Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka 2024/25

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,994
12,346
WhatsApp Image 2024-05-15 at 15.35.45_0ec0678a.jpg
TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2023/24 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2024/25

Upandishaji Vyeo

Mheshimiwa Spika,
kuanzia Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 Wizara imewapandisha vyeo jumla ya watumishi 9,397 katika ngazi mbalimbali za uongozi. Hali hiyo imeongeza morali ya utendaji kazi kwa watumishi hao. Katika mwaka 2024/25 Wizara itawapandisha vyeo jumla ya watumishi 26,876.

Mheshimiwa Spika, natoa pongezi nyingi na shukrani kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa upandishwaji vyeo wa kihistoria kwa vyombo vya usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Aidha, kwa kuzingatia jinsia miongoni mwa aliowapandisha vyeo ni Naibu Makamishna wa Polisi saba (7) ambao ni wanawake. Upandishwaji vyeo wa aina hii ni wa kwanza kutokea katika historia ya nchi yetu.

Ajira na Mafunzo kwa Askari na Watumishi Raia

Mheshimiwa Spika,
napenda nimshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kwa kuipatia Wizara na Vyombo vya Usalama ajira ili kuendelea kuimarisha usalama wa watu na mali zao. Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 Wizara imeajiri jumla ya watumishi 8,542. Katika mwaka 2024/25 Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inatarajia kuajiri jumla ya watumishi 4,857.

Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Wizara, mafunzo ya kuwajengea uwezo yametolewa kwa maafisa, askari na watumishi raia 11,167. Katika mwaka 2024/25 Wizara imepanga kuendelea kutoa mafunzo kwa watumishi 10,640.

Mapitio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2023/24

Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2023/24 Wizara iliidhinishiwa bajeti ya jumla ya Shilingi trilioni 1.29. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2024 jumla ya Shilingi trilioni 1.06 zimepokelewa sawa na asilimia 83 ya bajeti yote iliyoidhinishwa na Bunge. Aidha, jumla ya Shilingi milioni 303.01 zimekusanywa ikiwa ni maduhuli ya Serikali sawa na asilimia 77 ya lengo la mwaka 2023/24.

MAENEO YA KIPAUMBELE KATIKA BAJETI YA MWAKA 2024/25

Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2024/25 Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itatekeleza maeneo sita (6) ya kipaumbele yafuatayo:

Kuendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai;

Kukamilisha, kuendeleza na kuanza ujenzi wa ofisi, vituo na makazi ya askari;

Kuongeza vitendea kazi vya kisasa katika kutoa huduma ikiwemo magari, pikipiki, boti na helkopta;

Kuanza utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Miji Salama (Safer Cities), Mradi wa Ukaguzi wa Magari wa Lazima (Mandatory Vehicle Inspection), Mradi wa Udhibiti wa Barabara Kuu (Highway Patrol);

Kuimarisha mifumo na matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali; na

Kutumia nishati safi kwenye Magereza, Kambi za Wakimbizi na vyuo vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
WhatsApp Image 2024-05-15 at 15.36.06_a2dda141.jpg
JESHI LA POLISI
Mheshimiwa Spika,
wajibu wa Jeshi la Polisi ni kuhakikisha ulinzi wa raia na mali zao unaimarika na amani inatawala nchini ili kuwezesha wananchi kufanya kazi zao za kiuchumi na kijamii. Katika kutekeleza wajibu huo, Jeshi la Polisi hushirikiana na jamii na wadau wengine ili kuhakikisha uhalifu wa aina zote unadhibitiwa. Ushirikiano huu umewezesha nchi yetu kuendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu. Katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 makosa makubwa ya Jinai yaliyoripotiwa katika Vituo vya Polisi yamepungua kutoka 45,485 hadi 43,146 sawa na asilimia 5 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2022/23.

Mheshimiwa Spika, uhalifu umepungua kutokana na Jeshi la Polisi kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kufanya doria, misako na operesheni za kubaini, kuzuia, kutanzua na kupambana na uhalifu katika maeneo ya mijini, vijijini, barabara kuu na mipakani. Aidha, elimu kwa umma juu ya utekelezaji wa dhana ya Ulinzi Shirikishi katika kudhibiti uhalifu inaendelea kutolewa.

Mkakati wa Kuharakisha Upelelezi

Mheshimiwa Spika,
katika kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai, Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi wanaendelea kutekeleza agizo la kukamilisha upelelezi kabla ya kukamata watuhumiwa. Watuhumiwa hao ni ambao makosa yao yanadhaminika kwa mujibu wa sheria. Kwa wale ambao upelelezi umekamilika wanafikishwa mahakamani kwa wakati. Aidha, mafunzo na ukaguzi kwa vitendo umefanyika kwa wapelelezi 2,453 katika mikoa yote. Pia, ukaguzi wa pamoja wa Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, TAKUKURU na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali umefanyika katika mikoa 35 ya Kipolisi.

Hali ya Usalama Barabarani

Mheshimiwa Spika,
hadi Aprili 2024, jumla ya matukio ya usalama barabarani 1,463 yaliripotiwa ikilinganishwa na matukio 1,283 yaliyoripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2022/23. Hivyo, matukio 180 yameongezeka sawa na ongezeka la asilimia 12. Miongoni mwa sababu za ongezeko la ajali za barabarani ni pamoja na mwendokasi, uzembe wa watumiaji wa barabara, ubovu wa miundombinu ya barabara na uchakavu wa vyombo vya moto.

Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi katika kudhibiti ajali za barabarani ni udhibiti wa madereva wa magari ya abiria na mizigo kwa kuhakiki leseni zao na vyuo vinavyotoa mafunzo ya udereva na kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya barabara. Mikakati mingine ni kuongeza doria za masafa katika barabara kuu. Aidha, Jeshi la Polisi limepokea magari 43 yatakayotumika kufanya doria kwenye barabara kuu na kuyasambaza katika mikoa mbalimbali ya Kipolisi ikiwa ni miongoni mwa hatua za utekelezaji wa mkakati huo.
WhatsApp Image 2024-05-15 at 15.36.00_696254ef.jpg
Programu ya Polisi Jamii

Mheshimiwa Spika
, kupitia kauli mbiu ya “Polisi Jamii kwa Ulinzi na Usalama wetu” elimu ya uhamasishaji juu ya masuala ya usalama na uzalendo kwa Taifa imeendelea kutolewa kwa jamii. Elimu hiyo imetolewa kwa katika shule za msingi na sekondari, nyumba za ibada na vituo vya bodaboda kupitia Maafisa wa Polisi Jamii na Askari waliopo kwenye Kata zote 3,956 na Shehia zote 388. Nachukua fursa hii kuwapongeza askari kata wanaotekeleza majukumu yao kwa moyo wa kujituma na ubunifu wa hali ya juu kote nchi nzima. Kwa niaba yao leo tunaendeleza utaratibu wetu tuliojiwekea wa kuwatambulisha mbele yenu, kuwapongeza na tutawazawadia waliofanya vizuri zaidi kwa mwaka huu.

Upatikanaji wa Vitendea Kazi kwa Jeshi la Polisi

Mheshimiwa Spika,
mwezi Machi, 2024 Jeshi la Polisi lilipokea magari 44 aina ya GWM kati ya magari 200 ambayo yanatarajiwa kupokelewa. Magari 156 yaliyobaki yanatarajiwa kuingia nchini wakati wowote. Vilevile, Mhe. Rais ameridhia Jeshi la Polisi kupatiwa Shilingi bilioni 72 kwa ajili ya kununua magari ya polisi kuanzia ngazi ya Taifa hadi Vituo vya Polisi. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 15 zimeshapokelewa na taratibu za ununuzi zinaendelea kwa ajili ya kununua magari 147 ya Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wakuu wa Polisi wa Wilaya zote nchini.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/24 Shilingi bilioni 11.6 zimepokelewa kwa ajili ya ununuzi wa boti 10 za kufanya doria maeneo ya bahari na maziwa kote nchini, pikipiki 19 za kuongoza misafara ya viongozi na magari 24, ambapo mzabuni ameshapatikana. Katika mwaka 2024/25 jumla ya Shilingi bilioni 36 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa magari 181. Aidha, Shilingi bilioni 118.1 zimetengwa ili kununua vifaa vya kijeshi.

Ujenzi wa Nyumba za Makazi, Ofisi na Vituo vya Polisi

Mheshimiwa Spika,
hadi kufikia Aprili, 2024 Jeshi la Polisi limekamilisha miradi 15 ya ujenzi. Miradi iliyokamilika inahusisha ujenzi wa Ofisi za Makamanda wa Mikoa, ujenzi wa Vituo vya Polisi na nyumba za makazi ya askari Polisi kama ilivyooneshwa katika ukurasa wa 20 na miradi inayoendelea imeoneshwa katika ukurasa 21 hadi 22 wa kitabu cha Hotuba yangu, ambayo inajumuisha miradi inayotekelezwa kupitia Mfuko wa Tuzo na Tozo wa Jeshi la Polisi.

Miradi ya Kipaumbele ya Jeshi la Polisi katika Mwaka 2024/25

Mheshimiwa Spika,
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI imekamilisha andiko la mradi wa ujenzi wa Vituo vya Polisi Daraja “C” vya ngazi ya Kata. Utekelezaji wake utaanza katika mwaka 2024/25 ambapo Ofisi ya Rais – TAMISEMI kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa zitajenga vituo vipya vya Polisi Kata 12 na kukamilisha ujenzi wa Vituo vya Polisi Kata 77 vilivyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi. Natumia nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa maelekezo haya ambayo yatasaidia kuongeza kasi ya ujenzi wa Vituo vya Polisi Kata katika mikoa yote. Miradi mingine itakayotekelezwa katika mwaka 2024/25 ni kama ilivyooneshwa katika ukurasa wa 25 hadi 26 wa kitabu cha Hotuba yangu.

Kuboresha Mifumo ya TEHAMA

Mheshimiwa Spika,
kwa kutumia wataalam wa ndani ya nchi, Jeshi la Polisi limetengeneza mfumo wa kielektroniki utakaounganishwa na Taasisi za Haki Jinai (Case File Management Information System). Hadi kufikia Aprili, 2024 Vituo Vikuu vya Polisi (Central Police Stations) katika mikoa 23 vilivyounganishwa kwenye Mkongo wa Taifa vinasomana na mfumo wa kielektroniki wa vituo vya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Mahakama. Kazi ya kuunganisha mikoa mingine inaendelea.

SHIRIKA LA UZALISHAJI MALI LA JESHI LA POLISI

Mheshimiwa Spika,
Serikali inaendelea kuchukua hatua kwa lengo la kuimarisha usalama wa miji na majiji ili kuchochea shughuli za uwekezaji, utalii na ufanyaji wa biashara kwa wananchi na wageni. Hatua hizo ni pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati ifuatayo:

Mradi wa Miji Salama (Safer Cities)

Mheshimiwa Spika,
mradi una lengo la kuboresha mifumo ya usalama iliyopo nchini kwa kutumia teknolojia za kisasa. Mradi utaanza kutekelezwa mwaka 2024/25 katika majiji ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza, ambapo jumla ya Kamera 6,500 zenye Teknolojia ya Akili Bandia (Artificial Intelligency Technology) zinatarajiwa kufungwa katika maeneo mbalimbali. Mkataba wa kibiashara kati ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi na mkandarasi umesainiwa. Utekelezaji wa mradi utaanza baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Mkopo wa Dola za Marekani milioni 145.2 kutoka Serikali ya UAE.

Mradi wa Ukaguzi wa Magari kwa Lazima

Mheshimiwa Spika,
mradi una lengo la kutumia teknolojia ya kisasa na kupunguza ajali za barabarani zinazochangiwa na ubovu wa vyombo vya moto na kuongeza ufanisi kwa kulifanya Jeshi la Polisi kuwa la kisasa na lenye kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Mradi huo utaanza kutekelezwa baada ya taratibu za kumpata mbia kukamilika. Mradi huo wa miaka mitano (5) utatekelezwa kwa mkopo wa Dola za Marakeni milioni 112, sawa na takribani Shilingi billioni 286.16.

Mradi wa Udhibiti wa Barabara Kuu (Highway Road Patrol)

Mheshimiwa Spika,
kutokana na ongezeko la ajali za barabarani utafiti umefanyika na kubainisha maeneo yenye changamoto kubwa ikiwemo barabara ya Dodoma - Dar es Salaam. Taarifa ya upembuzi yakinifu wa mradi imewasilishwa Kituo cha PPP kwa ajili ya uchambuzi. Mradi utatekelezwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na sekta binafsi na utawezesha kufungwa kamera katika maeneo mbalimbali ili kufuatilia mienendo ya madereva na kutoa taarifa za hali za usalama wa barabara kwa watumiaji na kuwawezesha kuchukua tahadhari.

JESHI LA MAGEREZA
Mheshimiwa Spika,
hadi kufikia mwezi Aprili, 2024 jumla ya wafungwa na mahabusu 27,461 walikuwepo katika magereza yote nchini. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 91.8 ya uwezo wa magereza kuhifadhi wafungwa na mahabusu 29,902. Hii ni hatua kubwa iliyofikiwa na Serikali ikilinganishwa na kipindi cha miaka mitano (5) iliyopita, ambapo mwaka 2019/20 kulikuwa na jumla ya wafungwa na mahubusu 38,501. Kupungua kwa msongamano magerezani kumechangiwa na hatua zifuatazo:

Matumizi ya Adhabu Mbadala: jumla ya wafungwa 621 walitolewa magerezani kupitia utaratibu wa Kifungo cha Nje (EML) na wafungwa 93 waliachiliwa huru kupitia huduma za Parole.

Msamaha kwa Wafungwa: Wizara inamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa msamaha wa jumla ya wafungwa 3,326 walioachiwa huru katika siku za Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa.

Ushirikiano na Taasisi za Haki Jinai: Wizara inaendelea kufanya maboresho ya mfumo wa Haki Jinai ambapo watuhumiwa ambao upelelezi haujakamilika na makosa yao yanadhaminika hukaa nje ya magereza kwa dhamana; na

Huduma za Uangalizi wa Wafungwa wa Vifungo vya Nje: Wafungwa 2,675 walihukumiwa kutumikia adhabu zao kwenye jamii. Hatua hiyo pia imeiwezesha Serikali kuokoa jumla ya Shilingi bilioni 3.6 ambazo zingetumika kuwahudumia kwa chakula kama wangeendelea kukaa magerezani.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2024/25 Shilingi bilioni 1 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya upekuzi magerezani. Vifaa hivyo vitafungwa katika Magereza matano (5) ambayo ni: Karanga - Kilimanjaro, Maweni - Tanga, lilungu - Mtwara, Uyui - Tabora na Ruanda - Mbeya.

Huduma za Urekebu

Mheshimiwa Spika
, maboresho ya programu za urekebu, hususan mitaala ya mafunzo kwa Jeshi la Magereza ni maelekezo mahsusi ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kazi ya kuboresha mitaala ya mafunzo ya vyuo vya magereza imefanyika kwa kushirikiana na NACTVET, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na Chuo cha Ustawi wa Jamii. Rasimu ya mitaala hiyo imewasilishwa NACTVET kwa ajili ya kupata idhini ya matumizi. Mitaala hiyo itaanza kutumika katika vyuo vya Jeshi la Magereza mwaka 2024/25.

Matumizi ya Nishati Safi Magerezani

Mheshimiwa Spika
, Jeshi la Magereza linatekeleza mkakati wa nishati safi na hadi kufikia Aprili, 2024 Shilingi milioni 390.1 zimepokelewa kwa ajili ya kujenga mifumo ya bio-gas katika Magereza ya Kimbiji na Wazo Hill – Dar es Salaam pamoja na Ngara – Kagera. Ununuzi wa vifaa kwa ajili ya ujenzi wa mifumo hiyo unaendelea na umepangwa kukamilika mwezi Julai, 2024.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mkakati huo, Jeshi la Magereza linashirikiana na taasisi mbalimbali. Kupitia ushirikiano huo, Kampuni ya Taifa Gesi imefunga mfumo wa gesi (LPG) katika Magereza ya Ukonga – Dar es Salaam na Butimba – Mwanza ambayo ipo katika hatua ya majaribio. Aidha, programu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ya miaka mitatu (2023/24 – 2025/26) itakayogharimu Shilingi bilioni 35.44 imeandaliwa na itatekelezwa kwa kushirikiana na REA. Utekelezaji utafanyika katika vituo 211 vya Jeshi la Magereza vinavyohusisha magereza 129, kambi za magereza 47, vyuo vinne (4) na ofisi za magereza 31.

SHIRIKA LA MAGEREZA (SHIMA)

Mheshimiwa Spika,
Wizara imefanya maboresho ya kimkakati na kiuendeshaji wa Shirika la Magereza ili kujiendesha kibiashara. Maboresho hayo yamesaidia Shirika kutoka kwenye faida ya Shilingi milioni 162.1 mwaka 2021/22 hadi kufikia Shilingi bilioni 3.7 mwaka 2022/23. Aidha, Shirika limeongeza eneo la kilimo kutoka ekari 5,385 mwaka 2022/23 hadi ekari 7,400 katika msimu wa kilimo wa mwaka 2023/24, ambalo ni ongezeko la asilimia 45.

Shughuli za Viwanda na Ujenzi

Mheshimiwa Spika,
Shirika linatekeleza miradi ifuatayo: ujenzi wa miundombinu ya kiwanda cha kuchakata bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro International Leather Company Limited wenye thamani ya Shilingi bilioni 3.6 umefikia asilimia 94 na umepangwa kukamilika Julai, 2024; ujenzi wa majengo ya Ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Iringa wenye thamani ya Shilingi bilioni 1.4 umefikia asilimia 75; na ujenzi wa majengo ya Halmashauri ya Manispaa Singida wenye thamani ya Shilingi milioni 354.3 umefikia asilimia 85. Miradi hii miwili imepangwa kukamilika ifikapo Juni, 2024.

JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI

Mheshimiwa Spika,
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea kuimarisha usalama wa watu na mali zao ambapo hadi kufikia Aprili, 2024 limezima moto na kufanya uokoaji katika matukio 2,756 kwa kushirikiana na wadau. Aidha, ukaguzi wa kinga na tahadhari ya moto ulifanyika kwenye maeneo 58,064 na ramani za majengo 2,134 zimeidhinishwa baada ya kukidhi vigezo vya kinga na tahadhari ya moto. Jumla ya Shilingi bilioni 9.9 zilikusanywa kutokana na shughuli hizo.

Mheshimiwa Spika, vilevile, vikundi 14 vya wazimamoto wa kujitolea (fire volunteers) vimeanzishwa vyenye wanachama 178 katika Mikoa ya Katavi, Morogoro, Mtwara, Mwanza na Tanga. Vikundi hivyo vinasaidia katika utoaji wa elimu na kushiriki kwenye uokoaji pindi majanga yanapotokea.

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha huduma za zimamoto na uokoaji nchini, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limepokea magari 28. Kati ya hayo, magari 15 ni kwa ajili ya shughuli za utawala na ukaguzi wa kinga na tahadhari dhidi ya moto na magari 12 ya kuzima moto na uokoaji yaliyonunuliwa kupitia mkopo wa masharti nafuu uliotolewa na Serikali ya Austria na gari moja (1) la uokoaji ni msaada kutoka Serikali ya Ujerumani. Aidha, Halmashauri ya Mji wa Tunduma imenunua gari moja (1) la kuzima moto. Naipongeza Halmashauri ya Mji wa Tunduma kwa jitihada hizo.

Mheshimiwa Spika,
pia, Shilingi bilioni 1.8 zimepokelewa kwa ajili ya ununuzi wa magari 11 ya utawala na ukaguzi. Magari hayo yatapokelewa katika mwaka 2024/25. Aidha, katika mwaka 2024/25 Shilingi bilioni 1.4 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa magari tisa (9) ya utawala na ukaguzi na Shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kuzima moto na uokoaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha taratibu za upatikanaji wa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 95 uliosainiwa tarehe 15 Februari, 2024 kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya UAE. Aidha, Serikali imechangia Dola za Marekani milioni 5 sawa na asilimia 5 ya gharama za mradi huo, hivyo, ununuzi wote utagharimu Dola za Marekani milioni 100. Kupitia mkopo husika vitendea kazi vya kisasa vitapokelewa katika awamu nne (4) kwa miaka miwili (2) kuanzia 2024/25 hadi 2025/26. Vitendea kazi hivyo ni magari 150 ya kuzima moto na uokoaji, magari 40 ya kubebea wagonjwa, boti 23, command cars 30 na mobile workshops 6, magari matatu (3) ya kuzima moto wa kemikali, Helikopta moja (1), vifaa vya mawasiliano na vya kuzima moto na uokoaji.

Uboreshaji wa Makazi ya Askari na Vituo vya Zimamoto na Uokoaji

Mheshimiwa Spika,
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limekamilisha ujenzi wa majengo sita (6) ya makazi ya kuishi familia 60 za askari katika eneo la Kikombo Jijini Dodoma. Katika mwaka 2024/25 Shilingi bilioni 2.5 zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa majengo mawili (2) yenye uwezo wa kuishi familia 20 za askari katika eneo hilo. Aidha, Shilingi bilioni 2.6 zitatumika kukamilisha ujenzi wa vituo saba (7) vya Zimamoto na Uokoaji katika Mikoa ya Geita, Kagera, Katavi, Manyara, Njombe, Simiyu na Songwe na Shilingi milioni 236.5 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa viwanja vya ujenzi wa makazi ya askari na vituo vya zimamoto na uokoaji. Pia, Shilingi milioni 150 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya Fire Hydrants 140.

IDARA YA UHAMIAJI

Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 jumla ya wageni 1,695,350 waliingia nchini ikilinganishwa na wageni 1,143,645 walioingia katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23. Hili ni ongezeko la wageni 557,705 sawa na asilimia 48. Kuongezeka kwa wageni kumetokana na jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu za kuvutia uwekezaji, utalii, biashara na shughuli nyingine za kijamii.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili, 2024, jumla ya vibali vya ukaazi 18,813 vilitolewa. Katika kuongeza wigo wa uwekezaji kwenye miradi mikubwa ya makazi (Real Estate) na kurahisisha ukaazi wa wageni katika makazi hayo, Kanuni za Uhamiaji za Mwaka 1997, zimefanyiwa marekebisho kupitia Tangazo la Serikali Na. 428 la 2023. Marekebisho hayo yameweka vibali vipya vya ukaazi Daraja C11 kwa wanaotaka kununua nyumba za miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kupitia hotuba yangu ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2023/24 nilitangaza kuondolewa kwa nchi ya Ethiopia katika orodha ya nchi zinazohitaji Visa Rejea. Kufuatia uamuzi huo, napenda kulitaarifu Bunge lako kuwa kuanzia Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 jumla ya Waethiopia 3,569 waliingia nchini kupitia vituo rasmi na 3,531 walitoka ikilinganishwa na Waethiopia 2,290 walioingia nchini na 2,364 waliotoka katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23.

Mheshimiwa Spika, matokeo ya hatua hiyo ya Serikali ni pamoja na: kukusanywa kwa mapato ya Dola za Marekani 178,450 sawa na takribani Shilingi milioni 456 kutokana na huduma za Visa, kuokoa Shilingi bilioni 8.5 ambazo zingetumika kwa gharama za chakula kwa wafungwa raia wa Ethiopia; kupungua kwa wahamiaji haramu; kupunguza msongamano magerezani, ambapo kwa sasa raia wa Ethiopia waliopo magerezani ni 577 ikilinganishwa na 1,205 waliokuwepo mwaka 2022/23.

Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa na Idara ya Uhamiaji

Mheshimiwa Spika
, hadi kufikia Aprili, 2024 Idara ya Uhamiaji imepokea jumla ya Shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi milioni 200.2 ni kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mtwara ambao umefikia asilimia 89.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2024/25 Wizara kupitia Idara ya Uhamiaji itaendelea kuimarisha na kuboresha mifumo ya udhibiti na usimamizi wa uingiaji na utokaji wa watu ili kuhakikisha wanaingia nchini kwa mujibu wa Sheria. Aidha, utekelezaji wa miradi ifuatayo utaanza: ujenzi wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Songwe; ujenzi wa nyumba za makazi ya maafisa katika eneo la Msalato jijini Dodoma; na kuendeleza ujenzi wa makazi ya Wakufunzi katika Chuo cha Raphael Kubaga, Tanga. Jumla ya Shilingi bilioni 2.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi huo.

MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA (NIDA)
Mheshimiwa Spika
, kuanzia Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 jumla ya vitambulisho 7,698,819 vimezalishwa na hivyo kufanya jumla ya vitambulisho vilivyozalishwa kufikia 20,578,325 sawa na asilimia 99 ya idadi ya Namba za Utambulisho 20,701,956 zilizozalishwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2024/25 Shilingi bilioni 2.9 zimetengwa kwa ajili ya kusajili na kutambua watu 2,389,290 wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi mwenye namba ya Utambulisho Tanzania Bara na Zanzibar anapata Kitambulisho cha Taifa. Naomba nitoe rai kwa wananchi wote ambao bado hawajachukua vitambulisho vyao vya Taifa kufika katika ofisi za Serikali za Mitaa walipojiandikisha kwa ajili ya kuvichukua.

Mheshimiwa Spika,
hadi Aprili, 2024 NIDA imeunganisha taasisi 21 katika mfumo wa usajili na utambuzi, hivyo kufanya jumla ya taasisi zilizounganishwa kufikia 107. Katika mwaka wa fedha 2024/25 jumla ya Taasisi 35 za umma na binafsi zinatarajiwa kuunganishwa katika mfumo huo ili kuwezesha ushirikishanaji wa taarifa na hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii. Naomba nitumie fursa hii kuwahamasisha watoa huduma kujiunga na Mfumo wa NIDA ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi za wateja. Taarifa hizo, zitasaidia katika utambuzi wa wananchi kabla ya kutoa huduma na hivyo kupunguza udanganyifu ikiwemo ukwepaji wa kodi, utoaji wa mikopo na usajili wa namba za simu.

HUDUMA KWA WAKIMBIZI
Mheshimiwa Spika,
hadi kufikia Aprili, 2024, Tanzania inahifadhi jumla ya wakimbizi na waomba hifadhi 249,803. Kati ya hao, 160,948 ni wenye asili ya Burundi, 88,257 wana asili ya DRC na 598 ni kutoka mataifa mengine. Waomba hifadhi wapya 3,132 walipokelewa kutoka mataifa mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2024/25, Wizara kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika kambi na makazi ya wakimbizi kwa kufanya doria. Aidha, Wizara itaendelea kusimamia huduma zote muhimu zinazotolewa kwa wakimbizi na jumla ya Shilingi bilioni 1.7 zimetengwa.

USAJILI WA JUMUIYA ZA KIDINI NA ZISIZO ZA KIDINI

Mheshimiwa Spika,
kuanzia Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 jumla ya Jumuiya 213 zilisajiliwa ikilinganishwa na Jumuiya 371 zilizosajiliwa katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23. Kati ya hizo, Jumuiya 95 ni za kidini na 118 zisizo za kidini. Aidha, Wizara imeendelea kufuatilia utendaji wa Jumuiya zilizosajiliwa, kufanya ukaguzi pamoja na kufanya uhakiki wa Jumuiya hizo. Natoa wito kwa watu wote kuhakikisha wanafuata taratibu zote za kisheria katika kusajili Jumuiya na kuepuka kuendesha jumuiya zisizosajiliwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2024/25 jumla ya Shilingi milioni 880.3 zimetengwa kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za Ofisi ya Msajili. Wizara itaendelea kuziratibu na kuzisimamia Jumuiya za Kidini na zisizo za Kidini ili ziendelee kushirikiana na Serikali katika kudumisha amani, utulivu na usalama nchini. Aidha, Wizara inaendelea kuwahamasisha Viongozi wa Jumuiya za Kidini kuendelea kuliombea Taifa na Viongozi wa Kitaifa. Nachukua fursa hii kuwashukuru Viongozi wa Dini kwa kuitikia wito wa mwaliko wa kuhudhuria kwenye tukio hili muhimu. Hii ni ishara ya utayari wa Viongozi wa Dini na Taasisi zake kuendelea kushirikiana na Serikali katika kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa nchi yetu.

UDHIBITI WA USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU
Mheshimiwa Spika,
Wizara imewaokoa waathirika 184 waliokuwa wakitumikishwa kinyume na sheria. Wahalifu wanne (4) waliokuwa wakijihusisha na usafirishaji haramu wa binadamu walihukumiwa kifungo gerezani na watuhumiwa 11 kesi zao zinaendelea. Aidha, elimu kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu imetolewa kwa wadau 157 ambao ni Mahakimu, Waendesha Mashtaka, Polisi, Maafisa Kazi, Maafisa Uhamiaji, Maafisa Ustawi wa Jamii na watoa huduma kutoka taasisi zisizo za kiserikali.

Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha udhibiti wa biashara hii haramu katika pande zote za Muungano, Wizara imefungua Ofisi ya Sekretarieti Zanzibar. Aidha, tarehe 30 Julai, 2023 Wizara ilizindua mtandao wa kupinga usafirishaji haramu wa binadamu. Lengo ni kusaidia jitihada za Serikali katika kutoa huduma kwa waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu na kutoa elimu kwa umma. Mtandao huo unaundwa na mashirika 105 yasiyo ya kiserikali kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2024/25 Wizara imetenga jumla ya Shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya kazi zifuatazo: kujenga nyumba salama ya hifadhi ya muda na ulinzi kwa waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu; kuokoa, kusaidia na kuwaunganisha waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu na familia zao; kuandaa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu; na kutoa elimu kwa umma.

SHUKRANI
Mheshimiwa Spika,
nitumie fursa hii kuwashukuru Mhe. Daniel B. Sillo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Ndugu Ally S. Gugu Katibu Mkuu na Dkt. Maduhu I. Kazi Naibu Katibu Mkuu kwa kunisaidia kusimamia vema utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Vilevile, natoa shukurani kwa: Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi, Camillus M. Wambura; Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Mzee R. Nyamka; Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John W. Masunga; na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna P. Makakala. Pia, nawashukuru Wakurugenzi wa Taasisi na Idara zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuhakikisha uwepo wa amani na utulivu nchini na kuwezesha wananchi kutekeleza shughuli zao za kijamii na kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, pia, natoa shukrani kwa Mhe. Balozi Khamis Kagasheki ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Parole na Inspekta Jenerali wa Polisi Mstaafu Saidi A. Mwema, Mwenyekiti wa Bodi ya SHIMA, pamoja na wajumbe wote wa bodi hizo kwa kusimamia vema bodi husika na kuboresha utendaji kazi. Shukrani nyingine nazitoa kwa watumishi wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, natoa shukrani kwa Serikali za nchi mbalimbali, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Taasisi za Umma, Mashirikia yasiyokuwa ya Kiserikali, Taasisi za Kidini, Vyombo vya Habari na wananchi kwa ujumla kwa kuendelea kushirikiana na Wizara katika kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, mwisho na kwa umuhimu wa kipekee naishukuru kwa dhati familia yangu, Mke wangu Thania Ali Abdulla na Watoto (Riziki, Asha na Bareek), ndugu, marafiki na jamaa kwa kunipa nguvu na moyo wa kutekeleza majukumu yangu katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Aidha, nawashukuru na kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Kikwajuni kwa ushirikiano na imani kubwa wanayoendelea kunipa katika majukumu ya Jimbo letu na Taifa kwa ujumla ambao leo wamewakilishwa vema na Mabalozi wa Chama cha Mapinduzi waliokuja kuniunga mkono, nawashukuru sana.

HITIMISHO
Mheshimiwa Spika
, katika mwaka 2024/25 Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaendelea kuimarisha usalama wa watu na mali zao kupitia vyombo vya usalama vilivyopo chini yake. Jukumu hili litatekelezwa kwa kushirikiana na wadau muhimu wakiwemo wananchi katika maeneo yote nchini.

Makadirio ya Ukusanyaji wa Maduhuli kwa Mwaka 2024/25

Mheshimiwa Spika
, katika mwaka wa fedha 2024/25 Wizara imepanga kukusanya jumla ya Shilingi 403,300,000,000 kupitia vyanzo mbalimbali. Ili kuhakikisha kiasi hicho cha fedha kinakusanywa, Wizara itaimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa maduhuli; kuimarisha huduma za mtandao katika ofisi za uhamiaji; kuongeza wigo wa matumizi ya mfumo wa Uhamiaji Mtandao (e-immigration); na ununuzi wa vitendea kazi.

Maombi ya Fedha kwa Mwaka 2024/25
Mheshimiwa Spika
, naomba Bunge lako liidhinishe Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2024/25 yenye jumla ya Shilingi 1,711,710,987,000. Kati ya fedha hizo, Shilingi 551,583,381,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo, Shilingi 870,429,138,000 ni Mishahara na Shilingi 289,698,468,000 ni fedha za Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha za maendeleo, Shilingi 285,635,968,000 ni fedha za ndani na Shilingi 4,062,500,000 ni fedha za nje.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
 
Back
Top Bottom