Makala ndani ya RAIA MWEMA: CCM na Joka Lenye Vichwa Vitatu

Mzalendo_Mwandamizi

JF-Expert Member
Dec 12, 2007
1,117
4,764
RAIA MWEMA UGHAIBUNI

CCM na joka lenye vichwa vitatu!


Evarist Chahali, Uskochi
Aprili 20, 2011
Litasalimika viwili vikikatwa?
MARA baada ya kupata taarifa kuhusu mabadiliko ndani ya CCM kwenye vikao vyake hivi karibuni vya mjini Dodoma, niliandika makala katika blogu yangu na kuipa kichwa: Joka lenye vichwa vitatu linaweza kusalimika likikatwa vichwa viwili?”

Katika makala hiyo nilijaribu kuwakumbusha wasomaji jinsi CCM ilivyofika mahala ilipo sasa hadi kulazimika kuchukua uamuzi wa “kujivua magamba”. Baadhi ya wafuasi wa chama hicho wanaweza kabisa kutetea kwa kudai yaliyopita si ndwele tugange yaliyopo na yajayo.

Lakini sote tunafahamu busara inayotuasa kutoangalia tulipoangukia bali tulipojikwaa. Ili jaribio la CCM kujivua magamba lifanikiwe kuzaa matokeo yanayotarajiwa, ni muhimu kwa chama hicho kutafakari kwa makini imekuwaje hadi kikapata magamba hayo. Maana; pasipo kufanya hivyo kuna uwezekano baada ya muda mfupi chama hicho kikajikuta kikilazimika sio tu kujivua tena magamba bali safari hii kujichuna ngozi kabisa.

Asili ya magamba

Mara baada ya jina lake kutopitishwa kuwa mgombea wa CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, mwanasiasa Jakaya Kikwete alianza harakati za makusudi kuhakikisha kuwa dhamira hiyo inatimia katika chaguzi zijazo kwa gharama yoyote ile.

Kikwete akaunda timu ya ushindi iliyowajumuisha maswahiba wake Edward Lowassa na Rostam Aziz.Watu hawa wawili walikuwa viungo muhimu kwa ushindi wa Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Wanaowajua vema wanawaelezea “utatu” wa wanasiasa hao kwa mlolongo huu: Lowassa - mwanasiasa haswa (simaanishi kuwa ni mwanasiasa mwadilifu),Rostam -bwana fedha, na Kikwete - mtawala.

Wajuzi wa “siasa chafu” wanaeleza kuwa ushirikiano huo wa watu hawa watatu ulitumia kila aina ya mbinu kuhakikisha Kikwete anaingia Ikulu hapo 2005.Na ikawa hivyo; hasa baada ya viongozi hao wakuu wa "mtandao" kufanikiwa kupenya takriban kila kundi la jamii - kutoka viongozi wa dini hadi wakuu wa taasisi za dola, kutoka wanahabari hadi wasanii.Kadhalika kundi hilo lilifanikiwa kudhoofisha upinzani ndani na nje ya CCM kwa kile wanachoita Waingereza “character assassination”.

Na kwa vile siasa zetu zinategemea sana haiba ya mgombea; hata kama hana sifa za kutosha, mkakati huo wa kuwachafua wale wote walioonekana kama vikwazo kwa Kikwete kuingia Ikulu ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa “kuwamaliza” baadhi ya wanasiasa kama vile Dk. Salim Ahmed Salim aliyezuliwa tuhuma za u-Hizbu.

Baada ya kushinda uchaguzi huo, Kikwete alimteua rafiki yake Lowassa kuwa Waziri Mkuu huku Rostam akibaki kuwa mwanasiasa mwenye nguvu pengine kuliko yeyote ndani ya chama hicho. Inaelezwa kuwa Lowassa alitoa mchango mkubwa katika kutengeneza Serikali ya Awamu ya Nne.

Inaelezwa pia kuwa japo wote wawili (Kikwete na Lowassa) walishashika nyadhifa mbalimbali serikalini kabla ya uchaguzi huo wa mwaka 2005, Lowassa alikuwa amejijenga zaidi kiuchumi na kisiasa ukilinganisha na Kikwete.

Kadhalika-na hapa nafafanua kwanini niliandika hapo juu kuwa Lowassa ni mwanasiasa haswa (japo simaanishi ni mwanasiasa mwadilifu) - ni ukweli kuwa Lowassa ana ushawishi wa kisiasa zaidi ya Kikwete.

Japo wote wawili ni wapenda umaarufu (populists),wakati Kikwete amekuwa akitumia zaidi turufu ya "tabasamu la muda wote" na "kuwa karibu na watu", Lowassa amekwenda mbali zaidi na kujifanya anayafahamu kwa undani matatizo ya wananchi na kuyatolea ufumbuzi mapema (na ndio maana licha ya kulazimika kujiuzulu kutokana na ufisadi wa Richmond bado kuna wanaomwona kama mwajibikaji).

Kwa kifupi,wakati Lowassa ni mwepesi wa kuchukua maamuzi (hususan yale yatayopelekea yeye kuonekana kama "Sokoine fulani hivi"), Kikwete ni mzito wa maamuzi (huku ikidaiwa kuwa uzito huo wa maamuzi unatokana na yeye kutojua vipaumbele vyake).

Inaaminika kuwa Lowassa na Rostam wana ufuasi mkubwa ndani ya CCM na serikalini kwa ujumla. Kwa mujibu wa wajuzi wa mambo, sababu kuu ya nguvu na ushawishi wao ndani ya chama hicho ni uwezo wao mkubwa wa kifedha. Inaelezwa kwamba wanasiasa hao wamewasaidia viongozi mbalimbali wa CCM kiuchumi na kuwawezesha kupata madaraka waliyanayo sasa.

Kadhalika, wakiutumia vyema uswahiba wao na Kikwete, inadaiwa kuwa waliweza kutengeneza "mtandao ndani ya mtandao"; kwa maana ya kuwaweka madarakani watu wenye utiifu kwao zaidi kuliko CCM au Kikwete.

Inaaminika kuwa wateuliwa wengi kwenye nafasi za kiserikali na kichama ngazi za mikoa na wilaya ni wafuasi wa Lowassa - kwa mfano ma-RC na ma-DC,na wenyeviti na makatibu wa CCM mikoani na wilayani.

Swali la muhimu la kujiuliza ni je; kuondoka kwa Lowassa na Rostam katika wadhifa mmoja kutapunguza nguvu na ushawishi wao kwa wafuasi wao,wengi wakiwa ni watu walio madarakani kutokana na fadhila zao?

Inazungumzwa na haijakanushwa kwamba mkakati wa Lowassa ni kumrithi Rais Kikwete atakapomaliza muda wake mwaka 2015. Kadhalika kumekuwa na tetesi za muda mrefu kwamba kuna “makubaliano” ya siri kati ya Kikwete na Lowassa kuwa wangepokezana uongozi maara baada ya Kikwete kumaliza miaka yake 10.

Japo suala la Richmond lilizua mfarakano wa aina fulani kati ya wawili hao, lakini ukweli unabaki kuwa "heshima" aliyotoa Kikwete kwa Lowassa kwa kutomtimua; bali kusubiri ajiuzulu mwenyewe iliwaacha wawili hao wakiendelea na urafiki wao; japo si kama ilivyokuwa mwanzoni.

Katika hali ya kawaida ya ubinadamu, Lowassa na Rostam wanaweza kabisa kuhisi kuwa Kikwete aliwatumia tu kwa manufaa yake binafsi ya kisiasa. Ni sawa na kile wanachoita Waingereza “used and abused”. Nasema hivyo kwa vile ni Kikwete huyu huyu ambaye katika kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita sio tu alipanda jukwaani kuwakampenia Lowassa, Rostam na (Andrew) Chenge; bali pia aliwatetea kwenye mkutano wake na waandishi wa habari akidai kinachowakabili wanasiasa hao ni tuhuma tu.Sasa kama ni tuhuma tu, kwanini basi leo wawe magamba; ilhali hakuna mahakama iliyowatia hatiani?

Sio kama ninawatetea wanasiasa hao; bali najaribu kutanabaisha kuwa kama Lowassa, Rostam na Chenge ni magamba yaliyopaswa kuvuliwa, basi, napata shida kuelewa kwanini Kikwete mwenyewe si sehemu ya tatizo hilo. Maana kama si yeye kutegemea fadhila zao, basi, leo hii CCM isingelazimika kujidhalilisha mbele ya umma kwa kulamba matapishi yake (yaani kufanya kile kile ilichokuwa ikikanusha kila kukicha kuwa chama hicho sio kichaka cha mafisadi).

Ni dhahiri kuwa kuondoa magamba; ilhali aliyesababisha magamba hayo anaendelea kuwepo kunaweza kusababisha tatizo kubwa zaidi ya magamba. Na kwa hakika magamba ambayo CCM haijafanikiwa kuyavua ni mfumo wa kifisadi ambao, licha ya kuwasaidia wengi wa viongozi wake kuingia madarakani, umeendelea kukiwezesha chama hicho kubaki chama tawala.

Rushwa iliyotawala kwenye mchakato wa kupata wagombea wa chama hicho kwenye uchaguzi uliopita haihusiani moja kwa moja na Lowassa au Rostam; bali mfumo wa kifisadi ambapo chama hicho “cha wakulima na wafanyakazi” kimegeuza uongozi kuwa bidhaa ya kununuliwa na kila mwenye uwezo wa kuhonga.

Wakati baadhi ya viongozi wapya wa chama hicho wakitangaza hadharani kuwa moja ya vipaumbele vyao ni kuwamaliza wapinzani, busara ndogo tu ingepaswa kutumika kuelewa kuwa vyama vya upinzani; hususan CHADEMA vimeisadia sana kuiamsha CCM kutambua kuwa inakoelekea sio kuzuri.

Lakini hilo sio tatizo pekee linalokikabili chama hicho.Ukiangalia mwenendo wa Spika wa Bunge, Anne Makinda anavyoliendesha Bunge kidikteta dhidi ya baadhi ya wabunge wa vyama vya upinzani (hususan wa CHADEMA), utabaini kuwa wengi wa viongozi wa CCM hawawajali wananchi na ndio maana wanawapuuza hata baadhi ya wawakilishi wa wananchi hao.

Lakini la muhimu kuliko yote ni manufaa kwa Watanzania kutokana na mabadiliko hayo ndani ya CCM. Kwa kifupi, ukiacha vichwa vikubwa vya habari kwenye magazeti yetu, mabadiliko hayo hayana manufaa yoyote kwa masikini wasio na hakika ya mlo wao wa kesho, wanafunzi wanaokaa sakafuni kwa uhaba wa madawati, akina mama wanaoletewa bajaj za kuwawahisha hospitali wakiwa wajawazito japo wabunge wanapewa mashangingi ya uheshimiwa,nk.

Magamba kwa Tanzania ni CCM yenyewe. Wanaweza kubadili ngonjera kutoka “maisha bora kwa kila Mtanzania” hadi “kujivua magamba” lakini anayezidi kuumia ni Mtanzania wa kawaida. Twende mbali zaidi ya kusherehekea matukio, na tuangalie faida ya matukio husika. CCM na ufisadi ni sawa na kobe na gamba lake; maana uking’oa gamba la kobe, basi, umemuua kiumbe huyo.


Blogu: Kulikoni Ughaibuni

CHANZO: Raia Mwema
 
Hii habari imeandikwa vizuri sana. Huu ndio ukweli. CCM wamelazimika kuwatimua ili kujiokoa lakini siri yao ni moja. Rushwa ni mfumo siyo watu watatu tu. Hata wakiwafukuza kabisa ccm haitakuwa salama.
 
Lowasa kama anajiamini yuko safi ajisalimishe hadharani na kukataa kashfa zinazomkabili nakutuambia ukweli wa ufisad wa Richmond na nyingnezo nani mhusika!
 
Hii habari imeandikwa vizuri sana. Huu ndio ukweli. CCM wamelazimika kuwatimua ili kujiokoa lakini siri yao ni moja. Rushwa ni mfumo siyo watu watatu tu. Hata wakiwafukuza kabisa ccm haitakuwa salama.

You can say it again!

Kama vichwa vitatu ni hao mafisadi wakubwa watatu basi nachelea kusema kuwa ina vichwa vingi mno, ila vitatu ndio vinaonekana!

Kama kwa tafsiri inaleta mantiki, basi CCM karibu asilimia 99%ni mafisadi na hivyo ni vichwa, vinaumana na kutafuta chance ya kula wengine zaidi!

Rushwa ni mfumo. period
 
You can say it again!

Kama vichwa vitatu ni hao mafisadi wakubwa watatu basi nachelea kusema kuwa ina vichwa vingi mno, ila vitatu ndio vinaonekana!

Kama kwa tafsiri inaleta mantiki, basi CCM karibu asilimia 99%ni mafisadi na hivyo ni vichwa, vinaumana na kutafuta chance ya kula wengine zaidi!

Rushwa ni mfumo. period

Mkuu hapo sahihi kabsa, kama muandishi wa hii makala alivyosema kuwa, CCM na Ufisadi ni sawa na kobe na gamba, umetoa gamba kobe anabonyea., tht's th fact..!!
 
Lowasa kama anajiamini yuko safi ajisalimishe hadharani na kukataa kashfa zinazomkabili nakutuambia ukweli wa ufisad wa Richmond na nyingnezo nani mhusika!

hivi nyie mnamjua Lowassa nyie..subirini atawaacha mdomo wazi...haki ya mungu nawaaambia ngojeni muone
 
Mchambuzi amechambua vizurina,watanzania wengi bado tumelala mno.Juzi tu Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali alibainisha upotevu wa zaidi ya bilioni 48,bado wananchi wamekaa kimya.Serikali imepiga chenga kwenye hili hatujui upotevu huu wa pesa utashughulikiwa vp.Wamama wajawazito wanafariki sn vijijini kwa kukosa huduma ss hizo pesa bilion 48 zingejenga zahanati ngapi?Muda umefika ss wa kusema "basi"inatosha.Wenzetu Kenya kupanda kwa gharama tu za maisha wameandamana wote kuonyesha hisia zao,sisi Watanzania hasa viongozi tumebaki waimba mipasho tu.
 
Mkuu hapo sahihi kabsa, kama muandishi wa hii makala alivyosema kuwa, CCM na Ufisadi ni sawa na kobe na gamba, umetoa gamba kobe anabonyea., tht's th fact..!!

nyinyi wote ni wajinga tu,ukitumwa dukani kununua ccm utaileta kwa kipimo kipi? kila mtu ana nia yake anapoingia siasa msijifanye kwamba wana ccm wote tumezaliwa moshi au rombo.
 
hivi nyie mnamjua Lowassa nyie..subirini atawaacha mdomo wazi...haki ya mungu nawaaambia ngojeni muone

huyu lowasa kabla hajawa PM alikua wapi.nijuavomi aliwahi kuwa waziri wa madimbwi na mifuko enzi za ruxa ama mr clean mjuao zaidi mtanikosoa .je ufisadi alifanya lini kabla ya UPM.Je alikula pesa za miradi ama?kuna evidence?
Jk kawa prez akampa uPM ambao chahali anamsifia kuufanya kisokoine.lakni uwaziri mkuu kafanya mda mfupi two years ufisadi alifanya saa ngapi kwani hata deal la richmond halikufanikiwa?akawa kajiuzuru kuna watu wanampandisha chati ya ufisadi lakini hapa kuna kitu hatukifahamu.
 
huyu lowasa kabla hajawa PM alikua wapi.nijuavomi aliwahi kuwa waziri wa madimbwi na mifuko enzi za ruxa ama mr clean mjuao zaidi mtanikosoa .je ufisadi alifanya lini kabla ya UPM.Je alikula pesa za miradi ama?kuna evidence?
Jk kawa prez akampa uPM ambao chahali anamsifia kuufanya kisokoine.lakni uwaziri mkuu kafanya mda mfupi two years ufisadi alifanya saa ngapi kwani hata deal la richmond halikufanikiwa?akawa kajiuzuru kuna watu wanampandisha chati ya ufisadi lakini hapa kuna kitu hatukifahamu.

Hapo nilipo bold ndo kuna ukweli wote wa lowassa zingine ni porojo, kuna kitu cha mhimu sana tumefichwa watanzania hata kamat ya Mwakyembe iligundua nahisi ila ikatuficha, hukumu yao inasomeka ukutani sasa nani tena atatuambia kilichofichwa?
 
Mtu yuko ulaya anajifanya kujua zaidi ya alieko hapo.WTF?

Acha ufinyu wako wa mawazo. Kuwa ulaya kunamzuia nini kujua nchi yake, mtoa mada hakuzungumzia hapa kama amebadili urai wake, kwanini unamhukumu kuwa yuko ulaya, kwani kuwa ulaya kwa shughuli zake binafsi kunamfanya apotez uraia wake. Ninavyomfahamu mtoa mada huyo ni mpiganaji wa kweli na mzalendo tosha. Wivu unakusumbua, watanzania tukiwa na watu wenye mawazo kama ya kwako hatutafika mahali, maana hata huelewi dunia ilivyo kwa sasa.
 
Back
Top Bottom