Magazetini
JF-Expert Member
- Aug 16, 2014
- 593
- 1,712
Habari wakuu,
Leo Rais Magufuli anakutana na wazee wa Dar es Salaam baada ya kumpa mwaliko, wazee waliofika mpaka sasa kwa makadirio ni 5,000. Anayeongea kwa sasa ni mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam. Tuwe sote kujuzana yatakayojiri.
======
Meck Sadick: Baada ya kutangaza elimu bure, wanafunzi waliofikia umri wa kuanza shule na waliopitiliza wamekuwa wakiandikishwa kwa wingi. Kwa utaratibu wa wizara ya elimu uandikishaji unaendelea mpaka tarehe 31/3/2016, shule zimendikisha wanafunzi wengi kuliko malengo mfano Mzinga walilenga kuandikisha 100 lakini mpaka juzi walishaandikisha wanafunzi 541.
Niishukuru kampuni ya TSN kwa kukubali kujenga darasa moja katika shule ya majimatitu pia tuliiga mfano wako wa kubana matumizi na tulikutana kuangalia maeneo gani tuliyoyatengea fedha ili kuweza kubana ikiwemo safari na tumeweza kuokoa bilioni 4.6 na wewe tulikuomba kuhamisha hizi fedha kuelekea maeneo yenye tija na umeshaturuhusu kutumia hizo pesa kwenye mambo ya maendeleo, tunakushukuru sana.
Tunahamasisha wakazi wa Dar kuhamasika kuchangia elimu kwa hiari ikiwemo madawati na hapa hatupingani na sera ya elimu bure na wapo wenzetu wameshaonyesha nia ikiwemo Azim Dewji alietoa madawati 500, ubalozi wa China ambayo tumeyapeleka Majimatitu na wengine wengi.
Nichomekee tu, hata meza kuu wanaweza kuchangia kwa ajili ya maendeleo ya Dar es Saalaam.
Katika kuchangia kutatua changamoto za elimu, wanasiasa pia nawaomba washiriki bila kujali chama, sote tunajenga nyumba moja haina haja kugombania fito.
Samia Suluhu: Tunazungumzia leo mafanikio ya siku 100 katika ofisi, naomba niwaahidi, mwendo huu utakuwa ni wa kudumu, waliosema tuna nguvu ya soda naomba watuangalie. Hatutawaangusha, tuko pamoja nanyi, Tanzania Oyee, Nawashukuru sana.
Majaliwa Kassim: Dar es Salaam oyeee, nimepewa nafasi kuja kuwasalimia na si ndefu, ningependa nirudie aliyoyasema kiongozi wangu makamu wa Rais, leo tunatimiza siku 100 tangu tuanze kazi nami nimo humohumo kwenye siku 100.
Nataka niwaahidi tena mimi na mawaziri wenzangu, tutawatumikia, tutawahudumia na wala msiwe na shaka, tumejipanga vizuri, muhimu muendelee kutuombea, sina neno la ziada, tunawapenda sana watanzania na tunatambua mnayoyataka, tutapita huko huko na kufanya mnayoyataka.
======
Mwakilishi wa wazee: Watanzania walifanya uamuzi sahihi na wa busara walipokuchagua wewe kuwa Rais wa Tanzania, tunaamini tutapiga hatua kubwa, tunakuomba mheshimiwa Rais uendeleze kasi yako hio na usilegeze kamba, wazee wa Dar na nchi nzima tutakuwa nawe bega kwa bega.
Kwa mfano uliahidi elimu bure, umeanza kutekeleza na hukungoja. Uliahidi kuboresha huduma za afya, tunakushukuru sana ukiahidi unatenda. Umeokoa takribani bilioni 7 kwa kudhibiti safari za viongozi wa umma, uliahidi kutoa pesa kwa mahakama, umetekeleza ndani ya siku nne tu. Sote tunashuhudia, asante sana baba.
Uliahidi kuongeza mapato kwa kuongeza kukusanya mapato ya kodi mpaka sasa umekusanya trilioni 3.4. Tunajua wapo watakaobeza lakini kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala, mti wenye matunda hauishi kupopolewa, huwezi kupopoa mchongoma.
Hapa kazi tu.
========
Mama Janet Magufuli nae kasalimia wazee wa Dar es Salaam na anaekaribishwa baada ya hapo ni Rais wa Jamhuri wa muungano wa Tanzania.
======
Magufuli: Napenda niwahakikishie wazee na watanzania kwa ujumla, hatutawaangusha. Kwa niaba ya viongozi wenzangu, nawaahidi tutawafanyia kazi, ninachowaomba wazee na watanzania kwa ujumla, mtuamini.
Katika shughuli zozote za kufanya mabadiliko huwa kuna changamoto zake, watakaoguswa ni wachache sana kwa ajili ya watanzania wote hasa maskini. Haipaswi kuwa maskini, Tanzania hii ina utajiri wa kila aina, haipaswi kuwa na wanafunzi wanaokaa chini, watu wanaolala chini mahospitalini.
Lakini ni lazima tujue wapo watu wachache waliotufikisha hapa, mlituchagua kwa mioyo yenu wote, ndio maana nasema kwa dhati naomba mtuamini kwa sababu tunaamini tukiyatekeleza haya, nchi hii itakuwa ya mfano Afrika kama si duniani kwa ujumla.
Mimi na serikali yangu tumejitoa sadaka kwa ajili ya watanzania, tunaomba muendelee kutupa nguvu ili haya matamanio yetu kwa ajili ya Tanzania yote tena kwa haraka.
Yoyote atakaejaribu kutukwamisha serikalini tutambomoa kwa ajili ya watanzania.
Wapo watu kwao pesa si tatizo na angalau wangezipata kihalali, lakini ni za wananchi wenye hali mbaya sana. Kilometa moja imejengwa kwa bilioni mbili tena ni barabara ya halmashauri, nimekaa serikalini miaka 20 na sijawahi kutengeneza barabara kuu, kilometa moja kwa bilioni mbili lakini barabara ya halmashauri tena ya Bariadi inatengenezwa kwa mabilioni ya shilingi zilizokuwa zinatoisha kutengeneza zaidi ya kilomita 20
Waziri alienda kuangalia mafuta, PUMA na ORLX serikali ina share ya asilimia 50. Flow meter ambayo ndio inapima mafuta kiasi gani yanaingia nchini haifanyi kazi miaka mitano na Dar es Salaam kila kona kuna sheli.
Nilikutana na wakina mama wakaniambia twende ukaone, nilishaenda lakini ilikuwa upande mwingine, wasaidizi wangu wakaniambia usiende lakini nikaenda. Nikakuta maji ya kutoka chooni yanaingia, wakina mama wamelala chini wakati kuna jengo linajengwa tangu awamu ya mzee Mwinyi halijaisha mpaka leo.
Wazee tunapochukua hatua, sisi si wakatili sana, tunawawakisha nyinyi uchungu wenu. Ninafahamu mawaziri wangu wanafanya kazi nzuri. Ninawapa muda na nyinyi muwape muda na mimi mnipe muda.
Lile jengo linalotumika kama ofisi ya uzazi wa mpango wahame na waziri atajua atawapeleka wapi tena kwa kuwa ni ofisi kama ya waziri, anaweza kwenda kukaa nao ofisini kwake, wale kina mama waliokuwa wanalala chini wahamie hapo.
Ninawaomba katika kipindi hiki cha mpito mtuvumilie, majipu tutayambua kweli kweli.
Tanzania haiwezi kwenda mbele bila kuwa na fedha zake, wafanyabiashara wanakwepa sana kodi. Tunataka fedha tunazozikusanya ziende kuwasaidia watanzania wa hali ya chini.
Zipo kejeli nyingi kuwa ni nguvu ya soda, hata kama ni soda ukiweka gongo utalewa, kwa hio hii ni soda special.
Tumeweka bilioni 200 kwa ajili ya daraja la Coco beach hadi Agha Khan, barabara ya kutoka Rangi tatu pia tumeitengea fedha na interchange ya ghorofa tatu pale Ubungo.
Shirika la ndege tunataka kulifufua ndio maana tunachukua hatua mbalimbali. Yuko mmoja ameshikwa pale alikuwa anataka kubadilisha fedha kwenye akaunti tukamkamata, hatutaki kusema mengi kwa sababu hatua zinachukuliwa ikiwemo za kimahakama.
Watanzania tujifunze kulipa kodi, chochote unachoenda kununua omba risiti. Kuna sehemu inatakiwa kubaki kwa ajili ya kuhudumia watu.
Nimemuona Makonda akihamasisha, limekujengea heshima kubwa kwa hio ukipanda hata cheo, watu wasikuonee kwa sababu you deserve it.
Kwa sababu na sisi tunakaa Dar, nilikuwa nazungumza na makamu na waziri mkuu. Tunaokaa Dar ikiwemo mawaziri na makatibu wakuu, nikasema kwa sababu wakati nafanya uteuzi niliwateua na hawakuniomba, nikiwaambia leo watoe milioni moja moja ni vibaya? Tunakusanya milioni 80 bado kuna mimi, kisha tutatenga bilioni mbili tuzigawe hizo fedha Dar ili zikajengwe hizo shule.
Michango ni hiari, pasitokee watu kupitia hii hotuba wakaanza kulazimisha watu, watakaoguswa kuchangia wachangie.
Najua sijateua wakuu wa mikoa, ma-DC na wakurugenzi, nimefanya makusudi ili niendelee kuchanganua nani anatosha na nani hatoshi, kutosha kwao ni kutatua kero za wananchi.
Yapo magazeti mengine wanaandika mpaka unashangaa, unajiuliza yakitokea machafuko wana mahali pa kwenda kukaa. Nayapongeza magazeti mengi mfano gazeti la Jamhuri lilivyoenda kufufua uozo wa Flow meter.
Kuhusu Zanzibar, kama tume za uchaguzi nyingi duniani, haiwezi kuingiliwa na Rais yeyote ndiyo maana tume za uchaguzi huwa huru. Napenda kuheshimu sheria kwa hio ZEC ina uhuru wa kuamua mambo yake lakini kama kuna tafsiri mbaya, waende mahakamani, mahakama ziko pale halafu unamwambia Magufuli ingilia.
Jukumu langu kama amiri jeshi mkuu ni kuhakikisha amani ya Zanzibar inaimarika, yeyote atakaeleta fyoko fyko ajue vyombo vya usalama vipo.
Kwa niaba ya serikali ninayoiongoza, sisi tuko makini, niwahakikishie tutaweza na Tanzania tutaivusha, itaenda mbele kwa ajili ya maendeleo ya watanzania wote. Naomba wazee wangu na watanzania kwa ujumla mtuombee, wanaolalamika wachache muwapuuze kwa sababu ni miongoni ya waliofaidi matunda ya wanyonge kwa miaka ya nyuma.
Niwahakikishie wafanyabiashara tuko pamoja nao katika biashara zao zote halali, na wafanyabiashara watanzania huu ni wakati wao, taifa haliwezi kujengwa na watu kutoka nje.
Tunataka Tanzania iende mbele kwa ajili ya watanzania wote.