Habari kutoka Mahakama ya Kisutu inasema Maranda na Farijala wamefungwa jumla ya miaka kwa wizi wa EPA. Wakitoka wanalipa pesa walizokwapua
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu mfanyabiashara Rajabu Maranda na binamu yake, kifungo cha miaka mitano jela kwa makosa sita, likiwemo la kujipatia sh. bilioni 1.8 kupitia akaunti ya EPA. Maranda na binamu yake Farijala Hussein, pia wameamriwa kulipa fedha hizo, vinginevyo mali zao zitakamatwa na kufilisiwa. Hukumu hiyo ilitolewa jana na jopo la mahakimu watatu waliosikiliza kesi hiyo ya kujipatia fedha mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kupitia akaunti ya EPA.
Akisoma hukumu hiyo kwa saa mbili, Hakimu Ilvin Mugeta, alisema washitakiwa wametiwa hatiani katika makosa sita kati ya manane waliyoshitakiwa. Miongoni mwa makosa waliyotiwa hatiani ni ya kughushi, kuwasilisha hati za uongo na kujipatia ingizo la fedha kwa njia za udanganyifu. Mahakimu Mugeta, Saul Kinemela na Phocus Bampikya, waliyafuta mashitaka mawili ya kula njama kwa nia ya kutenda kosa na wizi. Kwa mujibu wa Mugeta, walipitia ushahidi uliotolewa mahakamani na kuridhika na upande wa mashitaka kuwa, washitakiwa walitenda makosa hivyo kuwahukumu kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka 21 jela.
Hata hivyo, Hakimu Mugeta alisema washitakiwa watatumika vifungo vya miaka mitano jela kila mmoja, kwa kuwa adhabu hizo zitatumikiwa kwa pamoja. Hakimu Mugeta alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai iliyotumika kuwatia hatiani, mahakama inawaamuru washitakiwa kurudisha fedha walizojipatia kwa mwenye mali, vinginevyo mali zao zitakamatwa na watafilisiwa. Alisema watuhumiwa wana uhuru wa kukata rufani. Awali, Wakili Mkuu wa Serikali Boniface Stanslaus aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washitakiwa kwa kuzingatia kiasi kikubwa cha fedha kilichochukuliwa na madhara yaliyotokea kwa wananchi.
Stanslaus aliiomba mahakama itumie mamlaka yake kupitia kifungu cha 358 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kutoa amri kwa watuhumiwa kurudisha fedha hizo BoT. Wakili anayewatetea washitakiwa hao, Majura Magafu, alidai kifungu cha 358 kama kilivyorekebishwa mwaka 2009 kinaangukia chini ya makosa ambayo yapo ukurusa wa 27 wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu. Alidai makosa hayo ni ya kughushi, hivyo ombi la kurudisha fedha halistahili na mahakama iangalie vifungu hivyo.
Majura aliiomba mahakama isitoe amri ya washitakiwa kurudisha fedha kwa kuwa serikali kama itaona kuna haja ya kurudisha, wanaweza kufanya mchakato wa kuzirudisha. Aliiomba mahakama iwaonee huruma wateja wake, kwani ni makosa yao ya kwanza na hawajawahi kutiwa hatiani kwa makosa ya jinai. Majura alidai washitakiwa wanategemewa na familia zao na kwamba, ukiangalia makosa yaliyotendeka, kuna namna moja au nyingine kuwa yalifanyika kwa kutokujua au kuelekezwa na vyombo husika.
Alidai 'Deed of Assignment' zilipelekwa BoT na walihakikishiwa kwa mawasiliano na hatimaye walitoa fedha. Alidai kuna watu walishiriki kuwapotosha washitakiwa. Magafu alidai washitakiwa wanasumbuliwa na magonjwa ya figo na wamekuwa wakipelekwa hospitali mara kwa mara kwa matibabu. Wakili huyo alidai kwa mamlaka waliyopewa mahakimu wanaweza kuwaachia huru washitakiwa, baada ya kuwatia hatiani au kwa masharti wasifanye kosa lolote kwa kipindi cha miezi isiyozidi 12.
Hakimu Mugeta alisema kwa kuzingatia uzito wa makosa, washitakiwa hawastahili kusamehewa. Baada ya hukumu kusomwa, Magafu alidai wateja wake hawajaridhika, hivyo watakata rufani. Washitakiwa hao wanadaiwa kughushi, kuwasilisha hatia za uongo na kujipatia ingizo la sh. bilioni 1.8 mali ya BoT kwa njia ya udanganyifu wakonyesha kuwa, Kampuni ya Kiloloma and Brothers imepewa idhini ya kukusanya deni la kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai, India.
Maranda na Hussein wanakabiliwa na kesi nyingine tatu za EPA, zikiwa ni miongoni mwa kesi kadhaa za EPA zilizofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu. Kesi hizo zinawakabili wafanyabiashara maarufu na waliokuwa watumishi wa BoT.
Ndugu, jamaa na washitakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi za EPA walikuwa miongoni mwa watu waliofika mahakama jana kusikiliza hukumu hiyo iliyoanza kusomwa saa 4.10 asubuhi. Baada ya hukumu kusomwa, baadhi ya ndugu na jamaa wa washitakiwa waliangua vilio. Saa 9.13 mchana washitakiwa walipandishwa kwenye gari lenye namba za usajili SCN 90008K lililokuwa na askari wawili wenye silaha na kupelekwa gereza la Ukonga. Wakati washitakiwa hao wakipanda kwenye gari, vilio na simanzi vilitawala mahakamani, huku baadhi ya ndugu wakiwa wamekusanyika kwenye makundi.
Fedha za EPA zawatupa jela