KWELI Maji yanayopatikana maeneo ya Mlima Meru yanasababisha Meno kuwa Meusi au Brown

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
Je, ni kweli maji ya mlima Meru husababisha meno ya watu wa Arusha kuwa meusi kwasababu ya kuwa na asili ya Volkano?

IMG_7103.jpeg
 
Tunachokijua
Mlima Meru huwa na asili ya volkano, kitaalam huitwa stratovolcano/composite volcano ambayo mlipuko wa mwisho unaohusisha Mlima huo ulitokea mwishoni mwa mwaka 1910.

Hupatikana Kusini Mashariki mwa Mkoa wa Arusha ukiwa na urefu wa mita 4,565. Aidha, Mlima huu hutajwa kuwa wa 5 kwa urefu Barani Afrika kwa vipimo vya urefu kutoka usawa wa bahari.

Chanzo cha Meno kuwa Meusi
Japokuwa idadi kamili ya waathirika haifahamiki, muonekano wa meno ya Wakazi wengi wa Mkoa huu huwa na rangi ya brown (hudhurungi) au weusi.

Kitaalam, kubadilika kwa rangi ya meno kutoka weupe kwenda rangi ya hudhurungi, weusi au njano husababishwa na mambo yafuatayo;
  • Vyakula na vinywaji
  • Kutokutunza usafi wa kinywa na meno
  • Magonjwa
  • Matumizi ya baadhi ya madawa
  • Uzee na sababu za kijenetiki
  • Sababu za kimazingira zinazohusishwa na matumizi ya kiasi kikubwa cha madini ya fluoride kwenye maji au vyakula
Fluoride hushika nafasi ya 13 kwa orodha ya madini yanayopatikana kwa wingi kwenye kokwa la dunia hivyo inaweza kutolewa nje ya ardhi ya dunia kupitia mlipuko wa volkano.

Pia, hupatikana kwa wingi kwenye mfumo wa Hydrogen Fluoride (HF) au kwa kiasi kidogo kama NH4F, SiF4, (NH4)2SiF6 na NaSiF6.

Kwa kiasi kikubwa, Fluoride huingia mwilini mwa binadamu kupitia maji ya kunywa. Huhitajika mwilini ili kujenga meno na mifupa imara. Hata hivyo, inapokuwa kwa kiasi kikubwa husababisha kubadilika rangi ya meno kuwa meusi, au yenye rangi ya hudhurungi, hali ambayo kitaalam huitwa Fluorosis.

Weusi wa Meno ya watu wa Arusha unasababishwa na Volkano ya Mlima Meru?
Kwa kurejea mambo yafuatayo, JamiiForums imebaini kuwa Uwepo wa Mlima Meru wenye asili ya Volkano ni sababu inayofanya watu wengi wa Mkoa wa Arusha wawe na meno meusi au ya hudhurungi;
  1. Kama tulivyobainisha awali, mlipuko wa volkano unaweza kusababisha uwepo wa kiasi kikubwa cha Fluoride kwenye mazingira ya eneo husika.
  2. Fluoride hii ikiwa nyingi sana inaweza kusababisha meno ya wakazi wa eneo hilo kuwa na meno meusi au yenye rangi ya hudhurungi.
  3. Arusha ni mkoa ulio na Mlima Meru wenye sifa zote tajwa, ambapo tafiti zimethibitisha kuwa fluoride inayopatikana huko ni chanzo cha weusi wa meno kwa wakazi wa mkoa huo.
Utafiti wa Edikafubeni Makoba wenye kichwa cha habari “Geochemical evaluation of volcanic rocks and soils around Meru volcanic complex, northern Tanzania: Implications for fluorine source, mobility and contamination of groundwater systems” unaeleza kuwa maji yanayopatikana kwenye maeneo yanayozunguka mlima Meru huwa na kiasi kikubwa cha Fluoride kuliko kile kinachotambuliwa Mamlaka za Tanzania ikiwemo TBS cha 4mg/l na kile cha WHO cha 1.5mg/l

Wingi huu usio wa kawaida unaweza kuleta changamoto mbalimbali kwa mhusika ikiwemo kubadilika kwa rangi ya meno.

Pia, Utafiti wa Godfrey K. Mbabaye et al “Fluoride occurrence in domestic water supply sources in tanzania: a case of meru district arusha region” unaonesha kuwa takriban 40% ya wakazi wote wanaopatikana maeneo ya Mlima Meru hutumia maji yenye kiasi kikubwa cha fluoride hivyo nao kuwa hatarini kupata changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo kubadilika kwa rangi ya meno.

Aidha, utafiti huu unashauri uanzishwaji wa mifumo rafiki itakayowezesha maji hayo kupunguziwa wingi wa madini ya fluoride kabla hayajatumiwa.

Uchunguzi uliohusisha watu 1243 wanaoishi maeneo yaliyo karibu na Mlima Meru uliofanywa na Michael C. Latham na wenzie, kisha ripoti yake kuchapishwa ikiwa na kichwa cha habari “The effects of Excessive fluoride intake” unathibitisha pia madai haya ambapo 95% ya watu wote waliofanyiwa uchunguzi walikuwa na meno yenye rangi sababu ya kunywa maji yenye fluoride nyingi.

Hivyo, hii sio nadharia tena bali ni ukweli unaothibitishwa kwa tafiti zilizoainishwa hapa.

Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa changamoto hii husababishwa pia na mambo mengine kama tulivyobainisha kwenye maelezo yetu wakati wa utangulizi.
Je, ni kweli maji ya mlima Meru husababisha meno ya watu wa Arusha kuwa meusi kwasababu ya kuwa na asili ya Volkano?

Je, ni kweli maji ya mlima Meru husababisha meno ya watu wa Arusha kuwa meusi kwasababu ya kuwa na asili ya Volkano?

View attachment 2614886
Mbunge wa ARUMERU mwenyewe meno yameoza na "SI MEUSI " naomba SERIKALI kwakuwa mbenge husika hataki kuwasilisha hoja bungeni basi tujengewe visima na tuletewe mitambo ya kusafisha maji na kuondoa calcim iliyopo kwenye maji ili kunusuru watoto wetu: Arusha unakuta mwanamke mzuri, mweupe na anatabasamu zuri ila meno sasa, naomba sana serikali iingilie kati maana mbunge hajui hata kuongea.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom