Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
SERIKALI imesema iko tayari kutoa mitaji kwa Watanzania wenye nia ya kuendeleza viwanda nchini, huku ikikusudia kuchukua hatua za kisheria na kuvirudisha katika miliki yake viwanda vilivyobinafsishwa kwa wawekezaji wa ndani na nje, vilivyoshindwa kujiendesha kwa faida ili kuangalia utaratibu bora wa kuviendesha.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa akizindua Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano 2016/2017, 2020/2021. “Tutachukua hatua za kisheria na kurudisha viwanda serikalini, tumejifunza na tuko tayari kuandaa mitaji kwa Watanzania wenye nia ya kuendeleza viwanda, mtu akiwa na nia ya kuanzisha kiwanda kidogo, cha kati na kikubwa afanye hivyo tumetoa uhuru kwa watanzania wenye mitaji,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema tangu kuanza kwa ubinafsishaji wa mashirika ya umma mwaka 1992, viwanda 106 vilibinafsishwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na lengo lilikuwa zuri la kuongeza ufanisi wa viwanda husika katika uzalishaji, kuvutia mitaji mikubwa na kufufua viwanda husika, teknolojia mpya kuongeza ajira, kupunguza uingizaji wa bidhaa zinazowezesha kuzalishwa hapa nchini na kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi.
Alisema wawekezaji katika viwanda 34 wamefanya vizuri na viwanda vyao vinaendeshwa kwa ufanisi na kuongeza ajira na mapato ya serikali. Waziri Mkuu alisema utafiti uliofanyika, unaonesha wawekezaji katika viwanda 33 wameendesha kwa hasara na wengine katika viwanda 39 vya bidhaa mbalimbali kama ngozi, chuma, korosho, zana za kilimo, sabuni na mafuta ya kupikia wamevifunga au kuvitokomeza kabisa viwanda hivyo kama walivyokubaliana na serikali.
“Ninategemea Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Msajili wa Hazina itaendelea na zoezi la kuchukua hatua za kisheria kuvirejesha viwanda hivyo serikalini kupitia mpango huu wa maendeleo utaangalia utaratibu mwingine ulio bora wa kuviendeleza,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema mpango huo pamoja na mambo mengine utajikita katika kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuendeleza viwanda vikubwa, vya kati, vidogo na vile vilivyobinafsishwa ili kuongeza fursa za ajira na kipato kwa wananchi wengi.
Alisema Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 - 2020/2021 kimsingi unalenga kuboresha maisha ya Watanzania walio wengi kwa kuhakikisha sekta zinazoajiri Watanzania wengi na walio maskini kama vile kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda zinakuwa kwa kasi ya kuridhisha ili kuongeza fursa za ajira na kupunguza umaskini.
Pia alisema kuna miradi iliyopewa sifa ya kuwa miradi ya kielelezo, miradi hiyo ni mikubwa na matokeo yake yanatarajiwa kuwa kichocheo au kuwezesha ufanisi wa utekelezaji na uwekezaji wa miradi mingine.
Miradi hiyo ni kama mradi wa chuma cha Liganga, makaa ya mawe Mchuchuma, maeneo maalumu ya uwekezaji, ujenzi wa reli ya Kati ya matawi yake kwa kiwango cha standard gauge.
Pia alisema serikali inatarajia kufufua Shirika la Ndege la Taifa kuanzia Julai mwaka huu. Aliwataka mawaziri kujipanga upya ili malengo ya mpango huo yanatekelezeka na wakuu wa mikoa wasimame katika kuandaa mazingira wezeshi. “Kila mmoja ajipange kuhakikisha mpango huu unatekelezeka,” alisema.
Source: Habari Leo