Majukumu na nafasi ya diwani katika halmashauri | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Majukumu na nafasi ya diwani katika halmashauri

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by LENGISHO, Nov 20, 2017.

 1. LENGISHO

  LENGISHO Member

  #1
  Nov 20, 2017
  Joined: Sep 15, 2017
  Messages: 79
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 25
  Diwani ni nani ?

  Diwani ni mwakilishi wa wananchi katika Halmashauri. Lakini maana hii haitoshi kumwelezea diwani ni Mtu au kiongozi wa aina gani, Tunaweza kuboresha maana hii kwa kusema kuwa :-

  Diwani ni kiungo na kitovu cha mawasiliano kati ya wananchi ndani ya kata na Halmashauri.


  Majukumu na kazi za Diwani zimegawanyika katika makundi matatu makubwa:

  (a) Kufanya maamuzi kwa kuzingatia madaraka Halmashauri iliyonayo kwa mujibu wa sheria. Katika kufanya maamuzi Diwani anapaswa kukutana mara kwa mara na wakazi wa eneo lake na kujadiliana nao kuhusu masuala yanayohusu ustawi na maendeleo yao ili anaposhiriki katika vikao vya Kamati za Halmashauri awe anazingatia mawazo na matarajio yao;

  (b) Kufuatilia utekelezaji wa maamuzi ya Halmashauri; na

  (c) Kuwaongoza wakazi wa eneo lake katika harakati za maendeleo.

  Majukumu na Kazi za halmashauri

  Chimbuko la majukumu na kazi za Diwani ni majukumu na kazi za Halmashauri kama zilivyoainishwa katika Katiba na Sheria za Serikali za Mitaa. Kwa muhtasari majukumu na kazi za Halmashauri ni pamoja na:

  • Kudumisha na kuendeleza udumishaji wa amani, usalama na utawala bora;

  • Kusukuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo la mamlaka yake na taifa kwa jumla kwa kuzingatia sera za taifa;

  • Kutekeleza upelekaji wa madaraka ya kisiasa, kiuchumi, kifedha, na utawala kwenye ngazi zote za Halmashauri na hasa ngazi za chini za vijiji, vitongoji na mitaa;

  • Kutafuta na kudumisha vyanzo vya mapato ya kutosha ili kuiwezesha kutekeleza majukumu na kazi zake;

  • Kuchukua hatua za kuondoa na kuzuia uhalifu, kudumisha amani, utulivu na kuwalinda wananchi na mali zao;

  • Kusimamia na kuendeleza kilimo, biashara na viwanda;

  • Kuendeleza na kuhimiza afya bora, elimu na burudani na kukuza maisha ya watu ya kijamii na kitamaduni;

  • Kuchukua hatua za kutunza na kuboresha mazingira ili kuleta maendeleo endelevu n.k.

  Kutokana na majukumu na kazi hizo za Halmashauri, Diwani ana majukumu na kazi zifuatazo:

  (a) Kuwakilisha wananchi katika Halmashauri:

  Diwani aliyechaguliwa katika Kata huwakilisha wakazi wote wa Kata kwenye Halmashauri na kwa ajili hiyo anatakiwa:

  (i) kuwa karibu sana na wapiga kura na kupata ushauri wa wananchi katika mambo yanayotarajiwa kujadiliwa kwenye Halmashauri. Katika kutekeleza jukumu hili Diwani atateua angalau SIKU MOJA KILA MWEZI kukutana na wananchi katika eneo lake la uwakilishi ili kupata maoni yao na kuwajulisha maamuzi ya jumla ya Halmashauri na hatua zilizochukuliwa na Halmashauri kuondoa matatizo yaliyowahi kuelezwa na wananchi wa eneo lake la uchaguzi. Pia Diwani anapaswa kuhudhuria mikutano ya Halmashauri na ya Kamati au Kamati ndogo ambamo yeye ni mjumbe

  (ii) Kufikisha mbele ya Halmashauri na kamati za Halmashauri maoni na vipaumbele vya wananchi ili vijadiliwe na kutolewa maamuzi. Kwa maana hii Diwani anatakiwa kuwa mdadisi, mbunifu na ajue mazingira na hali ya Halmashauri ili fedha na rasilimali za Halmashauri ziweze kuelekezwa katika kutekeleza vipaumbele na mipango ambayo italeta manufaa makubwa zaidi kwa wakazi wa Halmashauri.

  (a) Kuhamasisha Wananchi katika kulipa Kodi na ushuru wa Halmashauri:

  Diwani atawahamasisha na kuwaelimisha wananchi kutambua umuhimu wa kulipa kodi na ushuru wa Halmashauri ili waweze kupatiwa huduma bora.

  (c) Kusimamia Matumizi ya Fedha za Halmashauri:

  Diwani anawajibika kuhakikisha kuwa fedha za Halmashauri zinakusanywa na kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa na kwamba matumizi hayo hayavuki bajeti iliyoidhinishwa.

  (d) Kuwa kiungo kati ya Halmashauri na ngazi za chini za Serikali za Mitaa:

  Kwa mujibu wa mabadiliko ya sheria serikali za Mitaa yaliyofanywa na Sheria Na.6 ya 1999, Diwani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata kwa wadhifa wake. Hakuna shaka kwamba atatumia vikao vya Kamati hiyo kuwasilisha rasmi maamuzi na mapendekezo ya kamati kwenye vikao vya Halmashauri na kufikisha maamuzi ya Halmashauri kwenye ngazi za chini ya Serikali za Mitaa.

  (e) Kuhamasisha Wananchi Kuhusu Vita Dhidi ya Umaskini:

  Diwani kama kiongozi anapaswa kufahamu hali ya kiuchumi na kijamii inayowakabili wananchi anaowaongoza. Kwa maana hiyo, inabidi awaongoze katika kuondokana na baa la umaskini kwa kuhakikisha kuwa mipango ya uzalishaji, uboreshaji wa huduma na shughuli nyingine za maendeleo ambazo zinaweza kuwakwamua wananchi kutoka kwenye dimbwi la umaskini na hivyo kuboresha hali zao za maisha inaandaliwa na inatekelezwa kwa kuwashirikisha kikamilifu wananchi wa mahali husika.

  (f) Kufuatilia utekelezaji:

  Ni kazi na wajibu wa Diwani kuhakikisha kwamba mipango na maamuzi ya Halmashauri vinatekelezwa kama ilivyopangwa. Diwani ana wajibu wa kufuatilia utekelezaji wa miradi na utoaji wa huduma katika eneo analoliwakilisha, kukosoa hatua za utekelezaji au otoaji wa huduma na kupendekeza, pale inapobidi, kwenye vikao vya Halmashauri au Kamati za Halmashauri hatua za kuchukuliwa kurekebisha kasoro zilizoonekana.

  (g) Kutetea Maazimio ya Halmashauri:

  Wakati wa majadiliano katika vikao vya Halmashauri au Kamati zake, Diwani ataelekeza na kutetea maoni yake, au ya wakazi katika eneo lake. Iwapo suala linalojadiliwa litapigiwa kura ili kufikia maamuzi, kura za wengi ndizo zitakazozingatiwa katika kufikia maamuzi rasmi.

  Baada ya uamuzi kutolewa, Diwani anapaswa kuunga mkono uamuzi uliofikiwa na Halmashauri yake licha ya msimamo aliokuwa nao wakati wa kujadili hoja husika.

  Mwisho

  Madiwani wanayo nafasi, wajibu na kazi kubwa sana katika kusimamia utoaji wa huduma na kuchochea maendeleo katika eneo la Halmashauri zao. Zaidi ya hayo, Madiwani wanapaswa kutumia taarifa na habari walizo nazo kuhusu utekelezaji wa miradi na utoaji wa huduma katika maeneo yao ili waweze kushiriki ipasavyo katika mijadala ya Halmashauri na Kamati za Halmashauri na kuhakiki taarifa zinazotolewa na wataalam kuhusu utekelezaji wa mipango na utoaji wa huduma. Ili Madiwani waweze kuwakilisha, kuwaongoza na kuwahudumia wananchi kama inavyostahili, ni budi wawe karibu na wananchi wakati wote kufahamu hali halisi ilivyo na matarajio ya wananchi kuhusiana na hali iliyopo kwa upande wa shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma.
   
 2. F

  Fursa Pesa JF-Expert Member

  #2
  Nov 20, 2017
  Joined: May 30, 2012
  Messages: 2,548
  Likes Received: 992
  Trophy Points: 280
  Somo zuri.
  Nini umuhimu wa Mbunge katika halmashauri yake?
   
 3. Diwani

  Diwani JF-Expert Member

  #3
  Jun 9, 2018
  Joined: Oct 25, 2014
  Messages: 323
  Likes Received: 135
  Trophy Points: 60
  kweli
   
 4. J

  Joseph lebai JF-Expert Member

  #4
  Jun 9, 2018
  Joined: Jul 19, 2017
  Messages: 1,388
  Likes Received: 922
  Trophy Points: 280
  Hongera diwani kwa kutuelimisha, hivi wanalipwa na serikali?
   
 1. This site uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
  By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.
  Dismiss Notice
 1. This site uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
  By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.
  Dismiss Notice
Loading...