RUCCI
JF-Expert Member
- Oct 6, 2011
- 1,701
- 1,714
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kukamatwa kwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob baada ya kushindwa kuhudhuria katika kesi inayomkabili ya kumpiga na kumjeruhi mwandishi wa habari.
Hatua hiyo ilifikiwa mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa baada ya Wakili wa Serikali, Honolina Mushi kuieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilikuwa kwa ajili ya kusikilizwa huku upande wa Jamhuri ukiwa na shahidi mmoja ambaye ni Mwandishi wa Habari wa gazeti Uhuru, Christopher Lisu aliyefika mahakamani hapo kutoa ushahidi.
Mushi alisema katika hali isiyokuwa ikitarajiwa mshtakiwa Jacob hajafika mahakamani hapo na hakuna taarifa yoyote juu ya kutofika kwake na hivyo kuiomba mahakama kutoa hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa huyo.
Mstahiki Meya Jacob ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ubungo, anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kumpiga na kumjeruhi Mwandishi wa Habari wa gazeti la Uhuru, Lisu, katika tukio lililotokea Septemba 15, mwaka jana katika makao makuu ya CHADEMA.
Katika tukio hilo, mwandishi huyo alijikuta katika dhahama hiyo baada ya kuonekana akiwa na kundi la wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliodaiwa kujifanya wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wakiandamana kumpinga aliyekuwa Mgombea Urais kupitia Chadema, Edward Lowassa.
Pamoja na kutuhumiwa kumpiga na kumjeruhi mwandishi huyo, mshtakiwa anadaiwa pia kuharibu kamera aina ya Nikon mali ya Uhuru Publications Limited (UPL) yenye thamani ya shilingi milioni 8.
Kesi hiyo itaendelea tena Mei 23, mwaka huu.
Chanzo: HiviSasa