Maisha Bora kwa kila Mtanzania: Je, Mfumo wa Elimu una Mchango gani?

Baraka Sabi

Member
Mar 16, 2017
17
13
Elimu ni ujuzi, maarifa na stadi azipatazo mtu katika mazingira yanayomzunguka ama maisha yake ya kila siku, zinazomwezesha kufanikisha kwa ufanisi na weledi utekelezaji wa majukumu yake kwa faida yake mwenyewe na jamii kwa ujumla.

Chimbuko la mfumo wetu wa Elimu ni kipindi cha mkoloni Muingereza. Shabaha kubwa ya mfumo wake ilikuwa ni kuwapa vijana maarifa kiduchu yatakayowasaidia katika uendeshaji na ufanikishaji wa malengo ya Utawala na Serikali ya Kiingereza. Mfumo huu haukulenga hata kidogo kuwajengea vijana hawa wa kitanzania uwezo wa kujitegemea hata wasipoajiriwa na Serikali ya kikoloni.

Baada ya uhuru, Taifa limeendelea kusafiri na mfumo huu mpaka leo hii. Ndiyo maana vijana wengi wanaohitimu ngazi mbalimbali za Elimu (Drs vii, F4, Vyuo vya kati na Vyuo vikuu) tegemeo lao kubwa ni kuajiriwa na Serikali na si vinginevyo. Inapotokea Serikali imeshindwa ama imechelewa kuwaajiri, vijana hawa hupalalaizi. Si kweli kwamba wanadeka au hawana uwezo wa kufanya kazi mbalimbali, bali ni matakwa ya mfumo uliowapika. Mfumo una sura hiyo na ni lazima maji yafuate mkondo.

Ni wazi mfumo wa Elimu tulionao haukidhi mahitaji ya watanzania katika kuwaletea maisha Bora. Tunahitaji mfumo mpana zaidi (Extended Educational System) utakaotoa ajira kwa wahitimu wetu pindi wamalizapo ngazi mbalimbali za Elimu wasiishie kuitegemea na kuilaumu Serikali yao.

Pamoja na fani zilizopo, bado tunahitaji mfumo unaosadifu pia shughuli za kiuchumi zinazofanywa na jamii ya Kitanzania kama vile; kilimo, ufugaji, biashara, madini, uvuvi nk. ili mtoto anapomaliza ngazi fulani ya Elimu awe na maarifa, ujuzi na stadi juu ya nyanja hizi badala ya kuishia kumwagwa pale anaposhindwa kuendelea na ngazi ya juu. Kwa kufanya hivi, tutaongeza wigo wa ajira na uchumi wa nchi kimsingi utapanda. Hii itatufanya kuyafikia malengo ya Millenia kwa ujasiri mkubwa.

Tunaweza kutumia muda mwingi na rasilimali nyingi kuhubiri maisha Bora kwa kila Mtanzania ila pasipo kutumia mikakati kadha wa kadha bila kusahau ubadilishaji wa mfumo wetu wa Elimu, tutapata taabu sana.

Mungu ibariki nchi yetu Tanzania.
 
Back
Top Bottom