Majipu hadharani bunge mafichoni!

leonaldo

JF-Expert Member
Oct 26, 2014
2,583
3,181
  • Wakishamaliza kudhibiti uhuru wa habari bungeni, watahamia hata kwenye shughuli za Serikali. Rais akihutubia mahali, waandishi wa habari wataambiwa wasije na vinasa sauti wala kamera, habari watapewa na TBC.



Katika siku za hivi karibuni, Rais John Magufuli amekuwa akisimamisha kazi maofisa na watendaji wakuu wa idara za Serikali, mtindo maarufu kama
kutumbua majipu.

Hata wanaharakati za haki za binadamu walipomkosoa ametetea hali hiyo akisema watu walipoteuliwa walitangazwa hadharani, isitoshe walipowaibia wananchi hawakujua kama watafukuzwa hadharani.

Hata hivyo, wakati Rais Magufuli akiweka mambo yake hadharani, tangu aingie madarakani, kumekuwa na mazingira magumu ya upatikanaji wa habari bungeni.

Hivi karibuni Bunge la Jamhuri ya Muungano limekataza waandishi wa habari kuingia na vinasa sauti na kamera za video ndani ya ukumbi wa Bunge, badala redio na televisheni zote zinatakiwa kuchukua habari kutoka televisheni ya Bunge.

Taarifa hiyo ya Bunge imekuja hivi karibuni baada ya kutangazwa Februari mwaka huu kukatishwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya televisheni kwa Bunge hilo kwa kile kilichoelezwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Wasanii, Nape Nnauye kuwa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa utangazaji huo.

Nape alisema pamoja na mambo mengine, TBC imekuwa ikitumia zaidi ya Sh4 bilioni kila mwaka kwa matangazo ya moja kwa moja, fedha alizosema ni nyingi kuliko uwezo wa shirika hilo.

Sababu nyingine alizotoa ni pamoja na kuwapotezea muda wa kazi wananchi wakati wa mchana, hivyo alisema kipindi kitakachorushwa moja kwa moja ni cha maswali na majibu, halafu vipindi vya mijadala vitarekodiwa kisha kitaandaliwa kipindi cha saa moja kitakachorushwa saa nne usiku.

Tangazo hilo la Nape lilizua mtafaruku bungeni kwani Wabunge wa kambi ya upinzani walipinga na kuvuruga kabisa mwenendo wa Bunge wakitaka hoja hiyo ilijadiliwe huku uongozi wa Bunge ukipinga. Ilibidi waitwe Polisi wa kutuliza ghasia na kuwaondoa bungeni.

Suala hilo pia lilizua mijadala kwenye vyombo vya habari na mitaani. Maswali yaliyoibuka ni pamoja na gharama za kurusha matangazo hayo, je ni gharama tu au kuna sababu nyingine nyuma yake.

Watu wakahoji kuhusu watu kupoteza muda mwingi kuangalia Bunge, kwani kuna dhambi gani kufuatilia Bunge wakati unafanya kazi hasa kwa wale wanaofanya kazi za ofisini?

Watu wakahoji kuhusu kipindi cha saa moja kitakachoonyeshwa na na TBC baada ya kurekodiwa. Nani anayehariri kipindi hicho na kwa masilahi ya nani?

Maswali mengi yamebaki mpaka leo hayana majibu. Lakini kwa kuwa Serikali ndiyo imeamua, basi; mwenye nguvu mpishe.

Ni wazi kwamba Serikali ya CCM haifurahishwi na uwazi uliokuwapo bungeni. Hivi kama Rais Magufuli ameamua kutumbulia majipu yake hadharani, kwa nini Bunge liendeshewe mafichoni? Nini kinachoogopwa?

Katika Bunge lililopita tulishuhudia mijadala mizito mizito iliyoibuliwa hasa na kambi ya upinzani. Mijadala kama ya kashfa za akaunti ya madeni ya nje (EPA) ya Benki Kuu Tanzania (BoT), Richmond, Tegeta Escrow na taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).

Mijadala hiyo imekuwa ikiibuka baada ya kipindi cha maswali na majibu ambacho sasa Serikali kwa kushirikiana na Bunge hawataki kionyeshwe.

Ilifunika mahali kwa mijadala hiyo wabunge wa kambi ya upinzani walio wachache wanavutia kusikiliza unapofika wakati wa mijadala. Wabunge wa CCM walio wengi walijikita zaidi kuisifu Serikali na kuitetea hata inapofanya madudu.

TMF ilikwama

Kutokana na utamu huo wa Bunge, lilikuwa ni pigo kubwa mno kusema kuwa halitaonyeshwa moja kwa moja. Kwa kuwa sababu kubwa ilitajwa kuwa ni fedha, Mfuko wa Habari Tanzania (TMF) ukajitoa mhanga ukisema uko tayari kufadhili maonyesho hayo ya moja kwa moja.

Siyo vibaya kwa Bunge kuwa na televisheni yake, lakini isiwe sababu ya kuwazuia waandishi wa habari kuchukua habari wanazotaka. Televisheni ya Bunge iwe kwa ajili ya kuelimisha wananchi.

Ni bahati mbaya kwamba katika utawala huu, Serikali ndiyo inayoliendesha Bunge kwa kila hali. Maana yake ni kwamba sasa ile mihimili mitatu yaani Serikali, Mahakama na Bunge inapoteza maana yake.

Haiwezekani Serikali ikaliendesha Bunge kwa kila hali. Sababu inayotolewa ni kwamba hata mabunge mengine ya Jumuiya ya Madola yana mfumo kama huo. Ni sawa, mbona walisema tatizo ni fedha? Mbona fedha zipo?

Hivi Bunge letu limeanza lini kuwa la Jumuiya ya Madola? Au ni lazima kila kitu tufanane kwenye uendeshaji wa Bunge?

Hizi ni fikra za kikoloni. Kwamba kwa kuwa Wazungu ambao ni Waingereza waliotutawala wameamua uendeshaji wa Bunge uwe hivi, sisi Waafrika hatujiongezi hata kidogo tunafuata kila kitu wanachoamua? Hivi Waafrika hatuna fikra zetu kuamua Bunge letu liwe kama tunavyotaka?

Sasa kama huo ndiyo uendeshaji Bunge kwa mfumo wa Jumuiya ya madola, kumbe basi tulikuwa tumepotoka kurusha matangazo ya moja kwa moja kwa muda wote huo?

Tujifunze kutoka Afrika Kusini

Hebu tuangalie kwa mfano Bunge la Afrika Kusini ambalo pia ni la Jumuiya ya Madola. Wakati Bunge letu lina kanuni zinazozuia wabunge kumkosoa Rais wa Jamhuri ya Muungano, wenzetu wanatumia mwanya huo kumkosoa Rais wao, Jacob Zuma bila woga wowote.

Tumeona kwa mfano hivi karibuni wabunge wa Afrika Kusini wakimsulubu Rais Zuma kwa madai ya kutumia vibaya fedha za umma kwa ajili ya ujenzi wa nyumba yake binafsi. kwa mfumo wao, Rais pia anaingia bungeni na anajibu hoja za wabunge.

Kwetu, Rais ni kama Mungu mtu, hahojiki wala hasemwi kwa lolote. Ukitaka kumsema Rais wetu bungeni, basi umsifie tu. Ukiuliza utaambiwa ni mfumo wa mabunge ya Jumuiya ya Madola.

Sikatai na wala sipingi suala la nidhamu kwa Rais au kiongozi yeyote wa Serikali, lakini kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia lazima ahojiwe.

Leo tunamuona Rais Magufuli akitumbua majipu, siyo kwamba yamezuka tu. Yalikuwapo wakati wa marais wastaafu wakiwa madarakani. Wabunge wa upinzani walipohoji wakaambiwa wanakiuka kanuni za Bunge.

Yale yale waliyohoji, leo ndiyo tunaambiwa ni majipu. Ni suala la wakati na nani aliyeko madarakani. Lakini tunamuona Rais Magufuli ameingia na kasi ya kupambana na ufisadi huku akiua uhuru wa habari nchini. Anataka kujenga mfumo wa kuminya utoaji wa habari bungeni.

Kwanza kwa mfumo wa Bunge letu, Rais wa Jamhuri ya Muungano ana mamlaka makubwa ikiwa pamoja na kuteua Katibu Mkuu wa Bunge.

Kwa madaraka hayo ya Rais tayari Bunge limepoteza uhuru wake kama mhimili mmojawapo wa Serikali.

Bunge kuwa na televisheni yake sawa, lakini ni kuwadhibiti waandishi wa habari kupata habari wanazoziona wakati wowote wawapo bungeni. Unapomzuia mwandishi asiingie na kamera au kinasa sauti maana yake ni kwamba hata uwapo wake bungeni ni sawa na bure.
Source: gazeti la mwananchi

emsuya@mwananchi.co.tz
 
Hizi ndio hoja nzito ambazo serikali inatakiwa izijibu!Mashaka kwa awamu ya nne lazima yawepo!Kama u msafi,kwann unaogopa uwazi?
 
Santuri ya MCC, mshahara na posho ya Rais, Meya wa Dar na Tanga, lugumi naona zimechuja kidogo bora turudi kwenye bunge"live" tena!
 
Back
Top Bottom