BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,124
Majumbani, mitaani, shuleni, nyumba za ibada: mlolongo mrefu wa kuambukizana uzuzu
May 11, 2017 by Jenerali Ulimwengu in Makala
MAKALA yangu iliyopita iligusia suala la elimu inayomjenga mtu kuwa mtimilifu, mtu aliyekamilika. Bila shaka hii ni dhana ya kufikirika, kwa sababu sote tunajua kwamba hakuna binadamu anayeweza kuwa mkamilifu kwa maana kwamba anazo sifa zote anazotakiwa kuwa nazo binadamu. Hata hivyo, tunajua kwamba jitihada kubwa za binadamu huelekezwa katika kutafuta ukamilifu, hata kama tunajua kwamba ukamilifu haupatikani kwa binadamu.
Sote tunazo kasoro zinazotufanya tuwe binadamu, na kwa maana hiyo tunao ndani yetu upungufu ambao ndio unatuhakikishia kwamba tu binadamu, na si malaika au viumbe wengine wa ajabu. Kwa hakika, kutafuta na kusaka hali iliyo ya juu kabisa katika maisha ya binadamu ndiyo shughuli inayomfanya binadamu awe juu ya hayawani. Mbuzi hana shughuli hiyo, wala ng’ombe, wala mbwa mwerevu na mwenye ujanja wa kila aina.
Nilikwisha kujadili jinsi elimu yetu inavyoanzia nyumbani, kijijini na mitaani ambayo ndiyo mazingira yanayotulea, hadi shuleni ambako tunakutana na mfumo rasmi ambao unatufanya tuwe ni sehemu ya jamii pana ya nchi, na pengine hata dunia.
Sasa, tunapotoka nyumbani kwetu na kuingia katika jamii pana, tunakutana na mifumo mingine ya “elimu” ambayo mara nyingi inatufanya tuendelee kuwa mazuzu. Tunaporuhusu watu wajinga watufunze wanachotaka kutufunza, tunakubali kuchukua ujinga wao kama elimu.
Nimejiuliza mara kadhaa ni kwa nini wakuu wa serikali wanahangaika kufukuzana na vivuli vya mitandao ya kijamii inayowasema “vibaya” wakubwa badala ya kushughulikia sumu inayosambazwa wazi wazi na watu wanaotengeneza fedha kutokana na uzuzu wa watu wetu na ambao wanazidi kuongeza nguvu za uzuzu huo.
Mitaani kwetu, kwenye kona za barabara, kwenye matawi ya miti na kwingineko, tunaona matangazo ya waganga wa kila aina wanaodai kila aina ya sifa ya kuponya hiki au kile. Kuna waganga wanaodai wanaweza kutibu magonjwa lukuki, kila aina ya ugonjwa uliowahi kusikika; wengine wanaongeza “nguvu za kiume”; wengine wanawafanya wateja wao wawe na bahati katika mapenzi; wengine wanawawezesha wanafunzi kushinda mitihani, na mambo mengine mengi. Haya yote yangekuwa ni vichekesho na watu wakawa wanasimuliana katika vikao vya kahawa au pombe. Lakini hivi si vichekesho bali ni hatari kubwa kwa jamii inayokubali ujinga wa kiasi hiki. Hii ni jamii ambayo haiwezi hata siku moja kuendelea katika uchumi, au utamaduni, au jambo lolote lile. Ni jamii ya kubaki nyuma milele daima mpaka tutakapoachana na imani hizi za hovyo.
Ni imani hizi hizi zinazowafanya watu wetu, tena wengine wanazo sifa za “usomi” kujazana katika nyumba za ibada mambo-leo wanaambiwa na wachungaji wao kwamba wakiombewa watapata utajiri. Kila Jumapili wanakwenda huko huko na wanaombewa majumba, magari na fedha tele, nao wanaamini kwamba watapata yote hayo , na katika uzuzu wao hawaoni kwamba yule mchungaji aliyekuja na baiskeli miaka mitatu iliyopita ndiye huyu huyu aliyenunua Corolla, kisha Land Cruiser na kisha Hummer ya kwanza, kisha Hummer ya pili ya mkewe na sasa Hummer ya tatu ya kimada wake.
Wanazidi kuwa masikini, “mchungaji” anazidi kuwa tajiri. Wala hawafichi, anawaonyesha wazi wazi, lakini kwa kuwa wamekwisha kupumbazwa, hawaoni na wala hawaelewi. Vituo vingi vya ibada za aina hii vimeanzishwa siku hizi, na inaelekea mtu yeyote anayetaka kutajirika kwa haraka anatakiwa aanzishe ibada ya aina hii kwani mtaji wake mkubwa ni majuha na majuha tunao wengi.
Inaturudisha tena kwa yule bwana wa Loliondo, ambaye miaka michache iliyopita aliweza kulihadaa taifa zima kwa kuwafanya watu waamini, kama watoto wadogo, kwamba kunywa kikombe kimoja cha dawa yake kulitosha kuponya magonjwa kadhaa. Kwamba wakuu serikalini walifanya kazi ya upotoshaji wa bwana huyu, kwamba baadhi ya wakuu wa madhehebu yake nao waliingia katika utapeli huu, ni mambo yanayojulikana na kila mmoja wetu.
Kwamba watu walipoteza muda, fedha na maisha yao kwa sababu walidanganywa na wakadanganyika, hili pia linajulikana. Lakini kisichoeleweka ni kwa nini, baada ya kugundua kwamba ule ulikuwa ni utapeli, taifa hili halijachukua hatua ya kutafakari ili kupata kujua ni nini hasa kilikuwa kimetusibu hadi tukafikia hali kama ile ya uzuzu.
Hii inaweza kuwa na maana kadhaa. Kwanza inawezekana kwamba miongoni mwetu bado wapo watu ambao bado wanaamini kwamba yule bwana alikuwa na uwezo wa kutibu kama alivyodai. Wako watu waliosema hivyo wakati ule, na inawezekana bado wapo wanaoamini hivyo.
Inawezekana pia kwamba wale waliohamasisha misafara ya kwenda Loliondo wanaona haya kwa hicho walichokitenda, hasa kama walikuwa serikalini, na hawataki kukumbushwa jinsi walivyosaidia kusambaza hadaa ya Loliondo. Lakini inawezekana pia kwamba ndivyo tulivyozoea, kwamba jambo la hovyo linafanyika, watu wanaumia, halafu tunasahau, tunasema “yaliyopita si ndwele.”
Tatizo la “yaliyopita si ndwele”ni kwamba iwapo hatufanyi tathmini ya ndwele zilizopita, ipo hatari ya kushambuliwa na ndwele hizo hizo kwa mara nyingine bila kujua. Mimi najua kwamba haitapita muda mrefu kabla hajachomoka mtu mwingine na akatufanyia mambo kama alivyofanya yule bwana wa Loliondo.
Jamii ambayo inakataa kukiri kwamba ilifanya makosa katika siku zilizopita ni jamii ambayo itakuwa inayarudia makosa yale yale. Kukataa kujadili makosa yaliyopita ni njia moja kuu ya kuididimiza jamii katika lindi la “collective imbecilization” ambayo nimekuwa nikiijadili katika mfululizo wa makala hizi.
Watu kufanywa wakaamini kwamba unaweza kupata utajiri kwa kuomba, kupiga makelele na kulia na kugaragara, ni ujuha mkubwa. Kuenea kwa nyumba za ibada zinazohubiri mambo kama hayo ni dalili kwamba ujuha huo umetapakaa, na akili za watu zimetekwa.
Kuna kila ishara kwamba sasa tunaunganisha uzuzu katika mlolongo unaoanzia nyumbani, katika familia, kupitia mtaani na kijijini, kupitia shuleni, na kupitia vituo vya ibada. Kila hatua ya maisha yetu kama jamii tunakabiliwa ni mawakala wa uzuzu. Tufanyeje ili tuepukane na uzuzu huu uliotuzunguka?