Majaliwa, hata huku kuna TRA

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,531
WIKI nne za uhai wa Serikali ya Rais John Magufuli, zimebadili kabisa sura na mwelekeo wa mambo katika taifa letu. Yale tuliyokuwa tunayoana ni ya kawaida na tukazea kuishi nayo, sasa yanatuduwaza, yanatuacha midomo wazi.

Ile nchi tuliyokuwa tunadhani tunaijua na kuwafahamu vyema watu wake ambao ni ndugu na jirani zetu, ghafla tunawashangaa tunawaona kama wale viumbe wasioeleweka wanaoruka angani (UFO ? Unidentified Flying Objects), tumebaki tunatazamana bila kuamini kile kinachotokea, hawakukosea sana wasemao Tanzania ni zaidi ya uijuavyo.

Lakini bila shaka wala sitakosea pia nikisema Serikali ya Magufuli ni zaidi ya unavyodhani unaweza kuitabiri, inajitambua na inawatambua watu wake kwa sifa, hulka na mienendo yao, ndiyo maana ziara ya saa chache pale bandarini ilitosha kupeleka tufani tuliyoishuhudia kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Tufani kama hiyo inatakiwa sana kwenye mifumo yetu inayoongoza na kusimamia michezo hapa nchini. Watu wote makini wanajivunia vijana wao wenye vipaji mbali mbali ambao siyo tu kwamba wanasadia mataifa yao kwa kuyatangaza duniani kupitia michezo mbali mbali wanayoshiriki kwa umahiri mkubwa kimataifa, lakini pia wanapunguza matatizo ya ajira kwa kiasi kikubwa katika mataifa yao.

Katika ulimwengu huu wa leo ambao michezo ni miongoni mwa tasnia zinazopendwa na kuvutia uwekezaji mkubwa duniani kote, hatuwezi kuzungumzia maendeleo ya taifa letu pendwa la Tanzania bila kuweka mifumo imara, nidhamu na uwekezaji wa maana kwenye michezo.

Zamani kidogo tulikuwa maarufu duniani kwa kuzafirisha na kuuza nje pamba, mkonge, chai na kahawa, lakini katika upevu wa teknolojia na utandawazi wa leo bidhaa muhimu na ya kudumu tunayoweza kujivunia leo ni rasilimali watu, mashamba yetu hayawezi tena kutoa dhahabu nyeupe (pamba), hatuwezi tena kuzalisha kahawa ya kiwango bora kama tulivyokuwa, kitu tunachoweza kukifanya na kwa uhakika ni kuwekeza katika viwanjani kwenye vipaji vya vijana wetu.

Tupike vijana wetu katika riadha, soka la kike na kiume, mpira wa kikapu, kuendesha baiskeli, na michezo mingine mingi tu ambayo ikiwekewa miundo mbinu ya maana, itavutia vijana wetu wengi, na hii itatusaidia kwa kiwango kikubwa kuondokana na ?bomu linalosubiri? kulipuka.

Katika taifa ambalo vijana ni kundi kubwa kuliko jingine lolote, kuwaogopa na kuwapa majina ya bomu linasubiri kuleta machafuko katika taifa letu, ni kielelezo cha uwezo duni wa kufikiri. Tukiutumia wingi huu kwa akili nzuri na kwa mipango thabiti na makini, vijana wetu watakuwa tumaini la taifa hili badala ya bomu.

Kama ilivyo kwenye dhamana ya utumishi wa umma, ndivyo ilivyo kwenye dhamana za uongozi wa michezo, kunahitaji nidhamu, bidii, uzalendo na moyo wa kujituma kwa manaufaa ya wengi na kutokuwa na ubinafsi. Hivi ndivyo vilikuwa vikwazo vya maendeleo yetu kama taifa, hivyo ndivyo vinakwaza maendeleo katika sekta ya michezo nchini.

Ninatambua kwamba Msaidizi namba tatu wa Rais Magufuli, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa, ni mwanamichezo.
Si mwanamichezo wa wasi wasi kwa maana ya shabiki tu, ni Mwalimu wa soka kwa taaluma yaani kocha. Timu ya wabunge mashabiki wa Simba wanajua umahiri wake kama kocha wao, kama kuna kitu ?hawatamsamehe? Rais Magufuli ni kuwapokonya kocha wao. Akiwa mwanamichezo anajua kwa uhakika ubabaishaji ulioko katika michezo kuanzia vilabu mpaka vyama vya michezo.

Hivi vimegeuzwa vichaka vya watu kujinufaisha binafsi. Vilabu vyetu vya soka kwa mfano ni kama mali ya mlevi inayoliwa na mgema, vinaedeshwa kihuni, migogoro haiishi, hawafuati Katiba zao wenyewe na wakati mwingine hata sheria za nchi.

Ili uwe na timu ya taifa nzuri ni lazima uwe na vilabu imara, hali haiko hivyo hapa kwetu, mambo yote yako kama ilivyokuwa TRA kabla ya Novemba 5, mwaka huu, mambo yalikuwa yanakwenda kama wote tulivyokuja kujua baada ya ziara fupi ya Waziri Mkuu.

Tunahitaji nidhamu ya namna hiyo katika michezo yetu, ndiyo maana Waziri Mkuu anapaswa kuitupia jicho makini sekta ya michezo kwa kasi ile ile ambayo ameanza nayo kwa kushusha rungu la uwajbikaji kwa maafisa ya mamlaka ya mapato.

Kitu kimoja ambacho tuna uhakika nacho sasa ni kwamba, hakuna kisichowezekana, majuma manne tu ya uongozi wa Serikali ya awamu ya Tano umetuonyesha kwamba kwenye nia njia ipo.

Kama kodi sasa zitaanza kukusanywa kikamilifu, na vyeo vinaanza kuwa dhamana halisi na utumishi wa kweli, bila shaka nidhamu katika michezo inaweza kuja na siku moja Timu zetu mbali mbali za taifa zitatupa raha muda si mrefu.

Chanzo: Raia Mwema
 
Back
Top Bottom