Makala- Mbinu za biashara

cpmbusiness

Member
Jun 27, 2008
5
0
Ndugu wapendwa kuanzia sasa nitakuwa nikiwatumia makala za
kuwaelimisha juu ya ujasiriamali ifuatayo ni makala ya kwanza.

SIRI YA UTAJIRI


Watu wengi wanajiuliza, "Siri ya utajiri ni nini?" Jee ni mbinu gani
zinaweza kumsaidia mtu kupata utajiri? Siri kubwa ya utajiri ni
kujifunza elimu ya namna ya kutafuta mtaji, kuwekeza kwa busara kwa
namna ambayo daima panakuwa na ziada na faida. Kwa bahati mbaya
sana, elimu hii haifundishwi darasani ila wanayo wafanyabiashara
wachache na kila anayefanikiwa kujifunza siri hii huwa tajiri na
huendelea kuificha.

Kwa bahati nzuri, katika utafiti wagu nimeweza
kuigundua siri ya utajiri. Kwa kuwa ninapenda wasomaji wangu waweze
kufanikiwa na wapate manufaa kwa kununua kitabu hiki nimeamua
kuiweka siri hii wazi:-

- Siri ya kwanza ya kuelekea ukwasi ni kubuni mradi endelevu,
yaani unaoweza kuitoa ziada na faida.
- Siri ya pili ya kuelekea kwenye utajiri ni kujifunza na
kujenga tabia ya kuweka akiba
- Siri ya tatu ni kuwekeza fedha hizo za akiba katika vitega
uchumi ambavyo vinazalisha faida endelevu.
- Siri ya nne ni kujifunza namna ya kufanya biashara na
kuanzisha biashara yako ili iwe indelevu.

Kuna njia mbili za namna ya kupata utajiri zenye uhakika. Njia ya
kwanza ni njia ndefu ambapo wataalamu na watafiti wa masuala ya
fedha wameigundua njia hii ni rahisi kuifuata kwa sababu haihitaji
uwe na kipato kikubwa, wanashauri kwamba ujenge tabia ya kuweka
akiba, anza kuweka akiba ya T.shs 1,000 kila siku sawasawa na TShs
30,000 kwa mwezi, matokeo yake ni kwamba kama utaweka akiba yako kwa
kipindi cha miaka 65 bila riba yoyote utakuwa na akiba TSshs
23,725,000 (Milioni Ishirini na Tatu Mia Saba Ishirini na Tano
Elfu).

Kama utawekeza fedha hiyo na kupata riba ya asilimia 10% kwa
kila mwaka itazaa na kukuletea TShs 2,750,000,000 (Bilioni Mbili na
Milioni Mia Saba Hamsini). Hesabu hii inaweza ikakutisha na usiamini
macho yako lakini hiyo ni siri ya nguvu ya hesabu na riba kama
alivyozielezea mwanafizikia Enstein kwamba katika dunia hii hakuna
kitu chenye nguvu kama hesabu za riba.

Pengine njia hii inaweza kuwa
ni ndefu sana na ya kukatisha tamaa. Wengi wetu hatuwezi kusubiri
muda mrefu. Hivyo tungependa kuwa na mafanikio ya kiuchumi kwa
haraka. Lakini nasisitiza kama kipato chako ni kidogo anza leo
kuweka akiba ya TShs 1,000 kwa siku.

Dundulizo la akiba hii hukutiririshia utajiri bila wewe kukusudia

kwani utaweza kukidhi hitajiko la ghafla kama kuugua safari ya
dharura gharama za likizo na hata kutumia mbinu hii kama mpango wa
elimu kwa watoto wako iwapo utawaanzishia hivi mara tu kila
mmojawapo anapozaliwa au unaweza kuutumia kama upanga wa siku zijazo
kwa mirathi ukianza hivyo leo kwa kupangilia namna hiyo kwa kila
kusudio lako la baadaye.

Hebu tuangalie njia ya pili.


- Njia ya pili ya mkato ni kuongeza kiwango cha kuweka akiba kama
wewe ni mtu mwenye shughuli za kuzalisha ziada. Kipato chako
kinaweza kuwa kinaongezeka kila mara. Badala ya kuweka akiba ya TShs
1,000 kwa siku jiwekee malengo ya kuweka akiba ya TShs 10,000.

Anza kwa kutenga asilimia 10% ya mapato yako hadi utakapofikia lengo la
TShs 10,000 au zaidi kwa siku. Badala ya lengo lako kutimia kwa
miaka sitini na tano (65) litatimia haraka zaidi. Kwa mfano ukiweka
akiba ya TShs 10,000 kwa siku kwa muda wa miaka sita na miezi sita
bila riba yoyote utapata TShs. 23,725,000. Ukiwekeza fedha hiyo na
kupata riba ya asilimia 10% kwa miaka sita na miezi sita utapata
TShs. 33,917,505.78. Kama fedha hiyo utaendelea kuweka akiba kwa
riba hiyohiyo hadi kufikia muda wa miaka kumi utapata TShs.
63,112,201.43.

Kwa kuwa kitu cha muhimu hapa ni kuweka akiba na kuwekeza akiba hiyo
katika kitegauchumi chenye kutoa faida kubwa, utajiuliza jee uwekeze
kwenye kitega uchumi chenye kutoa faida kiasi gani? Wataalamu wa
mambo ya fedha wanashauri kuwa uwekeze fedha yako kwenye
kitegauchumi chenye kutoa faida ya angalau asilimia 10% Kwa mfano
unaweza kuwekeza kwenye Akaunti ya TAJIRIKA ya Standard Chatered
Bank" inatoa riba ya asilimia kumi 10% pia unaweza kuwekeza kwa
kununua hisa katika soko la hisa na mitaji.

Kwa wastani wa watafiti wa masuala ya fedha viwango vya mapato
yatokanayo na hisa kwa gawio pamoja na kukua kwa mtaji ni zaidi ya
asilimia 11% ambayo ni makubwa kwa kiwango cha kawaida cha asilimia
kumi (10%).

Baada ya kueleza siri ya namna ya kupata utajiri nitazitaja njia
zingine ambazo zinaweza kukuwezesha kuwa tajiri.

1. Unaweza kurithi mali na fedha kutoka kwa wazazi wako. Hii ni
njia ya kubahatisha kwani watu matajiri siyo wengi na hivyo watoto
wenye bahati kama hii ni wachache pia.

2. Unaweza kusomea ujuzi au utaalamu katika fani yenye malipo
mazuri na kujiajiri mwenyewe. Kwa mfano, unaweza kusomea fani kama
ya Uanasheria, Uhasibu na Udaktari au ufundi / sanaa na kadhalika.

3. Unaweza kuanzisha biashara yako na kuiendesha ili kupata
ziada kubwa.

4. Unaweza kuendeleza vipaji vyako na kuwa mwanamichezo au
msanii wa kulipwa.

5. Unaweza kutunga vitabu juu ya suala lolote unalolijua. Kwa
mfano, kama wewe ni mtu uliyebobea katika masuala ya muziki unaweza
kutunga kitabu kinachofundisha watu namna ya kuwa mwanamuziki.
Watunzi wengi wa vitabu ni matajiri wakubwa. Hii ni kazi unayoweza
kuifanya mara moja lakini ukavuna matunda yake kwa muda mrefu sana.

6. Unaweza kuwa mbunifu na kuanza kuuza mawazo yako au kutumia
chombo ulichokibuni kukuingizia fedha.

7. Unaweza kucheza bahati nasibu na kushinda. Tatizo hapa soko
na wateja wa aina hii ya huduma ni haba. Hiki ni kitu cha
kubahatisha na nimekitaja makusudi ili kuwapa onyo wasomaji kwani
watu wengi wanapenda sana kucheza michezo ya kubahatisha.
Uwezekano wa kutajirika kwa njia hii ni mdogo sana.

Hivyo,
nawashauri wasomaji kuachana na njia hii ya kutafuta utajiri.
Nawashauri wachague njia yoyote inayofaa na inawezekana kwa
kufuatana na mazingira yanayomzunguka mtu husika. Mkulima au mfugaji
anaweza kuzingatia fani hii na kutajirika sana. Kwa kweli hakuna
mipaka, hasa hapa kwetu Tanzania kwa sababu ya wingi wa fursa za
kuweza kujishughulisha na kuwa tajiri.

Maelezo ya kina juu ya aina ya biashara au mbinu unaweza kuzitumia
kutafuta na kupata faida utayapata katika sehemu ya pili ya kitabu
hiki.

Inawezekana kuwa tofauti kati ya mtu tajiri na mtu maskini inatokana
na kile tulichojifunza kutoka kwa wazazi wetu. Wazazi maskini
huwaambia watoto wao wajitahidi kusoma sana ili wapate maksi nzuri
darasani na ili baadaye waweze kupata kazi nzuri. Wakati wazazi
matajiri huwapa watoto wao elimu ya namna ya kutafuta fedha.

Kwa kawaida tukiwa shuleni tunapewa ripoti ya masomo. Katika maisha
tunatakiwa kuwa na ripoti yetu ya maisha nayo ni orodha ya mali
tulizonazo ikiwa ni pamoja na elimu ya kuzaliwa na ya kusomea na
fedha taslimu zile zilizo katika hifadhi mbalimbali.

Kwa kufuata tafsiri ya Umoja wa mataifa mtu masikini ni yule ambaye
kipato chake hakizidi TShs 1,000 kwa siku.

Inawezekana kuwa mfumo wa kifedha wa mtu maskini ni mfumo ambao
humfanya kutumia kipato chake chote kulipia matumizi huwa hana ziada
wala uwezo wa kuweka akiba hana madeni na hana mali.

Mfumo wa fedha wa mtu mwenye kipato cha kati ni mfumo ambao humfanya
kuwa na mali kama magari, nyumba na kadhalika. Mara nyingi mali hizo
huwa zinapatikana kwa mikopo na hutumia mshahara kulipia matumizi
na madeni, hasa kama madeni ni makubwa, mtu mwenye kipato cha kati
anapaswa kumuona mshauri wa maswala ya biashara.

Hatua anazoweza kuchukua ili kujikwamua na tatizo la madeni anaweza kulazimika kuuza
baadhi ya mali zake ambazo amezinunua kwa kutaka kuonyesha ufahari
tu na ambazo hazina umuhimu. Kwa mfano kama mtu ana magari matatu ya
kutembelea, anaweza kuuza magari mawili kubaki na gari limoja na
fedha atakayoiokoa kuiwekeza au kutumia kama mataji na kuanzisha
biashara ili kujiongezea kipato.

Mfumo wa mtu tajiri ni mfumo ambao unamwezesha kuwa na biashara
yake, kumiliki mali nyingi, kuwa na fedha nyingi katika akiba na awe
ameziwekeza kwenye vitega uchumi vinavyolipa faida kubwa zaidi ya
asiliamia kumi, kama vile nyumba za kupangisha na hisa. Mtu huyu
hana wasiwasi na maisha. Anaweza kusafiri au kuugua lakini
vitegauchumi vyake vinaendelea kumwingizia fedha. Siri kubwa ya
matajiri ni uwezo wa kutumia fedha na kuziwekeza kupata faida kubwa.

Hiki ni kitabu cha vitendo. Yote unayoyasoma humu inabidi uyafanyie

kazi ili yakusaidie. Tofauti kati ya maskini na tajiri iko katika
kuchukua hatua. Tajiri hujifunza mambo ya kumwendeleza na kuchukua
hatua kwa kutekeleza kwa vitendo yale anayojifunza na anayoyaona
yanaweza kumuinua kiuchumi. Maskini huwa anajifunza mambo na
kuyaacha kichwani bila kuchukua hatua au kuyafanyia kazi
aliyojifunza na hivyo fursa ya kupata utajiri inampita hivihivi. Kwa
hiyo, kama unataka kuwa tajiri anza mara moja kufanya yafuatayo:-

1. Anza kuweka akiba ya T.Shs 1,000 kila siku. Tengeneza

kisanduku na tumbukiza TShs. 1,000 kila siku. Zikifika TShs. 50,000
kafungue akaunti ya TAJIRIKA, kwenye Benki ya "Standard Chatered".
Kisha endelea kuweka TShs. 30,000 kila mwezi. Jinsi mapato yako
yatakavyokuwa yanaongezeka tenga asilimia kumi (10%) ya mapato yako
uweke akiba kila mwezi.

Lengo lako liwe ni kuweka TShs 10,000 au
zaidi kila mwezi. Fedha unayoweka ni kama unapanda mbegu. Kumbuka
hii ndiyo hatua ya kwanza kuelekea kwenye utajiri. Faida katika
benki hii ni kubwa. Inaanzia asilimia 6.5% kwa kianzio cha TShs.
50,000 hadi TShs. 5,000,000 na asilimia 10% kwa kiwango kinachozidi
TShs. 10,000,000. Fedha utakazoziweka huko usiziguse mpaka ukiona
zimekuwa nyingi ndipo utaamua na kupanga ukaziwekeze sehemu gani.

2. Jifunze pia mbinu za kutafuta fedha.

Njia rahisi ni ya uhakika ya kukuwezesha kufanikiwa kiuchumi katika maisha ni kutafuta
mshauri au mtaalamu anayejua mbinu za uongozi wa biashara ili
akushauri vizuri juu ya yale unayonuia kutekeleza.

3. Inawezekana pia bado hujawa na biashara ya aina yoyote.
Kama ndivyo anza kufanya utafiti kuona utafanya biashara gani.

Mawazo ya biashara gani ufanye unaweza kuyapata katika sehemu ya
pili ya kitabu hiki. Kila mara hakikisha unatenga asilimia 10% ya
mapato yako na kuweka kwenye akaunti yako ya TAJIRIKA. Kumbuka
kwamba kuwa na biashara yako ni siri ya pili ya kuelekea kwenye
kupata utajiri. Kama unayo biashara yako unaweza kumtafuta mtaalamu
wa biashara kuangalia jinsi unavyoweza kuiboresha au kuipanua.

4. Panga malengo ya muda wa mwaka mmoja miaka mitano na miaka
ishirini ili kuhakikisha kwamba unajikomboa kiuchumi. Malengo yako
makuu yawe ni:- kuwa na akiba ya fedha za kutosha katika akaunti
yako , kuwa na biashara yako, na vitega uchumi vya aina tofauti
ambavyo unaweza kuvisimamia vizuri.

5. Kama wewe ni mwajiriwa, kipimo chako cha mafanikio kiwe ni
kujiuliza swali, kama utaacha kazi yako ya mshahara utaweza kuishi
kwa kutumia kipato chako cha pembeni kwenye biashara yako kwa muda
gani? Mafanikio yako yatakuja pale utakapoweza kutumia kipato chako
cha ziada bila kutegemea mshahara, na hapo ndipo unaweza kuacha kazi
na kwenda kuimarisha biashara zako au kuendelea na kazi huku pia
ukijiimarisha kibiashara.

6. Kama utafuata mpango wa namna hii na kujituma kwa juhudi na
maarifa kwa muda wa miaka mitano (5) unaweza kuwa tajiri na maisha
yako yanaweza kuwa mazuri.


Makala nyingine nitawatumia hivi karibuni
CHARLES NAZI

Mwandishi wa makala hii ni mshauri wa biashara na mtunzi wa kitabu

cha Mbinu za biashara na maarifa ya kupata pesa na utajiri. Kwa
ushauri,maoni na mapendekezo piga simu 0755394701
 
Makala- Mbinu za biashara 2
NAMNA YA KUANZISHA BIASHARA.
Ukitaka kufanya biashara yoyote ile unatakiwa kufanya utafiti.
Kutokufanya utafiti ni chanzo cha biashara nyingi kuharibika. Lazima
ujiulize kwamba unataka kufanya biashara gani? Usiseme unataka
kufanya biashara yoyote ile kwani kusema kwamba unataka kufanya
biashara yoyote ile ni kupoteza mwelekeo kwa kuwa utakuwa hujui
unataka kufanya nini. Kama hujui cha kufanya hakuna kitu
utakachokifanya. Hili ni tatizo la watu wengi. Hata baadhi ya watu
niliokutana nao wakitaka ushauri wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo
hili. Njia ya kukusaidia kuamua ufanye biashara gani ni kwa
kujiuliza umewahi kufanya kazi au biashara gani? Umesomea nini?
Vipaji vyako ni vipi? Ni biashara ipi au kazi ipi unapenda zaidi
kuliko nyingine na kwa sababu gani? Ukisha jiuliza maswali haya
chukua kalamu na karatasi uandike maswali yako na kuyajibu. Ukikagua
maswali na majibu yako utagundua shughuli unayoipenda, unayoiweza na
una kipaji nayo na hiyo ndiyo inayokufaa. Ukishachagua biashara
unayoipenda ni rahisi sana kufanikiwa kwani shughuli utazifanya kwa
hiyari bila kujilazimisha. Kama unashindwa kuamua ni biashara gani
ufanye, soma sura ya sita katika kitabu hiki. Nimeelezea kuhusu
mawazo yanayoweza kukusaidia kuanzisha biashara mbalimbali ambazo
unaweza kuzifanya. Kama utakuwa bado hujafikia uamuzi baada ya hapo
basi tafuta na wasiliana na washauri ili mbadilishane mawazo na
ufundishwe jinsi ya kuamua ufanye biashara gani.

Mambo mengine unayotakiwa kuyafanyia utafiti ni:-
(i) Kujua siri ya bishara unayotaka kufanya ili upate mbinu za
kupata mafanikio. Unaweza kupata siri au kujifunza mbinu kutoka kwa
watu wanaofanya biashara kama unayotaka kufanya. Suala hili ni gumu
sana kwani wafanyabiashara wengi huwa wanaficha siri za biashara zao
ili kulinda wasizidiwe maarifa na washindani wao. Unaweza kuipata
siri hiyo kama utakwenda kupata ushauri toka kwa mfanyabiashara
ambaye yuko mbali na mahali unapofanyia biashara, au tafuta ushauri
kwa wataalamu wa mambo ya biashara.
(ii) Fanya utafiti wa soko la bidhaa unazouza au unazotarajia
kuuza. Jiulize, je bidhaa unazotaka kuziuza zina soko? Utawauzia
watu gani na utauzaje? Kama wewe ni mzalishaji, una mazao / bidhaa
unapaswa kuuza kwa jumla, mchanganyiko ama rejareja? Je utatangaza
vipi bidhaa zako? Maelezo ya namna ya kutangaza bidhaa zako
utayapata katika Sehemu ya Tatu ya Kitabu hiki. Utafiti wa soko
unaweza kuufanya kwa kuwauliza wafanya biashara waliotangulia
maswali hayo ya utafiti kwani wao wamekuwapo kwenye soko na
wanazijua siri za soko.
(iii) Tengeneza bajeti yako kwa kuorodhesha vitu vinavyohitajika
na gharama zake ili kuweza kuanzisha biashara yako. Vitu hivyo ni:-
(a) Gharama za Kujenga au kupanga ofisi
(b) Gharama za Leseni ya biashara
(c) Makadirio ya kodi toka TRA
(d) Garama ya vifaa vya ofisi yaani, Samani, makaratasi,
mitambo, mashine, nk
(e) Manunuzi ya malighafi au bidhaa za kuanzia biashara
(f) Idadi ya wafanyakazi na gharama za mishahara yao.
(g) Gharama nyinginezo kama vile, umeme, maji, nk.
(iv) Unatakiwa kujua ni mtaji kiasi gani unahitajika kuanzisha
biashara yako. Mtaji huo utaujua baada ya kujumlisha gharama
zilizoorodheshwa katika kupengele namba (iii)Gharama hizi ni za
mwaka ule wa kwanza wa kuanzia
(v) Tafuta Mtaji.
Mtaji unaweza kupatikana kutoka kwenye vyanzo vifuatavyo:-
(a) Akiba au mshahara
(b) Msaada au mkopo kutoka kwa ndugu na jamaa.
(c) Kuingia ubia na mtu mwenye mtaji
(d) Mkopo toka baadhi ya asasi kama vyama vya akiba na mikopo
(SACCOS), NGO za kifedha sipokuwa Benki kwani hizi huwa hazitoi
mikopo kwa mtu anayeanzisha biashara.

Makala nyingine nitawatumia hivi karibuni
CHARLES NAZI

Mwandishi wa makala hii ni mshauri wa biashara na mtunzi wa kitabu
cha Mbinu za biashara na
maarifa ya kupata pesa na utajiri. Kwa ushauri,maoni na mapendekezo
piga simu 0755394701
 
Mkuu cpmbusiness.

Ni ushauri mzuri sana Lakini unaweza kumesababisha uchukiwe bure kama wenzetu Wachaga. Sipendi hilo mimi.
 
TARATIBU ZA KISHERIA ZA KUFUATA ILI KUANZISHA BIASHARA
Baada ya kufanya utafiti na kupanga mipango ya kuanzisha biashara unatakiwa kwanza kuangalia taratibu za kisheria ambazo unatakiwa kuzifuata na kuzitekeleza. Kama biashara yako ni ndogo anza kama mtu binafsi. Faida ya kuanza biashara kama mtu binafsi ni urahisi wa kuanzisha biashara; urahisi na wepesi wa kutoa maamuzi kwani huhitaji ridhaa ya mtu mwingine kabla ya kutoa uamuzi; mtaji unaohitajika utakuwa mdogo kutokana na gharama za uendeshaji kuwa ndogo, biashara hii inaweza kuendeshwa kwa msaada wa familia kwa kumtumia mke au mume, watoto au ndugu na jamaa na raslimali za familia kama nyumba na samani. Unapoanzisha biashara na kuiendesha mwenyewe unakuwa huru tofauti na mifumo mingine. Matatizo ya kufanya biashara kama mtu binafsi ni:- Kushindwa kupanua biashara yako kwa ufinyu wa mtaji; kufilisiwa mali zako za binafsi iwapo biashara yako itafilisika kwani katika mfumo huu mali ya biashara na mali binafsi si rahisi kuzitenganisha; Kuongeza mtaji inakuwa ni vigumu, hivyo unaweza kushindwa kupanua biashara yako. Ili kuepukana na matatizo niliyoyataja hapo juu unaweza kuungana na watu wengine kufanya biashara kwa ubia. Faida za kufanya biashara kwa ubia ni: Kupata fursa ya kuongeza mtaji kwa kushirikiana na wafanyabiashara wengine ambao wataleta mitaji yao; Kuongeza ujuzi katika shughuli kwa kuleta wataalamu pale taaluma Fulani inapohitajika. Matatizo ya kuendesha biashara kwa njia ya ubia ni: Kufilisiwa mali zako binafsi endapo biashara yako itafilisika; kudhulumiana mali endapo moja wa wabia atakuwa si mwaminifu ambapo anaweza kuingia mikataba mibovu na kusababisha hasara ambayo itabebwa na wabia wote. Ni muhimu kuwachunguza watu tunaotaka kujiunga nao ili tujue kama ni waaminifu. Pia ni vyema kuwapo na mkataba wa maandishi mnapoanzisha biashara ya ubia mkimshirikisha mwanasheria kama shahidi ili kujikinga na kudhulumiana; Kufariki kwa mbia mmoja kunaweza kusababisha kuvunjika kwa ubia; kotokuelewana kwa wabia kunaweza kusababisha kuvunjika kwa ubia. Kama biashara ikikua unaweza kuanzisha kampuni. Mfumo wa uendeshaji wa kampuni unazo faida zifuatazo: unatenganisha majukumu ya wamiliki mali na kampuni yaani kampuni inaposajiliwa inakuwa inakuwa na hadhi na kutambulika kisheria kama ni mfumo tofauti na wamiliki. Mfumo huu unatenganisha majukumu kati ya menejimenti na wamiliki wa kampuni; madeni ya kampuni yatalipwa hadi kufikia kikomo cha mtaji uliowekezwa na wamiliki. Hivyo, mali binafsi za wamiliki wa kampuni haziwezi kukamatwa kufidia madeni ya kampuni endapo kampuni itafilisika. Mfumo wa kampuni unatoa nafasi ya kupanua mtaji kwa kukusanya mitaji kwa kuongeza wanahisa au kupitia soko la mitaji ya hisa. Mfumo huu ndiyo unafaa kwa biashara kubwa kwani unatoa nafasi ya kupanuka kwa biashara na kuendelea kuwapo kwa biashara hata kama baadhi ya wamiliki wake wakifa au kujitoa katika kampuni.

Mambo ya muhimu ya kutekeleza kisheria kabla ya kuanzisha biashara ni:-
(a) Kuwa na ofisi
(b) Kukata leseni
(c) Kusajiliwa na TRA kama mlipokodi na kupewa namba ya mlipakodi
(d) Kufanyiwa makadirio ya kodi ya mapato ya awali
(e) Kutimiza masharti mengine ya keshiria kuwa mfano kama wewe unataka kufanya biashara ya ukandarasi wa ujenzi wa majengo lazima usajiliwe kwenye Bodi ya Wakandarasi.

Kama unafanya biashara ya kati au kubwa unapaswa kufuata sheria. Ni makosa kufanya biashara bila kufuata sheria za nchi. Hata hivyo, kuna biashara zingine ndogo ndogo sana kiasi kwamba uanzishaji wake si rahisi kufuata sheria hizo hapo juu, mfano uuzaji wa maandazi, karanga na vitu vingine vidogovidogo. Hizi zinaitwa biashara zisizo rasmi au biashara ndogondogo. Ni vyema ukachunguza kama biashara unayoifanya ni ndogo au kubwa ili ujue kama unapaswa kufuata taratibu za kisheria au la, kwani kutokujua utaratibu na sheria siyo kinga ya kukufanya usishitakiwe.
Makala nyingine nitawatumia hivi karibuni
CHARLES NAZI

Mwandishi wa makala hii ni mshauri wa biashara na mtunzi wa kitabu
cha Mbinu za biashara na maarifa ya kupata pesa na utajiri. Kwa
ushauri,maoni na mapendekezo piga simu 0755394701
 
Wazo zuri, lakini hebu punguza urefu ili sisi wenginetunatafuna kidogo kidogo
 
Asante Ndg. Charles Nazi.
Nakumbuka kura zako hazikutosha wakati unagombea Ubunge jimbo la Mbogwe mwaka 2005, vipi kuhusu mipango yako ya mwaka 2015?
 
Mkuu CPMBusiness....unachokisema ni theory nzuri...

Ila realistically huwezi sema mtu aweke akiba kwa muda wa miaka 65 ambapo kwa opportunity missed na muda na factor ya uzee hiyo mil23 ni hasara kabisa.

Technic ya kuweka akiba primitively hivi ni ni kukwepa hoja kuu na ya msingi kwamba ili uwe tajiri ni LAZIMA TUZALISHE na UUZE na sio vinginevo...kuweka akiba ni chagizo kusaidia kufanya surplus unayopata iwe na meaning endelevu.

Kwanza utaweka akiba bila surplus kutoka kwenye uzalishaji?A million dollar question ni jee mtu azalishe nini ili apate success?
 
Shida ya business educators,na wengi wana lack field experience,wanaelekeza business theories ambazo ni kama cosmetics,mzizi hua hauguswi....

Zalisha,Uza,cut costs,investment more ile surplus,basi game over...

Mi naomba kama mkuu unaweza tuelimisha in 10 years to come,sector na uzalishaji utakao possibly be prominent,ambayo watu tunaweza teka mapema na jinsi ya kuiperfect well in advance....

Ukiniambia niwekeze akiba 1,000 kwa miaka 65 hiyo si kweli ni stori,ni hasara....Nataka unielekeze hiyo 1,000 naotoa wapi tu begin with!
 
Shida ya business educators,na wengi wana lack field experience,wanaelekeza business theories ambazo ni kama cosmetics,mzizi hua hauguswi....

Zalisha,Uza,cut costs,investment more ile surplus,basi game over...

Mi naomba kama mkuu unaweza tuelimisha in 10 years to come,sector na uzalishaji utakao possibly be prominent,ambayo watu tunaweza teka mapema na jinsi ya kuiperfect well in advance....

Ukiniambia niwekeze akiba 1,000 kwa miaka 65 hiyo si kweli ni stori,ni hasara....Nataka unielekeze hiyo 1,000 naotoa wapi tu begin with!

Mawazo mazuri mkuu!
 
Wakuu samahanini kwa ku-copy mzigo wote huo hapo juu...it is too long ku-reply kwa quote...
 
Kazi nzuri cpmbusiness mawazo ya Robert Kiyosaki yote katika Kiswahili masikini wanakosa uthubutu na kujifunza kusimamia na kuchukua maamuzi magumu.
 
Last edited by a moderator:
Kazi nzuri cpmbusiness mawazo ya Robert Kiyosaki yote katika Kiswahili masikini wanakosa uthubutu na kujifunza kusimamia na kuchukua maamuzi magumu.

Nakubaliana na wewe...ila watu wanakua fastinated mno na akina Kiyosaki...wanakua caught up na fastination wanazosema,watu tuko strongly chained up kiasi kwamba tukimsoma kiyosaki tunajihisi tuko kwenye biashara na infact ni illusion.

Issue ni jee huyu mtu azalishe nini ili awe kwenye biashara?Basics wanazotoa educators kama akina kiyosaki and others watu wanazijua vizuri tu sema confidence hakuna
 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom