Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,741
- 40,868
Niliamini pia kuwa CCM inapaswa kuvunjika ili Taifa lipone. Sikuona ni jinsi gani CCM inaweza kuokoleka; na hili sina shaka nilikuwa sahihi. Kitu ambacho labda sijawahi kukidhania kwa kina ni jinsi gani CCM inapenda kujifunga yenyewe kamba shingoni na kujitundika; wapinzani huwa hawana kazi zaidi ya kushabikia na kuchekelea.
Ujio wa Magufuli na ajenda ya mabadiliko umetufundisha jambo moja kubwa - CCM inaelekea kuvunjika kutokea ndani. Mjadala wa masuala ya posho kwa namna fulani na kauli za baadhi ya wana CCM kuonekana kutokuwa katika mstari wa kutaka mabadiliko unanifanya niamini kabisa kuwa CCM inaenda kuvunjika kutoka ndani kuelekea kambi mbili; kambi hizi mbili si mpya kwa wengi wetu kwani zilishakuwepo. Zilikuwepo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 na inaonekana pamoja na kuwa wote wanaonekana kuvaa kijani na njano, lakini ndani yao wako kama nyeusi na nyeupe!
Kuna kambi ya maslahi - hii ni kambi ya wale ambao uwepo wa CCM madarakani ni mafanikio kwao, watoto wao na jamaa zao. NI kambi ambayo imetusumbua sana kama taifa kwa miaka hii hasa ishirini; ni kambi ambayo haijali sana siasa, haijali sana utawala, haijali sana serikali inafanya nini; kambi hii inajali zaidi inapata nini. NI kambi ya kimahesabu sana; ilipoona kuwa Magufuli na Watanzania wanaelekea kumkubali Magufuli kuliko yule mtu wao; watu hawa hawa ambao waliapa "aliko tuko" wakajikuta wameamua kujibanza humo humo CCM ili wajue watapata nini.
Tatizo ni kuwa hadi hivi sasa hawajui kama wanapata; na dalili zinaoonesha kuwa wasipoangalia wanaenda kukosa zaidi! Na hili la kukosa wakati wao ni watawala linawasumbua na hivyo wanaanza kujikuta wanasumbua. Hawa ni unprincipled.
Kambi hii ya pili ya CCM mabadiliko inawezekana ni kambi inayoundwa na watu ambao walikataa kabisa kupiga magoti mbele ya mafisadi na inawezekana na wao walikuwa wanajua kuwa ile kambi nyingine ingepata basi wao pia wasingepata. Hata hivyo, kambi hii inaamini kuwa Tanzania inahitaji mabadiliko ya kweli na kuwa nafasi ya kuwa kiongozi au mtawala ni nafasi ya kuwaongoza watu kupitia utawala kufikia mafanikio. Kambi hii naweza kusema ni principled.
Hawa wako tayari kusimama na Magufuli hata kama wanajua kuwa na wenyewe wanaisoma namba; lakini wanasema na "tunaisoma namba pamoja na Watanzania wenzetu". Kambi hii sidhani kama ni kubwa sana kulinganisha na ile nyingine; ni kambi ambayo watetezi wake hawajajipambanua sana kama wa ile kambi nyingine.
Kuelekea Uenyekiti wa Magufuli CCM nina uhakika wa asilimia 100 wale wa kambi ile nyingine - wale wanaotaka kupata - sitoshangaa watajikuta wanaanza kurudi na kuanza kuimba sifa za Magufuli na kuanza kujibanza kwenye jukwaa la 'mabadiliko' ili na wao wawemo. Tatizo ni kuwa wanajua kwa uhakika mkubwa kuwa hilo peke yake siyo hakikisho la wao kuja kupata. Wengi wa hawa - nikiruhusiwa kutabiri - wataanguka sana kwenye chaguzi zijazo kwani walikuwa wanasimama miguu yote upande ule kaini vichwa tu viko upande wa CCM.
Uenyekiti wa Magufuli ni tishio; ni tishio kwa sababu nguvu ya Mwenyekiti wa Chama ni kubwa mno na hili linawatatiza watu kwa sababu 'ukichaa' wa Magufuli ambao ameuonesha hadi hivi sasa wa kugusa visivyoguswa, kusema visivyosemwa na kutenda visivyowahi kufikiriwa vinaweza kutendwa vinawasumbua. Itakuwaje akishika chama; hivi Sekretariati yake itakuwa na watu gani? Je, wataweka maslahi ya CCM mbele kama Katiba ya CCM inavyotaka au yale ya Taifa kwanza?
Binafsi nafurahia mgongano huu na mpasuko huu; kwani ni mpasuko wa kifikra kwanza. Ni mpasuko na mgongano kama uliowahi kutokea ndani ya ANC; ni mgongano ambao unaweza kuwa umewahi kutokea kwenye vyama vingine vikongwe. Mpasuko wa CCM ambao wengine tulikuwa tunausubiria kwa muda mrefu na kuuombea inawezekana unaelekea kutokea ndani ya miezi hii michache.
Kumchelewesha Magufuli kuwa Mwenyekiti na kumchelewesha kuongoza Chama ni aina fulani ya hujuma - sijali sababu zinazotolewa. Ni hujuma kwa sababu kwenye nchi kama ya kwetu yenye masalia ya mfumo ule wa kisoshalisti (ni kweli mfumo wetu wa kisiasa una masalia hayo) Chama tawala ndicho kina nguvu sana ya kusimamia nchi; Rais asipokuwa kiongozi wa chama vile vile ni sawasawa na Rais wa China kutokuwa kiongozi mkuu wa chama cha Kikomunisti; au yule wa Korea ya Kaskazini kutokuwa kiongozi mkuu au Cuba, au Viet Nam.
Mpaka pale mfumo wetu utakapoweza kujengwa na kutenganisha uongozi wa kisiasa na uongozi wa kiserikaake ili, Rais wa nchi ili afanikiwe ajenda zake ni lazima awe kiongozi wa chama chake cha siasa vile vile. HIli ni kweli si kwa CCM tu bali hata kwa chama kingine kikija kushika.
NI wito wangu, uamuzi wa kumkabidhi Magufuli Uenyekiti uharakishwe; kwani nje ya hapo ni kutengeneza nguvu mbili zenye kushindana kuongoza taifa. Kuna mmoja tu aliyepigiwa kura na taifa zima kuliongoza kwa miaka mitano (siyo baadhi ya miezi ya miaka hiyo mitano). CCM na uongozi wake waamue hata kuuza majengo yao yote ili wakamilishe makabidhiano hayo na nchi iwe katika utaratibu wake uliozoeleka. Hata kama hawapendi au wanaona labda wacheleweshe kidogo.
Kumkabidhi Rais Magufuli Uenyekiti wa CCM mapema ndio njia pekee ya kutenganisha kambi hizi mbili za CCM Maslahi na CCM Mabadiliko. Hakuna njia nyingine, kwa sasa.
MMM