Ben Saanane
JF-Expert Member
- Jan 18, 2007
- 14,580
- 18,225
Afrika na ICC: Ubeberu wa Mataifa Makubwa na Uharamia wa Viongozi wetu
Na Ben Saanane
Mwishoni mwa wiki iliyopita Viongozi wa Nchi za Africa walikua Makao Makuu ya Umoja huo Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kujadili mpango wa kujiondoa katika mkataba wa Roma unaoongoza Mahakama ya kupambana na uhalifu wa kivita na makosa makubwa ya Jinai dhidi ya Ubinadamu duniani, ICC (International Criminal Court).
Hoja kuu ni kuwa mahakama hii inawalenga Viongozi kutoka Mataifa ya Afrika tu. Hii ni hoja yenye ukweli kwa kiasi Fulani, maana asilimia kubwa ya kesi zilizoko kwenye Mahakama hii kwa sasa ni kutoka Afrika huku rekodi zikionyesha hata Kesi nyingi za nyuma zilizowahi kushughulikiwa na Mahakama hiyo zinahusu Watuhuniwa kutoka Afrika zaidi.
Ukiacha sababu hizo lakini pia Viongozi wa Afrika nao wana ajenda yao juu hili azimio lao la kutaka kujitoa ICC, azimio ambalo halikupata uungwaji mkono wa kutosha katika Kikao hicho cha juzi japo kuliibuliwa azimio jipya mwishoni mwa kikao la kumtaka Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kutohudhuria Mahakamani wakati wa Kesi yake inayopangwa kusikilizwa mwezi ujao.
Nchi 34 kati ya 54 za Umoja wa Afrika zimesaini Mkataba wa Roma wa kukubali kuanzishwa kwa Mahakama hii. Wakati Viongozi wa Nchi hizo waliposaini haraka haraka mkataba wa ICC na kuziingiza nchi zao walidhani wanazuia mapinduzi dhidi yao kutoka kwa waasi, na walikwenda hatua mbele zaidi ya kujifanya kuwa hawatatambua matumizi ya mtutu katika kubadilisha utawala kwa njia ya kupindua serikali.
Hawakufikiria wala kutilia maanani kuwa ili kukomesha ‘mapinduzi ya kijeshi' ni lazima kuimarisha utawala bora wa sheria bila kuminya demokrasia ili sauti huru zisikike na pia kujali zaidi maslahi ya wananchi wan chi hizo. Mapinduzi ya kijeshi Afrika yanachochewa kwa kiwango kikubwa na tawala kandamizi zilizominya uhuru wa maoni na kuzuia sauti za wananchi wenye mawazo kinzani pamoja na wanaharakati.
Jambo la kufurahisha ni kuwa wapo Viongozi zaidi ya 12 wa Nchi za Afrika waliopo Madarakani na ambao ni wanachama wa AU ambao waliingia madarakani kwa mtutu wa Bunduki na wengine wakisalia madarakani kwa kupora chaguzi. Kipindi wanapitisha azimio la kutotambua mapinduzi ya kijeshi idadi hii ilikua kubwa zaidi na hao hao walioingia madarakani kijeshi au kwa wizi wa kura ndiyo waliotangaza kutotambua mapinduzi hayo ya kijeshi.
Kwa mujibu wa Maandishi ya Vitabu vya Kitafiti kuhusu Mapinduzi ya Kijeshi katika Mchi za Kiafrika kama 'Coup D'Etat' cha Mwandishi Edward Luttwak na 'Political Order In Changing' kilichoandikwa na Samuel P.Huntngton, ilionekana kuwa pamoja na ushawishi kutoka mataifa ya nje lakini Upendeleo,Ufisadi na hali ngumu ya kiuchumi na kijamii ni mojawapo ya vichocheo vikubwa kwa mapinduzi ya kijeshi yaliyoikumba Afrika.
Kwa kipindi cha karibia miaka 60 tangu Nchi za Kiafrika zipate Uhuru, Afrika Imeshudia Mapinduzi ya Kijeshi zaidi ya 40 huku Nchi ya Nigeria ikiongoza kwa kukumbwa na Mapinduzi 10 ya kijeshi Kati ya mwaka 1966-1999 ikifuatiwa na Ghana iliyokumbwa na zaidi ya Mapinduzi 9 ya Kijeshi.
Kwa hiyo badala ya kufikiria namna ya kuondoa sababu na vichocheo vinavyochochea uwezekano wa Mapinduzi ya Kijeshi huko baadae, Viongozi wetu hawa wa Afrika waliamua kufumba macho na kuchagua njia waliyoiona ni rahisi zaidi kwa wakati huo bila kutazama athari zake kwao pia, yaani Mkataba wa Roma wenye kuasisi Mahakama ya ICC.
Kwa mfano suala la Uchaguzi kwa nchi za Afrika ni kichocheo kikubwa cha uvunjifu wa amani na mapinduzi kwa njia ya mtutu. Viongozi wa Afrika wanaogopana kuambiana ukweli au hawaheshimiani kwa kuwa tabia zao za ukiukaji wa sheria na kutowajali raia wao zinafanana. Labda tuangazie kwa kifupi tu nchini Kenya ambako ndipo chanzo cha hatua hizi za AU.
Wakati Mwai Kibaki, Uhuru Kenyatta na wanasiasa wengine wa kilichokuwa Chama Tawala cha Kenya cha PNU walipofanya udanganyifu kwenye uchaguzi wa Rais na wabunge nchini Kenya Mwaka 2007, hali iliyosababisha wapinzani kutoka chama cha ODM wakiongozwa na Willium Ruto na Raila Odinga kwa upande mwingine kuingia barabarani kupinga kuporwa uchaguzi huo na kusababisha mauaji ya watu zaidi ya 1000 na wengine zaidi ya 600,000 ya wasiokuwa na hatia kukosa makazi, Umoja wa Afrika, AU haukutangaza moja kwa moja kumchukulia hatua Mwai Kibaki na Watawala wengine.
Umoja huu haukutangaza kumtenga Mwai Kibaki na serikali yake na hata Rais Benjamin Mkapa wa Tanzania na Dk. Koffi Annan walipopelekwa kusuluhisha mgogoro huo walipata wakati mgumu kwa kuwa Kibaki alikuwa akiwadharau wote wawili kwa sababu ya rekodi zao za Ufisadi wakati wakiongoza Tanzania na Umoja wa Mataifa. Mkapa akituhumiwa kwa kufisadi mgodi wa Kiwira na Annan akitajwa kwa kashfa ya ‘Mafuta kwa chakula' ya Iraq.
Wakati wote huo wa vurugu za Kenya waliokuwa wanapoteza maisha ni raia wanyonge tu kutoka maeneo mbalimbali wan chi hiyo. Sasa' swali la kujiulia ni kuwa kuna haja gani ya kufanya uchaguzi ikiwa aliyeshinda uchaguzi anaporwa ushindi? Kuna tofauti gani kati ya Mapinduzi ya kijeshi (Coup d'tat) na wizi wa kura? Unapopora haki ya raia kuchagua,unapopora haki ya raia kutoa sauti. Hayo ni mapinduzi ya matakwa ya umma (coup D'Civillien). Hayo ni mapinduzi mapya baada ya Coup d'tat. Viongozi wa Afrika wamelibariki hilo.Unafiki ulioje?
Mara zote mapinduzi ya aina hii yasipofanikiwa kwa asilimia kubwa husababisha vita ya wenyewe kwa wenyewe.Tulishuhudia jaribio hili kule Cot de'Ivore. Laurent Gbagbo alishindwa uchaguzi na Mpinzani wake Allasaine Outtara, akaamua kufanya ‘Coup de' civillien'.Afrika haikufua dafu,walitoa sauti za kinafiki kukemea na hali ilizidi kuwa mbaya na kuhatarisha amani kiasi kilichopelekea uwezekano wa kuzuka vita ya wenyewe kwa wenyewe hadi jumuiya ya kimataifa ikiongozwa na Mkoloni wa zamani wa nchi hiyo, Ufaransa walipoingilia kati na hatimaye Gbagbo akakamatwa akiwa amejificha kwa aibu. Leo anashtakiwa mbele ya mahakama ya ICC, Mahakama hii ndiyo ambayo Viongozi hawa wanataka kujitoa ili kujiepusha na haya yanayomkuta Gbagbo.
Kwa hiyo tunaona kwamba mjadala wa Viongozi wa AU na nia yao ya kujadili suala la kujiondoa ICC linalenga pia kuwalinda viongozi hawa ambao wengi wao wamekiuka haki za binadamu na pia kuua na kutesa wapinzani wao. Ni azimio la kikatili.
Mbona hawajitoi kwenye Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Dunia (WB) na kwenye Shirika la Biashara Duniani (WTO)? Inatambulika kuwa Benki ya Dunia na Shirika la fedha Duniani ni nyenzo kuu za mabeberu zinazotumika kuzinyonya nchi zinazoendelea na hasa zile nchi zenye viongozi wasiofikiria mbele. Heri yao wananchi wa Venezuela waliojiondoa kutokana na ushupavu wa Rais wao Kamaradi Hugo Chavez.Vyombo hivi vya mabeberu (IMF, WB na WTO) ni hatari kwa Afrika na Ustawi wa wananchi wa Afrika kuliko Al-Qaeda na Al-Shaabab ambayo ni makundi hatari kwa Mabeberu, Vibaraka na maslahi yao popote pale duniani. Jambo kubwa la kinafiki kutoka kwa viongozi wetu hawa ni kuwa Viongozi wengi wa Afrika walioshitakiwa ICC walipelekwa huko na serikali za nchi zao ambazo viongozi wake walikusanyika huko mjini Addis Ababa kulalama kuwa ICC inawashtaki wao tu.
Serikali zilizopeleka kesi na watuhumiwa wenye asili ya kiafrika huko ‘The Hague' ni pamoja Serikali za nchi za Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cote d'Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda. Kesi nyingine mbili za Darfur na ile ya Libya zilipelekwa mbele ya mahakama hiyo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mamlaka yake zikiwa na sapoti ya wanachama wa baraza hilo kutoka barani Afrika.
Nilishawahi kusema baadhi ya viongozi wa Afrika ni ‘mambumbumbu'. Hata Makao Makuu mapya ya AU walipokaa kujadili hili la kujitoa ICC yamejengwa kwa Msaada wa ‘Beberu Mpya' wa dunia, UCHINA, ambaye rekodi yake juu ya ukiukwaji wa haki za binaadam inajulikana namna ilivyo mbaya, zaidi sasa Nchi hiyo imekuwa bingwa wa kuzuia Demokrasia Duniani. Viongozi wa Afrika ni wabinafsi na hawawezi kuona mbele hadi hatari iwaguse wao binafsi. Hawajali maslahi ya nchi zao. Si wale Viongozi wa kaliba ya kina Kwame Nkrumah, Julius Nyerere, Nelson Mandela, Ahmed Sekou Toure, Thomas Sankara, Gamal Abdel Nasser, Patrice Lumumba. Viongozi tunaowaheshimu katika ujengaji wa hoja kwa maslahi ya nchi na bara la Afrika kwa vitendo tofauti na hawa madikteta waoga.
Viongozi wa sasa wa Afrika walipotia saini mkataba wa Roma walikuwa na akili zao timamu, waliona namna Marekani, China na Urusi ambao ni Wajumbe watatu muhimu wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa aidha walipokacha kusaini mkataba wote au hata kujiwekea sharia zao za ndani za kuzuia matumizi ya Mkataba huo wa Roma kwa raia wao. Leo wanalalamika na kuhoji uhalali wa wajumbe hao wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wasioikubali ICC kisheria kupitisha kukamatwa kwa Rais Omar Hassa Al-bashir wa Sudan kwa kadhia ya Darfur. Wameiona hatari tayari kwa kuwa wamejiuliza, kama Rais Kenyatta na Makamu wake wanashtakiwa wakiwa Madarakani je wao watapona kweli? Wameona Hati ya kukamatwa iliyotolewa dhidi ya Rais Omar Bashir wa Sudan ikiwanyemelea. Wameshtuka na kujiona kuwa sasa hawapo salama tena. Leo Omar Bashir hawezi kusafiri kwenda nchi za Magharibi au kukanyaga ardhi za washirika wao ambao wameridhia itifaki ya Roma.
Kwa mujibu wa Mtandao wa Vyombo vya Usalama vya Marekani,Mei 6, 2002 Utawala wa Rais George Bush wa Marekani ulimtaarifu rasmi Katibu Mkuu wa umoja wa mataaifa juu ya Uamuzi wa Taifa la Marekani kujitoa katika mkataba huo. Kulingana na matamshi ya aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani wakati huo Donald Rumsfeld alisema kulikua na uwezekano wa baadhi ya maofisa wa Marekani wakiwemo maofisa wa jeshi la nchi hiyo kushtakiwa na mahakama hiyo na pia Marekani haikubaliani na baadhi ya vipengele vinavyoinyima Marekani kutekeleza wajibu wake hasa katika kipindi ambacho taifa hilo lilikuwa linakabiliana na vita dhidi ya ugaidi.
Marekani walidhamiria kulinda maslahi yao na mwanya wa kuendelea kupelea majeshi yao popote duniani pale wanapoona maslahi yao yapo hatarini. Hapa viongozi wa Afrika hawakushtuka na pia tangu muda huo walibweteka na hawakufikiria namna bora na mbadala wa kujiandaa kitaasisi ili kuwa na chombo chao cha kimahakama chenye hadhi, imani na uwezo wa kushughulikia masuala kama ICC ili kuepuka matatizo kama haya wanayoyajadili leo hii. Kwao waliona busara na ufahari kuwaomba CHINA kuwajengea jengo la kifahari la makao makuu ya Umoja huo badala ya kufikiria ujenzi wa mahakama na taasisi zenye hadhi na uwezo wa kushughulikia matatizo yetu
Kuna kila dalili kuwa Mabeberu wanaitumia ICC kwa maslahi yao. Lakini pia kupitia udhaifu wa viongozi wa Afrika kutoheshimu mifumo ya kutoa haki kama mfumo wa kimahakama, mataifa haya ya kibeberu yanapata mwanya wa kujenga hoja kuwa Afrika haina mfumo thabiti wa kushughulikia kesi bila kulindana(Impunity).
Kwa mfano,Viongozi wa Kenya walitoa taswira hii pale walipoamua kupeleka kesi ya Uhuru na Ruto wenyewe huko ICC. Kipindi hicho Uhuru na Ruto hawakuwa Marais. Viongozi wa Umoja wa Afrika walikaa kimya kwasababu hawa hawakuwa marais wenzao. Nilikerwa sana lakini wao hawakukerwa. Fedheha ya Afrika. Leo wanasema mahakama ya Afrika inalenga Viongozi wa Afrika? Hoja hii itaonekana nyepesi kwa kuzingatia mazingira niliyoyaainisha.
Inatambulika kuwa Haki za Binadamu ni kanuni ya msingi kwenye Mkataba wa umoja wa Africa (AU Chatter) na imepewa uzito katika mkataba huo maarufu kama ‘Banjul Charter . Kwa hiyo jitihada zozote za kutaka kujiondoa au hata hili la kujadili kama Marais wa Afrika waliopo madarakani wasishtakiwe mbele ya mahakama ya kimataifa ya ICC kupitia Umoja wa Afrika (AU) itatuma ujumbe mzito na mbaya juu ya dhamira ya dhati ya viongozi na umoja huo katika kulinda haki za binadamu na kukataa utamaduni wa kulindana (culture of impunity) ambazo ni tunu na nguzo kuu katika madhumuni ya Uanzishwaji na uwepo wa Umoja huu.
Hii ni ajenda iliyojaa hila na ubinafsi kwa viongozi dhidi ya raia wa bara hili. Naungana na msimamo wa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Askofu Desmund Tutu wa Afrika Kusini kuwa Nigeria na Afrika Kusini zikiwa kama mataifa yenye nguvu na ushawishi ndani ya umoja huu ziongoze katika mjadala kuzuia azimio hilo lenye sura mbaya na aibu kwa bara hili. Wito ambao pia umetolewa naye Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Dk. Koffi Annan.
Kama viongozi wa Afrika wanaona uchungu kweli basi waimarishe taasisi zetu na hasa mfumo wa Mahakama ambazo mara nyingi viongozi wa Afrika wamekuwa wakizitumia kuwaadhibu wapinzani wao. Mahakama hizi haziheshimiwi na hazipo huru kiasi cha kubeba matumaini na imani kwamba zitatenda haki. Hii ndiyo sababu kuu kwamba hata baada ya uchaguzi na inapotokea utata wa udanganyifu wa kura wapinzani wanaamua kuingia barabarani kudai haki kuliko kwenda mbele ya mahakama hizi ambazo zinaoneka kutumika kama mkono mwingine wa watawala kunyonga haki
Waafrika ni lazima tusimame imara na kujenga misingi ya kitaasisi. Hakuna wa kulitetea bara la Afrika zaidi ya Waafrika wenyewe na ili tupate mafanikio ni lazima tuachane na kasumba chafu ya kutegemea suluhisho la matatizo yetu kutoka nje ya bara la Afrika. Hatuwezi kuingiza suluhisho la matatizo yetu kutoka nje kama tunavyoagiza bidhaa kutoka nje kwa ajili ya kutatua matatizo tuliyojitengenezea wenyewe. Tuache kutegemea Mataifa makubwa ya kibeberu maana maumivu ya Afrika ni nafuu ya mataifa hayo ya Kibeberu.
ICC ina changamoto kama lilivyo Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa .Baraza hili la kudumu nalo lina changamoto ambazo tumekua tukizipigia kelele hasa juu ya upanuzi wa wigo wa kidemokrasia na utendaji wake unaozingatia maslahi ya wachache na hivyo kubeba ajenda za mataifa yenye nguvu kuaamua juu ya masuala mazito ya dunia. Amani ya dunia imewekwa rehani kwa mataifa haya matano tu.
Kwa hiyo ICC inatakiwa pia iangalie uhalifu uliofanyika Iraq, Afghanistan, Palestina na Lebanon. Ukweli ni kuwa ‘Silaha za Maangamizi' za Iraq ya Saddam Hussein hadi leo hii hazijawahi kuonekana kama ilivyonenwa na Wavamizi wa Nchi hiyo, lakini Bush na Blair walioendesha vita yenye uharibifu mkubwa kwa madai ya kumnyang'anya Saddam Hussein silaha za maangamizi wapo huru mtaani tu.
Ukweli ni kuwa tunaishi katika mazingira yaliyojaa laana ya uhalifu dhidi ya binadamu uliofanyika pia sehemu nyingine duniani kama vile Iraq, Lebanon, Libya na Palestina uliofanywa na unaondelea kufanywa na Israel, Marekani, Uingereza, Ufaransa na Washirika wao wa Umoja wa kujihami wa nchi za Magharibi na Marekani (NATO) ambao haukuvuta hisia na dhamira ya kiutendaji ya ICC pamoja na kuwa uhalifu huo pengine ni mkubwa na wa kutisha zaidi kuliko kesi zilizofanyiwa na zinazoendelea kufanyiwa uchunguzi za Afrika Kwa hiyo Viongozi wa Afrika kutumia sababu hii ya madai ya kuachwa kwa uhalifu mwengine duniani iwe ni kwa lengo la kutaka ‘hatua zichukuliwe kwa kila upande' na si kwa lengo la kupinga hatua kuchukuliwa kwao kwa udhalimu wao kwa raia wao kama alivyokuwa akidai Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn wakati wa Kikao cha juzi. Hailemariam amekwenda mbali zaidi kwa kuongeza sababu nyingine ya ubaguzi wa rangi (Racism) kuwa ni miongoni mwa vigezo ambavyo ICC inatumia ili kuwashughulikia zaidi Viongozi wa Kiafrika huku wakisahau kuwa Mwendesha mashtaka Mkuu wa Mahakama hiyo, Fatou Bensouda ni Mwafrika Mwenzao kutoka Gambia ikiwa pamoja na uwepo wa baadhi ya Majaji wa Mahakama hiyo ambao ni Waafrika.
Kama nilivyosema hapo awali ni jambo la kawaida kwa Viongozi wa Afrika kutumia mfumo wa mahakama zetu dhaifu kuendekeza utawala dhalimu, jambo linalopelekea kuoza zaidi kwa mfumo mzima wa mahakama. Kwa vyovyote vile hadi ninapoandika makala hii, wanaharakati na hata vyama vya upinzani haviwezi kupeleka visa vya uchaguzi au madai yao ya msingi kwenye mahakama hizi zinazolinda watawala na badala yake siku zote mahakama kuu kwao ni zile "Mahakama za Umma" ambazo ni tishio kwa watawala.
Kwa hiyo linapotokea jambo kama hili la "Mahakama za Umma" mara moja watawala hawasiti kutumia majeshi na hata silaha za kivita kuzima maandamano na mikutano itakayotishia utawala wao dhalimu na hivyo kupelekea mauaji ya kutisha kwa raia wasiokuwa na hatia wanaodai haki zao za msingi. Hapa ndipo mahakama ya Kimataifa ya ICC inapowakamata viongozi dhalimu wa Kiafrika na kuwashikisha adabu bila kujali kama Bush na Tony Blair wamewajibishwa kwa makosa yao ama la.
*Mwandishi ni Mhitimu wa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Siasa na Mahusiano ya Kimataifa,na pia shahada ya Uzamili katika Uchumi. unaweza kuwasiliana naye kupitia barua pepe; saananeben@gmail.com au +255768078523
NB:Makala hii imechapishwa Katika Gazeti la SAUTI YA MTANZANIA