Story of Change Maisha baada ya chuo

Kilenzi _Jr

JF-Expert Member
Sep 10, 2021
306
1,000
Mwaka 2017 wakati nakaribia kumaliza masomo ya shahada yangu ya kwanza pale chuo kikuu cha Sokoine cha kilimo (SUA) nilipata nafasi ya kipekee sana ya kuhubiri mbele ya wanfunzi wenzangu na baadhi ya wakufunzi.

Nilifanikiwa kuhubiri pale kanisa la CCT — SUA na kila aliesikiliza mahubiri yale alipata kujifunza angalau kitu kimoja. Mahubiri yangu yalikua na kichwa kilichosema “the three P’s of life”.

Haikua mara yangu ya kwanza kuhubiri mbele za watu lakini hii imebaki kuwa kumbukumbu ya muhimu sana kwenye maisha yangu. Kila nikikumbuka na kuangalia namna ambavyo yale mahubiri yaliwagusa watu ndivyo ninavyozidi kuamini kwamba Mungu ana jambo lake na maisha yangu.

Kwanini basi nimeamua kugusia kuhusu siku hii na mahubiri niliyoyatoa? Hii siku iliweka alama ya muhimu kati ya maisha yangu ya chuo na yale ambayo nilikuja kuyaanza mtaani.

Kuna maisha baada ya chuo na haychelewi kuja ila jambo la msingi zaidi ni kwamba hakuna kurudi nyuma. Hii ina maanisha kwamba ukimaliza chuo kuna jambo moja tuu ambalo huwezi kulikwepa nalo ni maisha baada ya chuo.

Maisha ya chuo yako tofauti sana na yale unayoyakuta mtaani. Huku mtaani hakuna maigizo kila kitu kipo katika uhalisia wake. Wakati namaliza chuo nilikuwa na mipango na ndoto nyingi sana lakini nilipofika mtaani ilinibidi nivute pumzi kidogo na kupunguza mwendo kwani mambo mengi niliyokuwa nikiyawaza hayakua rahisi kama nilivyodhani.

Huu ni mwaka wa tatu sasa tangu nimalize chuo na kuna mengi sana ambayo binafsi nimejifunza. Naomba nikushirikishe pengine ukapata kujifunza au labda ukampatia mwenye uhitaji wa kujifunza.

Maisha Yako Ni Juu Yako Mwenyewe

Maisha ya chuo hayakua magumu sana kuyaishi kwani kulikuwa na urahisi wa kufanya mambo mengi sana huku majukumu yakiwa machache lakini ukikwama mahali pia ilikua rahisi sana kuchomoka.

Asilimia kubwa ya maisha yangu ya chuo niliyaishi kwa mikopo, nilikua nikiazima pesa kwa marafiki na jamaa ili nilipe sehemu ya ada mwanzoni mwa semester halafu nazirudisha kadri ambavyo boom lilikua likiingia. Wakati huo wengi hawakua na majukumu kwahiyo kupata pesa haikua changamoto kabisa.

Lakini sasa baada ya kumaliza chuo, hakuna kazi na hakuna boom huwezi kusema utapiga simu kwa washkaji wakuazime pesa, na hata kama wakikuazima utazirudisha vipi wakati wewe mwenyewe huna chanzo chochote cha pesa?

Ukiachana na swala la pesa kuna uhalisia mwingine unakutana nao mtaani kuhusu ajira. Ukweli ni kwamba kuipata ajira mtaani hakutegemei sana marafiki uliokua nao wakati ukiwa chuo na wala hakutegemei sana ulipata GPA gani.

Kuna sababu nyingi sana zinazoweza kukupa au kukunyima kazi. Mojawapo ya sababu hizo ni unamjua nani au nani anakujua wewe? Kingine ni ukweli kwamba mahali pekee ambapo unaweza kupata ajira bila kutumia nguvu nyingi sana ni serikalini pekee lakini serikali nayo wala haihitaji sana kuajiri kwa sasa. Wasomi kama wewe wapo wengi sana na tayari walishajaza nafasi.

Kwahiyo basi kama hukutoka chuoni na skills ambazo zinaweza kukusaidia huku mtaani unaweza ukashangaa miaka inakatika tuu na wewe wala huna chochote cha kufanya kinachokuingizia pesa huku deni lako pale bodi ya mikopo likiendelea kukua kwa kasi.

Kila Mtu Anafanikiwa Kwa Wakati Wake

Wazungu wana msemo wao maarufu sana “every dog has its own day” yaani kwa tafsiri isiyo rasmi “kila mbwa ana siku yake”.

Ukifika mtaani unagundua kwamba maisha ni kama yameanza rasmi sasa na labda unahitaji kuwa serious kidogo maana wenzako wanakuacha. Ukiongea na marafiki zako au wale ambao mlihitimu Pamoja unaanza kuona kama vile unachelewa sana.

Kiukweli hakuna kuchelewa wala kuwahi kwenye maisha na nna uhakika umeshawahi kusikia kuhusu time zone na jinsi ambavyo unaweza kuonekana umechelewa na kumbe uko tuu kwenye wakati wako.

Kuna nchi ambazo huwahi kuuona mwaka mpya tofauti na nchi nyingine lakini hii haimaanishi kwamba nchi hizo ni bora zaidi, ni suala la time zone tuu.

Sasa kama unafikiri kwamba umechelewa na pengine huu ni mwaka wako wa kwanza au wa pili mtaani fahamu tuu kwamba wapo ambao huu ni mwaka wao wa tano au wa saba mtaani.

Kuna wale ambao walipata ajira ndani ya mwaka wao wa kwanza mtaani na wapo ambao wanaweza kusubiri muda mrefu zaidi. Ni suala la time zone tuu na kila mtu anayo siku yake ya kwako pia itafika.

Mtaa Nao Ni Shule Pia

Kama bado upo mtaani na haujapata jambo la kufanya linaloendesha maisha yako usiogope sana kwani bado upo shuleni lakini hii ni shule ya mtaa. Shule ya mtaa ni ngumu kidogo maana hakuna mfumo rasmi. Hakuna walimu, hakuna mitihani na hakuna kushindana kwamba nani kafaulu kuzidi mwenzake.

Ili uweze kufaulu katika shule ya mtaa inabidi ujitume sana tofauti na kwenye elimu ya chuo. Huku mtaani hakuna atakaye kufanyia assignment zako wala hutoweza kukopy ya mwenzako na kukusanya maana mtaa unampa kila mmoja assignment ya pekeake.

Naipenda sana shule ya mtaa kwani haibagui. Shule hii haijali wewe ulikua nani chuo na kwamba ulikua ukifaulu au ukifeli masomo yako hapa wote tunawekwa kwenye daraja moja.

Ukiwa mwanafunzi bora wa shule ya mtaa na ukachanganya na kile ulichokipata chuo nina uhakika matokeo utayaona.

Mabadiliko Hayaepukiki

Kuna kitabu kimoja niliwahi kusoma kikanifikirisha sana. Kitabu kinaitwa “who moved my cheese?” kimeandikwa na Spencer Johnson kipitie ukipata nafasi ni kitabu kizuri sana.

Kitabu hiki kinaongelea mabadiliko katika maisha na kazi pia. Jambo la msingi zaidi ambalo kitabu hiki kinajaribu kutuambi ni kwamba mabadiliko yatatokea tuu hilo hatuwezi kulikwepa lakini namna ambavyo tunaweza kuyapokea mabadiliko haya na kufanikiwa kuendelea mbele na maisha.

Mambo mengi yatakuwa mapya katika maisha yako baada ya chuo utakutana na mabadiliko ya aina nyingi sana mtaani lakini inakupasa wewe ujue namna ya kuyapokea na kutafuta kitu cha kufanya juu yake.

Inawezekana Kabisa Kufanya Kazi Tofauti Na Kile Ulichosomea Chuo Kikuu

Wengi wetu tunapomaliza chuo tunakuja mtaani tukiwa tayari kuzifanyia kazi shahada zetu. Mara nyingi tunakua na mtazamo wa kuzitumia shahada hizi aidha kupitia serikalini au kwenye makampuni binafsi.

Ni kweli na ni vizuri kuzitumia shahada zetu kupitia njia hizo lakini vipi kama usipopata nafasi? Idadi ya wale wanaohitimu elimu zao za juu ni kubwa sana kuliko idadi ya nafasi za ajira zilizopo. Ingefaa sana kama tungejiweka tayari kufanya kazi zaidi ya zile taaluma tulizosomea chuoni.

Naamini kwamba chuoni hatukujifunza taaluma pekee bali zilikuwepo na elimu nyingine nyingi sana. Tumia mojawapo kati ya hizo au hata zile ambazo unakutana nazo mtaani.
NB. Usisahau kunipigia kura
 
Upvote 0

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom