Maji ni Mtego wa Umasikini (poverty trap)

Zitto

Former MP Kigoma Urban
Mar 2, 2007
1,562
10,880
Changamoto ya Maji inachangia sana kuwashikilia watu wa vijijini kwenye dimbwi la umasikini na kuongeza tofauti ya kipato Kati ya mijini na vijijini na kati ya wenye nacho na wasio nacho. Gharama za maji ni kubwa mno maeneo ya vijijini kiasi kwamba zinazidi wastani wa pato la mtu mmoja ( per capital income) kwa siku nchini Tanzania.

“Pato la Taifa mwaka 2016 lilikuwa shilingi milioni 103,744,606 kwa bei za mwaka husika. Aidha, idadi ya watu Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa watu 48,676,698 mwaka 2016. Hivyo, Pato la wastani la kila mtu lilikuwa shilingi 2,131,299 mwaka 2016 ikilinganishwa na shilingi 1,918,897 mwaka 2015, sawa na ongezeko la asilimia 11.1. Pato la wastani kwa kila mtu katika Dola za Marekani liliongezeka kutoka Dola 967.5 mwaka 2015 hadi Dola 979.1 mwaka 2016 ikichangiwa na kupungua kwa kasi ya kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania. Mwaka 2015, shilingi ya Tanzania ilipungua thamani dhidi ya dola ya Marekani kwa asilimia 16.8 ikilinganishwa na asilimia 8.8 mwaka 2016.” Hali ya Uchumi wa Taifa Juni 30, 2017. Kwa kutumia takwimu hizi za Serikali Ina maana kila Mtanzania ana kipato cha wastani wa shilingi 2.1 milioni Sawa na USD 980 kwa mwaka.

Hanang wanatumia kipato chao kikubwa kununua Maji

Mwananchi wa kijiji cha Gehandu Huko Hanang Mkoa wa Manyara ananunua maji pipa moja la lita 200 kwa shilingi 7000 na familia moja inahitaji angalau pipa moja kwa siku kwa matumizi ya kujibana kabisa ya maji. Kwa hiyo mwananchi huyu atahitaji takribani shilingi 2.5 milioni kwa mwaka kwa ajili ya Maji tu ya kutumia yeye na familia yake. Kwa familia ya Watu 6, huu ni wastani wa 16% ya kipato cha kila mwanafamilia hata mtoto mdogo wa siku 1 kutumika kununua Maji.

Hivyo familia moja inatumia wastani wa kipato cha mtu mmoja kwa mwaka kwa ajili ya Maji tu. Lazima familia hii iendelee kushikwa kwenye mtego wa umasikini. Mwananchi mmoja kijijini Gehandu alitueleza kuwa bajeti yake yote inaishia kwenye maji wakati wa kiangazi. Alieleza kwa uchungu sana namna anaamka saa 10 alfajiri kufuata Maji kilometa 20 kutoka nyumbani kwake na huko huchukua muda mrefu kwani foleni ni kubwa sana. Hanang hutumia sana Punda kubeba Maji na hubidi wakati mwengine kuyafuata mpaka mkoa jirani wa Singida.

Mijini ni tofauti

Miji mingi nchini kwetu hupata maji kutoka mamlaka za Maji safi na salama. Wastani wa bei ya maji kwa pipa la lita 200 kwa mamlaka za maji nchini ni shilingi 300 tu. Mwananchi wa Uzunguni jijini Arusha au Mikocheni jijini Dar es Salaam au Shanty Town Manispaa ya Moshi au Capri Point jijini Mwanza hutumia wastani wa shilingi 108,000 kwa mwaka kama gharama za Maji kwa familia yake. Ikumbukwe kuwa maji yanayosambazwa na Mamlaka za Maji Mijini ni masafi, yana madawa ya kuua wadudu wanaosababisha magonjwa kama kuhara nk. Mtu wa mjini haoni mzigo mkubwa wa matumizi ya Maji kwenye kipato chake kwani ni chini ya 1% ya wastani wa kipato cha familia ( wastani wa familia 1 watu 6 ). Wakati kule Hanang familia itatumia kipato chote cha mwanafamilia mmoja kununua maji ya familia nzima, Arusha au Dar es Salaam familia itatumia 4% tu ya kipato cha mwanafamilia kugharamia maji ya familia nzima. Hii ni nchi moja yenye mataifa mawili!

Ni zaidi ya Maji

Kwa kuwa maji yanayotumiwa na watu wa vijijini si safi na salama, Wananchi hao hutumia fedha nyingine nyingi zaidi kwenye matibabu kutokana na magonjwa kama kuhara, kichocho, typhoid, amoebae na kadhalika. Serikali inaingia gharama kubwa kununua madawa ya kutibu magonjwa haya kwa watu wa vijijini pale ambapo dawa hizi zinapatikana. Lakini pia nguvu ya kufanya kazi za uzalishaji hupungua kwa sababu ya Watu kuwa na siha duni na hivyo mzunguko wa umasikini kuendelea kuzunguka. Kwa nchi ambayo haina Mfumo madhubuti wa Bima ya Afya kwa Wananchi wake, gharama za Afya kwa masikini ni kubwa mno.

Tufanye nini?

Serikali yeyote makini lazima ijikite kwenye kuboresha hali ya maisha ya Wananchi wake kwa kuwaondolea vikwazo vya Maendeleo na kuvunja mitego ya umasikini ( poverty traps ) inayowashika na kuwadidimiza kwenye umasikini. Maji safi na salama kwa gharama nafuu yaweza kuwa ni hatua kubwa ya kuwaondoa Wananchi kwenye mtego mmoja wapo wa umasikini ( water poverty trap ). Hivyo Serikali iwekeze vya kutosha kwenye usambazaji wa Maji vijijini.

Miradi ya Maji sio miradi rahisi sana hivyo kunahitajika fikra mpya Katika kupata fedha za kujenga miradi ya Maji, kutunza vyanzo vya maji na kuendesha miradi ya Maji. Katika kata ambazo ACT Wazalendo ina madiwani tumeona tufanye majaribio ya ushiriki wa Wananchi kupitia Jumuiya za watumiaji Maji na sekta binafsi Katika kusambaza maji na kuendesha miradi ya Maji. Tunafanya majaribio haya kata za Tomondo Morogoro, Gehandu Hanang na Sumbugu Misungwi. Kupitia majaribio haya tutaweza kuboresha na kushawishi sera ya Taifa ya Maji kutokana na ushahidi kwenye kata hizi.

Ni vizuri Serikali kutazama upya vipaumbele vyake vya kimaendeleo. Kwa mfano kuna tija kujenga barabara ya Morocco - Mwenge Kwa shilingi 80 bilioni wakati Wananchi wa Tomondo, Morogoro wanakunywa Maji na mifugo?

==========​
 
Karibu Mh. Zitto,

Pili pokea salamu zangu maana nimekuwa mlevi wa Sera na aina siasa unazoziendesha!

Tatu, naomba nijikite kwenye hoja thabiti uliyokuja nayo , ni ukweli usiopingika kuwa maji yamekuwa mtego wa masikini hapa nchini kwetu tangu tupate Uhuru na mwarobaini wake haujapatikana!

Kwetu huko Singida hususan wilaya ya Manyoni tumekuwa tukihangaika na shida ya maj mpka tunajihisi sisi sio watanzania, huenda tulizaliwa Tanzania kwa bahati mbaya!

Wakati serikali hii iliyo madarakani ikijinasibu kuwa inatetea wanyonge, huku kwetu wanawake na Dada zetu bila kuwasahau wafugaji hawajui wanapata wapi maji! Nimeshukuru umeamua kuwaamsha wa Tanzania dira na kuelewa kuwa MAJI BADO NI MTEGO WA UMASIKINI HAPA TANZANIA!

HAPO nimejaribu kuelezea hali ilivyo katika vijiji vya kasanii, Chikola,mbugani, sasilo, kashangu, mamba, ukitoa sehemu kama HEKA, wao hawana shida kwani kanisa katoriki la Roma kupitia parokia yao ya heka wananeemeka na maji!

Mh Zitto, angalia wilaya ya Tarime, pamoja na utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu yaliyoko wilayani humo, bado maji ni kitendawili kisicho na majibu! Nimekaa Tarime kwa zaidi ya miaka minne MAJI TARIME NI CHANGAMOTO KUBWA, hiyo ni research ndogo tu ambayo nimeifanya Mh Zitto!

Maswali yangu kwako na wanasiasa wengine:

Je, hawaoni kero hizi?

Je, hama hama za wanasiasa hizi zinatija gani kwa sasa tungali bado tunachangamoto nyingi za kushughulikia?

Chama chako kwa maana ya ACT, kilijipambanua vizuri hapo 2015, na niliamini kinakuja kuwa mbadala wa vyama vya upinzani tulivyo navyo maana havioneshi upinzani wa kweli, lkn sasa naona kinamegukameguk, je, utaweza kuyafanya haya uliyoweza kuyaandika? Au ni kuwahadaa wananchi tu?

Mwisho, japo chama chako kinazidi kumeguka, bado Nina imani na katiba ya chama chenu, natamani kukiona kinasonga mbele!

Wasaalam!
 
Karibu sana Mh umepotea sana jukwaani.

Ni kweli kabisa tatizo la maji vijijini ndio kikwazo kikubwa cha maendeleo na ndio chanzo cha umasikini pia.
Kuna mambo ambayo serikali inayafanya na hayana tija kabisa kwa wananchi kama hili la ukosefu wa maji kwa wananchi vijijini.

Ikumbukwe pia wananchi wa vijijini ni wazalishaji kupitia kilimo, kama kiasi kikubwa cha fedha wanakitumia kugharamia maji, mipango na bajeti ya uzalishaji mali kupitia kilimo japo sio cha kisasa lazima ipungue hatimaye wanaendelea kudumbukia kwenye umasikini.
 
Tatizo ambalo naliona kwa wanainchi ni kwamba wanapenda mteremko sana. Niliishigi Kwimba nakumbuka tulifanyaga mpango wa kupata maji ya bomba tukajichanga changa sisi watumishi wa tatu tukavuta maji yakaja. Cha ajabu nashangaa mama mwenye nyumba akaja na biashara yake ya mama ntilie.

Mi nasema wacha wengine wakose maji tu na waumwe matumbo kwa sababu hawataki kuwajibika maana wanataka maji alafu kuyalipia hawataki.

Mimi nilifundishwa na baba yangu kwamba unafanyia kazi kila kitu. Wanainchi waonyeshe njia sio kukaa na kuletewa mradi
 
Hakuna ubishi kwamba maji ni muhimu. Labda swali kwa Mh. Zitto ni kwamba, analysis hiyo ya gharama ya maji kwa watu wa vijijini, ni kweli kwamba wananchi hao wanacho kipato cha kiasi hicho? Kama maji tu gharama yake ni hiyo, je, mahitaji mengine yanagharimu kiasi gani na kwa kipato kipi?

Aidha, tunapaswa kujiuliza, ni kwa nini vyanzo vya maji vilivyokuwa vinatiririsha maji siku za nyuma vimekauka na kupelekea kuzuka tatizo la maji vijijini?

Kuhusu miundo mbinu ya usafiri na usafirishaji ni muhimu pia kwa vile kutokuwa na ubora unaotakiwa, muda wa uzalishaji na namna ya kufikia masoko huathirika.

Hebu fikiria, kwa mfano; kuna kipindi watu walilalamikia foleni ya magari jijini Dar es Salaam kwamba ilikuwa inatia nchi hasara kwa vile muda mrefu ulikuwa ukitumika kwenye safari badala ya uzalishaji.

Inashangaza na kusikitisha mtu anapokebehi jitihada za kupunguza msongamano wa magari kwa jiji kama la Dar es Salaam.

Cha msingi, nafikiri, ni kuhakikisha kwamba tunatunza vyanzo vya maji na kuhakikisha kwamba miundo mbinu inayojengwa na serikali au wadau wengineo wa maji inajengwa kwa viwango na kulindwa na watumiaji wa maji na wananchi kwa ujumla. Namna nyingine ni kujenga utamaduni wa kuvuna maji ya mvua.

Kama wananchi wa vijijini wanao uwezo wa kutumia kiasi hicho kilichosemwa na Mh. Zitto kwenye kukabiliana na tatizo la maji, iweje wasiwe na uwezo wa kujenga au kununua matenki ili wayatumie kuvuna maji ya mvua? Au iweje halmashauri za Wilaya zisiwe na mkakati wa kujenga mabwawa ili kuvuna maji ya mvua vijijini?
 
Kwanza nikusalimu kaka yangu Zitto

Nimesoma bandiko hili linafikirisha kwa hakika. Kwa ufupi niseme kuna changamoto za aina nyingi zinazotokana ukubwa wa taifa letu. Wakati mahali pengine maji ni tatizo, pengine maji yapo ila tatizo ni ubora wa maji yanayopatikana. Kwenye mikoa mingine tuna maji ila tuna matatizo makubwa kwenye utoaji wa huduma za elimu (mikoa ya Pwani kuna tatizo hilo).

Kimsingi poverty trap ina various dimensions kwenye taifa letu. Vijijini tatizo linaweza maji na mjini tatizo linaweza kuwa mazingira bora ya ushirikishwaji wa vijana kwenye uchumi.

Tunafanyaje?

Ni vema kufanya uchambuzi wa kina kuhusu visababishi vya umasikini kijiografia ili kuwa na vipaumbele vinavyolenga wananchi mmoja mmoja. Vipaumbele tulivyonavyo vinalenga kutimiza ndoto kubwa ya kitaifa ambayo haina ushirikishwaji wa watu wote. Yafuatayo yanaweza kufanyika;

1. Ni wakati wa kuongeza ushirikishwaji wa wadau wote kutatua vipaumbele vya kijiografia. Tuanishe vipaumbele vyetu kimkoa halafu tushirikishe wadau wa maendeleo wakiwamo wenye mitaji na ubunifu wa kutatua changamoto za eneo husika. Hapa namaanisha kama tatizo ni maji tuwe tayari kumpa sekta binafsi kazi ya kuchimba visima karibu na makazi ya wananchi na serikali za mitaa wachangie kiasi pamoja na wananchi. Kwenye maji pia tunaweza kushirikisha wadau kwenye uvunaji kipindi cha mvua na kuweka mifumo sahihi ya utunzaji wa vyanzo vya maji. Rwanda hili eneo wamefanya vizuri sana.

2. Tuviangalie tena vipaumbele vya taifa.
Tunakasumba ya kudhani kila mahala panaweza kuwa ni sehemu ya kujenga viwanda.Viwanda vinahitaji rasilimali nyingi na zinazotegemeana hali ambayo inaweza kutoleta tija. Viongozi wetu wako focused sana kwenye majengo na mitambo bila kuangalia uendelevu wa viwanda husika. Badala ya kung'ang'ana na viwanda majengo tutoe nafasi kwa mambo mengine hasa biashara za huduma na teknolijia. Pamoja na bidhaa za kushika (physical ) tukimbie pia kwenye uwezeshaji wa digital products. Tukiendelea hivi tutajilaumu mbeleni.

3. Tunahitaji mipango endelevu.
Kila tunalofanya liendane na dira yetu ya taifa. Kwa sasa tunachangamoto ya kuamua mambo abruptly bila kuangalia dira yetu. Mipango hii tuhakikishe inashirikisha jamii yote bila kuacha mtu nyuma.
 
Mhe zitto nimefurah Leo nimepata mtu anayeongelea maji kwa nadharia ya uchumi.

Sasa kuna vitu muhimu vitatu ama.vinne ambavyo mimi binafsi nitachangia kwenye hoja hii.

1) Kupata maji (water accessibility): Hili swala ni moja ya vitu ambavyo wewe umeviongelea. Nakiri kwamba ni tatizo kubwa sana kwa wananchi wa vijijin ukilinganisha na wa mjini. Lakini tatizo hili kaweza kuwa linasababishwa na mambo yafuatayo

a) Kutokuwa a vyanzo vya maji vya kutosha hivyo watu kutegemea zaidi maji ya mvua
b) Kuwa na vyanzo lakin Sasa kukakosekana mgawanyo sahihi maji haya. Hili kufanya watu wachache hasa walioko kwenye vyanzo kupata huduma lakin walioko mbali na vyanzo kukosa maji. Hili ndilo huleta migogoro kati ya wakulima, wafugaj na wakazi. Maji hayo hayo mkulima anataka kwaajili ya kilimo, lkn mfugaj anataka kwa ajili ya mifugo yake na bado maji hayo hayo yanahitajika kwa matumizi ya ndani
c) Mabadiliko ya tabia ya nchi. Mai mengi hupokea kwasabb ya ukame mkubwa, lkn pia hata mafuriko huaribu vyanzo hivi vya maji.

2 ) Safe water availability: Hili ni nje kabisa ya accessibility. Na kwenye safe water availability ndipo kuna shida ambayo haiongelewi sana. Unakuta familia hata ni ya mjini inalazimika kutumia gharama kubwa sana kwenye kutibu maji. Wakichemsha kwa Lita 5 familia hutumia sh Adi 1000 kuchemsha maji haya.

Gharama hizi ni gharama ambazo watu wa mjini hiziingia Kila siku. Lkn pia gharama hizi huwa kali zaidi kwa vijijin ambapo mama hulazimika kuokota Kuni kwaajili ya kupika na pia kucjemsha maji. Muda mwingine huyu mama huchoka na kuamua kutumia maji yasiyo salama kwa matumiz ya kunywa.

Kukinzana kwa kauli za viongozi wetu ambapo kwasababu ya kukosekana vipaumbele basi Kila mtu huvutia ngozi kwake.

Waziri wa kilimo atasema watu walime kilimo cha umwagiliaji, waziri wa maji atasema maji yapelekwe kwa watumiaji hasa majumbani, Waziri wa Nishati atasema maji yatumike kwenye kuzalisha umeme. Waziri wa Misitu na Utalii atasema maji yapelekwe kwenye wanyama Pori. Wote hawa ni mawaziri wa serikali moja lakini hawajui kipaumbele ni kipi ili waweze ku-fit kwenye kipaumbele hicho.

Nimechoka kuandika kwenye simu...

Gfsonwin
 
Ni kweli hili ni tatizo. Lakini kwa upande mwingine, na sisi wenyewe ni matatizo makubwa.

Hii hapa ni mifano:
  • Zitto akishatoa lawama, anatoweka hata kurudi kusoma na kutoa michango ya watu wengine hataki. Mfano huu sio kwa Zitto pekee yake bali kwa viongozi wengine. Kila mtu anataka kutoa lawama lakini hataki kuwa sehemu ya ubunifu wa utatuzi.
  • Imefika wakati tuanze kujiuliza je muundo wa serikali uliopo unaweza kutoa ufumbuzi wa matatizo yetu? Serikali kuu ikitoa ufumbuzi wa matatizo ya maji inatoa ufumbuzi kama vile watanzania wote wanaishi kando ya ziwa Victoria au kama watanzania wote wanaishi kwenye ukame. Imefika wakati kila jamii na wakazi waanze kuangalia matatizo yao kutokana na rasimali zinazopatikana katika mazingira yao. Na hii itakufanikiwa iwapo tutaanza de-centralization
  • Tanzania ni moja ya nchi iliyoanza kwa vishindo. Ilianzisha chuo cha maji kusomesha wataalamu. Ilianzisha chuo cha ardhi. Je wapo wapi hao wataalamu?
 
Bwana Zitto, Kosa kubwa lililofanyika na nyie wabunge mlihusika ni pale ambapo miradi wa maji vijijini kupitia mkopo wa benki ya dunia ulifanyika pasipo weledi.

Nitafafanua:

1. Mradi ulihusisha manunuzi ya kimataifa kuanzia utafutaji wa vyanzo vya maji hadi utekelezaji. Hivyo gjarama ikawa kubwa sana.

2. Mradi ulilenga maji ya visima. Kwa kudhani kila eneo la nchi hii lina maji chini ya ardhi. Hata pale kijiji kilikuwa pembeni mwa ziwa waliambiwa kuchimbiwa kisima. Hapakuwa na utafiti madhubuti kuhakikisha kwamba maji chini ya ardhi yapo eneo hisika. Siasa iliingilia hasa diwani au mwenyekiti wa kijiji alipolazimisha kisima kichimbwe nyumbani kwake. Matokeo yake visima vingi vilikosa maji.

3. Dhana ya kila kijiji kuwa na chanzo chake huongeza gjarama za miradi. Huongeza gharama za uendeshji na haiwezekani. Tulitakiwa kuwa na miradi mikubwa ya kuhudumia eneo kubwa. Kuchagua vyanzo vichache visambaze maji nchi nzima. Mijini na vijijini.

Mfano ni kama hii miradi ya kitaifa inavyofanya kazi. Au mradi wa KASHWASA. Maji hutolewa kwenye chanzo kimoja na kusambazwa maeneo mengi ya nchi. Mijini na vijijini.

Nchi hii tunahitaji vyanzo vya maji visivyozidi vitano. Kwanza ni ziwa Victoria. Maji yake yasambazwe mikoa ya Mara, Manyara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Dodoma, Kagera, Singida, Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Pwani, Morogoro, Dar na maeneo ya jirani.

Pili ni bwawa la Stieglers Gorge. Maji yake yasambae maeneo ya Dar, Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Morogoro na Iringa.

Chanzo kingine ni Ziwa Nyasa. Maji yake yasambazwe maeneo ya mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Mbeya, Njombe na Iringa.

Mwisho ni Ziwa Tanganyika ambalo litagawa maji maeneo ya mikoa ya Katavi, Kigoma, Rukwa na maeneo ya jirani.

Mabwawa makubwa kama Mtera na Ziwa Rukwa vitakuwa ni vyanzo vya ziada kwa maeneo ya jirani.

Kusambaza maji kwa kuchimba visima kila kijiji ni aghari sana na si endelevu kuliko BULK SUPPLY.
 
Siku moja tulitembelea sehemu pembezoni mwa nchi, tukahisi njaa ikabidi tuingie kwenye mgahawa wa mama lishe kupata msosi, kwa kuwa tulikuwa na njaa tulikula na tulifurahia sana chakula kilikuwa kizuri.

Tulipomaliza chakula na kuhitaji maji ya kunywa(hapa ni kijijini hakuna maji ya chupa), ndipo tulipopata picha kubwa kuhusu tatizo la maji. Yule mama alituambia kuwa inawapasa kuamka saa kumi alfajiri ili kuwahi kuchota maji ambayo ni ya kisima kilichochimbwa kwa mkono, tulimuuliza umbali wa sehemu wanapochotea maji akatuambuia wanatumia takribani dakika 45 au lisaa limoja, na hutumia kichwa kubeba ndoo. Yule mama ana mabinti wawili kwa mantiki hiyo wakienda wote kisimani wanapata ndoo tatu kwa tripu moja.

Kwa kuwa tulikuwa tumeshiba tukasema tutupie jicho kuangalia katika eneo lile kuna ndoo ngapi za maji, kiukweli kulikuwa na ndoo moja ya maji hayakuwa yamejaa na kulikuwa na ndoo nyingine haina maji ilikuwa na vyombo vilivyotumika. Tafakari ikaanzia hapo: Yapi ni maji ya kunywa? Yapi ni maji ya kunawa? Yapi ni maji ya kuoshea vyombo?

Akili ikaenda mbali zaidi: Huyu bi mkubwa anayetuhudumia au ma binti zake wakitaka kwenda haja/kujisaidia wanatumia maji gani kwa kunawa n.k? Wanapokuwa kwenye siku zao/hedhi wanafanyaje kujistiri kwa kuwa watahitaji maji kujisafisha?

Baada ya hapo nikajisahaulisha na mawazo niliyokuwa nayo tukamuaga bi mkubwa aliyetuhudumia baada ya kumlipa, tukaondoka zetu kuendelea na safari
 
Shida inakuwa kubwa vijijini kwa sababu wasomi wamekosa uzalendo na zaidi tumekuwa wabinafsi kwa kiwango kikubwa mnoo.

Asilimia kubwa tumezaliwa au kukulia vijijini na mjini zimetuleta ajira tu, tena wengine hata hatuna ajira ya maana tunajibanza kwa shemeji.

Hakuna mtu anayeumia kuona wazazi wake, babu, bibi, na ndugu kule kijijini ni masaibu gani wanapitia isipokuwa ni yeye tu KUTOKA KIMAISHA TENA KWA KUYAKIMBIA MAZINGIRA MAGUMU YA KIJIJINI.

Tukirudi likizo hata INTANETI haipatikani tunajioba kama wazungu wa meli, aah huku vipi mtandao shida kabisa.

Kila mtu anaifikilia zaidi nafsi yake, hatufikirii japo hata kizazi chako kijacho wataishi vipi kijijini.
 
Mh. Zitto, kama ulivyo hitimisha kwa swali zuri. Tatizo la hii nchi ni priority!! (vipaumbele!), katika suala la maji hii nchi tumelaliwa kuwa na vyanzo vingi lakini ni kama hatuna macho.

Mfano, Mji wa dodoma na wilaya zake zingeweza kupatiwa maji kwa kujenga mabwawa badala ya kufikiria kusafirisha maji kutoka ziwa victoria. Tuna hazina kubwa ya maji ya chini ya ardhi! Lakini hayatumiki ipasavyo. Mimi nakuunga mkono kwamba tukiboresha huduma za upatikanaji wa maji hasa vijijini tutajikwamua kama nchi kutoka wenye umaskini japo kwa kiasi fulani.
 
Itapendeza zaidi Kitila akipita hapa akachota mawili matatu. Bila shaka ataangalia zaidi big picture badala ya kuanza kuhoji uhalali wa takwimu tajwa maana ukishasogezwa kwenye meza ya JPM, seems akili zinatengana na mwili.
 
Sasa unataka masisiemu yaje kutudanganyia nini ili tuyape kura!?

Hili tatizo la maji halitakiwi liishe maisha! kila mwaka watakuja na ngonjera yao hio, huku vipaumbele ikiwa ni bambardia na yale magari meupe i mean landrova!
 
Kutokuwa na vipaumbele vinavyogusa maisha ya wananchi hasa wa chini ni TATIZO kubwa kwa serikali..

Maji ndio UHAI wa Mwanadamu..

Popote pakishakuwepo na maji, Mwanadamu ataishi..

Unajiitaje Kiongozi wa wanyonge wakati hauwajali katika suala la muhimu kama maji??

Unanunua mindege kwa pesa cash halafu unatamba, mnyonge gani ana uwezo wa kupanda ndege..??

Upofu.
 
Back
Top Bottom