Makala Raia Mwema Ughaibuni: Kelele za kujivua gamba CCM ni moto wa karatasi

Mzalendo_Mwandamizi

JF-Expert Member
Dec 12, 2007
1,117
4,764
Raia Mwema Ughaibuni
Nakala chapishi
Mtumie mwenzio
Jiandikishe utaarifiwe

Kelele za kujivua gamba CCM ni moto wa karatasi

Evarist Chahali, Uskochi Mei 18, 2011


Punde tu umeshazimika

BAADA ya majigambo na kelele za huku na kule, hatimaye, "moto wa karatasi" wa CCM kujivua magamba, umezimika. Umezima sio kwa maji au upepo; bali umefifia na kuzimika wenyewe.

Pengine kuzimika kwa moto huo ni matokeo ya namna ulivyopokelewa na umma. Sio siri kwamba licha ya jitihada kubwa zilizofanyika kutangaza "kuzaliwa upya kwa CCM baada ya chama hicho kujivua magamba", Watanzania wengi walionyesha wasiwasi kama hiyo sio sehemu tu ya ‘usanii wa kisiasa' wa chama hicho kikongwe.

Wasiwasi kuhusu hatua hiyo ya CCM ilichangiwa zaidi na ukweli kwamba, kimsingi, tatizo la CCM halikuwa kwenye ngozi au magamba yake; bali ndani kabisa ya mwili wa chama hicho kinachotumia muda mwingi kujitetea kuliko kuwatumikia wananchi.

Baadhi ya watu walikwenda mbali zaidi na kuichambua kauli ya ‘kujivua magamba' wakitumia mfano halisi wa viumbe wenye tabia ya kujivua magamba; hususan nyoka.Walidai kuwa kwa kawaida nyoka anapojivua magamba anakuwa hatari zaidi kuliko kabla ya tendo hilo.

Wengine walikejeli kauli hiyo ya CCM kwa kubainisha kuwa nyoka anapojivua gamba hageuki kuwa mjusi; bali anaendelea kuwa nyoka.Yayumkinika kuamini kuwa hata kabla moto wa kujivua magamba haujazimika, kuna baadhi ya viongozi wa chama hicho waliotambua kuwa kauli hiyo (ya kujivua magamba) ilikuwa feki.

Kilichowakwaza wengi kuiamini CCM ni ukweli kwamba ustawi wake kwa sasa unategemea sana magamba hayo hayo iliyodai inayaondoa.Na mfano hai na sahihi kabisa ni jinsi Mwenyekiti wa sasa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alivyofanikiwa kuingia madarakani.

Asiyejua namna baadhi ya viongozi wa chama hicho wanaotajwa kama magamba walivyomsaidia Kikwete kupata urais mwaka 2005, atakuwa anaishi sayari nyingine.

Tupo wengine tulioenda mbali zaidi na "kumchimba" mwasisi wa wazo la kujivua magamba; yaani Kikwete.Tulijaribu kuangalia harakati zake za kupata urais, kuanzia jaribio lililoshindikana mwaka 1995 hadi alipofanikiwa kuingia Ikulu mwaka 2005. Kimsingi, kipindi hicho ni muhimu sana katika kuelewa baadhi ya mambo yanayoendelea hivi sasa; hususan suala la ufisadi.

Kama ni kwenye kilimo, basi, kipindi hicho kilikuwa mithili ya msimu wa kupanda mbegu shambani. Na tunachoshuhudia sana ni mavuno. Japo ili mwanasiasa afanikiwe kuingia Ikulu anapaswa kuunda mtandao mpana na wenye nguvu, kwa bahati mbaya (au makusudi) mtandao ulioundwa na Kikwete ulijumuisha pia watu wenye wasifu usiopendeza.

Kama tunavyofundishwa kwenye sosholojia kuwa mara nyingi mahusiano kati ya binadamu ni ya mtindo wa "ninakupa ili nawe unipe". Wengi wa waliochangia katika jitihada za kumwingiza Kikwete Ikulu wamejipa uhalali wa "kuchukua chao" katika kila upenyo unaojitokeza.

Kwa mantiki hiyo, CCM wanaweza kuwa sahihi kabisa kutumia kauli ya kujivua magamba; kwani hata kwa baadhi ya mimea inafika mahala inamlazimu mkulima kuchuna magamba, sio kwa minajili ya kuupendezesha mmea; bali kufanya ushamiri zaidi.

Lakini si kila mmea unaoweza kuendelea kuwa hai ukichunwa magamba. Katika elimu ya viumbe, gamba la mmea ni sawa na ngozi katika mwili wa viumbe (mfano binadamu).Ukimchuna ngozi mwanadamu utakuwa unahatarisha uhai wake na pengine kusababisha kifo chake.

Kadhalika, miongoni mwa madhara yanayotokana na ngozi ya binadamu kuchunwa ni pamoja na maambukizi ya vimelea vya magonjwa. Katika harakati zake za kujivua magamba, CCM imejikuta ikikumbwa na tatizo kama hilo ambapo kuondoka kwa watu kama Yusuf Makamba kumesababisha ujio wa watu kama Nape Nnauye.

Jina la Nape lilianza kuvuma baada ya kauli zake ambazo kwa namna fulani ungeweza kudhani zinatoka kwa mwanasiasa wa chama cha Upinzani. Napenda kukiri kwamba nilikuwa miongoni mwa watu waliomwamini sana kijana huyo; kwani kauli zake zilishabihiana na wazalendo wengine wenye uchungu wa nchi yao.

Sasa, kama ilikuwa ni gea yake tu ya kusaka umaarufu au alikuwa akiamini kwa dhati alichokuwa anasema,hilo ni suala jingine. Lakini kilicho bayana ni ukweli kwamba kauli hizo za kizalendo; hususan msimamo wake ulioonekana thabiti kukemea ufisadi ulisababisha aingie kwenye tsunami ya kisiasa kabla ya kuibuka na "ulaji" alipoteuliwa na Kikwete kuwa Mkuu wa Wilaya.

Baada ya kukabidhiwa ukatibu mwenezi wa CCM, Nape ameibuka kama kamanda wa kuwaaminisha Watanzania kuwa, hatimaye, chama hicho kimeamua, kwa gharama yoyote ile, kuachana na baadhi ya viongozi wake muhimu lakini wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Haikuwa vigumu kuhisi kuwa licha ya kutekeleza wajibu wake kama msemaji wa Chama, Nape pia alikuwa akisukumwa na kinyongo dhidi ya baadhi ya wanasiasa waliomsababishia matatizo makubwa ya kisiasa huko nyuma.

Binafsi, naamini kuwa Nape alikuwa na imani kubwa kuwa chama chake kimedhamiria kwa dhati kujivua magamba. Alipita huku na kule kusisitiza kuwa watuhumiwa wa ufisadi wana siku 90 tu za kuwajibika wenyewe; vinginevyo watawajibishwa .

Kuna msemo wa Kiingereza unaotahadharisha kutoweka hisia mbele ya akili (putting emotions in front of common sense). Kwamba alikabidhiwa rungu huku taarifa zikieleza kuwa ana sapoti ya bosi wake Kikwete, Nape akapuuza busara kwamba kamwe haiwezekani kukata tawi ulilokalia au mkono unaokulisha.

Kama alikuwa anasukumwa na uzalendo au kiu ya kulipa kisasi, kijana huyo akafumbia macho ukweli kuwa wanasiasa anaowaandama ni sehemu muhimu ya uhai wa Kikwete kisiasa.

Ni watu wanaomjua kiundani, na yayumkinika kuamini kuwa wana siri muhimu za mkuu huyu wa nchi; hususan katika ushiriki wao katika mtandao uliomwingiza Kikwete madarakani mwaka 2005.

Lakini kabla ndoto za Nape kuona magamba yanaondoka hazijatimia, tukasoma taarifa katika baadhi ya magazeti kuwa mmoja wa "wabaya" wa Nape alikutana kwa faragha na Kikwete. Siku chache baadaye, Katibu Mkuu wa CCM,Wilson Mukama akaweka bayana msimamo wa chama chake kuwa hakuna kiongozi yeyote aliyepewa siku 90 kuwajibika.

Kwa lugha nyingine, Mukama alizika rasmi kauli ya CCM kujivua magamba, na hivyo ‘kumkata maini' Nape na watu wote walioanza kuamini kuwa chama hicho kimeamua kuivunja ndoa yake ya mkeka na mafisadi.

Badala ya kutulia na kusoma mwelekeo wa upepo, Nape akaamua kuhamishia machungu yake ya "kuingizwa mkenge katika suala la kujivua magamba" kwa chama kikuu cha Upinzani - CHADEMA. Akadandia hoja iliyokwishatolewa maelezo na CHADEMA kuhusu mshahara wa katibu wake mkuu, Dk. Willibroad Slaa na ununuzi wa magari (yaliyotumika) ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe. Akajaribu kuwahadaa Watanzania kuwa Dk. Slaa naye ni fisadi kwa vile analipwa mshahara mkubwa.

Naamini Nape anazungumza hayo kwa hasira tu za kubaini ameingizwa mkenge katika suala la kujivua magamba lakini anaelewa bayana kuwa hata katika zama za Ujamaa, haikuwa dhambi kulipwa mshahara mkubwa halali.

Watanzania hawana matatizo na mshahara wa Dk. Slaa kama anawatumikia kwa uadilifu. Kila Mtanzania anajua kuwa kelele za Dk. Slaa na CHADEMA zinasaidia sio tu kuikumbusha CCM wajibu wake; bali pia zimesaidia kumsukuma Kikwete kuchukua hatua katika utatuzi wa matatizo ya wananchi kama vile bei ya sukari.

Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha CCM kuwa kamwe haiwezekani kutatua tatizo kwa kulikwepa.Ugonjwa hautibiki kwa kujidanganya kuwa haupo mwilini.CCM wanafahamu fika kuwa tatizo la msingi lipo kwa Kikwete.

Ni yeye aliyeletwa na kuwalea hao wanaoitwa magamba (mafisadi). Anaweza kuzungumza hadharani kuwa anataka kuua vimelea vyote vya ufisadi, lakini nafsi itamsuta kuwageuka watu waliomfikisha alipo sasa.

Blogu: chahali.blogspot.com

CHANZO: Raia Mwema
 
"hata katika zama za Ujamaa, haikuwa dhambi kulipwa mshahara mkubwa halali."

Nimekapenda kweli haka kamstari!!!!
 
Back
Top Bottom