Halisi
JF-Expert Member
- Jan 16, 2007
- 2,802
- 612
Imetolewa na:Ni kweli Tanzania inapaa kufikia malengo
· Maendeleo ya kuridhisha yamepatikana katika uchumi, ustawi wa jamii na siasa
· Utafiti unathibitisha asilimia 80.5 ya Watanzania wanaridhika na jitihada za kuleta Maisha Bora Kwa Kila Mtanzania
· Lakini, wapo walalamishi wachache wanaotaka kupotosha ukweli kwa sababu zao za binafsi
KATIKA toleo la Jumatano, Julai 11, 2007, gazeti la Tanzania Daima, linalotolewa kila siku na kampuni ya Free Media Limited zilichapishwa makala mbili zinazokejeli kauli aliyoitoa Waziri Mkuu Edward Lowassa Bungeni Dodoma hivi karibuni kuwa Tanzania inapaa akiimaanisha kuwa inapiga hatua katika kujiletea maendeleo.
Makala ya kwanza, yenye kichwa cha habari: Ndege ya Lowassa inayopaa na abiria walioachwa wameduwaa! imeandikwa na anayejiita M.M. Mwanakijiji ambaye, japokuwa hakujieleza katika makala hiyo, lakini anafahamika kuwa ni Mtanzania anayeishi Marekani. Ya pili, yenye kichwa cha habari: Lowassa: Huu ni mzaha mbaya kwa Watanzania imeandikwa na anayejiita Chris Alan, ambaye haikuelezwa kuwa ni Mwandishi wa gazeti hilo au la, au mtaalamu wa jambo Fulani, msomi au ni mtu gani. Hakuweka anuani yake wala namba ya simu.
Makala ni mbili tofauti, lakini zote kwa pamoja zina maudhui yanayofanana: kujaribu kukejeli ukweli kuwa Tanzania inapaa, kwa maana ya kuwa inapiga hatua katika kujiletea maendeleo, kama alivyoeleza Waziri Mkuu.
M.M. Mwanakijiji anaanza kwa kunukuu maneno ya Mwalimu Nyerere kuwa maendeleo maana yake ni maendeleo ya watu. Vile vile hapa anajibiwa kwa kutumia kaulimbiu ya Mwalimu Nyerere: Maadui wetu watatu wakubwa wa maendeleo ya Taifa letu ni Umaskini, Ujinga na Maradhi.
Serikali ya sasa ya Awamu ya Nne inayaona mambo hayo matatu aliyoyasema Mwalimu Nyerere kuwa bado ni maadui wakubwa wa maendeleo ya Taifa. Umaskini, Ujinga na Maradhi ni mambo yaliyotiliwa maanani katika kupambana nayo na yalizingatiwa katika kuandaa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Serikali hii imedhamiria kwa dhati kabisa kuendeleza mapambano dhidi ya maadui hao na tayari mafanikio yameanza kuonekana.
Ingefaa M.M. Mwanakijiji na Chris Alan wakumbuke kuwa Serikali ya Awamu ya tatu iliweka misingi ya kujenga uchumi imara. Ilijenga sera mbali mbali za kufuatwa katika kurekebisha uchumi. Misingi hii ya uchumi (Kwa Kiingereza: Macroeconomic Fundamentals) ndiyo ambayo mchumi mmoja maarufu Walter Rostow aliita kuwa ni mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kuanza kupaa (Kwa Kiingereza: Pre-conditions for take-off) kuelekea katika kujenga uchumi imara. Hivyo Waziri Mkuu alipotumia neno kupaa alikuwa anamaanisha dhana hiyo ya hatua ya pili ambayo ni take-off baada ya kuwekwa misingi ya kukuza uchumi katika Awamu ya Tatu.
Waziri Mkuu anasisitiza kuwa ahadi za Ilani ya Uchaguzi zinatekelezeka katika kupambana na maadui wale watatu na sasa matokeo yake yameanza kuonekana. Inasikitisha kwamba M.M. Mwanakijiji amepata shida kuelewa dhana hiyo, hata baada ya wiki mbili za kutafakari, kama alivyosem mweyewe. Hata hivyo ifahamike kwamba kujenga uchumi imara na mafanikio hayo yawafikie wananchi siyo kazi ya miezi 18 kama M.M. Mwanakijiji anavyojaribu kupotosha umma wa Watanzania bila kufanya hata utafiti mdogo na kuangalia takwimu na hali halisi. Uelewa mdogo wa M.M. Mwanakijiji sawa na wa mwenzake Chris Alen. Kama watu hao wangekuwa na hoja ya maana wangetoa takwimu katika maeneo yale muhimu yaliyonukuliwa kutoka kwa Baba wa Taifa.
Kupambana na Umasikini: Inashangaza kuwa M.M. Mwanakiji amesahau fursa zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Nne katika mkakati wa kupambana na umaskini sambamba na utekelezaji wa sera za uchumi mpana zinazoendelea. Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia madarakani iliahidi kuongeza ajira kwa vijana ili kukabiliana na umaskini. Ili kuchangia katika utekelezaji wa azma hiyo Serikali ilitenga jumla ya sh. bilioni 21, yaani sh. bilioni moja kila mkoa kwa ajili ya mikopo yenye masharti nafuu kwa wajasiriamali. Mikopo hiyo tayari imekwishatolewa kwa mtu mmoja mmoja na vikundi vya SACCOS. Jumla ya Sh. Bilioni 17.9 tayari zimekwishatolewa na Benki za CRDB na NMB chini ya utaratibu huo.
Katika jitihada za kuondoa umasikini, maendeleo katika sekta ya Kilimo ni muhimu kwa sababu mpaka sasa ndiyo ajira kwa asilimia zaidi ya 80 ya Watanzania. Na kilimo ndiyo tegemeo kwa chakula na kuuza nje mazao kupata fedha za kigeni. Baba wa Taifa alisema Kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu na njia ya kuondokana na umaskini. Tayari Serikali ya Awamu ya Nne imeanza kulitekeleza hili kwa vitendo.
Katika mwaka 2006/2007 Serikali ilitenga Sh. Bilioni 21 kwa ajili ya ruzuku ya mbolea, dawa za mifugo na mbegu bora. Katika mwaka 2007/2008 Sh. Bilioni 19.5 zililitengwa kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo. Aidha fedha zimetengwa kwa ajii ya kuajiri Maofisa Ugani 2,005 na hivyo kukifanya Kiimo kuwa moja ya sekta za kipaumbele kwenye bajeti. Hizi ni jitihada za dhati na makusudi za kupambana na umaskini. Kuna mfano wa hivi karibuni wa maendeleo ya kilimo katika Wilaya ya Mpwapwa. Waziri Mkuu alitembelea Mpwapwa mapema mwaka 2006 kukagua hali ya njaa. Wakati huo wananchi waikuwa wanaomba chakula kutokana na mazao yao kukauka kwa ukame. Serikali iliwapatia chakula cha kujikumu ikiwa ni hatua ya dharura. Pamoja na hatua hiyo Serikali ilisambaza mbegu za mtama na mahindi na kuwakumbusha wanakijiji watekeleze maelekezo ya kila kaya kuwa na angalau eka mbili za mazao ya chakula. Waziri Mkuu ambaye anahudhuria mkutano wa Bunge la Bajeti mjini Dodoma alitumia mapumziko ya mwisho wa wiki Juni 30 2007 kutembelea tena Mpwapwa, zaidi ya kilomita 100 kutoka Dodoma . Katika ziara hiyo ilidhihirika kuwa wananchi wamepata mavuno mazuri na hawana tena njaa.
Waandishi wa Habari waliofuatana na Waziri Mkuu katika msafara huo walishuhudia vihenge vya kuhifadhia mahindi na mtama karibu katika kila nyumba vimejaa mazao. Baadhi ya vihenge hivyo vilikuwa vimeanguka kutokana na uzito wa mahindi! Ipo mifano mingi na ukweli ni kwamba pamoja na ukame wa mwaka 2004 hadi 2006 na athari zake, hakuna mtu aliyekufa na sasa kuna ziada ya mazao. Katika hotuba yaake Bungeni hivi karibuni, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhe. Stephen Wassira, alisema kutakuwa na ziada ya chakula katika msimu wa 2007/2008 ya zaidi ya tani milioni moja kwa kuwa mavuno ya mwaka 2006/7 ni tani milioni 11 wakati mahitaji halisi ni tani milioni 10!
Kufuta Ujinga: Haieleweki M.M. Mwanakijiji na Chris Alan wanazungumzia Tanzania ipi. Hivi kweli hawana habari kuwa Tanzania imeweza kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kuingia shule za msingi na kufikia asilimia 97.3 kwa mwaka 2007 au kwa makusudi wanakataa ukweli huu usiofichika! Tayari Umoja wa Mataifa umekiri kuwa jitihada hizi za Serikali ya Tanzania zitaifanya kuwa nchi itakayoweza kuandikisha watoto wote wenye umri wa kuandikishwa shule kabla ya mwaka 2015 kama Malengo ya Maendeleo ya Milenia yanavyosema.
Hakuna hakika pia kuwa M.M. Mwanakijiji na Chris Alan wana habari au la kuwa Serikali kwa kushirikiana na wananchi imeweza kujenga shule za sekondari 1,090 katika mwaka mmoja na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari kutoka wanafunzi 243,359 mwaka 2006 hadi 401,011 mwaka 2007, sawa na ongezeko la asilimia 65. Ongezeko hilo limefanya idadi ya wanafunzi walioingia kidato cha kwanza mwaka 2007 kufikia asilimia zaidi ya 87 ya wanafunzi wliofaulu mtihani wa darasa la saba. Hivyo Siyo hivyo, bali udahili wa wanafunzi katika vyuo vikuu umefikia wanafunzi 68,929 katika mwaka 2006/2007 ikilinganishwa na wanafunzi 55,134 katika mwaka 2005/2006. Hili ni ongezeko la wanafunzi 13,795 sawa na asilimia 25. Ni Tanzania hii anayoizungumza Waziri Mkuu ambayo inaanzisha Chuo Kikuu Cha Dodoma kwa kuanza na wanafunzi 1,000 na baadaye kufikia wanafunzi hadi 40,000 ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupiga vita adui Ujinga!! Haya ni mafanikio makubwa ambayo hayajawahi kutokea katika historia ya nchi yetu.
Kupambana na Maradhi: M.M.Mwanakijiji na Chris Alan watakuwa wanakubaliana na Waziri Mkuu na Serikali kuwa afya ni muhimu na haina mbadala na kwamba ili upae ni lazima uwe na afya njema. Serikali imelizingatia jambo hili . Katika mwaka 2006/2007 tu jumla ya zahanati 225 zimejengwa kupitia kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, TASAF. Serikali pia imetenga fedha za kukarabati hospitali 11 za mikoa katika mwaka huu wa fedha. Ili kutimiza azma ya kupiga vita maradhi na kwa kuelewa kuwa wataalamu wa sekta hiimuhimu wanapatiwa mafunzo stahili, kazi ya kusomesha wauguzi na wakunga imeanza. Sh. Bilioni 6 zimetengwa mwaka 2007/2008 kwa kazi hiyo. Ujenzi wa zahanati kwa kila kijiji, kituo cha afya kwa kila kata utaanza mwaka 2008l2009. Wananchi wenyewe, kama walivyofanya katika ujenzi wa shule kwa kuibua miradi hiyo na wao wenyewe pia kuchangia, licha ya msaada wa serikali, wako tayari kwa kazi hiyo! Hawajaka tamaa wala kuikimbia nchi yao na kwenda kuishi ughaibuni kama alivyofanya M.M. Mwanakijiji!
Kuhusu maendeleo kwa jumla, inashangaza kwa nini Mwanakijiji na Chris Alan hawaoni kuwa nchi inapaa. Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni baada ya Utafiti wa 12 wa REDET (Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia nchini Tanzania) katika mikoa yote ya Tanzania (21 ya Bara na mitano ya Visiwani) asilimia 80.5 ya wananchi waliohojiwa wanaridhishwa na utendaji wa Serikali za Mitaa. Msimamo huo wa wananchi unatokana na ukweli kuwa matunda na manufaa ya juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia Halmashauri mbalimbali nchini yameanza kujionyesha katika sehemu za vijiji na mijini, ripoti hiyo imeeleza.
Ni ukweli katika miaka ya karibuni, Serikali Kuu imekuwa ikitoa fedha moja kwa moja kwa Halmashauri zote nchini ili kugharimia mipango na miradi ya maendeleo hasa katika nyanja za elimu, afya, barabara, maji na huduma nyingine za umma.
Ripoti hiyo imesema: Utendaji kazi wa Serikali za Mitaa unaonekana kuwaridhisha watu wengi labda kutokana na mageuzi ambayo yametokea katika mfumo wake wa uendeshaji hasa kwa kuwa mtekelezaji mkuu wa mipango na programu za sarikali zinazojikita katika kuondoa umasikini.
Je, huku siyo kupaa? Sasa maelezo ya M.M. Mwanakijiji kwamba hoja ya Waziri Mkuu kuwa Tanzania imeanza kupaa haina msingi, haina ukweli na imetokana na hisia za kisiasa zaidi kuliko ukweli ardhini zinatokana na utafiti alioufanya wapi? Au maelezo ya Chris Alan kwamba awamu hii (ya nne) bado haijajenga uchumi wowote endelevu ikiwa imewasilisha bajeti ya pili yanatokana na utafiti gain?
Je, umma huu ambao REDET imeugundua katika utafiti kuwa unaridhika na maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanayotokea huko vijijini, ni viongozi wa juu wa CCM. Si wananchi tu wa kawaida waliohojiwa katika utafiti huo!
Je, umma huo ndiyo watu wachache ambao wamebahatika kupanda ndege hiyo wanafurahia viti vyao vya daraja la kwanza huku lile daraja la tatu likiwa tupu na abiria wote wakiwa bado wameachwa Kipawa(eneo karibu na uwanja wa ndege wa Dar es Salam) wakiwa wameduwaa , kama anavyodai M.M.Mwanakijiji?
Je, asilimia 80.5 ya Watanzania waliobainika katika Utafiti wa REDET kuwa wanaona hatua kubwa iliyopigwa kuleta maendeleo ni Mzaha Mbaya kwa Wanzania kama anavyoona Chris Alan?
Wote hao wawili, Mwanakijiji na Chris Alan, walioandika makala hizo mbili katika Tanzania Daima, wanajaribu kutulazimisha tuzikubali na tuzithibitishe hisia zao ambazo kamwe hazilingani na hali halisi ya mafanikio ya jitihada za kuleta maendeleo nchini, kama tunavyoshuhudia katika ripoti iliyotokana na utafiti wa REDET.
Ni ukweli kwamba M.M. Mwanakijiji na hata Chris Alan hawaijui kabisa hali halisi ilivyo sasa Tanzania na hasa vijijini. Ni kweli kwamba ndege ya Tanzania inapaa. Isipokuwa inaelekea M.M. Mwanakijiji na mwenzake Chris Alan wamelala usingizi mzito wakati ndege hii imeanza kupaa. Na kweli tumesema tunataka Maisha Bora kwa Kila Mtanzania. Maisha hayo hayapatikani kulala na na kukaa vijiweni bali kila mmoja atumie fursa zilizowekwa na Serikali kujiendeleza.
Ofisi ya Waziri Mkuu,
S.L.P. 980
DODOMA
Alhamisi Julai 12, 2007