Elections 2010 Makala Ndani ya Raia Mwema Kuhusu Maslahi ya Umma

Mzalendo_Mwandamizi

JF-Expert Member
Dec 12, 2007
1,117
4,764
RAIA MWEMA UGHAIBUNI



Maslahi ya umma ni zaidi ya vyote


Evarist Chahali
Agosti 11, 2010

MARA ya mwisho makala zangu kuonekana katika jarida hili ilikuwa katikati ya Juni mwaka 2008. Nilipokea barua pepe na sms nyingi kutoka kwa baadhi ya wasomaji wa Raia Mwema wakihoji kwanini niliacha kuandika safu yangu ya Raia Mwema Ughaibuni.

Miaka miwili baadaye nimeonelea ni vema nikaufahamisha umma (kwa kifupi) kilichonisibu hadi kufikia uamuzi huo mgumu wa kusitisha uandishi wa makala. Kwa hakika haikuwa uamuzi wangu kwa vile nililazimishwa na aliyekuwa mwajiri wangu kuacha mara moja uandishi wa makala. Kosa langu kuu (kwa mtizamo wa mwajiri wangu) lilikuwa kukemea ufisadi.

Makala iliyosababisha mwajiri wangu kunipiga stop uandishi wa makala ilikuwa ikichambua habari kwamba baadhi ya viongozi wa CCM walikuwa wakiwakemea wenzao waliotaka wahusika katika utapeli wa Richmond wawajibishwe. Katika makala hiyo niliwakumbusha watetezi hao wa mafisadi umuhimu wa kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi yao binafsi au ya maswahiba wao.

Nilitoa pia tahadhari kwamba (nanukuu) "CCM inaweza kuwadanganya Watanzania wachache kwa muda fulani kwamba tuhuma za ufisadi dhidi ya baadhi ya viongozi wake ni uzushi tu. Inaweza pia kuwadanganya Watanzania wote kwa muda fulani kwamba masuala ya Richmond, EPA na maskandali mengine ni porojo tu za kisiasa. Lakini kamwe haiwezi kuwadanganya Watanzania wote kwa muda wote kwamba chama hicho si kichaka kinacholea mafisadi"

Kadhalika niliitahadharisha CCM kwamba (nanukuu tena) "...haiwezi kuudanganya umma wa Watanzania kwamba waliolazimika kujiuzulu kutokana na kuhusishwa kwao na utapeli wa Kampuni ya Richmond walifanya hivyo kulinda maslahi ya Taifa. CCM isiwafanye Watanzania ni wajinga kiasi hicho wakati wanakumbuka vizuri jitihada zilizokuwa zikifanyika kila vilipojiri vikao vya Bunge kuhakikisha kuwa suala la Richmond halijadiliwi katika chombo hicho cha kutunga sheria".

Makala hiyo iliwachukiza sana mabosi wangu huku wakinituhumu kuwa nimewatukana viongozi wa chama tawala ambacho ndicho kilichounda serikali niliyokuwa nikiitumikia. Makala hiyo "ilitonesha kidonda" kilichosababishwa na makala nyingine niliyoandika mwaka 2006 (sio katika jarida hili) kuonya kuhusu tabia ya viongozi wa CCM kuitisha vikao vya wabunge wake kwa minajili ya kuandaa mikakati ya kuwa na msisamo wa pamoja kwenye mijadala yenye maslahi ya kitaifa. Niliandika makala hiyo baada ya kusoma habari kwamba Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa alipanga kukutana na wabunge wa CCM ili kuandaa mkakati wa kuzima hoja ya utata wa mkataba wa uzalishaji umeme uliohusisha kampuni ya kitapeli ya Richmond.

Katika sakata hilo la awali, bosi wangu mmoja alinipigia simu kuhoji kama niko Uingereza kusoma au kukosoa Serikali? Kisa cha swali hilo ni hiyo makala ambayo japo sina taaluma ya utabiri lakini niliyoyaandika ndiyo yaliyotokea miaka miwili baadaye ambapo Lowassa alilazimika kujiuzulu kutokana na sakata la Richmond.

Wakati nahukumiwa kwa makala hiyo ya mwaka juzi mabosi wangu hawakutaka kutupia macho ukweli kwamba makala niliyoandika 2006 ilizungumzia mambo ya msingi ambayo yalijidhihirisha miaka miwili baadaye. Badala yake, mabosi hao walikumbushia onyo walilonipa mwaka huo (2006) la kutoikosoa serikali na chama tawala.

Ninakiri kuwa makala yangu ya Juni 2008 ilikiuka onyo hilo lakini si kwa vile mie ni kiburi bali kwa sababu nilishindwa kujizuia kunyamaza huku mambo yakizidi kwenda mrama. Ni dhahiri kuwa laiti walionipa onyo hilo wangetimiza wajibu wao vizuri wala nisingekuwa na hoja ya kuandika dhidi ya ufisadi au watetezi wa ufisadi.

Nafahamu bayana kuwa uamuzi wangu wa kurejea kuandika safu hii utazua mengi, pengine zaidi ya yaliyonikumba mwaka juzi. Lakini kwa sisi Wakristo tunafundishwa kuwa mwenye haki ataanguka saba mara sabini lakini mwishowe atasimama.

Kwa vile siandiki kwa kutafuta sifa, maslahi au kumridhisha mtu au kikundi fulani, naamini Mwenyezi Mungu ataniongoza na kunilinda katika jukumu hili nililojikabidhi la kuwasemea wanyonge na walalahoi.

Haikuwa rahisi kwangu kukaa kimya katika kipindi hicho cha miaka miwili huku nikishuhudia kila aina ya madudu ya kukera na kusikitisha katika namna nchi yetu inavyopelekwa kusikostahili.

Pengine utajiuliza nimepata wapi ujasiri huu ambao yayumkinika kuamini utapelekea usumbufu mkubwa kwangu na kwa watu wangu wa karibu. Naamini ninachofanya ni kuwasaidia, kwa upande mmoja, hao waliokuwa wakikerwa na makala zangu japo kimsingi zilikuwa zikiwarahisishia kazi zao za kila siku, na kwa upande mwingine, ni kuweka mbele maslahi ya Taifa badala ya maslahi yangu binafsi.

Mwandishi mmoja aliyekuwa akifahamu masahibu yaliyonipata alinifahamisha kuwa hata yeye na wenzake walikuwa wakikumbana na kila aina ya vitisho kwa vile tu wanaandika yasiyowapendeza "wenye milki ya keki ya taifa".

Alinishauri kutokuogopa vitisho nilivyokuwa napewa bali vitisho hivyo viwe changamoto zaidi kwangu kukemea kwa nguvu zaidi maovu mbalimbali katika jamii. Japo sikuweza kufuata ushauri wake kwa wakati huo, lakini maneno yake yaliendelea kugonga kichwani mwangu kila niliposoma habari kuhusu ufisadi unavyozidi kuitafuna Tanzania yetu.

Katika miaka miwili hiyo nilikuwa najiona kama msaliti kwa nchi yangu kwamba nimeacha kuandika kwa vile tu nimetishwa na kufungwa mdomo kwa ajili ya maslahi ya wachache wanaotumia nguvu za dola kuwalinda wahalifu basi inabidi nami nikae kimya.

Sikuwahi kumtukana mtu wala sikuwahi kuandika makala kwa minajili ya kumpendezesha mtu fulani. Makala zangu zilisimamia ukweli na hali halisi. Zote ziliongozwa na uchungu wa dhati na uzalendo nilionao.

Kwa sababu za kisheria na kimaadili sintoweza kuelezea kinagaubaga kuhusu masahibu niliyokumbana nayo katika "awamu ya kwanza" ya makala zangu zilizotengeneza safu hii. Nataraji nitaweza kukabili zahma zote zitakazonikabili baada ya kuamua kuendeleza "libeneke" hili la makala. Kwa upande mmoja najipa matumaini kuwa busara itatawala katika "kuhukumu" safu hii na makala zangu kwa ujumla. Kwa upande mwingine, naamini kuwa kukaa kimya si ufumbuzi wa matatizo lukuki yanayoikabili nchi yetu.

Ni dhahiri nchi yetu isingekuwa huru laiti Mwalimu Julius Nyerere na wenzake waliopigania uhuru wangeendekeza vitisho vya mkoloni dhidi ya harakati zao za kumkomboa Mtanzania.

Japo baadhi ya watu wanahoji mantiki ya uhuru tuliopata mwaka 1961 wakihusisha namna kikundi kidogo cha mafisadi kinavyoitafuna nchi yetu kama mchwa, ukweli unabaki kuwa tuko huru japo baadhi ya wenzetu wanafanya kila wawezalo kuturejesha kwenye-na kuendeleza-aina mpya ya ukoloni yaani ufisadi.

Na ni kwa mantiki hiyo nami naamini kuwa nitakuwa msaliti wa daraja la kwanza iwapo nitaendekeza vitisho na usumbufu niliopata kwa vile tu nilikuwa naandika kisichowapendeza watu flani. Watakaochukizwa na makala zangu wachukie tu lakini siwezi kukaa kimya wakati nchi yetu inazidi kusukumwa isikopaswa kwenda.

Ni muhimu kwa kila Mtanzania kutambua kwamba maslahi binafsi na ya kisiasa hayapaswi kuwa mbele ya maslahi ya nchi. Tusiporekebisha mwenendo wa mambo sasa tutaishia kulaumiana mbele ya safari wakati ambapo hatutokuwa na fursa ya kuzoa maji yaliyokwisha kumwagika.

Profesa Kighoma Malima (sasa marehemu) aliwahi kutufundisha kuwa haki haiombwi bali inadaiwa. Makala hii na zijazo zitakuwa mwendelezo wa kudai haki zetu za msingi na kukumbushana wajibu wetu badala ya kutegemea ridhaa ya watu wachache wanaolinda maslahi yao binafsi.

Barua-pepe: epgc2@yahoo.co.uk

Blogu: chahali.blogspot.com


CHANZO: Raia Mwema
 
Back
Top Bottom