Rasimu ya katiba na uhuru wa mahakama

Getstart

JF-Expert Member
Oct 13, 2012
6,658
2,235
RASIMU YA KATIBA NA UHURU WA MAHAKAMA
Utangulizi
Mihimili mikuu ya Dola lolote inahusisha Serikali (ambayo ni mtendaji), Bunge na Mahakama. Mihimili hii inatakiwa kuwa huru katika utendaji wa majukumu yake bila mhimili mmoja kuingilia mwingine katika mgawanyo wa majukumu yao. Kwa Mahakama msingi huu ni wa mhimu sana ili siyo kuiwezesha itoe haki bila hofu ya kuingiliwa lakini pia kuiwezesha kujenga taswira kwa raia kuiamini kama kimbilio lao la kupata haki.

Sura ya Kumi ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazungumzia Mahakama ya Jamhuri ya Muungano. Katika Sura hii inaainisha misingi ya utoaji haki na uhuru wa Mahakama, muundo wa Mahakama, Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mfuko wa Mahakama. Jamhuri ya Muungano itakuwa na Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani.

Kama nilivyosema umuhimu wa uhuru wa Mahakama ni kitu cha msingi katika utoaji haki. Hata hivyo ukisoma Rasimu hii ni dhairi Mahakama kwa muundo huu haina uhuru tuanaotarajia iwe nao sisi raia. Hapa chini ni uchambuzi na mapendekezo ambayo yangezingatiwa kuifanya Mahakama iwe huru katika utoaji wa haki.

Uhuru wa Mahakama
Msingi huu umewekwa katika Ibara ya 145(1) ambayo inasema "Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, Mahakama ya Jamhuri ya Muungano itaongozwa na masharti ya Katiba hii na haitaingiliwa ama kwa kudhibitiwa, kushinikizwa au kupewa maelekezo na mtu au chombo chochote." Ibara hii haina tofauti sana na Ibara ya 107B ya Katiba tunayoitumia sasa.

Wote ni mashuhuda wa vitendo vilivyoashiria Mahakama kuingiliwa na mihimili mingine ya Dola ama kwa kutengeneza mazingira ya maamuzi ya shahuri au shughuli iliyo mbele ya jaji, au kutunga sheria ambayo inafifisha uhuru wa Mahakama. Kwa hiyo waingiliaji wakubwa wa uhuru si mtu au chombo kingine chochote cha kawaida zaidi ya Mihimili hii miwili. Ninapendekeza Ibara ndogo hii iweke kipengele cha dhairi kuzuia Mahakama kuingiliwa na Mihimili hii. Muhimu wa ili utaonekana katika aya zifuatazo.

Mahusiano ya Mahakama na Serikali
Mahusiano makubwa yanaonekana hasa katika uteuzi na kuapishwa kwa Jaji Mkuu na Naibu wake, Majaji wa Mahamaka ya Juu, Mwenyekiti na Majaji wa Mahakama ya Rufani.

Sifa za watu hawa zinafanana ingawa Tume inashauriwa izipitie ili kuzifanya ziwe kamilifu na linganifu zaidi. Kuna maeneo hasa yanayohusiana na shahada yanatofautiana. Sehemu kadhaa inatamka ni shahada ya chuo kikuu, nyingine ni shahada ya chuo. Pia katika kufafanua chuo au chuo kikuu yanatumika maneno tofauti kama vile … kinachotambulika na mamlaka inayoshughulikia elimu ya juu katika Jamhuri ya Muungano na sehemu ingine ni kinachotambuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Tofauti hizi ni hatari kwa Katiba ya nchi.

Ibara za 151 na 152 ya Rasimu, zinampa madaraka Rais kuwateua Jaji Mkuu na Naibu wake kwa mapendekezo ya Tume ya Utumishi wa Mahakama. Tume hii ya Utumishi itamplekea Rais majina matatu katika kila nafasi na yeye anakuwa na uhuru wa kuchagua yeyote miongoni mwa hao. Mchakato huu si sahihi.

Ninafikiri ili kuondoa dhana kuwa Rais, ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Mhimili mmoja wa Dola, ana madaraka juu ya Mahakama, ni vyema Rais akapelekewa Jina moja la kuteua. Akilikataa awe na sababu za msingi ambazo zitaainishwa ili mchakato uanze upya. Hata kama akipelekewa majina zaidi ya moja, asiwe na uhuru wa kuacha jina la kwanza bila sababu kwa uwazi.

Mbaya zaidi katika Ibara ya 162 Rais kapewa mamlaka ya kutengua sifa za Mwenyekiti wa Mahakama ya Rufani na kumwezesha mtu asiyefikia sifa hizo kuajiriwa. Wakati huo huo hakupewa mamlaka hayo kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani (Ibara ya 163)! Hii si sahihi, mamlaka haya yasiwekwe katika Katiba. Kuna uwezekano kuwa na
Mwenyekiti mwenye sifa za chini kuliko Majaji anaowaongoza. Ibara ya 165 (2) inamtaja Naibu Mwenyekiti wa Mahakama ya Rufani, lakini hakuna sehemu inayoelezea uteuzi na sifa zake!

Katika Mahakama zote mbili (ya Juu na ya Rufani) kumewekwa utaratibu wa kuwapata Majaji wa kukaimu katika nafasi hizo (Ibara 156 na 166). Ibara hizi zinampa Rais uhuru wa kuchagua mtu mwenye sifa za kuwa Jaji wa Mahakama ya Juu au Jaji wa mahakama ya Rufani. Rais akishashauriwa na Jaji Mkuu kuwa kunahitajika Jaji wa kukaimu, yeye anateua, wala hahitaji kupata mapendekezo ya Tume ya Utumishi au hata ya Jaji Mkuu!

Tume ya Utumishi wa Mahakama pia imejaa wateule wa Rais – wale wanaoingia kwa mujibu wa nafasi zao, na wengine wote wanaoteuliwa kuingia. Tume hii ambayo inaajiri watumishi wa Mahakama na inapendekeza watu wa kusika nafasi za Jaji Mkuu, Naibu jaji Mkuu, Mwenyekiti na Majaji wote wa Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani imewekewa utaratibu katika Ibara ya (173). Ibara hii inaitaka Tume kuzingatia uwazi katika mchakato wa uteuzi wa Majaji na ajira zingine za watumishi wa Mahakama.

Hii ni habari njema lakini ninapenda iwe wazi zaidi kwa kuweka mazingira haya katika mchakato wa Jaji Mkuu na Naibu wake na pia kwa Mwenyekiti. Lakini isiishie kwa uwazi tu, bali iruhusu watu kushiriki katika mchakato kwa kutoa taarifa za siri au wazi kwa wanaopendekezwa. Ndiyo maana katika uwazi huu ni mhimu nafasi hizi zote zikatangazwa na watu wenye sifa wakaomba. Na kwa mantiki hiyo ama ndani ya Katiba hii au katika Sheria itakayoweka utaratibu wa mpito, hata hawa Majaji (na mahakimu) waliopo sasa itabidi wawekewe utaratibu wa kuchujwa kwa uwazi.

Mahusiano ya Mahakama na Bunge
Bunge linawajibika kuthibitisha uteuzi wa Rais katika nafasi za Jaji Mkuu na Naibu wake tu. Mwenyekiti na Majaji wengine (wa Mahakama ya Juu na Rufani) uteuzi wao hauhitaji kuthibitishwa na Bunge.

Bunge kazi yake kubwa ni kutunga sheria. Katika sheria zinazohitajika kutungwa ni zile zitakazoweka masharti zaidi ya uendeshaji wa Mahakama ya Juu, Ibara ya 149(4), Mahakama ya Rufani, Ibara ya 160(3) na ya majukumu ya Tume (173(5)). Lakini pia Bunge linawajibika kutunga sheria zitakazoweka utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani. Bunge pia litaweka viapo vinavyohusika na utendaji wa jaji Mkuu, Naibu jaji Mkuu, Majaji wa Mahakama ya Juu, Mwenyekiti wa Mahakama ya Rufani na Majaji wa Mahakama ya Rufani.

Kuwapa Bunge mamlaka ya kutunga sheria za taratibu za nidhamu si sahihi. Tunao ushuhuda kilichotungwa miaka ya hivi karibuni katika Bunge ili tulilo nalo sasa! Kama Mhimili wa Dola , mahakama inao uwezo wa kuweka taratibu zake za kinidhamu au ikiwezekana taratibu hizi ziwekwe ndani ya Katiba hii. Pia Ikiwa utaratibu wa kumteua jaji Mkuu, Naibu Jaji Mkuu na Majaji wote utakuwa wa wazi na shirikishi, sioni sababu ya kupeleka majina yao Bungeni kuthibitishwa.
Pamoja na utaratibu wa uteuzi wa jaji Mkuu na Naibu wake kuainishwa, hakuna Ibara inayoweka utaratibu wa kuwaondoa kazini. Ibara ya 167(3) inaweka marejeo kwa utaratibu huo ambao haupo!

Tamati
Jaji Mkuu, kwa mujibu wa Rasimu hii ni Rais wa Mahakama ya Juu (Ibara 147(1)(a)) na Mkuu wa Mhimili wa Mahakama katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo kwa mujibu wa Rasimu hii hana mamlaka yoyote kwa Majaji, Msajili na watumishi wengine katika Mhimili huu. Hausiki na uteuzi wao wala kuondolewa kwao.

Kwa sisi wananchi na uzoefu tuliokwishauona miaka 50 iliyopoita, tunataka tuhakikishiwe na Katiba hii kuwa tutakuwa na chombo huru kitakachotoa haki bila kuingiliwa au kuelekezwa. Ni vizuri Jaji Mkuu akapewa nyenzo na madaraka ya kushughulikia Mhimili wake ili kukitokea mapungufu tumbebeshe mzigo yeye mwenyewe.

Tume ya Jaji Warioba, kama inavyojulikana, ilisheheni wanasheria akiwemo na Jaji Mkuu mstaafu aliyewahi kulalamika kuhusu kuminywa uhuru wa Mahakama. Jaji Mkuu aliyepo katika moja ya mapendekezo yake kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari ni kutaka uhuru zaidi wa Mahakama na kuzuia kutoingiliwa. Kulikoni?
 
Ni fedheha kwa ccm kuingilia uhuru wa mahakama zetu,iko wapi Democrasia?Ni kweli ccm wanatumia udhaifu wa katiba yetu kufanya watakavyo maana Mwenyekiti wa ccm ndio mteuzi wa majaji na mahakimu. Hawa wanafata maelekezo na wanaogopa kutunbuliwa.
 
Ni fedheha kwa ccm kuingilia uhuru wa mahakama zetu,iko wapi Democrasia?Ni kweli ccm wanatumia udhaifu wa katiba yetu kufanya watakavyo maana Mwenyekiti wa ccm ndio mteuzi wa majaji na mahakimu. Hawa wanafata maelekezo na wanaogopa kutunbuliwa.

Katiba mpya ndio suluhisho, Mkuu.
 
Ni fedheha kwa ccm kuingilia uhuru wa mahakama zetu,iko wapi Democrasia?Ni kweli ccm wanatumia udhaifu wa katiba yetu kufanya watakavyo maana Mwenyekiti wa ccm ndio mteuzi wa majaji na mahakimu. Hawa wanafata maelekezo na wanaogopa kutunbuliwa.
Mahakama haifanyi kile unacho kitaka wewe !!
Mkishinda mnajitapa Serikali haina wasomi
Mkishindwa
Mahakama ya ccm!!
Utoto nao ni Upumbavu mwingine!!
 
Back
Top Bottom