kwa umahiri wao katika teknolojia ya mawasailiano, famasia na katika nyanja za utabibu huku mataifa kama Ujerumani, China na Japan, raia wake wakionekana kuwa mahiri katika Uhandisi.

Ni lazima sera msukumo sahihi wa sera zetu za ndani kama nilizoeleza katika mfululizo wa makala zilizopita ulenge kuhakikisha Watanzania wanabobea katika nyanja mbalimbali ambazo zitaleta ushawishi katika diplomasia yetu kimataifa na kuwa sura ya Tanzania nje ya mipaka yetu.

Ndio maana katika ilani ya Chadema inayoungwa mkono na Ukawa tumewekeza na kuipa kipaumbele elimu kwa sababu ni kupitia elimu tu tunapoweza kutoa vichwa ambavyo vitaweza kuiweka Tanzania katika ramani ya juu kimataifa.

Iwe katika soka, filamu au muziki ni lazima elimu ipewe kipaumbele ili tuweze kufikia hatua walizofikia wenzetu kama Nigeria na Nollywood yao, Marekani na Hollywood yao.

Katika ushawishi kimataifa, mataifa makubwa kama Marekani yalitambua umuhimu wa kuitumia burudani kupitia muziki, mpira wa vikapu, filamu katika kueneza ubeberu wa kiutamaduni (cultural imperialism) kiasi ambacho vijana wengi duniani wakafikia hatua ya kuiga utamaduni wa Marekani katika mavazi, katika kutembea na pia hata watu wa daraja la kati wa nchi mbalimbali wakawa wanaiga staili za maisha za Wamarekani katika maisha ya kila siku ili waonekane kuwa wameendelea na hata katika lugha imekuwa hivyo hivyo.

Hiyo yote ni mikakati iliyosukwa kueneza ubeberu wa kiutamaduni.
Kupitia mkakati huo taifa la Marekani likaendelea kupata ushawishi katika maisha ya kila siku ulimwenguni na wakati huo huo wanamuziki, wacheza filamu na wanamitindo wa Marekani wakaendelea kunufaika kiuchumi kutokana na kazi zao kuwa na ushawishi kwa watu wengi duniani na kuwa soko la shughuli zao huku pia taifa la Marekani likiingiza fedha nyingi.

Hapa Afrika, Nigeria na Afrika Kusini zinakuja kwa kasi katika kutumia tasnia ya filamu na muziki kueneza utamaduni wao hapa Afrika na kuwa na ushawishi. Tanzania haiwezi kuendelea kubaki nyuma.

Vilevile, katika kulenga kuitumia nafasi ya kidiplomasia kukuza uchumi wetu; serikali ijayo ya Ukawa itaandaa sera maalumu kati ya Tanzania na nchi au kanda mbalimbali ambazo ni muhimu kimkakati kama Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU), Tanzania na nchi za Asia Mashariki (SEATO), Tanzania na nchi za Ukanda wa Pacific, Tanzania na Mashariki ya Kati na pia Sera ya Tanzania katika ushirikiano wake na mtangamano wa kikanda (regional Intergration) kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), SADC na katika njia ya kuelekea (roadmap) katika Umajumui wa Afrika (Pan-Africanism) kupitia dhima ya Tanzania kwa Umoja wa Afrika (AU).

Ni kupitia mikakati hii tutakapoweza kutumia utalii wetu kukuza uchumi, pia kulinda rasilimali za nchi yetu na kukomesha uporwaji wa rasilimali za taifa letu.
Kwa mfano, Tanzania ina uhusiano na baadhi ya nchi ambazo sio wazalishaji wa vito vya Tanzanite lakini nchi hizo ndio wauzaji wakubwa wa Tanzanite duniani kuliko mzalishaji wake halisi Tanzania. Kama Balozi zetu zingekuwa makini hali hii ingerekebishwa.

Kuna nchi ambazo korosho ya Tanzania imeuzwa kwenye soko la kimataifa kuliko Tanzania wakati wazalishaji halisi ni Tanzania. Haya yote ni kutokana na serikali yetu kutokuwa makini katika diplomasia ya uchumi.

Teuzi za mabalozi wetu nje zimekuwa teuzi za kulipa fadhila badala ya teuzi zinazozingatia taaluma. Tuna mabalozi na wanadiplomasia wasioifahamu sera iliyopo na pia hawaelewi maana ya diplomasia ya uchumi. Wanadhani kuiwakilisha Tanzania nje ni kushiriki dhifa za kitaifa wanazoalikwa na viongozi wa nchi wenyeji na kutoa visa kwa raia wa kigeni kuja Tanzania tu basi.

Serikali ijayo ya Ukawa itazingatia weledi katika teuzi za mabalozi na maofisa wa balozi zetu nje. Ni lazima idara muhimu ya Usalama wa Taifa ihusishwe kikamilifu katika teuzi za maofisa hawa. Ni lazima tuzingatie taaluma na uzoefu katika nyanja za uchumi, biashara, uhandisi na intelijensia ya uchumi ili tuweze kubadili mfumo wa ushirikiano kati ya Tanzania na jamii ya kimataifa.

Teuzi ni lazima zizingatie msingi mkuu wa uadilifu na uzalendo. Watanzania waliowahi kwenda nje ya nchi na waliopo watakubaliana name kuwa mabalozi wetu wengi na baadhi yao maofisa wa ubalozi wamepoteza uzalendo na hadhi ya kutumikia nafasi zao.

Watanzania waliopo nje hawaoni ofisi za balozi zao kama nyumbani kwao kutokana na jeuri, viburi na manyanyaso wanayopewa na baadhi ya maofisa wa ubalozi kinyume na ilivyo kwa nchi nyingine. Wafanyabiashara wanaofanya biashara za nje hawapewi ushirikiano wa kutosha kutoka ofisi za ubalozi wa Tanzania. Hii yote ni kutokana na balozi zetu kujaza maofisa wasiokuwa na uzalendo, wavivu, wazembe na wabinafsi waliopindukia huku wakilipwa kwa kodi za Watanzania. Hatuwezi kuendelea kwa namna hii, tutaishangaza dunia.

Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi maarufu kama wana-diaspora wanaweza kuwa mabalozi wetu wazuri kiuchumi ikiwa mikakati thabiti itawekwa. Watu hawa wana mchango mkubwa sana katika maendeleo ya nchi yetu kiuchumi hasa katika sekta ya elimu, afya na nyinginezo, Watanzania hawa wanaofanya kazi au biashara wamekuwa wakitafuta fursa za kuwekeza nchini na kurudisha nyumbani walichovuna nje na pia kuwasaidia ndugu zao.
Kwa mfano nchi kama Nigeria mwaka 2013 wana-diaspora (Wanigeria waishio nje ya nchi) walirudisha kati ya dola za Marekani bilioni tano hadi 10 kwa mwaka yaani zaidi ya trilioni 10 na 20 kwa fedha za Kitanzania ambazo zinakaribiana na bajeti yetu ya mwaka 2014/2015.

Tanzania inapaswa kufuata nyayo hizi kwa kuwapa wana-diaspora umuhimu mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa letu.
Pia serikali mpya ya Ukawa itatetea haki za binadamu, usawa wa nchi na kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika diplomasia ya kimataifa. Tanzania haitakubali kufumbia macho ukandamizaji wa haki za binadamu na itasimama kidete kupitia nafasi yake kulinda ustawi wa demokrasia, utawala bora na kutetea haki za binadamu kwa kuwa tunaamini dunia ni yetu sote na hakuna mwenye haki ya kukandamiza haki ya mwingine.

Tutasimama kidete kusimamia misingi ya uanzishwaji wa Umoja wa Afrika, Mkataba wa Uanzishwaji wa Umoja wa Mataifa (UN Charter) kama ambavyo Tanzania chini ya Mwalimu Julius Nyerere ilivyofanya katika medani za kimataifa.

Ni katika misingi hii, tutaheshimu ujirani mwema, kulinda na kuheshimu mikataba na majukumu ya kimataifa (International Obligation) ambayo Tanzania iliridhia.

Tutaimarisha Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kudai mabadiliko ya mfumo ili kuleta usawa wa nchi shiriki. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN Security Council) lina changamoto ambazo tumekua tukizipigia kelele hasa juu ya upanuzi wa wigo wa kidemokrasia na utendaji wake unaozingatia maslahi ya wachache na hivyo kubeba ajenda za mataifa yenye nguvu kuamua juu ya masuala mazito ya dunia. Amani ya dunia imewekwa rehani kwa mataifa haya matano tu.

Naomba nimalizie kwa leo, kwa kuwataka wasomaji wangu na Watanzania kwa ujumla mtafakari sana siku ya leo tunapoadhimisha miaka 16 ya kifo cha Baba wa Taifa. Tunayo fursa ya kuirejesha Tanzania inayojisikia fahari na itakayotembea kifua mbele miongoni mwa mataifa na pia raia wenye ujasiri wa kujitambulisha kuwa Watanzania miongoni mwa raia wa mataifa mengine.

Kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015, tunayo fursa kupitia sanduku la kura kumchagua Rais atakayesimamia kuirejeshea Tanzania nafasi yake kimataifa na kuwanufaisha Watanzania kupitia nafasi ya Tanzania kimataifa.

Ni hatari sana kuendelea na uongozi na mfumo wa chama tawala, CCM, ulioporomosha heshima ya taifa letu mbele ya uso wa dunia. Kwa bahati mbaya, CCM wamemsimamisha mgombea John Magufuli ambaye ameonyesha upeo mdogo sana katika masuala ya kimataifa. Ndio maana sikuona ajabu kuona akimtaja Rais wa zamani wa Iraq Saddam Hussein, kama Rais wa Kuwait mbele ya mkutano wa hadhara.

Sikushangaa zaidi alipoonyesha upeo mdogo kwa kutaja kuwa Muammar Ghaddafi wa Libya aliondolewa madarakani na wananchi wa Libya wakati Watanzania na hata dunia inajua kuwa Muammar Ghaddafi aliondolewa kwa njama za mataifa ya nje kupitia azimio namba 1973 la Baraza la Umoja wa Mataifa, lililoweka zuio la kuruka kwa ndege za kivita (no-fly zone) na kusababisha Majeshi ya Kujihami ya Marekani na Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia Libya. Ndiyo maana hapo juu nimegusia umuhimu wa kupanua wigo wa kidemokrasia ndani ya Umoja wa Mataifa. Haya ya Libya yasingefanyika kama kungekuwa na haki tunayoipigia kelele ndani ya Umoja wa Mataifa.

Magufuli bila haya au kutokana na kutoelewa masuala ya kimataifa haoni kuwa Serikali ya Tanzania ilikuwa na fursa ya kuitetea Libya kupitia Umoja wa Afrika na au Balozi wake wa kudumu kule Umoja wa Mataifa. Ni kutokana na Tanzania kupoteza imani kimataifa ndio maana imekosa ujasiri wa kupaza sauti kama Tanzania ya Nyerere ilivyokuwa mstari wa mbele kutetea haki na kulinda amani ya dunia.

Naamini Serikali ya Chadema itakayoundwa kwa ushirikiano wa vyama washirika wa Ukawa itairudishia Tanzania ujasiri wake wa awali. Edward Lowassa ambaye anatazamia kushinda Uchaguzi Mkuu kwa bahati nzuri ana uzoefu mkubwa kimataifa na hadi Bunge lilipovunjwa alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje. Kutokana na ufinyu wa nafasi, naomba kuishia hapa kwa leo. Tukutane Jumatano ijayo Mungu akipenda.

Mwandishi wa makala haya ni Ben Saanane,Ni Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti CHADEMA anapatikana kwa namba 0768078523.

- See more at:
Raia Mwema - Ukawa tutarejesha heshima ya Tanzania kimataifa
 
Ukawa tutarejesha heshima ya Tanzania kimataifa

Toleo la 427
14 Oct 2015
Na Ben Saanane


Itakuwa hatari sana kumchagua Rais mwenye upeo mdogo kimataifa. Rais asiyejua hata Saddam Hussein alikuwa Rais wa nchi gani? Anasema hadharani kwa ujasiri kuwa alikuwa Rais wa Kuwait? Yaani kama hajui mtu maarufu wakati wa vita ya Marekani na Iraq, Saddam Hussein alikuwa Rais wa nchi gani ataelewa nini kuhusu sera ya Tanzania Mashariki ya Kati na Bara Asia? Kweli ataweza kuirejesha heshima ya Tanzania ya Mwalimu Nyerere katika ramani ya dunia? Ataelewa nini kuhusu diplomasia ya uchumi?

Mwandishi wa makala haya ni Ben Saanane,Ni Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti CHADEMA anapatikana kwa namba 0768078523.


- See more at: Raia Mwema - Ukawa tutarejesha heshima ya Tanzania kimataifa

Asante Mkuu kwa Makala.
Ila na sikitika kumfikiria Magufuli na urejeshwaji wa Heshima ya Tanzania kwa level ya Nyerere.
Magufuli hata level ya Jakaya Mrisho Kikwete hataifikia na itashuka kuliko ilivyo sasa.

Hivi kweli inakuingia akilini mtu mzima kwenye mkutano wa Kampeni kuwaelezea Umma namna ya kuondokana na umaskini wewe unawapigia push up! Uko nje unadhani watamchukulia vipi?



 
Asante Mkuu kwa Makala.
Ila na sikitika kumfikiria Magufuli na urejeshwaji wa Heshima ya Tanzania kwa level ya Nyerere.
Magufuli hata level ya Jakaya Mrisho Kikwete hataifikia na itashuka kuliko ilivyo sasa.

Hivi kweli inakuingia akilini mtu mzima kwenye mkutano wa Kampeni kuwaelezea Umma namna ya kuondokana na umaskini wewe unawapigia push up! Uko nje unadhani watamchukulia vipi?

Ha ha ha! Yaani hata niliona aibu kuandika jina lake katika makala ile
 
Hongera sana Mkuu. Naishiria kusema juhudi zako ni mchango mkubwa kwa maendeleo ya watanzania wote wenye kusoma hoja na makala zenye mishiko kwani hukusita kutoa michango yenye kuuweka uwazi katika yale yote yanayo hitajika katika kulijenga" UPYA " Taifa hili la Tanzania. " Aluta Continua"
 
Back
Top Bottom