Majanga kuzuia shughuli za muziki si mara ya kwanza nchini

John Kitime

Verified Member
May 25, 2020
6
75
Ukubwa wa janga la Corona umeilazimu serikali kutangaza kusitisha shughuli zenye mikusanyiko ya watu ikiwemo shughuli za muziki. Katika historia yangu kama mwanamuziki, hii itakuwa mara ya tatu kwa muziki kusimamishwa nchini kwa amri ya serikali.

Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1984, wakati huo nikiwa mwanamuziki wa bendi ya Orchestra Mambo Bado, bendi iliyokuwa inaongozwa na Tchimanga Kalala Assossa (Mtoto Mzuri). Bendi ilikuwa ni moja ya bendi zilizokuwa pendwa wakati huo, mtindo wetu ulikuwa ni Bomoa. Neno hili lilitokana na wimbo wa Bomoa Tutajenga Kesho, wimbo ambao baadae kwa sababu ambazo mpaka leo sizijui, ulikuja kupigwa marufuku na Umoja wa Vijana wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati ule. Tukawa tunaupiga dansini tu lakini haukuruhusiwa kupigwa wenye redio ya Taifa, na ndio kilikuwa kituo cha redio pekee nchini.

Orchestra Mambo Bado ilikuwa na watu ishirini hivi, Tchimanga Assossa kiongozi na mwimbaji. George Mzee muimbaji, Lucas Faustin muimbaji, Jenipher Ndesile muimbaji, Banza Tax muimbaji, Athumani Cholilo muimbaji, John Kitime muimbaji, Likisi Matola mpiga gitaa la bezi, Andre Milongo akipiga gitaa la second solo, Huluka Uvuruge na Kazembe wa Kazembe wapiga gitaa la solo, William Maselenge akiwa kwenye gitaa la rhythm, Sadi Mnala alikuwa akizikung’uta drums. Kulikuweko na wacheza show wanne, mafundi mitambo watatu na mweka hazina mmoja na meneja wa bendi.

Tarehe 12 April 1984, kundi zima tulitua katika mji wa Shinyanga baada ya kuwasili hapo kwa treni tukitokea Dar es Salaam, nia ya safari hiyo ilikuwa kuzunguka wilaya zote za Kanda ya Ziwa, na kuporomosha muziki na kupata rizki.

Wanamuziki tulionyeshwa vyumba vya kulala kwenye guest house moja, mambo yalionekana kuwa yatakuwa mazuri kwa siku ile, matangazo yalikuwa yamebandikwa kwenye kuta na nguzo za umeme sehemu mbalimbali za mji, na hali ya kuonyesha kuwa watu walikuwa na taarifa ya ujio wetu.

Ilikuwa ni muda wa saa kumi hivi ilipotangazwa kuwa nchi imepata msiba mkubwa sana. Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine amefariki katika ajali ya gari jirani na Morogoro. Kwanza ilikuwa ni mshtuko, halafu akili ilipotulia tulijua kuwa na sisi kama bendi tunaingia kwenye tatizo kubwa sana, kwanza tulikuwa na nauli ya kuja tu mpaka Shinyanga, na fedha ya kula ya siku moja tulikuwa tunategemea kupiga dansi ili kuweza kulipa malazi ya siku hiyo na kupata fedha ya kula na kuendelea na safari kesho yake. Kwa tangazo la msiba ule mkubwa, tulijua mambo sasa yamebadilika.

Kwanza tulirudisha vyumba vyote mara moja na kubaki na viwili tu kimoja walipewa wasichana waliokuwa kwenye bendi, wengine wote ikalazimu tuhamishie mizigo yetu chumba kilichobaki. Baadae tulikaa na Afisa Utamaduni kutafakari kama dansi lingeweza kulia siku ile, na kama halitalia nini hatima ya watu hawa 20 wageni kutoka Dar es Salaam?

Kama kiasi cha saa moja jioni, Afisa Utamaduni akaruhusu tupige dansi ili tuweze kupata nauli ya kurudi Dar es Salaam, kwani ilijulikana wazi kitaanza kipindi kirefu cha maombolezo na wakati huo madansi yatasimamishwa na hakuna mtu alijua kitaisha lini, hivyo hakukuwa na sababu ya kuendelea na safari kutoka hapo. Maombolezo yalichukua mwezi mmoja, bendi zilizuiwa kupiga muziki katika kipindi hicho.

Bendi tena zilizuiwa tena kupiga muziki ulipotokea msiba wa Baba Taifa. Zuio la kipindi hiki lilikuwa refu zaidi, lilikuwa miezi mitatu. Katika kipindi hicho wanamuziki walitunga nyimbo nyingi za kuomboleza na kuzirekodi wakati wa kipindi cha msiba, wajasilia mali waliweza kupata pesa kwa kuuza kanda za nyimbo hizo, lakini ulikuwa wakati mgumu kwa wanamuziki ambao njia yao pekee ya kuishi na familia zao ni kwa kufanya maonyesho.

Na sasa ni hili janga la korona, na shida ya janga hili ni wazi litaendelea kuweko katika ulimwengu kwa muda mrefu. Shughuli za muziki 'live' zitalazimika kupata sura mpya.
Tunamuomba Mungu maisha yarudi katika kawaida yake mapema.
tangazo orchestra mambo bado.jpeg
 

Dreadnought

JF-Expert Member
Mar 25, 2013
1,312
2,000
Siku zote historia hujirudia, kumbe haya mambo ya kuzuia dansi si mara ya kwanza.

Ahsante kwa historia nzuri mkuu, poleni kwa msiba wa babu njenje.
 

Guasa Amboni

JF-Expert Member
Aug 13, 2015
8,028
2,000
Hii sio hadithi Mkuu. Hadithi maana yake ni jambo la kufikirika sio la kweli
Hadithi yaweza kuwa ya ukweli au uongo au ningeandika KISA? kama inavyotokea katika kitabu au filamu wanaposema Based from the true story nadhani ni hivyo.Ila visa vimezidi siku hizi mpaka visa vya corona? (Jokes )
 

Babu Kingo

JF-Expert Member
Nov 2, 2019
415
250
Ukubwa wa janga la Corona umeilazimu serikali kutangaza kusitisha shughuli zenye mikusanyiko ya watu ikiwemo shughuli za muziki.
NATOA PONGEZI KWA VYOMBO VYA DOLA KUSIMAMIA HILO NA KUZUIA HILO LITAMASHA KWANZA HALINA MAANA, SANA SANA NI KUHAMASISHA STAREHE NA ANASA AMBAZO HAZIMSAIDII MTANZANIA
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom