JamiiTalks Mahojiano ya moja kwa moja na Mhe. Zitto Zuberi Kabwe katika JamiiForums

Status
Not open for further replies.

JamiiForums

Official JF Response
Nov 9, 2006
6,200
4,984
Habari wana JF,

Kama tulivyoahidi tarehe 19/11/2012 katika Jukwaa la Siasa (katika thread hii), leo tumemkaribisha Mhe. Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia CHADEMA, Zitto Zuberi Kabwe kama mgeni wetu rasmi katika mahojiano ya moja kwa moja.

attachment.php


Tunawashukuru wanachama wote walioshiriki katika kutuma maswali ya kumhoji Mkuu Zitto na pia wale wote waliokuwa wakifuatilia kwa karibu na kusubiri kwa hamu hadi siku ya leo.

Mjadala utaongozwa na AshaDii kwa niaba ya wanachama wa JamiiForums; side comments zitakuwa kwenye Jukwaa la Siasa, hapa - Side comments: Zitto in JF Exclusive Interview on the 22nd of November, 2012

*Kwa wenye access ya kuweza ku-post kwenye forum hii ya Great Thinkers, tunaomba msiingilie mjadala; shiriki kwenye link iliyotolewa ya side comments*

Karibuni
 

Attachments

  • zitto-kabwe.jpg
    zitto-kabwe.jpg
    27.7 KB · Views: 76,845
Wana JF,

Nashukuru kwa mara nyingine tena kwa ushirikiano wenu na pia kwa kupata fursa hii ya kuwawakilisha katika huu mjadala. Nawasihi kila mmoja ya anayefuatilia kuwa makini na kuyasoma vema maswali na majibu yanayotolewa.

Ni matumaini yangu kuwa tutapata 'majibu', 'mitazamo mipya' na mapya juu ya yale ambayo tayari twafahamu juu ya Mh. Zitto Kabwe na yale ambayo yana ambatana nae hasa ki-siasa.

Karibuni saana, na pia Karibu Mheshimiwa Zitto katika huu mjadala.

Mkuu Zitto kwa kuanzia naomba utueleze machache juu ya Zuberi Kabwe, Zitto.
 
Awali ya yote itoe shukrani zangu za dhati kwa kupewa fursa hii adimu ya kuhojiwa na wana JF wenzangu.

Nashukuru pia kwa kuwa ni heshima kubwa sana kwangu maana mimi ni mtu wa pili kufanyiwa mahojiano kama haya baada ya kijana mwenzetu Maxence kama 'founder' wa jukwaa letu. Napenda pia ifahamike kuwa mimi ni mmoja wa wanachama waanzilishi wa jukwaa hili na ninafurahi kuona limekuwa na kwa kweli its a force to reckon with.

Zitto ni Mtanzania aliyezaliwa Kigoma, Kijiji cha Mwandiga. Nimekulia katika kitongoji cha Mwanga, nimekwenda shule ya Msingi Kigoma, Sekondari Kigoma, Kibohehe Moshi, Galanos Tanga na Tosamaganga Iringa. Nimepata Elimu ya Juu Chuo Kikuu cha Zanzibar kwa mwaka mmoja, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Uchumi, Scholarship ya InWent Biashara ya kimataifa na Bucerius School of Law and Business Mineral Economics.

Ninaishi Kijijini Kibingo, Kata ya Mwandiga Wilaya ya Kigoma. Pia Tabata wilaya ya Ilala na Dodoma nyakati za Bunge. Ninaishi na mama yangu mzazi na wadogo zangu.
 
Napenda pia ifahamike kuwa mimi ni mmoja wa wanachama waanzilishi wa jukwaa hili na ninafurahi kuona limekuwa na kwa kweli its a force to reckon with.

Mkuu, nafurahi sana kusikia kuwa wewe ni moja ya waanzilishi wa hili jukwaa. Hilo ni jipya kabisa kwangu, kama ninavyoamini na kwa wengine wengi. Nashukuru kwa taarifa hiyo na majibu ya post yote kwa swali la awali.

Mkuu utaratibu ni kuwa utakuwa unapewa maswali lenye vipengele vya maswali juu ya suala moja. Kwa kufungua rasmi orodha ya maswali hayo nawakilisha swali la kwanza:

A. Zitto na Ombwe la itikadi miongoni mwa vyama vya siasa

Ni dhahiri CCM na Chadema sera zao ni zile zile katika mazingira ya soko huria, tofauti yao pengine ni ukosefu wa sheria zenye meno kudhibiti mambo Fulani Fulani, au mapungufu katika uwajibikaji, utekelezaji n.k; Kutokana na hili, ni vigumu kutofautisha kwa kina CCM ikulu 2015, hasa ile ambayo itaamka kutoka usingizini, na Chadema ikulu 2015 ambayo itapatikana pengine kutokana na vita dhidi ya ufisadi na pia ukali dhidi ya utekelezaji mbovu wa sera za CCM, usimamizi mbovu wa rasilimali za taifa, na tabia ya viongozi kutowajibika.

Hayana yote matatu hayana itikadi, na iwapo CCM itabadilika, Chadema itakuwa katika wakati mgumu kuendelea kuipa ushindani CCM; Ndio maana unakuta comments za Chadema kuhusu mabadiliko ya uongozi CCM etc ni za kuponda tu kwamba ‘hakuna kitakachobadilika', kwani nje ya kusema hayo, hakuna hoja nyingine yenye mashiko kwani hoja ya ufisadi itapotea hivi hivi….

1. Unalizungumziaje Ombwe la Itikadi Miongoni mwa Vyama vyetu vya Siasa, ambapo tangia mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yaingie nchini, ni vigumu kutofautisha itikadi za vyama vya siasa - kinadharia na kivitendo, hasa ukizingitia ukweli kwamba kwa kila chama, sera na itikadi zinazouzwa au kutekelezwa ni za kiliberali, huku wananchi wengi (hasa vijijini) wakiwa hawana ufahamu juu ya madhara na faida ya itikadi hii ni nini.

2. Unaiongeleaje sera ya Majimbo ya CHADEMA?

3. Unaona tofauti ya msingi kati ya CCM na CHADEMA ni IPI?

4. Nini kinakuvutia ndani ya CCM ambacho hakipo CHADEMA?

5. Bado unafikiri wewe kuwa CHADEMA ni tija kwa jamii kuliko kuwa Chama kingine mfano CCM?

6. Unalizungumziaje suala la kuwa na utitiri wa vyama vingi vya siasa vinavyokula pesa za walipa kodi halafu havina tija wala mchango wowote kijamii zaidi ya kutufilisi, je kuna umuhimu wa kuifanyia sheria mabadiliko ili kuwe na limitation mfano, vyama vitatu tu?
 
Maswali marefu sana. Nitajibu kidogo kidogo.

1. Unalizungumziaje Ombwe la Itikadi Miongoni mwa Vyama vyetu vya Siasa, ambapo tangia mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yaingie nchini, ni vigumu kutofautisha itikadi za vyama vya siasa - kinadharia na kivitendo, hasa ukizingitia ukweli kwamba kwa kila chama, sera na itikadi zinazouzwa au kutekelezwa ni za kiliberali, huku wananchi wengi (hasa vijijini) wakiwa hawana ufahamu juu ya madhara na faida ya itikadi hii ni nini.
- Hii ni changamoto kubwa sana kwa nchi yetu. Itikadi za kisiasa husaidia kunyoosha sera za vyama. Hivi sasa chama chochote chaweza kuwa na sera yeyote ile kwa kuwa hakuna uti wa mgongo ambao ni itikadi. Lazima vyama vijipambanue kwa itikadi zao. Kwa kukosekana kwa itikadi zinazoeleweka vyama vimekuwa kama 'electoral machines' tu. Kukosekana kwa itikadi kunafanya vyama kudandia masuala. Mfano juzi hapa mmesikia Mkutano Mkuu wa CCM umeazimia elimu iwe bure.

CHADEMA tulisema hivi mwaka 2010, CCM wakasema huo ni uwendawazimu kwani haiwezekani. Nakumbuka nilikuwa kwenye mdahalo pale Serena (hivi sasa) mwaka 2010, vijana wa CCM wakaniuliza mtapata wapi pesa za kusomesha watu bure. Nikawajibu kama tuliweza kuwasomesha bure kwa Tumbaku, Kahawa na Pamba, tutawasomesha bure kwa dhahabu, tanzanite nk. Leo CCM wanasema elimu bure. Nimemsikia Lowassa juzi anasema inawezekana. Lowassa huyu nilibishana naye sana mwaka 2010 akisema haiwezekani. Huu ni ukosefu wa itikadi sahihi.

Sababu kubwa pia viongozi wetu hawasomi na hivyo bongo zao hazipo 'sharp' kuweza kuona ni mwelekeo gani wa itikadi wa kufuata. At best tunaimba kama kasuku itikadi zilizoendelezwa nje, hakuna originality
 
Unaiongeleaje sera ya Majimbo ya CHADEMA?

- Ni utekelezaji wa kushusha madaraka mikoani, kupanua uwajibikaji na kuleta maendeleo kwa wananchi. Sera hii ya utawala ndio suluhisho la masuala mengi ya uwajibikaji hapa nchini. Kuna haja ya kuwa na DC? Kwa nini wakuu wa mikoa wasichaguliwe na wananchi? Tulipoamua kupendekeza sera hii kwa wananchi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 tuliambiwa sisi tuna lengo la kuleta ukabila nchini. Inawezekana kuna maeneo fulani fulani tulikosea mkakati. Kwa mfano tulianza kusemea suala hili tukiwa mkoani Kilimanjaro, kwa hiyo CCM ikadakia 'unaona wachaga hawa' sasa wanataka ka nchi kao. Kimkakati tulikosea.

Tulipaswa kuzindua sera hii kanda ya Ziwa au kanda ya Kusini. Tulijifunza kutokana na makosa haya. Hivi tumejiandaa vizuri zaidi kuielezea sera hii. Tunataka kuimarisha Halmashauri za Wilaya/Miji/Manispaa/Majiji kwa kuoondoa nafasi ya Wakuu wa Wilaya na kada nzima pale Wilayani. Majukumu yote ya kisiasa ya DC atayafanya Mwenyekiti wa Halmashauri. Majukumu yote ya Kiutendaji ya Ofisi ya DC atayafanya Mkurugenzi wa Halmashauri. Wakuu wa mikoa wachaguliwe na Wananchi moja kwa moja na wawe na 'executive powers' kwa mambo ya mkoa husika. Tutayaweka kisheria mambo haya. Hii mambo ya Rais kuteua wakuu wa Mikoa nchi nzima hapana. Watu wachaguliwe.

Ninaamini kabisa kuwa Sera hii ikitekelezwa tutaweza kutumia rasilimali zetu vizuri na mikoa itashindana kimaendeleo badala ya kushindana kwa namna walivyompokea Rais mkoani kwao
 
Unaona tofauti ya msingi kati ya CCM na CHADEMA ni IPI?
- CCM imeshindwa kupambana na adui ufisadi, CHADEMA tunapambana na tutapambana na ufisadi kwa nguvu zetu zote. CCM inaamini katika soko holela, CHADEMA tunaamini katika soko linalojali. CHADEMA inaamini katika nguvu ya Umma, CCM inaamini katika nguvu ya Dola.
Nini kinakuvutia ndani ya CCM ambacho hakipo CHADEMA?
Sijakiona bado
Bado unafikiri wewe kuwa CHADEMA ni tija kwa jamii kuliko kuwa Chama kingine mfano CCM?
- Jamii imefaidika sana na kuwa kwangu CHADEMA. Kupitia Bunge na nje ya Bunge nimeweza kuisimamia Serikali kwenye mengi na hasa masuala ya rasilimali za Taifa kama madini na kufanikiwa kupata sharia mpya ambayo imetoa fursa kwa Watanzania kufaidika na utajiri wao wa madini. Mengi sana ninayofanya nikiwa CHADEMA nisingethubu kuyafanya ningalikuwa CCM.
Unalizungumziaje suala la kuwa na utitiri wa vyama vingi vya siasa vinavyokula pesa za walipa kodi halafu havina tija wala mchango wowote kijamii zaidi ya kutufilisi, je kuna umuhimu wa kuifanyia sheria mabadiliko ili kuwe na limitation mfano, vyama vitatu tu?
Ndio Demokrasia.

Tusiminye kabisa watu kuwa huru kuanzisha vyama vya siasa. Baada ya muda ni vyama vyenye uwezo wa kukonga nyoyo za wananchi ndio vitabakia. Wala hatuna haja ya kuweka sheria. Huko mbele ninaona Tanzania yenye vyama sio zaidi ya 4. Vyama vikubwa 2, CCM and CHADEMA. na CUF watakuwa a balancing party kama ilivyo LibDems UK au Greens and Liberals Ujerumani. Kwa hali ya sasa ya muungano ninaona kuwa CUF yaweza kuwa kama The Bloc Québécois ya kule Canada. Sioni NCCR ikidumu. Soini future ya UDP bila Cheyo na TLP bila Mrema.

Lakini pia kuna uwezekano mkubwa sana wa Kundi moja la CCM kuunda chama kingine cha siasa ambacho kinaweza kuwa na nguvu hata zaidi ya CHADEMA. Baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 tutaona hivi new configurations. Tuache watu wawe huru kuunda vyama. Vyenye nguvu vitabakia
 
Mkuu Zitto nashukuru kwa majibu yako kina kwa swali la kwanza, swali linalofuata;

B. Zitto na CHADEMA

1) Nini kipaumbele chako cha sasa kama mwanachama wa CHADEMA?

2) Mkuu, ni kweli kuwa CHADEMA ni chama cha kidini/kikabila? Na kama ni kweli, tatizo hilo lishughulikiwe vipi? Kama si kweli, unaweza kuueleza umma wa watanzania una kauli gani juu ya mitizamo hii dhidi ya chama chenu?

3) Mh. Zitto, unaizungumziaje demokrasia ndani ya chama chako katika chaguzi, teuzi na kupanga safu za uongozi?

4) Kwanini CHADEMA haiwatumii viongozi wa Mikoa na Wilaya na badala yake inatuma watu toka makao makuu hata kwa mambo madogo madogo ambayo yangemalizwa na uongozi wa ngazi husika?

5) Mh Zitto, unazizungumziaje harakati za M4C na athari (impact) yake kisiasa na kijamii? Chama kimeweka taratibu gani nzuri za malezi kwa wanachama wapya wanaojiunga kwenye M4C, kama bado, huku si kusuka kamba inayoungua?

6) Inadaiwa hushiriki kikamilifu M4C, ni kweli? Nini kauli yako dhidi ya tuhuma hizi?

7) Je, utaratibu wa kupita mikoani katika kutafuta nafasi ya kugombea uenyekiti kama ilivyokuwa wakati wa Mbowe unafaa au CHADEMA irudi katika utaratibu kama wa CCM?

8) Mhe. Zitto, Viongozi/CHADEMA imekuwa mstari wa mbele kufichua ufisadi. Kuna taarifa kuwa kuna mwanachama wenu katafuna fedha za M4C, ni kweli? Kama ni kweli, ameshughulikiwaje? Kama hajashughulikiwa, ni kwanini mko kimya?

9) Zitto wewe ni naibu katibu mkuu wa CHADEMA, Mara nyingi matamko ya chama yametolewa na Katibu, Mwenyekiti, Mnyika (tangu kabla hajawa msemaji) na mara chache wanasheria km Lissu, Marando na Prof.Safari. Kwanini Zitto umekuwa mbali sana na matamko haya ya CHADEMA ukiwa kama Naibu Katibu mkuu? (Naamini hutojibu ni mgawanyo wa kazi)

10) Unafikiri CHADEMA uliyoikuta mwanzo ndiyo hii ya sasa au kuna mabadiliko? Kama kuna mabadiliko ni yepi na unafanya nini kufanya CHADEMA iwe kama ambavyo ulitaka iwe?

11) Unafikiri namna CHADEMA inavyoendesha siasa zake kuna uwezekano wa kushika dola mapema (2015)? Kama ndiyo kwanini na kama hapana unafikiri mabadiliko gani yanatakiwa kufanyika kuelekea 2015?

12) CCM wanadai kuwa nyinyi CHADEMA hamna presidential materials, una kauli gani juu ya hili?

13) Una muono gani kuhusu upinzani nchini na nini nafasi ya upinzani hasa CHADEMA kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ukilinganisha na chama tawala CCM?
 
Nini kipaumbele chako cha sasa kama mwanachama wa CHADEMA?
- Kutumikia chama chetu kwa nafasi nilizonazo.

Natumia nafasi yangu ya Ubunge na Uwaziri kivuli kuhakikisha kuwa chama kinapata taswira chanya mbele ya jamii, Na kinaleta mabadiliko ambayo chama tawala, yaani CCM, kinashindwa kuwafikishia wananchi. Utaona kwamba, kama unafuatilia Bunge, hakuna mkutano wa Bunge unaopita bila hoja mahususi inayojenga taswira chanya ya chama.

Ni bahati mbaya sana kuwa hatutumii baadhi ya mafanikio yetu Bungeni kwenye ulingo wa siasa ma hivyo kuwaacha CCM wanachukua credits.

Kwa mfano, ni kwanini mafanikio ya hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu hatujayafanyia kazi ya kisiasa? Ingawa hatukufanikiwa kumtoa Waziri Mkuu lakini tuliilazimisha Serikali kufanya mabadiliko. Kikwete alisema ni upepo tu, lakini upepo huu ulikuwa na joto kali ukamshinda na tukaacha yeye achukue credit kwa kazi yetu ya uwajibikaji.

Hoja ya juzi ya Mheshimiwa Halima Mdee kuhusu Ardhi inabidi kuifanya ni ajenda ya kisiasa. Hoja ya Mkonge tulikwenda Tanga na ilikuwa na mafanikio makubwa sana. Hoja ya Mabilioni ya Uswiss nayo tunaiachia wanaisemea watu wa CCM kuififiza. Historia inatuonyesha kuwa hoja zote tulizozitumia vizuri nje ya Bunge zilijenga taswira nzuri ya chama ie Buzwagi na EPA. We ignore this at our own peril
Mkuu, ni kweli kuwa CHADEMA ni chama cha kidini/kikabila? Na kama ni kweli, tatizo hilo lishughulikiwe vipi? Kama si kweli, unaweza kuueleza umma wa watanzania una kauli gani juu ya mitizamo hii dhidi ya chama chenu?
- Chadema ni chama cha kitaifa. Kingekuwa chama cha kidini au kikabila kingefutwa. Katika uongozi wa Chadema unapata watu toka mikoa na kabila mbali mbali, pia watu toka dini mbali mbali. Diversity hii haipatikani katika vyama vingi humu nchini. Nadhani mtazamo huu unapandikizwa na watu ambao hawakipendi chama chetu na wanao ona chama kama threat kwa maslahi yao binafsi.

Pia sisi kama chama tunapaswa kuwa makini sana, hasa viongozi tunapofanya kazi zetu ili kutothibitisha taswira hii mbaya dhidi ya chama chetu. Baadhi ya wanachama wa CHADEMA ndio mabingwa wa kueneza jambo hili. CCM nao humo humo wanapandikiza mbegu za chuki. Unakuta Waziri wa CCM anamwita Mbunge wa CHADEMA na kumwambia, fulani bwana mdini sana. Mwangalieni. Kiongozi wa CHADEMA anajiona kapata bonge ya issue na kueneza. Tunachinjwa na CCM kwa upuuzi wetu. Kwa ujinga wetu wenyewe. Chama chetu kimesambaa nchi nzima na viongozi wake ni wa dini zote na makabila yote.

Mh. Zitto, unaizungumziaje demokrasia ndani ya chama chako katika chaguzi, teuzi na kupanga safu za uongozi?
CHADEMA ina demokrasia ya aina yake na wanachama tunaridhika nayo. The Party deploys for or against your wishes and every member must oblige a just deployment. Tuna utaratibu mzuri sana wa kujieleza na kutetea hoja zetu ndani ya chama, na baada ya watu wote kukubaliana tuna hakukusha tunasimama wote kwa kauli moja sehem zote tunapo wakilisha chama. Sio katika kupanga safu za uongozi tu, ni sehem zote za uongozi wa chama.

Kwanini CHADEMA haiwatumii viongozi wa Mikoa na Wilaya na badala yake inatuma watu toka makao makuu hata kwa mambo madogo madogo ambayo yangemalizwa na uongozi wa ngazi husika?
Huo mtazamo unaweza kutokana na kulinganisha Chadema na vyama vingine. Ieleweke kua Chadema ni chama tofauti na kina utaratibu wake. Katika chama chetu Viongozi wa mikoa na wa wilaya wana majukumu yao, na makao makuu pia yana majukumu yake.

Inaweza kutokea mara kwa mara hizi level mbili zishirikiane katika kutekeleza kazi za chama. Hata hivo, tunaendelea kujenga chama kama taasisi, hivyo tunaendelea kujenga uwezo wa viongozi wetu wa mikoa na wilaya ili waweze kumudu majukumu mengi zaidi na kuwaachia wenye kukaa makao makuu kuhusika zaidi na strategies za chama.
Mh Zitto, unazizungumziaje harakati za M4C na athari (impact) yake kisiasa na kijamii? Chama kimeweka taratibu gani nzuri za malezi kwa wanachama wapya wanaojiunga kwenye M4C, kama bado, huku si kusuka kamba inayoungua?
Kwa sababu jina lake liko wazi kabisa, M4C ni moja ya operesheni inayo fanikisha watanzania kujiunga katika chama huku wakijua kabisa kua malengo ni kuleta mabadiliko chanya.

Impact yake kwa jamii ni kubwa sababu inawaweka wanachama wenyewe kua vyanzo vya mabadiliko. Baada ya kujiunga, ni obvious kua Chama kinatoa mafunzo kwa wanachama wake wapya na hivyo kuwalea kuwa makada wazuri. Hii sio opresheni ya kwanza ya Chama, na haitakua ya mwisho.

M4C sio chama ndani ya chama, M4C ni operesheni ya kujenga chama na kuleta mabadiliko nchini.
 
Inadaiwa hushiriki kikamilifu M4C, ni kweli? Nini kauli yako dhidi ya tuhuma hizi?
Ninashiriki sana kazi za kujenga chama. Nimeshiriki sana operesheni mbalimbali za chama. Nitaendelea kushiriki nikiwa mwanachama na kiongozi wa chama.

Halikadhalika wengine tunashughulika zaidi katika kuwakilisha chama Bungeni na mikakati mengine ya kuhimarisha chama, ila tukipata nafasi tunajiunga pia katika kazi za kujenga chama. Mikutano yetu ya chama tunagawana maeneo.

Mimi, kwa mfano kwenye M4C nimepangiwa mkoa wa Manayara na Singida nikiwa na Tundu Lissu na Christina Lissu na Rose Kamili. Mtakumbuka mwanzo mwa mwaka nilifanya ziara Tanga bila viongozi wenzangu. Mtakumbuka nilikwenda Marekani kufungua tawi la chama kule. Nimefanya mikutano Iringa, Hanang nk. Nimeshiriki kampeni za udiwani maeneo mbalimbali nchini. Siwezi kuonekana kila mkoa kila wakati. Pia ninapangiwa kazi.
Je, utaratibu wa kupita mikoani katika kutafuta nafasi ya kugombea uenyekiti kama ilivyokuwa wakati wa Mbowe unafaa au CHADEMA irudi katika utaratibu kama wa CCM?
Hatujawahi kufanya utaratibu unaosema isipokuwa kwenye Urais mwaka 2005. Hatujarejea tena utaratibu huo. Mfumo wowote ambao unapanua demokrasia ya chama ni bora zaidi katika kuimarisha chama. Chama kinakomaa kwa wanachama kushindana kwenye chaguzi za ndani. Natumai uchaguzi mkuu ujao wa chama utakuwa na wagombea wengi zaidi ili wanachama wapate uchaguzi wa kweli. Sipendi chaguzi za kupita bila kupingwa katika chama kinachotaka kujenga demokrasia ya nchi.

Mheshimiwa Zitto Viongozi/CHADEMA imekuwa mstari wa mbele kufichua ufisadi. Kuna taarifa kuwa kuna mwanachama wenu katafuna fedha za M4C, ni kweli? Kama ni kweli, ameshughulikiwaje? Kama hajashughulikiwa, ni kwanini mko kimya?
Nasikia suala hili hapa, tupeni ushahidi na tutachukua hatua mara moja.

Zitto wewe ni naibu katibu mkuu wa CHADEMA, Mara nyingi matamko ya chama yametolewa na Katibu, Mwenyekiti, Mnyika (tangu kabla hajawa msemaji) na mara chache wanasheria km Lissu, Marando na Prof.Safari. Kwanini Zitto umekuwa mbali sana na matamko haya ya CHADEMA ukiwa kama Naibu Katibu mkuu? (Naamini hutojibu ni mgawanyo wa kazi)
Naibu Katibu Mkuu sio msemaji wa chama. Katika kujibu suala la demokrasia katika chama nilisema kuwa kuna utaratibu wa kujadili hoja mbali mbali ndani kwa ndani, yakiwemo matamko ya chama.

Katibu mkuu wa CHADEMA anapotoa matamko ya chama anatoa yale yaliyojadiliwa na wanachama wote, nikiwemo mimi, hivyo kuwakilisha maoni yangu pia. Sidhani kama kuna umuhimu wa kuifanya kazi hiyo wakati nimeridhika kua maoni yangu yanawakilishwa kupitia utaratibu wa chama.

Unafikiri CHADEMA uliyoikuta mwanzo ndiyo hii ya sasa au kuna mabadiliko? Kama kuna mabadiliko ni yepi na unafanya nini kufanya CHADEMA iwe kama ambavyo ulitaka iwe?
CHADEMA ni chama kinachokua kwa kasi sana, na kadiri kinavyokua kinabadilika positively. Moja ya mabadiliko hayo ni idadi ya wanachama, nyingine ni kuweza kushika Uongozi wa Upinzani Bungeni, nafasi ambayo ilikua ya CUF nilipo ingia chama. Chama hivi sasa kipo kila mahala.

Nakumbuka mwaka 2005 tulikwenda Mafinga kuhutubia tukapata watu 20 tu kwenye mkutano. Leo tunaombwa kwenda huko. Chama kina influence maamuzi ya nchi hivi sasa. Hayo yote ni mabadiliko makubwa na mazuri, na ninafurahi kuwa sehemu ya mafanikio ya chama changu.

Unafikiri namna CHADEMA inavyoendesha siasa zake kuna uwezekano wa kushika dola mapema (2015)? Kama ndiyo kwanini na kama hapana unafikiri mabadiliko gani yanatakiwa kufanyika kuelekea 2015?
Sina mashaka na hili. Nitafafanua zaidi baadaye
CCM wanadai kuwa nyinyi CHADEMA hamna presidential materials, una kauli gani juu ya hili?
Kweli unategemea kuwa chama tawala kinaweza kukisifu chama cha upinzani kwa kuwa na presidential material? Mimi ni Presidential material kwa mfano.

Nina Uwezo, Uadilifu na Uzalendo wa kuweza kuwa Amiri Jeshi Mkuu. Dkt. Slaa ni Presidential Material. Mbowe ni Presidential material. Kitila Mkumbo ni Presidential material. Wapo wengi sana ndani ya CHADEMA wenye sifa za kuwa Marais. Sina mashaka kabisa hilo.

Una muono gani kuhusu upinzani nchini na nini nafasi ya upinzani hasa CHADEMA kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ukilinganisha na chama tawala CCM?
Ili Tanzania iwe salama ni lazima CCM ishindwe uchaguzi. CCM ikishinda tena mwaka 2015 itavunja sana moyo wa wananchi na wengine wanaweza kukata tama. Lakini pia CCM imechoka na haina nguvu za kutosha kukabiliana na changamoto za nchi hivi sasa.

Njia pekee ya kuisadia CCM iweze kujipanga upya ni yenyewe kondoka madarakani. CHADEMA ina nafasi kubwa sana ya kushinda na kuongoza dola. Muhimu chama kijipange na kuonekana kama chama kilichotayari kushika dola. Tuyatende tunayoyasema na tujiimarishe zaidi.
 
Ni bahati mbaya sana kuwa hatutumii baadhi ya mafanikio yetu Bungeni kwenye ulingo wa siasa ma hivyo kuwaacha CCM wanachukua credits.

Kwa mfano, ni kwanini mafanikio ya hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu hatujayafanyia kazi ya kisiasa? Ingawa hatukufanikiwa kumtoa Waziri Mkuu lakini tuliilazimisha Serikali kufanya mabadiliko. Kikwete alisema ni upepo tu, lakini upepo huu ulikuwa na joto kali ukamshinda na tukaacha yeye achukue credit kwa kazi yetu ya uwajibikaji.

Hoja ya juzi ya Mheshimiwa Halima Mdee kuhusu Ardhi inabidi kuifanya ni ajenda ya kisiasa. Hoja ya Mkonge tulikwenda Tanga na ilikuwa na mafanikio makubwa sana. Hoja ya Mabilioni ya Uswiss nayo tunaiachia wanaisemea watu wa CCM kuififiza. Historia inatuonyesha kuwa hoja zote tulizozitumia vizuri nje ya Bunge zilijenga taswira nzuri ya chama ie Buzwagi na EPA. We ignore this at our own peril- Chadema ni chama cha kitaifa. Kingekuwa chama cha kidini au kikabila kingefutwa. Katika uongozi wa Chadema unapata watu toka mikoa na kabila mbali mbali, pia watu toka dini mbali mbali. Diversity hii haipatikani katika vyama vingi humu nchini. Nadhani mtazamo huu unapandikizwa na watu ambao hawakipendi chama chetu na wanao ona chama kama threat kwa maslahi yao binafsi.

Mkuu kwa mara nyingie asante,

Personally nimependa maelezo yako ya Movement for Change (M4C) na nanukuu… "sio chama ndani ya chama M4C ni operesheni ya kujenga chama na kuleta mabadiliko nchini", naona kama wananchi wengi ni kweli wanajua kuna M4C ila hawajajua hasa nini malengo makuu ya M4C nje ya kueneza ‘awareness' kwa wananchi.

Kuna mahala nimepata kitu na nipo curious kidogo (hapo nime quote), inakuwaje kwa chama kubwa na viongozi wazoefu kama CDM mkashindwa hilo na kufanya CCM wachukue credits wanazo stahili CDM? Tatizo unadhani lipo wapi na nini suluhu ya hilo tatizo?

SWALI kwa members:-

Kwa wote wanaofuatlia, aliyeuliza (samahani sikumbuki jina) swali la 8 umeambiwa lete ushahidi na litashughulikiwa mara moja!

" Mhe. Zitto, Viongozi/CHADEMA imekuwa mstari wa mbele kufichua ufisadi. Kuna taarifa kuwa kuna mwanachama wenu katafuna fedha za M4C, ni kweli? Kama ni kweli, ameshughulikiwaje? Kama hajashughulikiwa, ni kwanini mko kimya?"
 
Tatizo lipo wapi? sioni kama tatizo bali ni changamoto.

Naamini tutaifanyia kazi lakini tunapochelewa kuifanyia kazi tunashindwa kujiimarisha zaidi. Nina wasiwasi sana kuwa CCM imeanza kujua hili. Namna walivyojadili na kupitisha hoja ya Halima na yangu ni ishara kuwa CCM imezinduka. Kwa mara ya kwanza toka niwe Mbunge nimeona hoja ya mbunge wa Upinzani imepitishwa kwa kuungwa mkono na pande zote bila mizengwe. Inawezekana tukashangilia lakini lazima tutoe macho haswa haswa.

Tusiwadharau CCM. Tujue siasa is dynamic.

Mfano wa CCM kuchukua hoja kuweza kufanikiwa. Soma habari hii ya mwananchi leo

Kinana atangaza vita viwanda vya korosho - Kitaifa - mwananchi.co.tz
 
Asante mkuu nimekupata, swali linalofuata;

C. Zitto na kuhusishwa na CCM


  1. Kumekuwa na shutuma za mara kwa mara kuwa una ukaribu uliokithiri na Chama kuu pinzani kwa CHADEMA yaani CCM. Unasemaje kuhusiana na tuhuma hizo?
  2. Inasemekana kuwa ukaribu huo unaweza kuonekana kupitia ukaribu wako na Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni rais wa Jamhuri wa muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete. Unasemaje hapa?
  3. Mkuu, vipi kuhusu kuonekana kwako in public pamoja na rais sehemu tofauti hadi safari za nje ya nchi.
  4. Inasemekana kuwa ni Kwa sababu yako ndio maana rais JK hakumnadi mgombea wa ubunge wa CCM wa jimbo lako katika uchaguzi mkuu uliopita na kwamba ndio maana hukushiriki katika kuungana na wanachama wako katika kumsusia JK siku ile anafungia bunge.
  5. Vipi madai kuwa unatumwa na CCM ili kupunguza nguvu ya CHADEMA? Kama si kweli unadhani kwanini watu wanakuona kama pandikizi ndani ya CHADEMA?
  6. Ni kweli kuwa una mkakati wa kuhamia CCM kabla ya 2015?
  7. Vipi tetesi kuwa wewe na Kafulila mmeanzisha chama na una mkakati wa kutimkia huko?
 
Kumekuwa na shutuma za mara kwa mara kuwa una ukaribu uliokithiri na Chama kuu pinzani kwa CHADEMA yaani CCM. Unasemaje kuhusiana na tuhuma hizo?
Ukitaka kummaliza mwanasiasa yeyote wa upinzani hapa Tanzania mhusishe na ama usalama wa Taifa au CCM. Ndivyo ilivyokuwa kwa Mabere Marando miaka ya Tisini. Marando ameishi kuweka sawa historia ingawa propaganda dhidi yake zilikuwa kali sana kiasi cha kuogopwa kweli kweli. Napita njia hiyo hiyo ya Marando na wanaonipaka matope haya wataona aibu sana ukweli utakapodhihiri.
Siku za mwisho za uhai wake ndugu Chacha Wangwe naye aliambiwa ni CCM na kwa kweli alikufa akiwa na chuki sana kuhusu tuhuma hii.

Faida kubwa niliyonayo mimi ni kwamba, mtaji wangu wa kisiasa ulikuwa ni mkubwa mno na ndio maana tuhuma hizi hazijaniathiri. Ninaamini tuhuma kama hizi zingekuwa kwa watu wengine wangekuwa wameshafutika kwenye historia ya siasa. Sijawahi kuwa mwanaCCM, familia yangu yote kabisa ni waanzilishi wa CHADEMA. Sina historia na CCM. Inawezekana wanaosema mimi ni CCM wengi wao wamewahi kuwa CCM, wana familia zao ndani ya CCM na wamewahi kula matunda ya CCM. Mimi sijawahi na wala sitawahi.
Inasemekana kua ukaribu huo unaweza kuonekana kupitia ukaribu wako na Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni rais wa Jamhuri wa muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete. Unasemaje hapa?
Kuhusu Rais Kikwete, kwanza ifahamike Jakaya Kikwete na Zitto Kabwe wana mahusiano yao nje ya siasa na hata siku moja hatujadili vyama vyetu. Rais Kikwete anaamini katika uzalendo wangu.

Mimi ninamheshimu Rais Kikwete kama Mzee wangu. Kuita sisi ni marafiki is understatement, yeye ni mzee wangu. Tunaheshimiana, lakini ninaiheshimu zaidi Tanzania na ninaipenda zaidi Tanzania. Kama inavyoonekana, kazi zangu zinajihidhirisha Bungeni kwamba ni mmoja wa wabunge ninayeisumbua sana Serikali yake. Kutokana na hoja zangu nimemlazimisha kufanya mambo kinyume na mipango yao. Leo tuna sheria mpya ya Madini kwa sababu ya hoja ya Buzwagi. Ninafurahi sasa mgodi wa TanzaniteOne hisa asilimia 50 zinachukuliwa na Watanzania kutokana na mapendekezo yangu mahususi kwamba vito vya thamani, mgeni asiwe na zaidi ya asilimia 50.

Mwaka huu nimemlazimisha kupangua baraza la mawaziri kufuatia hoja yangu ya kutokuwa na imani na waziri mkuu iliyoungwa mkono na wabunge wengi bila kujali vyama. Hebu niambie kama ningeweza kupata mafanikio kama haya dhidi ya Serikali ya mtu mnayesema rafiki yangu. Wengine watasema, aah JK huwa anamtuma kufanya haya. Iwe jua au mvua ni lawama tu. Lakini maisha ya kisiasa haya. Yana mwisho, Rashidi wa KULI alisema.

Mkuu, vipi kuhusu kuonekana kwako in public pamoja na rais sehemu tofauti hadi safari za nje ya nchi.
Suala la kusafiri na Rais ni suala la kawaida sana. Nashangaa sana namna linavyokuzwa wakati ni wazi kabisa kua Rais lazima asafiri na wabunge, na anae wateua wabunge ni Spika wa Bunge. Kila Rais, Makamu wa Rais au Waziri mkuu wanapo safiri huambatana na wabunge wa kambi zote mbili.

Kwa kuweka rekodi sawa Rais amesha safiri na wabunge wafuatao wa Chadema: Christina Lissu (Australia), Chiku Abwao (Burundi), Grace Kiweli (Scandinavia), Lucie Owenya (US), nk. Makamu wa Rais kesha safiri na Ezekiah Wenje (Uturuki) na Esther Matiko (Uturuki) Waziri Mkuu pia kesha safiri na wabunge wa Chadema.

Toka nimekuwa mbunge nimesafiri na Rais mara mbili tu: Mara ya kwanza ilikua sherehe za uhuru za Sudan Kusini. Nilikwenda kwa taratibu hizo za Bunge. Mara ya pili ni Ethiopia, Kumzika Meles Zenawi. Hii niliomba mwenyewe kwani nilipenda kwenda kumzika mwanasiasa huyu niliekuwa namheshimu sana barani Afrika.
Inasemekana kuwa ni Kwa sababu yako ndio maana rais JK hakumnadi mgombea wa ubunge wa CCM wa jimbo lako katika uchaguzi mkuu uliopita na kwamba ndio maana hukushiriki katika kuungana na wanachama wako katika kumsusia JK siku ile anafungia bunge.
Rais Kikwete hakufika jimboni kwangu kumnadi mgombea wa chama chake. Napenda niwakumbushe, sio mwaka 2010 tu, toka nimekuwa mbunge Rais Kikwete hajawahi kuja kwenye kampeni jimboni kwangu. Hakuna makubaliano yeyote, bali anaheshimu mchango wangu kwenye nchi yangu. Mwaka 2005 hakuja Kigoma Kaskazini. Mwaka 2010 hakuja Kigoma Kaskazini. Lipumba pia hakuja Kigoma Kaskazini kunadi mgombea wake wa CUF.

Mwaka 2005 katika Jimbo la Musoma Mjini, aliyekuwa mgombea Urais CHADEMA ndugu Mbowe, hakumnadi mgombea wa CHADEMA bali alimnadi mgombea wa CUF. Mwaka 2010 Slaa alipofika Kyela alimnadi mgombea wa CCM dkt Mwakyembe. Kama ilivyo kwa wengine wenye maamuzi ya kuthamini kazi za wagombea wa vyama vingine, Rais Kikwete naye anayo haki ya kuheshimu na kuthamini kazi zangu katika nchi yetu. Mwakyembe yupo kwenye majukwaa ya CCM licha ya kwamba alinadiwa na Mgombea Urais wa CHADEMA.
Vipi madai kuwa unatumwa na CCM ili kupunguza nguvu ya CHADEMA? Kama si kweli unadhani kwanini watu wanakuona kama pandikizi ndani ya CHADEMA?
Baadhi ya watu wanapandikiza chuki hizi kwa sababu zao wenyewe. Hawanisumbui maana najua ni kikundi kidogo cha watu wachache wenye malengo yao ovu. Wajue tu kwamba hawawezi kuwadanganya Watanzania ambao wanafanya maamuzi yao sio tokana na propaganda ila kutokana na matendo ya kila mmoja.

Onyo:
Watu hao hawawezi kummaliza Zitto kisiasa bila kuiathiri CHADEMA maana the imaage of Zitto is so intimately intertwined with CHADEMA that you couldn't attack Zitto without jeopardizing the image of Chadema, and vice versa.

Wanaoeneza sumu hii hawana nia njema wala mapenzi na CHADEMA. Hawaelewi siasa. Wanafurahisha maadui wa CHADEMA. Maadui wanawachochea kwa kuwapa habari za uwongo na wao wanadhani watammaliza Zitto. Huwezi kummaliza Zitto bila kuiathiri CHADEMA. Hawatafanikiwa.
Ni kweli kuwa una mkakati wa kuhamia CCM kabla ya 2015?
Sijawahi wala kufikiria kuhamia CCM. Kama nilivyosema hapo awali, sijawahi kuwa mwanachama wa chama kingine chochote tofauti na CHADEMA. Namwomba mungu kuwa niondoke duniani nikiwa chama hiki hiki. Siamini katika kuhama vyama. Ninaamini katika mfumo imara wa vyama vingi nchini. Ninaamini katika demokrasia pana.

Vipi tetesi kuwa wewe na Kafulila mmeanzisha chama na una mkakati wa kutimkia huko?
Swali hili na lililotangulia yanaonyesha kuwa hizi kweli ni tetesi tu. Sasa kama unasema nina mkakati wa kuhamia CCM. Tena kuna tetesi nimeanzisha chama na nataka kuhamia huko, sasa mimi nina vyama vingapi nitakavyohamia. Sijawahi hata kufikiria kuanzisha chama cha siasa. Chama changu ni CHADEMA na sitaondoka CHADEMA. Kinachonisikitisha ni kwamba kuna viongozi wa CHADEMA wamekula sumu hii na bila woga wanaisema kana kwamba ni kweli.

It is very unfortunate Kiongozi wa chama makini kama CHADEMA kuamini ujinga na kuingia kwenye mitego kama hii. Nataka ijulikane wazi kabisa kwamba, CCM haitachoka kutugawa. Haitachoka kupandikiza chuki miongoni mwetu. Wameshajua udhaifu upo wapi na wahenga walisema kamba hukatikia?
 
Nashukuru kwa majibu yako ya kina na ilikuwa moja swali ambalo majibu yake nilikuwa na kiu nayo sana. Shukrani.

Swali linalofuata;

D. Zitto na Kigoma

Katika kipindi chako chote cha Ubunge wa miaka 10 katika eneo lako umejizolea umaarufu na wafuasi wa kutosha ambao wamejenga ‘Imani' juu yako. Nguvu na jitihada zako ni dhahiri, mabadiliko toka umeshika nafasi ya kuwakilisha jimbo lako ni ya wazi. Umejenga taswira inayoonesha wazi kuwa ungegombea tena ungepita kwa kipingamizi kidogo na sasa ndio wapanga kuachia ngazi.

  1. Unaweza orodhesha utofauti wa Kigoma ya sasa na Kigoma kabla ya Zitto kuwa mbunge wake?
  2. Mkoa wa Kigoma unanufaika/utanufaikaje na ukaribu wako na serikali ya Ujerumani?
  3. Umeandaa mikakati gani kuhakikisha Chadema inatetea vema hicho kiti chake?
  4. Kuna mtu ambaye umemuandaa kugombea nafasi ya Ubunge Kigoma Kaskazini? Ni kwa tiketi ya chama gani? Kama yupo tunaweza mfahamu au bado ni siri kwa sasa? Vipi ndugu Yared Fubusa ana nafasi gani kuelekea 2015?
  5. Mgodi wa chumvi wa Uvinza uliouzwa kwa bei ya hisani kwanini hawalipii yale maji ya chumvi ambayo yapo ardhini toka kugunduliwa kwake miaka ya 1800's ("Brine") kwa kutumia "flow meter" kama mwananchi wa kawaida wa Kigoma Mjini ambaye analipia maji ya KUWASA kutoka ziwa Tanganyika? Je, wawakezaji hao waliuziwa hata mkondo wa maji ya chumvi yaliyopo ardhini wakati wao hawakuwa wagunduzi?
  6. Pamoja na kuuziwa kiwanda hicho kwa bei ya hisani, kwanini bado wanaendelea kutumia nishati ya kuni kutoka kwenye miti asili ambayo hawakupanda wao badala ya kutumia nishati mbadala?
  7. Katika vipindi vyote hivi vya ungozi wako wananchi wa Kigoma Kaskazini ungependa wakukumbuke kwa lipi?
 
Unaweza orodhesha utofauti wa Kigoma ya sasa na Kigoma kabla ya Zitto kuwa mbunge wake?
Hili watasema watu wa Kigoma wenyewe. Sio watu wa jimboni kwangu tu bali watu wa mkoa mzima wa Kigoma. Kigoma ya mwaka 2005 na Kigoma ya mwaka 2012 ni sawa na kichuguu na mlima Kilimanjaro. Tunaendelea kusukuma maendeleo zaidi ya Mkoa huu. Nafurahi sana kuwa sehemu ya mabadiliko haya ya mkoa wangu. I am very proud.

Hata hivo naamini bado kuna mengi zaidi yanayo takiwa kufanyika na nitashirikiana na wabunge wetu watakao kuja kuhakikisha Kigoma inasonga mbele. Ni vema watu wa Kigoma watoe hukumu yao wao wenyewe badala ya mimi kuanza kubrag hapa. Watasema barabara zilikuwaje na sasa zipoje. Watasema hali ya umeme. Watasema hali ya kilimo cha kahawa. Watasema hali ya elimu na afya. Humu kuna watu wa Kigoma, waseme wenyewe!

Mkoa wa Kigoma unanufaika/utanufaikaje na ukaribu wako na serikali ya Ujerumani?
Sina ukaribu na Serikali ya Ujerumani.

Umeandaa mikakati gani kuhakikisha Chadema inatetea vema hicho kiti chake?
CHADEMA ni chama imara sana Kigoma Kaskazini. Kina mtandao kila kitongoji na kina viongozi mahiri kwenye vijiji. Tunachohitaji ni kupata mgombea mzuri.

Napenda niseme hapa kwa uwazi kabisa. Viti vyote walivyoshinda NCCR Kigoma isipokuwa Kimoja vilichukuliwa na vijana waliokuwa CHADEMA. Kwanini walitoka ni jambo ambalo sote twapaswa kutafakari (wana chadema) maana naona kuna watu wanatoa majibu mepesi sana kuhusu suala hili. Wengine wanadiriki kusema niliwasadia vijana hawa. Sikuwasaidia lakini nilikataa kwenda kufanya kampeni dhidi yao maana matokeo yake ingekuwa ni CCM kushinda kwa sisi wapinzani kugawa kura.

Kuna wenzangu wangependa bora CCM ishinde kuliko mtu kama Kafulila kushinda, nilikataa nadharia hiyo. Hivi sasa Kigoma ina wabunge wa upinzani 5 kati ya majimbo 8. Wabunge 4 kati ya hao ni wana CHADEMA by nature lakini kushindwa kwetu kuvumulia tofauti zetu kumefanya kuwapa NCCR viti. Ukiangalia kura za Urais Kigoma ilipata asilimia 45 ya kura zote na hata kushinda kwenye baadhi ya majimbo. Lakini tulipata kiti kimoja tu tena kwa mbinde sana. Hili ni somo. Tukijifunza tutashinda viti vyote vya mkoa wa Kigoma bila shida yeyote ile.
Kuna mtu ambaye umemuandaa kugombea nafasi ya Ubunge Kigoma Kaskazini? Ni kwa tiketi ya chama gani? Kama yupo tunaweza mfahamu au bado ni siri kwa sasa? Vipi ndugu Yared Fubusa ana nafasi gani kuelekea 2015?
Sijaandaa mtu. Nachukia siasa za kuandaa watu. Mimi sikuandaliwa kugombea Kigoma Kaskazini. Nilitaka kuwa Mbunge na nikaomba ridhaa. Yeyote anayetaka kuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini lazima aanze sasa kushiriki kazi za chama chetu, tumjue na tumpime na wengine kasha Mkutano Mkuu wa chama katika Jimbo utateua mmoja aliyebora kabisa.

Yared Fubusa ni kijana mzuri sana mwenye maono na mwenye mapenzi ya dhati ya Kijiji chake cha Kiganza na Kata yetu ya Mwandiga na mkoa wa Kigoma. Ninamshauri aanze sasa kushiriki katika kazi za chama chetu cha CHADEMA ili wanachama wamjue na wampime. Anaweza kuwa Mbunge mzuri sana. Nitafurahi kama nitapata mtu wa aina yake kuendeleza jimbo letu. Yeyote anayetaka Ubunge Kigoma Kaskazini ajitokeze sasa. Mimi sitaandaa mtu yeyote. Nataka, kama mpiga kura, tupate mtu safi.
Mgodi wa chumvi wa Uvinza uliouzwa kwa bei ya hisani kwanini hawalipii yale maji ya chumvi ambayo yapo ardhini toka kugunduliwa kwake miaka ya 1800's ("Brine") kwa kutumia "flow meter" kama mwananchi wa kawaida wa Kigoma Mjini ambaye analipia maji ya KUWASA kutoka ziwa Tanganyika? Je, wawakezaji hao waliuziwa hata mkondo wa maji ya chumvi yaliyopo ardhini wakati wao hawakuwa wagunduzi?
Nitafuatilia suala kwenye kamati yangu. Sikuwa nimelitilia maanani.
Pamoja na kuuziwa kiwanda hicho kwa bei ya hisani, kwanini bado wanaendelea kutumia nishati ya kuni kutoka kwenye miti asili ambayo hawakupanda wao badala ya kutumia nishati mbadala?
Ndugu Kafulila anafuatilia suala hili kwa kina sana. Kuna kazi inaendelea hivi sasa kuhusu suala hili sipendi tuiseme hadharani.
Katika vipindi vyote hivi vya ungozi wako wananchi wa Kigoma Kaskazini ungependa wakukumbuke kwa lipi?
Ufahari wa Utu wao. Leo watu wa Kigoma hawaoni aibu kujitambulisha hivyo. Haikuwa hivyo miaka ya nyuma. Hili ni kubwa sana kwangu kuliko mamia ya kilometa za barabara au makumi ya megawati za umeme au Uwanja wa ndege wa Kimataifa.
 
Status
Not open for further replies.
69 Reactions
Reply
Back
Top Bottom