Mahakama ya Kisutu imewatia hatiani Viongozi wa CHADEMA na kuwahukumu kulipa faini ya Tsh. Milioni 350 au kwenda jela, Wapelekwa Segerea

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
1,148
2,000
Mahakama ya Kisutu leo Machi10, inatarajia kutoa hukumu kwa Viongozi wa CHADEMA wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi Mahakamani hapo, Viongozi hao ni pamoja na Mwenyekiti CHADEMA, Freeman Mbowe, pia John Mnyika, Halima Mdee, Ester Bulaya, Ester Matiko, Heche, Msigwa na Mashinji.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, vigogo hao wanakabiliwa na mashtaka 13, wakituhumiwa kwa uchochezi, katika kesi iliyoanza kusilikizwa Machi 7, 2018.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na 16, mwaka 2018, wakiwa Kinondoni jijini Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani kwa kutenda kosa la jinai na kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Pia soma
> Mbowe na viongozi 6 wa CHADEMA wafikishwa Mahakamani Kisutu, wasomewa mashitaka 8

>
Viongozi wa CHADEMA wakutwa na kesi ya kujibu kwenye mashtaka ya uchochezi

UPDATE

4:30 Asubuhi : Hukumu yaahirishwa mpaka saa 7:30 mchana

Awali kesi hiyo ilipangwa kusomwa saa 4:30 wakati washtakiwa wakiwa ndani ya ukumbi, walifahamishwa kupitia kwa Wakili wao Peter Kibatala kuwa muda umesogezwa hadi saa 7:30 mchana.

7:30 Mchana : Hukumu ya kesi imeanza

Hukumu hiyo inasomwa kwenye Mahakama ya wazi na Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba. Ulinzi umeimarishwa ndani na nje ya Mahakama.

Kukaa.jpg
Idadi kubwa ya wananchi na wafuasi wa chama hicho wamezuiwa kuingia mahakamani, kutakiwa kutoka nje. Waliamua kukaa chini karibu na mlango mkuu wa kuingia kwenye jengo la Mahakama mpaka Polisi walipowafukuza kwa vitisho. Baadhi yao wamesikika wakiimba nyimbo za kulituhumu Jeshi la Polisi kuwa CCM.

Video: Taswira ya hali ilivyo ndani na nje ya viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu


UPDATE: Wafuasi wa CHADEMA waanza kukamatwa

M1.jpg

Baadhi ya Wafuasi wa CHADEMA wamekamatwa na Polisi baada ya kukaidi amri ya kuondoka katika eneo la Mahakama ya Kisutu ambapo wamejikusanya ili kushuhudia hukumu dhidi ya Viongozi wa chama hicho


9:25 Alasiri: Hakimu Simba amehitimisha kusoma ushahidi upande wa Mashtaka

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba amemaliza kusoma ushahidi wa mashahidi 8 wa upande wa mashtaka. Sasa ameanza kusoma ushahidi wa mashahidi 13 wa upande wa utetezi.

10:20 Jioni: Mahakama yawakuta na hatia washtakiwa kwenye mashtaka 12 kati ya 13

Hakimu Simba amesema maneno haya yaliyotamkwa na Mbowe kwenye kampeni ni ya uchochezi ''Nchi imedharaurika,kwa lugha nyingine wanaume tunaonekana kama mademu,Lissu amepigwa risasi na vyombo vya dola watanzania mko kimya,ili tupate haki nchi hii Lazima tubebe majeneza''

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewatia hatiani washtakiwa wote katika mashtaka 12, isipokuwa shtaka la kwanza ambalo ni kula njama ambalo limefutwa na Mahakama. Ndugu wa washtakiwa waanza kuangua vilio ndani ya Mahakama.

UPDATE: Wakili Kibatala aomba washtakiwa kulipa faini

Wakili Kibatala amemwomba Hakimu kutoa hukumu ya washtakiwa walipe faini badala ya kuwapa adhabu ya kifungo baada ya washtakiwa wote kukutwa na Hatia kwenye makosa 12 kati ya makosa 13 yaliyokuwa yanawakabili.

ADHABU
Baada ya kuwatia hatiani washtakiwa kwa makosa 12, Mahakama imetoa adhabu kama ifuatavyo;

Hakimu: Madai ya kesi ya Akwilina hapa haipo. Isipokuwa maelezo yaliyopo hapa ni kwamba hali ile ilisababisha kuuwawa kwa mtu anayeitwa Akwilina. Siwezi sema Akwilina alikufa maana sina ripoti ya daktari inayothibitisha hilo. Suala la Akwilina siwezi kulizungumzia na siligusii kabisa.

Shtaka la 2: Mahakama imeamuru washtakiwa kulipa faini ya Tsh. Milioni 10 au kwenda gerezani miezi mitano

Shtaka la 3: Mahakama imeamuru washtakiwa kulipa faini ya Tsh. Milioni 10

Shtaka la 4: Mahakama imeamuru washtakiwa kulipa faini ya Tsh. Milioni 10

Shtaka la 5: Mahakama imeamuru Freeman Mbowe kulipa faini ya Tsh. milioni 10

Shtaka la 6: Mahakama imeamuru Freeman Mbowe kulipa faini ya Tsh. million 10

Shtaka la 7: Mahakama imeamuru Halima Mdee kulipa faini ya Tsh. milioni 10

Shtaka la 8: Mahakama imeamuru John Heche kulipa faini ya Tsh. millioni 10

Shtaka la 9: Mahakama imeamuru Freeman Mbowe kulipa faini ya Tsh. milioni 5

Shtaka la 10: Mahakama imeamuru Freeman Mbowe kulipa faini ya Tsh. milioni 5

Shtaka la 11: Mahakama imeamuru Freeman Mbowe kulipa faini ya Tsh. million 10

Shtaka la 12: Mahakama imeamuru Peter Msigwa kulipa faini ya Tsh. million 10

Shtaka la 13: Mahakama imeamuru Ester Bulaya kulipa faini ya Tsh. milioni 10

JUMLA YA KIASI CHA FAINI ATAKACHOTAKIWA KULIPA KILA MSHTAKIWA
John Mnyika - Tsh. milioni 30
Salum Mwalimu - Tsh. milioni 30
Ester Matiko - Tsh. milioni 30
Vincent Mashinji - Tsh. milioni 30
John Heche - Tsh. milioni 40
Peter Msigwa - Tsh. milioni 40
Halima Mdee - Tsh. milioni 40
Ester Bulaya - Tsh. milioni 40
Freeman Mbowe - Tsh. milioni 70

Mahakama imesema endapo washtakiwa wakishindwa kulipa faini, wataenda gerezani kwa miezi mitano kwa kila kosa.

Viongozi wa Chadema, akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe wamepelekwa katika gereza la Segerea baada ya kushindwa kulipa faini

MWISHO: Mahakama imeahirishwa

Kwa wanaohofia itaathiri kugombea Ubunge: KATIBA INASEMAJE?

A60AE7AF-6C91-4EED-A69C-C14B66A9480F.jpeg


TUJIKUMBUSHE MASHITAKA

Mashitaka 13 waliyoyatenda, ikiwemo ya kufanya mkusanyiko usio halali, uliosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.

Alipokuwa akisoma mashitaka hayo February 22, 2018, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja Nchimbi alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa ,washitakiwa kwa pamoja walitenda makosa hayo Februari 16, mwaka 2018 maeneo ya Viwanja vya Buibui na Barabara ya Kawawa, Mkwajuni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Katika mashitaka ya kwanza la kula njama: Kwa pamoja inadaiwa Februari Mosi na 16, 2018, Dar es Salaam, walikula njama pamoja na wenzao ambao hawapo mahakamani, ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali, mkusanyiko wenye ghasia na kukiuka tamko kutawanyika.

Inadaiwa kuwa Februari 16,2018 katika ya Viwanja vya Buibui na Mwananyamala Kinondoni, washtakiwa hao wakiwa wamekusanyika na azma ya pamoja waliitekeleza, walifanya mkusanyiko usio halali na kusababisha watu waogope na kusababisha uvunjïfu wa amani.

Katika mashitaka ya tatu, Washitakiwa hao wanadaiwa kuwa Februari 16,2018 katika viwanja vya Buibui Mwananyamala na Barabara ya Kawawa Kinondoni, kwa pamoja na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani, walitekeleza mkusanyiko ama maandamano yasiyo halali wakiwa na lengo la kuvamia ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na kuĺeta hofu ya uvunjifu wa amani.

Nchimbi alidai kuwa Februari 16,2018 katika Barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni, washtakiwa hao wakiwa na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la Ofisa wa Polisi, Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kupelekea uvunjifu wa amani, ambao ulisababisha hofu na hatimaye kifo cha Akwilina na majeruhi kwa askari wawili ambao ni H.7856 PC Fikiri na E.6976 CPL Rahim Msangi.

Katika mashitaka ya tano, linamkabili Mbowe ambalo ni la kuhamasisha chuki inadaiwa kuwa Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Mbowe wakati akihutubia wananchi wa jimbo hilo, alihamasisha chuki isivyo halali kwa kutoa matamshi yafuatayo “Ninapozungumza hapa kiongozi wetu wa Kata ya Kinondoni Hananasif yupo mochwari..amekamatwa na makada wa CCM kwa msaada wa vyombo vya ulinzi na usalama...wamemnyonga wamemuua.

Halafu sisi tunaona ni jambo la kawaida...tunacheka na polisi...tunacheka na CCM” Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa na lengo la kuamsha hisia za chuki miongoni mwa Watanzania.

Katika mashtaka ya sita, Mbowe anadaiwa kuwa Februari 16, 2018 katika mkutano wa umma uliofanyika viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni Dar es Salaam, Mbowe alitamka maneno yafuatayo “Tumejipa kibali cha kutangulia mbele ya haki...haiwezekani wanaume wazima na akili zetu na wake zetu na watoto wetu tukafanywa ndondocha..hiii ni nchi ya ajabu. Mimi leo nipo hapa kulinda taifa...kule Afrika Kusini Jacob Zuma amelazimishwa kujiuzulu...Robert Mugabe wa Zimbabwe kang’olewa, kang’olewa Waziri Mkuu wa Ethiopia...juzi ameondoka kwa People’s Power. Magufuli ni mwepesi kama karatasi”.

Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa ya kuinua hali ya kutoridhika miongoni mwa watanzania dhidi ya serikali halali iliyopo Mdee anadaiwa kuwa Februari 16,2018 akiwahutubia wakazi wa Kinondoni alitamka kuwa “Sihitaji kuwasïmuĺia madhila yanayomkumba kila mmoja wetu kutokana na utawala wa awamu ya tano... tunamba kesho tukamchinje Magufuli na vibaraka wake wote...kama mbwai na iwe mbwai”.

Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa na lengo kuhamasisha hisia za chuki miongoni mwa watanzania.

Katika mashtaka ya nane, la kuhamasisha hali ya kutoridhika, Heche anadaiwa kuwa Februari 16,2018 katika Viwanja vya Buibui alitamka kuwa “Kesho patachimbika, upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii... wizi unaofanywa na serikali ya awamu ya tano...watu wanapotea...watu wanauawa wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome..”.

Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa na lengo kuamsha hali ya kutoridhika miongoni mwa watanzania dhidi ya utawala uĺiopo madarakani. Katika mashtaka ya tisa ya uchochezi wa uasi, linalomkabili Mbowe, anadaiwa kuwa Februari 16,2018 katika maeneo hayo, alihutubia mkutano wa hadhara, alitamka maneno kuwa

“Ninaongoza mapambano nchi hii kwasababu tumechoka kuuawa...matokeo ya watanzania mia watakaokufa wataleta haki katika taifa hili. Wangapi wapo tayari kuchukua bei hiyo.” Nchimbi alidai kuwa maneno hayo, yalikuwa na nia ya kuleta chuki na hali ya manung’uniko miongoni mwa jamii dhidi ya utawala ulïopo madarakani.

Katika mashitaka ya 10 ya uchochezi wa uasi, linalomkabili tena Mbowe anadaiwa kuwa Februari 16,2018 katika maeneo hayo mkoani Dar es Salaam, Mbowe alitoa matamshi ya kupandikiza chuki na dharau kwa upande wa raia wa Tanzania dhidi ya mamlaka halali kuwa “Hii nchi inadharaulika...imejengewa misingi wa uwoga, kwa lugha nyingine wanaume ni kama mademu, si unawaona hao wanavaa suruali, waoga, bure kabisa...juzi ametekwa kijana wetu wanasema yupo mochwari, haki ya Mungu ingekuwa nchi nyingine Kinondoni ingekuwa majivu...

Lissu amepigwa risasi machine gun na vyombo vya dola...watanzania mnarudi nyuma...kuna mwandishi wa habari leo ana siku 86 amebebwa na vyombo vya dola... suluhu ya nchi hii haipi bungeni. Suluhu ya nchi jii ipo kwa wananchi wenyewe...

lakini ili tupate suluhu hiyo, ni lazima tukubali kubeba majeneza...Inawezekana leo mnaogopa kufa...Ni bora tuwabebe wachache hata wakiwa 200 waliokufa katika ukombozi ili hatimaye nchi hii isimame kama nchi ya wanaume wengine katika dunia hii” Mbowe pia anadaiwa kuwa alishawishi wakazi wa Kinondoni, kutenda kosa la kufanya maandamano na mkusanyiko usio halali.

Katika mashitaka ya 12 ya kushawishi utendaji wa kosa la jinai, linalomkabili mshtakiwa wa pili Msigwa, katika maeneo hayo hayo, Msigwa anadaiwa kushawishi raia na wakazi wa eneo hilo, kutenda kosa la jinai, kwa kutembea mbele ya umma wakiwa na silaha

Mashtaka ya 13 ambayo yanamkabili mshtakiwa, Ester Bulaya anadaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu katika Viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni, Dar es Salaam alïtenda kosa la kukaïdi amri halaĺi ya tamko.

Zaidi, soma: Jinsi ya kuchangia faini ya Tsh. Milioni 350 waliyohukumiwa Viongozi wa CHADEMA
 
For the English Audience
Dar es Salaam: Kisutu Resident Magistrate Court has found Tanzania’s Main Opposition Party (CHADEMA) Chairman, Freeman Mbowe and eight other co accused guilty of the 12 counts out of the 13 that they were charged with.

All the nine accused were sentenced to either pay fines of at least Sh 30 million each or serve a jail term of up to five months.

Former party Secretary General Vincent Mashinji (who moved to the country’s ruling party, CCM), Salum Mwalimu, John Mnyika and Ester Matiko were found guilty of counts 2, 3 and 4. Therefore, each is required to pay a fine of Sh30 million.

On the other hand John Heche, Peter Msigwa, Halima Mdee and Ester Bulaya who are members of parliament, are all required to pay TSh 40 million, whereas the Party chairman Freeman Mbowe has been fined TSh 70 million.

This is after Resident Magistrate Thomas Simba found that the prosecutor had proved beyond reasonable doubt in 9 counts out of 13, which were counts 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12 and 13. He, however, said the prosecution failed to prove their case in counts 1, 2, 3 and 4.

They are charged with conspiracy to commit offences, unlawful assembly, rioting after proclamation, raising discontent and ill-will for unlawful purposes, sedition and inciting commission of offenses.

These offenses are alleged to have been committed between February 1 and 16, 2018 in Dar es Salaam.

WIGWA

JF-Expert Member
Jul 27, 2019
1,004
1,000
hakimu yupo likizo mpaka mwezi ujao watahukumiwa october hao miezi mitatu jela
 

johnthebaptist

JF-Expert Member
May 27, 2014
50,925
2,000
Ni tukio la kihistoria.

Wapiga kura kutoka majimbo ya Iringa mjini, Tarime mjini, Tarime vijijini, Bunda, Hai, Kawe na Kibamba bila kujali itikadi " watajikuta" wamekutana katika mahakama ya kisutu kusikiliza hukumu za wabunge wao.

Tunamwomba mwenyezi Mungu haki ikatendeke mahakamani pale.

Nawatakia Kwaresma yenye baraka.

Maendeleo hayana vyama!
 

mculture3

Senior Member
Feb 24, 2017
126
250
Leo ndio hukumu juu ya mashitaka ya viongozi wa CHADEMA kwa kufanya maandamano kudai haki yao ya mawakala kupewa barua za utambulisho kwa mawakala na kusabisha kifo cha Aquilina.

#NipasheHabari Leo ni hukumu, ikiwa inatimu miaka miwili na siku tano, tangu kuanza kwa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, na viongozi wanane waandamizi wa chama hicho. Hatima kina Mbowe kortini leo
Tuombe Mungu haki itendeke
IMG-20200310-WA0009.jpeg


Sent using Jamii Forums mobile app
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom