Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
- Kuanzia sasa vituo vya ukaguzi kuanzia Dar mpaka mpakani mwa Rwanda vitakuwa vitatu tu.
- Mpango wa kujenga Reli kutokea Tanzania kwenda Rwanda na kwenda Burundi uko pale pale na tayari kampuni 13 zimeshajitokeza kuanza kazi.
- Awataka wafanya biashara wa Rwanda kuacha kupitisha mizigo yao Kenya na Uganda warudi kupitishia Tanzania.
Akizungumza baada ya shughuli hiyo, Rais Magufuli aliagiza kupunguza vizuizi vya ukaguzi wa mizigo inayotoka na kwenda nje ya nchi akiagiza vibaki vitatu; vya Nyakahura, Singida na Vigwaza kutoka Dar es Salaam hadi mpakani hapo.
Alisisitiza umuhimu wa nchi hizo kuimarisha umoja wake na Afrika kwa ujumla ili kuwa na nguvu ya pamoja kujitegemea na kubadilishana bidhaa na ujuzi ili kupunguza umaskini.
Rais Magufuli alisema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu na kwamba mpango wa kujenga reli itakayounganisha nchi tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi uko palepale na kampuni 13 zimeshajitokeza kufanya kazi hiyo.
Rais Magufuli alisema kuanzia sasa, wafanyabiashara wa nchi hizo wako huru kutafuta bidhaa ndani ya Afrika ya Mashariki na kuingia katika nchi zao bila vizuizi njiani.
Alisema wafanyabiashara walikuwa wanafanyiwa urasimu kwani madereva wao wa walikuwa wakicheleweshwa na kulazimishwa kutoa rushwa jambo ambalo lilisababisha kudorora kwa upatikanaji wa bidhaa kwa wakati.
“Kuanzia leo, waliokuwa wakihitaji rushwa ya fedha, mkaa, vyakula na kuchelewesha wananchi kupata uchumi wao ni marufuku kufanya hivyo vinginevyo wajiondoe kazini,” alisema Dk Magufuli.
Alisema wafanyabiashara wa Rwanda wasitumie gharama kubwa kusafirisha bidhaa zao kupitia Kenya na Uganda, bali wapitie Tanzania na kukuza mitaji yao kiuchumi. Aliwataka wananchi wa pande zote mbili kuitunza miundombinu hiyo na kulinda amani na umoja wao kuhakikisha kila nchi inakuwa na usalama na kuendeleza uhusiano na nchi hizo.
Kuhusu uhusiano, Rais Kagame alisema ushirikiano wa Tanzania na Rwanda ni wa siku nyingi na kuahidi kwamba utaimarishwa zaidi kwa kuwahamasisha watu wa nchi hizi kufanya kazi kwa bidii na kupanua wigo wa biashara.
Alisema watu wanaoingia Tanzania na Rwanda kwa siku wanafikia 2,000 na kwamba idadi hiyo haina budi kufikia 10,000 hadi 15,000.
“Historia ya Rais Magufuli kutembea nje ya nchi imeanzia katika nchi yangu, hii ni kutokana na urafiki wetu hadi majina ya wake zetu yanafanana, sijui Mungu alipangaje kuonyesha upendo wa dhati,” alisema Kagame.
Chanzo: Mwananchi