Majambazi watimka na kuacha SMG yenye risasi 20 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Majambazi watimka na kuacha SMG yenye risasi 20

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, Dec 28, 2010.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Dec 28, 2010
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  WANANCHI wa Kijiji cha Nyamililo katika Kata ya Kasungamile Tarafa ya Katunguru wilayani Sengerema mkoani Mwanza, wamekamata bunduki moja aina ya SMG pamoja na risasi 20,
  baada ya kupambana na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi kwa kutumia mapanga, marungu na mawe.

  Kutokana na tukio hilo, Polisi mkoani Mwanza inawashikilia watu wanne akiwemo Mtendaji wa Kijiji cha Nyamililo, Charles Rushibika (48) na mganga wa kienyeji, Mayalla Shikonoke (72) kwa tuhuma za kufanya ujambazi katika maeneo ya Sengerema, Geita na katika msitu wa kuelekea Katoro, mkoani hapa.

  Aidha, katika tukio hilo, zaidi ya nyumba 10 za wakazi wa kijiji hicho wanaosadikiwa kushirikiana na majambazi hao zimeteketezwa kwa moto na kuharibu mali zote zilizokuwemo, huku watuhumiwa 10 wakiwemo wanawake wanne wakishikiliwa na Polisi wilayani Sengerema.

  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 26, saa 3 usiku katika Kijiji cha Nyamililo wilayani Sengerema.

  Aliwataja wengine wanaoshikiliwa kuwa ni wanawake wawili wanaodaiwa kuwa na uhusiano na kundi la majambazi wanane wanaodaiwa kufanya uhalifu katika maeneo hayo ambao ni Anastazia Kornel (30) na Siwema Julius (18), ambao waliwapeleka polisi mahali ambapo kulifichwa silaha, lakini hawakuzikuta.

  Akifafanua Sirro alisema Desemba 24, mwaka huu walipokea taarifa kutoka kwa raia wema juu ya kuwepo kwa majambazi na kumhusisha mtendaji wa kijiji hicho.

  Alisema walipokamatwa mganga wa jadi, alikiri kuwasafisha majambazi akiwemo mtendaji huyo ili waonekane watu wazuri mbele ya jamii na kwamba wanawake hao walipohojiwa waliwataja majambazi wanne ambao wamekuwa wakifanya uhalifu na kuwapeleka polisi mahali silaha zinapofichwa.

  Alisema Desemba 26 usiku, majambazi watatu wakiwa kwenye pikipiki yenye namba ya usajili T592BKM waliingia kijijini hapo kwa nia ya kufanya uhalifu, lakini waliwashtukia na kuanza kuwarushia mawe ambapo walitelekeza SMG yenye namba UA 8353 waliokuwa nayo na pikipiki kisha kutokomea kusikojulikana.

  Hata hivyo, baada ya majambazi hao kutokomea wananchi waliamua kuiteketeza kwa moto pikipiki hiyo ambayo polisi inamsaka mmiliki wake.

  Kamanda Sirro alisema jeshi la polisi linaendelea kusaka majambazi waliotoroka ikiwa ni sehemu ya operesheni ya kanda ya Ziwa inayoendelea ili kuwezesha wananchi wake kuishi kwa amani.

  Hata hivyo, aliwapongeza wananchi kwa ushirikiano waliuonesha kwa jeshi hilo na kudai kuwa hiyo ni sehemu ya polisi jamii ambapo wananchi wamekuwa wakilinda mitaa yao na kuchukia uovu.

  Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamililo, Happiness Butindi, akifafanua tukio hilo alisema, “na kwa sababu watuhumiwa hao wanafahamika, wakati kundi moja la wananchi likiendelea na
  ufuatiliaji wake……lilikutana na majambazi hao wapatao wawili wakiwa na pikipiki moja ambapo waliwasimamisha, lakini walikaidi hawakusimama ndipo wananchi wakaanza kuwashambulia kwa mawe.”

  Alisema baada ya majambazi hao kuona mashambulizi ya mawe yamezidi kutoka kwa wananchi, waliacha pikipiki yao na kukimbia ili kujinusuru ingawa mmoja wao, mkazi wa kijiji hicho anayetuhumiwa kujihusisha na ujambazi, alijaribu kufungua bunduki waliyoifunga kwenye pikipiki ili kupambana na wananchi hao.

  Alisema mtu huyo alishindwa kuifungua bunduki hiyo na kukimbia, na baada ya watuhumiwa hao kukimbia na kutokomea kusikojulikana, wananchi walipiga yowe na kujikusanya kisha kuanza kuwataja watuhumiwa wengine wa ujambazi na kuanza kuteketeza nyumba zao kwa moto huku nyingine zikibomolewa.

  Kutokana na hali hiyo, mwenyekiti huyo alidai zaidi ya watu 100 ambao ni wakazi wa kijiji hicho hawana makazi kutokana na nyumba zao kuchomwa moto na kubomolewa.

  Pia hawana chakula na mavazi kwa sababu wananchi waliwaondoa raia tu ndani ya nyumba na kisha kuteketeza nyumba na vyote vilivyomo.

  Katika tukio jingine, Polisi Mwanza wanamshikilia Gerald Kalema kwa tuhuma za kukutwa na bastola yenye namba CZ 83 iliyoibwa kwa Revocatus Damas (38) ikiwa na risasi 10.

  Sirro alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi mchana Buzuruga jijini Mwanza akiwa katika harakati za kutafuta majambazi wenzake wataokwenda kushirikiana kufanya uhalifu.

  Alisema alikiri kushiriki katika matukio mbalimbali ya uhalifu, atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
   
Loading...